Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Dr. Alice Karungi Kaijage

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. DKT. ALICE K. KAIJAGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwani katika kipindi chake cha uongozi kumekuwa na mafanikio makubwa katika Wizara hii ya Katiba na Sheria.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze pia Mheshimiwa Dkt. Pindi Hazara Chana, Waziri wa Katiba na Sheria, Naibu Waziri Mheshimiwa Jumanne Sagini, bila kuwasahau viongozi wa Mahakama ya Tanzania na Viongozi Wakuu wa Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Katiba na Sheria na pia watendaji wote na watumishi wote wa Wizara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikiwa kama mmoja wa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria tumefanya ziara mbalimbali za kukagua miradi na tumeweza kuona mafanikio na changamoto mbalimbali za taasisi zilizo katika Wizara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze na Fungu 41 - Wizara ya Katiba na Sheria; katika vipaumbele walivyokuwa wamepanga kuvitekeleza kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 mojawapo ilikuwa ni kuimarisha huduma za kisheria kwa umma (Kipengele Na. 6) ambapo katika huduma za kisheria kwa wateja wameanzisha Kituo cha Huduma kwa Wateja ambapo mwananchi anaweza kupiga simu na kueleza malalamiko ya masuala ya rushwa na ukiukwaji wa haki. Ni hatua kubwa sana imeleta wepesi wa huduma hii kwa wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kwa sasa ofisi hii imeendelea na mchakato wa kuanzisha Kituo cha Usuluhishi Tanzania. Katika changamoto mbalimbali ambazo wanakutana nazo ni uhitaji mkubwa wa matumizi ya TEHAMA ikilinganishwa na miundombinu na mifumo iliyopo. Ushauri wangu ni kuwa Serikali iangalie maeneo ya pembezoni ya halmashauri zetu, hivyo Serikali ishirikiane na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania ili kwa pamoja waweze kulitatua tatizo hili, pia Serikali iwekeze katika kutoa vitendea kazi kwa mfano vishikwambi na kompyuta ikiwa ni sambamba na upatikanaji wa mtandao wa uhakika ili kuleta tija zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali - Fungu Na. 16; ofisi hii majukumu na vipaumbele vyake wamevitekeleza ila bado pia wana changamoto ya uwepo wa miundombinu duni ya TEHAMA ambayo inapelekea ugumu wa upatikanaji wa taarifa mbalimbali za kiutendaji wa ofisi hiyo na hivyo wananchi kukosa haki ya kufahamu masuala yanayoendelea katika sekta ya sheria.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kumekuwa na tatizo la kukosekana kwa mafunzo ya mara kwa mara ya watumishi wa ofisi hii kuhusu masuala mbalimbali ya kisheria, pia wana changamoto ya kukosekana kwa ofisi katika mikoa mbalimbali hivyo kupelekea kutokusogeza huduma hizo karibu na wananchi, hivyo naishauri Serikali kuhakikisha fedha zote zinazoidhinishwa na Bunge za ofisi hii hususani za fungu la maendeleo zipelekwe kwa wakati ili kupunguza changamoto hizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nichangie kuhusu Ofisi ya Taifa ya Mashtaka - Fungu Na. 35; ofisi hii ilianza kufanya kazi mwaka 2018 na mojawapo ya majukumu yake ni kukagua magereza na mahali popote wahalifu na mahabusu wanapohifadhiwa kwa mujibu wa sheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, baadhi ya wahalifu kwenye baadhi ya magereza wamekuwa wakipata magonjwa mbalimbali na katika kipindi hiki cha ugonjwa wamekuwa wakikosa chakula kinachofaa pamoja na matibabu hususan vipimo na dawa. Ushauri wangu ni kuwa baadhi ya magereza wanalima mbogamboga na matunda, tunashauri wagonjwa hawa japo wapatiwe mbogamboga hizo hasa wanapokuwa wagonjwa, tunashauri pia Serikali iwapatie dawa na vipimo bila kulipa gharama maana wengi wanakuwa hawana kipato wawapo magerezani au mahabusu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukitembelea baadhi ya magereza haya na ukawatembelea wagonjwa hawa unaweza kutokwa na machozi, jambo hili liangaliwe kwa umakini mkubwa. Tunawapongeza kwa kwenda kukagua, tunawaomba wanapoondoka kwenye ukaguzi waweke mifumo mingine ya ufuatiliaji wa haki za wahalifu hawa, hata wakiwa hawapo eneo la tukio.

Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza Serikali kuiwezesha Ofisi hii ya Taifa ya Mashtaka kuendelea kujenga ofisi zao katika mikoa 10 ya Tanzania ambapo miradi hii ya ujenzi ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali iiwezeshe ofisi hii katika suala la usalama wa watumishi, iwapatie vibali vya ajira kwa ajili ya kupunguza uchache wa watumishi na kuwaongezea vitendea kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nichangie pia kuhusu Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali - Fungu Na. 19; ofisi hii tumeona kupitia utendaji kazi uliotukuka na wa kizalendo wa watumishi mahiri wa ofisi hii nyeti kupitia kusimamia uendeshaji wa mashauri mbalimbali ya kitaifa na kimataifa, pia kupitia usuluhishi wa mashauri, madai mahakamani na usuluhishi nje ya mahakama. Ofisi hii imeweza kukomboa kiasi cha shilingi trilioni 3.48 za Kitanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye suala la usuluhishi wa kitaifa na kimataifa, ofisi hii imekomboa kiasi cha shilingi bilioni 223.69, kwa kazi hii iliyotukuka kwa ofisi hii, lakini bado ina changamoto mbalimbali kama vile jengo la Makao Makuu ya ofisi yao Jijini Dodoma limefikia 47% ya utekelezaji ambayo ni nyuma ya muda. Kwa sababu hiyo, tunaiomba Serikali kwa kazi iliyotukuka iliyofanywa na watumishi wa ofisi hii, tunaomba fedha za ujenzi wa ofisi hii zikamilishwe kulipwa chini ya mkandarasi SUMA JKT. Aidha, tunashauri kwa jicho la tofauti watumishi wa ofisi hii wapewe vitendea kazi hususani magari. Pia nashauri watumishi wa ofisi hii wapelekwe kusomea zaidi kwenye ubobezi katika maeneo ya gesi, mafuta, uwekezaji, anga, madini, uchumi wa bluu na TEHAMA.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuwatia moyo watumishi wa ofisi hii, tunaomba pia maombi haya ambayo wameomba kwa muda mrefu na ni ya msingi, Serikali iwatekelezee kwa jicho la udharura.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuchangia hayo, naomba kuunga mkono hoja.