Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Salome Wycliffe Makamba

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Naungana na Waheshimiwa Wabunge wenzangu, kwanza kuipongeza Wizara yetu ya Katiba na Sheria kwa kazi kubwa wanayoifanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijaanza kuongea leo tukiwa tunajadili Wizara ya Katiba na Sheria, nimeona chama changu wameandamana hapa Dodoma Bungeni na moja kati ya kilio chao kikubwa kilikuwa ni Katiba mpya. Nimeingia kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri, ukurasa wa 16 nimeona mchakato unakwenda kwa kasi kweli kweli kuhakikisha kwamba tunapata katiba mpya. Pia, naona kuna awareness kubwa inafanyika kupitia makongamano, semina, warsha na kupitia hii huduma yetu ya msaada wa kisheria unaotokana na Mama Samia Legal Aid. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa watutambue na sisi kwamba na sisi tunawasaidia kutoa elimu kupitia maandamano haya ambayo wameyaruhusu na wanaona ni ya amani na tunakwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuwapongeza, nataka niseme jambo moja kubwa ambalo kiukweli Mheshimiwa Naibu Waziri anatoka Kanda ya Ziwa na wale Wabunge ambao wanatoka Kanda ya Ziwa tuna changamoto kubwa sana ya mimba na ndoa za utotoni. Wabunge wenzangu wengine wanasema ni za udogoni kwa sababu mtoto hawezi kubeba mimba. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwenye bajeti iliyopita, Wizara hapa tuliiomba kwa dhati na bahati nzuri aliyeshika shilingi sasa hivi ni Mheshimiwa Naibu Waziri wa TAMISEMI, Mheshimiwa Zainab. Wakaweka commitment kubwa kweli kweli kwamba wataleta mabadiliko ya sheria na wakatuita kwenye kongamano kubwa ambalo lilikuwa live Tanzania nzima wanaona. Tukawaleta wazee wetu kutoka maeneo mbalimbali; waganga wa jadi waliletwa, viongozi wa kimila waliletwa na viongozi wa dini zote waliletwa wakatoa maoni yao. Mkwamo upo wapi? Shida ni nini na kwa nini hawaleti mabadiliko ya sheria? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilisema humu Bungeni, hata ule mchakato wenyewe wa kusema wanakwenda kukusanya maoni ya wadau ni kinyume na taratibu ya utungaji wa sheria. Mahakama ilishasema kwamba vifungu vile ni batili na watoto hawa wanaishi kwenye mazingira magumu. Walichotakiwa kufanya ni kuleta mabadiliko ya Sheria Bungeni na si kwenda kukusanya maoni ya wadau. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi Wabunge kwa sababu Mungu alitujalia busara na hekima tukamruhusu Waziri akajiridhishe. Alikuwepo Mheshimiwa Dkt. Ndumbaro hapo, leo Mawaziri wamekuja wengine, lakini kiukweli niwaambie kwenye hili kidogo tutatofautiana. Tunataka sheria inayoruhusu mtoto chini ya miaka 18 kuolewa kwa ridhaa ya wazazi wake iletwe hapa tuifanyie mabadiliko na watoto hawa waendelee kuwa salama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, uwekezaji mkubwa unafanyika kwa watoto hawa, tumerudisha re-entry program, Mheshimiwa Rais ameruhusu watoto warudi shuleni hata kama wamepata ujauzito. Tumetengeneza shule nyingi na madarasa mengi, watoto wa kike wanapewa hamasa kubwa ya kujiunga kwenye masomo hasa masomo ya sayansi. Kwa nini tunawawekea kikwazo hiki? Sisi kule kwetu Shinyanga tupo kwenye top three, sio sifa kuwa na watoto ambao wanaolewa katika umri mdogo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka huu ni mwaka wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa tukiwa tunaelekea kwenye uchaguzi mkuu. Waziri wa Katiba na Sheria, Naibu wake na Attorney General wanajua taratibu za utunzi wa sheria. Wizara ya TAMISEMI imekasimiwa mamlaka ya kutunga kanuni za uchaguzi, lakini kasma hiyo waliyopewa wanatakiwa kuleta Bungeni pamoja na kwamba tumewakasimu, wanatakiwa walete hapa kwa ajili ya Bunge kufanya scrutinization. Hawajaleta kanuni zile tuweze kuona, rules za mchezo ule zinakwendaje? Wanaendeshaje uchaguzi wa Serikali za Mitaa? Hakuna Mbunge hata mmoja hapa anayefahamu uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaendeshwa kwa kanuni za aina gani na sasa hivi wameshaanza kufanya uhuishaji wa daftari la mpiga kura; hawatutendei haki.

Mheshimiwa Naibu Spika, watuletee kanuni tuzione na nasema hivyo kwa uzoefu. Mwaka 2018, Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa zilikuwa mbaya sana na zililalamikiwa sana. Wazilete Bungeni tuweze kuzichambua na turidhike nazo, tujue kile ambacho tumekasimisha Wizara ya TAMISEMI kuweza kusimamia uchaguzi kupitia Tume ya Uchaguzi kinafanyika kama ambavyo Bunge linatarajia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza Serikali kwa kuanzisha msaada wa kisheria kupitia Mama Samia Legal Aid Campaign. Nataka niseme labda kuna changamoto fulani, tafiti haikufanyika ya namna ya utekelezaji wa zoezi hili ndiyo maana tunaona hata utekelezaji wenyewe unasuasua. Kusema kwamba watumishi wa Serikali au hii Idara ya Serikali inahusika na mambo ya legal aid ndiyo iende ikafanye legal aid, ikaweke mahema kule chini kwenye mikoa, ni kujidanganya wenyewe. Mategemeo ya Watanzania yalikuwa makubwa sana hasa ya kada ya sheria, tuna mawakili wengi, tuna wanasheria wengi, ni kwa nini wanatoa watu Wizarani? Ni kwa nini wanatoa watu kwenye maofisi yao kwenda kufanya hiyo kazi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana mpaka leo takribani mwaka mzima umepita wameenda kwenye mikoa sita tu kati ya mikoa 26 ambayo wametakiwa kuifikia. Hebu washirikishe wanasheria, wamesema wenzangu hapa vizuri, nilisema mimi nisiseme kuhusu law school, wamesema vizuri wenzangu. Kila mwaka tunatoa wanafunzi law school maelfu na maelfu, wale wanafunzi wapo mitaani, hawana kazi, lakini uwezo wa kutoa ushauri wa kisheria wanaweza. Kwa nini wasifanye kazi hiyo badala yake watumishi wa Serikali wanakwenda kufanya wenyewe? Dhana ya PPP ipo wapi katika jambo hili?

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kwa nia ya dhati, wapo wanasheria wanaoweza kufanya kazi hii ya legal aid, zipo NGOs. Kazi ya Serikali ibaki kuwa ya uratibu, kuratibu kwamba kile kinachokwenda kuwasilishwa kwa wananchi hakipotoshi. Hata ukiangalia kwenye misingi tu ya dhana ya haki, yaani hizo kesi nyingi zilizopo kule ni kesi za ardhi, ni kesi zinazohusiana na mambo ya mirathi ambazo wakati mwingine Serikali ni sehemu ya watu wanaoshtakiwa au kulaumiwa kwenye kesi hizo. Wanakwenda kutoa msaada wa kisheria, wao ndiyo Serikali, wanatoa msaada wa kisheria, wakipelekwa mahakamani wao ndiyo washtakiwa. Hapo haki itatendekaje? Kwa hiyo naomba kwa nia ya dhati hii kazi Serikali ibaki kwenye dhana ya uratibu na wabaki wanasheria wengine na si lazima wawe mawakili, hata wanasheria wa kawaida waweze kufanya kazi hiyo ya legal aid campaign. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza sana nimeona mwalimu wangu Sisti Mramba amekuwa ndiyo Mkuu wa Chuo hiki cha mafunzo kwa vitendo (Law school) cha sheria. Naomba, najua kuna utafiti ulifanyika kuhusiana na suala la Law School na tulitukanwa sana tukaitwa sisi vilaza. Niseme darasa langu mimi nililoingia mwaka wa kwanza sheria, mtu aliyefaulu kwa ufaulu wa chini alikuwa na division 1.9 na hakukuwa na kilaza pale, tukaambiwa sisi ni vilaza. Naomba utafiti ufanyike, kwa nini wanaingia 600 wanafaulu wanafunzi 14? Ufanyike utafiti na najua sina wasiwasi na mwalimu wangu huyu najua atakwenda kusimamia.

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kuna watu wanasoma pale Law School, mtu anatoka pale ana supplementary amefeli, lakini akiamua kuahirisha asiendelee na Law School aende masters, kule Masters masomo hayo anapata A, masomo hayo hayo kwenye masters anapata B+. Iweje leo uite huyu mtu ni kilaza? Umepewa cream of the nation uifundishe, wanafeli 90% ya wanafunzi halafu unasema wewe ni mwalimu. Huu ni uongo, ningeomba suala hili tusifanye utafiti wa kisiasa. Ufanyike utafiti wa kitaalam kwa sababu hakuna kilaza anayesoma sheria kwenye nchi hii. Kila anayesoma sheria kwenye nchi hii ni mtu ambaye alipata wastani wa juu wa ufaulu form four, form six na mpaka ameweza kuingia chuo kikuu alifaulu vizuri. Huko ni kulionea eneo la sheria.

Mheshimiwa Naibu Spika, niende moja kwa moja kwenye suala la bajeti ya Mahakama na labda hili tunaweza kuwa tunalichukulia kwa wepesi. Mahakama ndiyo chombo cha juu cha utoaji wa haki nchini. Katika watumishi wa Mahakama hawawezi kwenda kuomba kwa mtu, hawawezi kufadhiliwa na mtu, hawawezi kupewa asante na mtu. Leo Bunge hili limekaa limepitisha bajeti tunasema wapelekewe fedha kwa ajili ya maendeleo, kweli tunapeleka 24% tu ya bajeti?

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi haya majengo mazuri ambayo tunayajenga leo katika nchi hii ambayo ni kwa ajili ya Mahakama, bila watendaji wa Mahakama, bila vifaa vya utendaji wa Mahakama, haki itatolewaje? Hili jambo niseme na niombe kwa dhati tupeleke fedha, hawa watu tusiwaweke kwenye majaribu na ndiyo maana ni moja kati ya mhimili ambao umetengenezwa kikatiba; maana yake wanalindwa kikatiba. Sasa tusiwavunjie ile kinga yao ya kikatiba kuwaingiza kwenye vishawishi. Hawana makazi wana changamoto, hawapewi vipaumbele mbalimbali, hawapati hizi fursa ambazo tunazipata sisi kwenye mihimili mingine, lakini hata lile la kwao la msingi la kikatiba wanashindwa kupelekewa bajeti kweli ili wasimamie?

Mheshimiwa Naibu Spika, pale Shinyanga tuna jengo zuri sana pale kwetu la Mahakama, limejengwa la kisasa lakini ukiangalia upungufu wa mahakimu na majaji, hata ripoti yao wenyewe wanasema hapa. Wanasema upungufu wa watumishi, katika watumishi 6,247 wanaotakiwa kuna upungufu wa watumishi 1,562 na kwa bahati mbaya suala la mtumishi wa Mahakama halina kusema atafanya msaidizi. Hakimu ni hakimu, lazima akae hakimu aamue kesi. Ukisema leo kuna upungufu wa mahakimu maana yake pale haki haitatolewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika upungufu wanaousema kwenye mahakama za mwanzo, wanatakiwa wawepo watumishi 3,999, leo wana watumishi 960 sawa na 24% tu ya watumishi wanaotakiwa katika Mahakama hizi. Hivi unategemea kupata matokeo ya aina gani? Unategemea haki itatendeka vipi? Ndiyo maana leo mtu anaona kuliko niendelee kuzungushwa Mahakamani ni afadhali nisubiri mikutano ya wanasiasa niende nikashtaki pale, kwa sababu anaona huku Mahakamani kuna ukiritimba, anaona huku Mahakamani mambo hayaendi, ni afadhali niende kwenye mikutano ya wanasiasa. Matokeo yake yule mtu hatopata haki yake na unatengeneza mazingira ya rushwa katika kumhudumia mtu yule.

Mheshimiwa Naibu Spika, niende haraka haraka kwenye Tume ya Haki za Binadamu. Kiukweli hii Tume ipo kikatiba na Tume hii hata kwenye mikataba ya kimataifa ambayo tumekubaliana ni Tume ya muhimu. Inatakiwa itoe ripoti ambayo ripoti hiyo itakuwa ni ya wazi, kila mtu anaweza kuiona. Leo hii ukiuliza Wabunge humu ndani ambao wanajua hata ripoti ya mwaka jana tu ya Tume ya Haki za Binadamu ni wachache sana. Sisi tunataka kufahamu hiyo ripoti na ni moja kati ya ripoti ambayo kiukweli ikitolewa hadharani itam-brand vizuri sana Mheshimiwa Rais. Kwa sababu katika kipindi ambacho Haki za Binadamu zimesimamiwa na kutekelezwa vyema ni wakati huu ambao Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan yupo madarakani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini ripoti hii imebaki kukaa kwenye draw za Ofisi za Katiba na Sheria? Ni kwa nini? Nasisitiza na amesema vizuri sana Mheshimiwa Agnesta wakati anachangia. Wabunge tuletewe ripoti hii na ikibidi utengwe muda wa Bunge kwa ajili ya kujadili na kupitia ripoti hii. Kwa sababu wakati mwingine mambo mazuri yanafanyika hayajulikani kwa sababu hayasemwi na kwa sababu hayajulikani kwa watu wengine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nisisitize kwa nia ya dhati, tuletewe ripoti ya Tume ya Haki za Binadamu lakini tuimarishe Kitengo cha Tume ya Haki za Binadamu. Malalamiko hayawezi kuwa mengi kama Kitengo hiki kitafanya kazi na of course, as a matter of fact hata hiyo kazi inayofanywa na Mama Samia Legal Aid Campaign, hawa watu wa Tume ya Haki za Binadamu wanatakiwa kuwa sehemu ya hawa watu wanaokwenda huko chini kufanya kazi ya kutoa ushauri wa kisheria kwa sababu mwisho wa siku huko ndiko watakakoenda kukusanya taarifa za namna gani ambavyo haki za binadamu zinazingatiwa kwa mujibu wa Katiba yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri asiponijibu vizuri kuhusiana na suala la ndoa za utotoni, nitashika shilingi yake. Ahsante sana. (Makofi)