Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Dr. Eliezer Mbuki Feleshi

Sex

Male

Party

Ex-Officio

Constituent

None

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kukushukuru kwa fursa ambayo umenipatia. Pia nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuongoza nchi hii kwa misingi ya utawala wa sheria na utawala bora na halikadhalika, Mhimili wa Bunge kuendelea kusimamia hayo. Mheshimiwa Spika, Naibu Spika, Wenyeviti wetu pamoja na Kamati zetu tunawapongeza sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumefika hapa kwa mchango mkubwa wa mhimili wa Mahakama, ambao kwa kazi kubwa inayofanywa na Bunge hili pamoja na Serikali, basi utekelezaji mwingine wa sheria zetu kutafsiriwa na migogoro inayotokea hupelekwa Mahakamani na kutolewa maamuzi ya kisheria. Kwa hiyo nampongeza sana Mheshimiwa Jaji Mkuu, Majaji wote pamoja na watendaji wanaokwenda Mahakamani wakiwemo DPP na mawakili kutoka katika ofisi yake, mawakili wa ofisi yangu, mawakili kutoka Ofisi ya Solicitor General na mawakili wote 3,479 waliopo kwenye sekta ya umma ninaowasimamia.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri wa Katiba na Sheria, Mheshimiwa Balozi Dkt. Pindi Hazara Chana na Mheshimiwa Naibu Waziri na niko hivi kwa sababu yao; kwa sababu ni viongozi wangu wanaonilinda, kuniongoza na kuhakikisha natimiza majukumu yangu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza sana Kamati ya Katiba na Sheria pamoja na Kamati ya Bajeti kwa hotuba zao ambazo waliziwasilisha asubuhi ya leo. Walitoa ushauri japo upo ushauri uliotolewa kuhusiana na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na ofisi zingine za kioperesheni, hasa kuhakikisha kwamba tunawajengea uwezo Mawakili wetu. Ushauri huu tumeupokea.

Mheshimiwa Naibu Spika, nieleze kwamba, kama Wabunge watakuwa wamepitia kitabu cha mapendekezo ya bajeti cha Mheshimiwa Waziri wataona kwamba kuna kiwango cha kiasi cha fedha bilioni tatu kimetengwa kwa ajili ya kuwajengea uwezo mawakili wetu kwa ajili ya kuongeza ufanisi katika kushughulikia mikataba na makubaliano mbalimbali na kazi nyingine za kisheria zinazotekelezwa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Vivyo hivyo kuna fungu la fedha limetengwa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kwa minajili hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia Kamati ilishauri kwamba uwekwe mfumo wa kutoa motisha kwa mawakili. Jambo hili ni jema na niahidi tu kwamba tutaendelea kulifanya. Yapo mengi yanayofanyika kwa wanaotenda kazi vizuri. Miongo mitatu ambayo nimekuwa kwenye utendaji kazi katika tasnia ya sheria naelewa watu wengi ambao wameajiriwa na Serikali katika tasnia yetu tumejitahidi kuhakikisha hawabaki hapo walipo. Wapo walioajiriwa kwa sasa ni majaji na wakurugenzi. Kwa hiyo, tutaendelea kuimarisha na kutoa motisha zaidi kwa wote wanaotenda kazi vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna hoja nyingi zimetolewa na Waheshimiwa Wabunge na tunawashukuru sana kwa sababu, yote yaliyowasilishwa yanalenga kutuwezesha kuboresha mifumo na kuhakikisha kwamba nchi yetu inaongozwa kwa utawala wa sheria na misingi ya utawala bora. Mheshimiwa Mashimba Ndaki pamoja na yote aligusia changamoto mbili, moja kwenye eneo la ukazaji wa hukumu (exclusion) na lingine ni kuhusiana na nyaraka hasa hati zinazowasilishwa Mahakamani na kusitisha shughuli nyingine za kiuchumi kwa wanaozipeleka Mahakamani kwa njia moja au nyingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa kumtoa hofu Mheshimiwa Mashimba Ndaki kwa sababu maboresho yanayoendelea sasa hivi yataendelea kuhakikisha kwamba hili eneo la ukazaji wa hukumu, kama ambavyo amegusia, ni eneo ambalo linaendelea kufanyiwa kazi. Eneo hili kwa kesi za madai linaangukia kwenye haki madai.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama wote tulivyofuatilia, Mheshimiwa Rais baada ya kusikiliza hotuba ya Mheshimiwa Jaji Mkuu na hotuba nyingine zilizosomwa wakati wa maadhimisho ya Siku ya Sheria Duniani yaliyofanyika Februari Mosi aliielekeza Wizara ya Katiba na Sheria na Serikali kwa ujumla kuhakikisha kwamba baada ya kuwa ameunda tume ya kuangalia namna ya kuboresha mifumo ya utoaji wa haki jinai na ile ya mambo ya kuchunguza namna ya kuboresha huduma za Wizara ya Mambo ya Nje alielekeza sasa eneo hili la haki madai nalo lifanyiwe kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, yapo mambo mengi ambayo najua tayari yanahusisha chunguzi na tafiti kupitia Law Reform Commission. Kwa hiyo, naamini kadri tunavyoendelea kufanya kazi kupitia Kamati za Kudumu za Bunge bila shaka tutaendelea kutoa taarifa ya mambo mbalimbali yatakavyokuwa yameendelea kufanyiwa kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimtoe wasiwasi kwa sababu kama amefuatilia jedwali la sita bila shaka ataona sheria iliyotajwa pale, ile ya mabadiliko ya sheria mbalimbali kupitia mabadiliko ya sheria za sekta za kisheria. Kuna maeneo mengi ambayo Serikali imekwishaanza kuyafanyia kazi. Kwa mfano, mojawapo kwa sasa kwa mtu anayepeleka shauri kwenye Mahakama ya Rufani hahitaji kuomba kibali (leave). Ilikuwa ni njia mojawapo, ni maeneo ambayo pia tujue kwamba mtu anapopata tuzo, tuzo hiyo ikakatiwa rufani basi hawezi akakaza hukumu mpaka uamuzi wa mwisho wa Mahakama ya Juu unapokuwa umetolewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna hatua pia za kupunguza ile milolongo ya upatikanaji wa nyaraka za kimahakama (record of appeal), ni mambo ambayo Mahakama imepiga hatua kuhakikisha kwamba yanapatikana kwa haraka zaidi. Kuhusiana na zile nyaraka ambazo nafikiri kwa dhana ile, kwamba zinakwama mahakamani kwa sababu tu zinahusiana na kesi na mtu akashindwa kuendelea na mambo yake mengine ya kiuchumi na kijamii, nimtoe tu wasiwasi kwamba sheria zetu, Sheria ya Mwenendo wa Madai, kupitia amri ya 7(14) zinaruhusu anayepeleka nyaraka hizo pamoja na hati yake ya madai baada ya kuwasilisha anaweza akaacha certified true copies. Lakini pia, kupitia Sheria yetu ya Ushahidi, Sura ya Sita, Kifungu cha 64 na 65 vinaeleza namna ya kutumia nyaraka mbadala na zile nakala halisi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Wakili Msomi Edward Olelekaita alipokuwa akichangia alielezea kero ambayo ilikuwa imewapata baadhi ya wapigakura wake ambao walikuwa na kesi ya mifugo yao kuhusishwa kwenye kesi na baadaye kukawa na maamuzi ya kwamba warejeshewe lakini hawajarejeshewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza, nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa kuwatendea haki wapigakura wake na kuwasemea wengine wengi ambao wanakutana na kadhia ya namna hiyo. Nipende tu kueleza kwamba baada ya kuwepo kwa malalamiko haya Wizara ya Katiba na Sheria chini ya Mheshimiwa Waziri na Katibu Mkuu waliwaketisha Wizara nyingine zinazohusika na jambo hilo ikiwemo Wizara ya Mifugo na wadau wengine kama vile Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka. Kwa sasa kinachoendelea ni kwamba kuna vikao ambavyo vinaendelea, vimefanyika tarehe 23 Aprili, 25 Aprili na kingine kitafanyika tarehe 2 Mei na hiki nafikiri ndicho kitakuwa cha kuhitimisha. Kwa hiyo Mheshimiwa Wakili Msomi endapo jambo hili litaendelea kutopata suluhisho, basi naamini Ofisi ya Waziri mwenye dhamana na Katiba na Sheria na ofisi nyingine tutaendelea kuhakikisha kwamba jambo hili linashughulikiwa na kupata ufumbuzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na hoja ambazo ziliwasilishwa na Mheshimiwa Mbunge Shally Raymond, dada yetu mkubwa. Mojawapo ilihusiana na kesi za mauaji kuchelewa au wanaohusishwa na kesi hizo baada ya kutiwa hatiani, basi hukaa muda mrefu bila hatima zao kujulikana. Nipende tu kumhakikishia Mheshimiwa Shally kwamba, baada ya Mheshimiwa Rais kupokea ile Taarifa ya Haki Jinai tarehe 15 Julai, 2023, jambo hili lilikuwa ni moja ambalo lilikuwa likifanyiwa uchunguzi, kuhusiana na hatma ya watu wenye vifungo vya maisha pamoja na hatma ya watu ambao wanahukumu za kunyongwa (hukumu za kifo) na hazijatekelezwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama walifuatilia bila shaka taarifa ile ilikuwa na mapendekezo ambayo sasa yanafanyiwa kazi; kuangalia namna ya kubadilisha Kanuni ya Adhabu. Kwa upande wa adhabu ya maisha basi kuwe na vigezo vingine, isiwe kwamba maisha maana yake ni Maisha, lakini kwa maana ya adhabu ya kifo vilevile kuna mapendekezo ambayo yalitolewa, kwamba Mahakama isifungwe mkono, Jaji anayesikiliza au Mahakama inayosikiliza iweze kutoa adhabu nyingine kutegemeana na mazingira.

Mheshimiwa Naibu Spika, hii ni kutokana na sababu kwamba taarifa ile na mapendekezo yake Mheshimiwa Rais aliyatolea maelekezo kwamba yafanyiwe kazi na Kamati ambayo inatengeneza mkakati wa utekelezaji wake. Kwa hiyo jambo hili litaendelea, yale mabadiliko ya sheria lazima yatakuja hapa Bungeni.

Mheshimiwa Naibu Spika, kadhia nyingine za kuhusiana na hayo nipende tu kueleza mimi kama Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na ofisi nyingine na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka tunayo dhamana ya kushughulikia lalamiko moja moja ambalo linakuwa na mazingira ya kipekee. Kinachohitajika ni kupewa lalamiko ambalo inakuwa ni rahisi kulifuatilia. Tumekuwa tukifanya hivyo mara nyingi pamoja na kufanya kaguzi Magerezani na kufanya vikao na vyombo chunguzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Joseph Kakunda, kaka yangu, nafikiri pamoja na mengine aliongelea ile Taarifa ya Tume ya Haki Jinai, kwamba ilipowasilishwa kwa Mheshimiwa Rais ilikuwa na mapendekezo mengi na kwamba hakuona kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri kama ameitaja.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nilipokuwa naangalia, nimejiridhisha kwamba Mheshimiwa Waziri amelitaja jambo hili kwenye paragraph ya 39 ambapo ameeleza baada ya kupokea taarifa ile Wizara iliketi na kuweka mpango wa utekelezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naelewa mpango wa utekelezaji huu tayari Wizara na kama zilivyo Wizara zingine zilizoguswa kwa sasa zimekwishakwenda mbele ya ile Kamati inayotengeneza mikakati. Kwa hiyo, mikakati ile maana yake itakuja kuzaa Sheria, itakuja kuzaa miongozo na Sera mbalimbali. Ukiangalia kwenye hiyo paragraph ya 39 kwa sasa Wizara inaendelea kufuatilia utekelezaji kadri unavyofanyika na ile Kamati.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nafikiri inatosha kukushawishi kwamba kilicho kwenye Taarifa hii ni sahihi na nisingetegemea Mheshimiwa Waziri atoe zaidi ya alichokitoa kwa sababu yeye amekwishapakua na kupeleka kwenye chombo kingine ambacho kimekwishapewa mamlaka ya kufanya hivyo na Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile lilijitokeza suala la mabaraza nafikiri huyu alikuwa ni, lilijitokeza suala la kule ngazi ya kata, kwamba taarifa ile imeongelea maeneo ya kuboreshwa kwenye maeneo mbalimbali lakini haikueleza nini kifanyike katika ngazi ya kata. Sasa kwa taarifa hiyo hiyo pendekezo moja kubwa ni kuundwa kwa chombo kimoja chenye dhamana ya kufanya upelelezi ambacho kitakuwa na hadhi ya Taifa na ule mkakati sasa upo kwenye hatua ya kuandaliwa maana yake utakwenda mpaka ngazi ya kijiji yaani kule walipo wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama unafuatilia nini kinafanyika na kinafanywa na polisi kwa sasa huwa wamekwishapeleka hao mapolisi kata. Kwa hiyo nafikiri ule mpango utakapokuwa umekamilika kwa sababu utazihusisha taasisi zote zinazofanya uchunguzi wa jinai wa kisheria, naamini hapatakuwa na ombwe lingine ambalo litajitokeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Dkt. Stephen Chaya aliongelea kuhusu Sheria ya TAKUKURU kufanyiwa marekebisho, ni kweli hii Sheria ni zao la Mkataba wa Kimataifa (United Nations Convention Against Corruption) na baada ya Serikali yetu kuwa sehemu ya mkataba ule ndiyo tulitunga Ile Sheria ya Rushwa, Na. 11 ya mwaka 2011.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kama iliyo kawaida, sheria yoyote inayohusu maisha ya mtu, maisha ya nchi, shughuli za kijamii, shughuli za kiuchumi, mara kipindi kinavyoenda lazima ifanyiwe marejeo. Kwa hiyo, naelewa TAKUKURU wenyewe, lakini hata kwenye ile Tume ya Haki Jinai walielekeza kwamba hizi sheria zote pamoja na ile Sheria ya Uhujumu Uchumi zifanyiwe mapitio ili tuwe na vifungu vinavyoakisi uhalisia wa sasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naamini kwamba kama tumeendelea kuangalia lile jedwali la sita, tutaona jinsi ambavyo Serikali kwa kile inachokikamilisha kinaletwa hapa Bungeni na kitu kikubwa kabisa ambacho naipongeza Kamati ya Utawala, Katiba na Sheria ni jinsi ambavyo imekuwa ikifanya kazi kuhakikisha kwamba Miswada ya Sheria inayopelekwa kule basi haigandi, inawasilishwa kwenye Bunge hili. Ni faraja yangu kwa kipindi ambacho nimekuwemo humu, tayari kuna sheria nyingi na mfumo huo huo zimefanyiwa marekebisho makubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nirudie kukushukuru wewe, lakini na kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote kwa michango yao ambayo wameitoa na kumshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa kunipatia fursa hii. Nashukuru sana. (Makofi)