Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Amb. Dr. Pindi Hazara Chana

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa naomba nichukue nafasi hii kuendelea kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kusimama tena mbele yenu kwa mara nyingine. Nichukue nafasi hii kuendelea kukushukuru wewe binafsi, lakini pia nichukue nafasi hii kuendelea kumshukuru Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu kwa umakini wake wa kusimamia shughuli za Serikali ndani ya Bunge.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru pia Mheshimiwa Naibu Waziri, Jumanne Sagini kwa kunipa ushirikiano katika kutekeleza majukumu yangu na nimshukuru Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Pia niwashukuru sana kwa ufafanuzi mzuri ambao wametoa mbele ya Bunge letu Tukufu. Napenda kuendelea kuishukuru sana Kamati yetu ya Katiba na Sheria, Kamati ambayo imetoa maoni muhimu, ushauri na mapendekezo na Waheshimiwa Wabunge wote tumepata wachangiaji takribani 13 michango yao ni muhimu na ni mizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia michango ya Waheshimiwa Wabunge, kwa kweli nimepokea changamoto nyingi, critics, hali inayoonyeha dalili za dhati kabisa za mwamko mkubwa katika suala zima la masuala ya Katiba na Sheria na haki kwa ujumla. Aidha, katika michango hiyo imedhihirika wazi umuhimu wa kuimarisha Wizara kupitia Sera, Sheria, Kanuni, taratibu na Miongozo mbalimbali ambayo kimsingi inaongoza Wizara yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli ni dhahiri kuwa masuala ya huduma za msaada wa kisheria, masuala ya Mahakama, ujenzi na miundombinu ya Mahakama, ni miongoni mwa vipaumbele vya Wizara yetu na maeneo mengi sana yamechangiwa katika maeneo hayo. Hivyo kwa ruhusa yako naomba nianze kufafanua kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, lipo suala hapa tumeambiwa umuhimu wa makusanyo ya maduhuli kimsingi yanayoakisi uwezo wa ukusanyaji na hali halisi ya vyanzo vya mapato. Sisi tunaungana kabisa na maoni haya muhimu kwamba maduhuli lazima yaakisi uwezo wa ukusanyaji lakini ukweli ni kwamba katika Mhimili wa Mahakama na Mhimili wa Katiba na Sheria, Wizara yetu na Mhimili wa Mahakama vyanzo vingi vinategemeana na zile sheria ambazo tumezitunga hapa sisi.

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati tunatunga sheria tunasema atakayefanya makosa katika sheria hii atahukumiwa labda kifungo cha miezi sita ama faini. Tunaposema zile faini ndiyo maduhuli ya eneo letu sisi la Katiba na Sheria kwa sababu Wizara ya Katiba na Sheria jukumu lake hasa ni kutoa huduma, ukichukua upande wa Law Reform Commission ni kutoa huduma siyo chanzo cha mapato, ukichukua Tume ya Utumishi wa Mahakama jukumu lake ni kutoa huduma.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunapokuwa tumeweka maduhuli ni kweli tunakuwa tumeweka, lakini kuna wakati tunafikia viwango na kuna wakati hatufikii kwa sababu tunakuwa labda kwa namna moja au nyingine hatujatoza zile faini kwa sababu watu wanatii sheria pasipo shuruti. Wanapotii Sheria pasipo shuruti maana yake ndiyo utawala bora wenyewe, maana yake nchi ina amani na utulivu, mambo yanaenda vizuri, lakini kwa wale wanaokosea ndipo tunaposema kuna faini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, wakati mwingine siyo rahisi sana kukidhi na kufikia maduhuli tuliyojiwekea, inategemeana kama sheria zimekiukwa ama hazijakiukwa, lakini hoja bado ni ya msingi kwamba tuone namna gani tunaweza tukafikia suala zima la maduhuli ambayo kimsingi tunakuwa tumejiwekea. Kuna suala zima la Mama Samia Legal Aid, hili ni jambo la msingi, tunamshukuru sana sana Mheshimiwa Rais kwa kweli kwa kutupa maelekezo thabiti kabisa kwamba mwende kwa Watanzania muwasikilize kero zao, hoja zao na muone namna gani ya kuendelea kuzitatua.

Mheshimiwa Naibu Spika, niungane kabisa na Waheshimiwa Wabunge wengi ambao kwanza na Kamati imesema, tufike katika mikoa ambayo bado. Kimsingi tunachokifanya sasa hivi tunapoenda katika mikoa tunazindua suala zima la Mama Samia Legal Aid na baada ya uzinduzi kunakuwa na mashirika ambayo yamesajiliwa kutoa huduma za msaada wa kisheria yakiwa katika mkoa husika au katika wilaya husika. Yale mashirika tunashirikiana nayo, lakini siyo tu mashirika pia kuna wasaidizi wa Sheria na hadi hivi sasa tuna wasaidizi wa sheria takribani 1,888 wamesajiliwa kutoa huduma za msaada wa kisheria na wanapopata taarifa wanawasaidia wananchi katika ngazi husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, upande wa mashirika tunayo mashirika tuliyosajili takribani 270 na nimeshaelekeza, lazima tuwe na directory, unapoenda Kigoma mtu ana shida, ukatili umefanyika au jambo lolote mirathi au ardhi, anapohitaji huduma za kisheria ni wapi anaweza akapata na kuna wale ambao wanatoa huduma bure. Nichukue nafasi hii mbele ya Bunge lako Tukufu kuzishukuru taasisi zote zinazotoa huduma za kisheria bure, miongoni mwao kuna Chama cha Wanasheria Wanawake wanatoa huduma bure.

Mheshimiwa Naibu Spika, Tanganyika Women Lawyers, Tanganyika Law Society, Vyuo Vikuu, Kitivo cha Sheria ikiwemo Chuo Kikuu ch Dar es Salaam, Chuo Kikuu cha Dodoma, Law School of Tanzania na maeneo mengine mengi wanatoa huduma pro bono, bila malipo yoyote, tunawashukuru sana kwa ushirikiano mkubwa ambao wameendelea kuwasaidia Watanzania. Watanzania wana changamoto nyingi na ukitembelea huku nimeshuhudia baadhi ya watu wanapata changamoto kwa kuwa alikosa ushauri au kwa kuwa hakujua nini cha kufanya wakati ule.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimewahi kushuhudia katika magereza unakutana na mama anakwambia, nimeingia kwa ajili ya murder, murder kutokana na nini anasema mume wangu hakuleta matumizi nyumbani na nilikuwa na Watoto, nikakaa nikaona bora niondoke, nikakoroga sumu kumbe ungempa huduma ya kisheria kwamba kuna ustawi unaweza kwenda kudai haki za kulea Watoto, ingeweza kuponya watu wengi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Mama Samia Legal Aid niwaambie Watanzania wote ni huduma ambazo ni haki za Watanzania. Katika mikoa yetu, katika wilaya zetu, vijiji, mitaa unapokuwa na changamoto za kisheria hapana kubaki nyumbani na manung’uniko na masikitiko, tutoke tuulizane, tutoke katika taasisi zetu, katika ofisi zetu za Serikali, tuombe msaada wa kisheria, tunazo ofisi zetu hata Ofisi za ma-DC wanasikiliza, Ofisi za Serikali za Mitaa, lakini Wanasheria.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tunao kila halmashauri na taasisi zinazotoa huduma ambazo zimesajiliwa mashirika 270 wasaidizi wapo. Kwa hiyo tutatoa hiyo directory na tutazindua rasmi na tutaitangaza na ku-share vizuri kabisa na mikoa yote na wilaya. Mtu anapokuwa na changamoto ni muhimu kujua aende wapi.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mwaka huu wa Fedha 2024/2025, tumeona pia tutenge fedha, kwa hiyo tunachofanya ni kuzindua, baada ya kuzindua huduma ile tuhakikishe kila siku lazima inaendelea, siyo kwamba baada ya kuzindua tunaahirisha. Wito umetolewa hapa na Mheshimiwa Makamba kwamba, tuone namna gani ya kuwashirikisha wanasheria na mashirika mbalimbali, jambo hili tumelichukua alisema tutashirikiana vizuri kabisa na hivi karibuni kuna mkoa ambao tumepanga kwenda kuzindua. Basi wale ambao wako tayari ku-volunteer, iwe ni Wabunge au sio Wabunge, tutahakikisha tunashirikiana nao kwa ajili ya kutoa huduma, kupata uzoefu na kadhalika. Kwa hiyo, huduma hii ya Mama Samia Legal Aid imeendelea kusaidia sana. Wengine wamechukua mkopo, baba amechukua bila kumshirikisha mama, yamkini baba ametangulia mbele ya haki, mama anaambiwa nyumba inanadiwa. Ilikuwaje, anasema baba alikwenda kuweka nyumba dhamana.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumekuwa tukiokoa hati za watu, tunalipia. Hivi karibuni tulipata kisa mkasa, mama mmoja alikwenda mpaka Ikulu, nyumba yangu inataka kuuzwa na benki, akaambiwa iliwekwa dhamana, mama akasema sikuwa na habari, naenda wapi na watoto? Kupitia Ofisi ya Rais mwenyewe ametoa maelekezo kwamba, wasikilizeni Watanzania muwasaidie. Kwa hiyo, Mama Samia Legal Aid imekuwa ni mkombozi sana kwa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tusisubiri viongozi wakubwa waje ndio tupange foleni kwenda kusema changamoto tulizonazo, tuzitatue kabla. Wapo viongozi wetu, ofisi zetu zipo na sisi Wanasheria tupo katika Mikoa na katika Wilaya, kwa hiyo, natoa wito kwa Watanzania wenye changamoto, karibuni tuzungumze tuyajenge tupate utatuzi na ufumbuzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, kama nilivyosema awali, pia Wizara imeanzisha Kituo cha Huduma kwa Mteja (Contact Centre) ambacho namba ya Mahakama ipo, lakini pia Mama Samia Legal Aid kwa kushirikiana na Wizara yetu kitengo cha TEHAMA tumeweka namba maalum ambayo niliitaja wakati nawasilisha taarifa yangu asubuhi, naomba nirudie kuitaja tena namba hiyo, ambayo ni 0262160360. Hii namba tutahakikisha Watanzania wanaijua ili wanapokuwa na changamoto waweze kupiga simu.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunataka ifanyike kama Voda, Voda wanakwambia ukituma hela kwenda mtandao tofauti, tiGO/Airtel, kuna namba unapiga unapokelewa na unaelekezwa ni namna gani ya kuweza kurekebisha changamoto yako. Kwa hiyo, hata huduma hizi tunataka zijulikane kwa Watanzania ili waweze kuzitumia kuuliza mambo yao, kuuliza mambo ya jirani yako, ya ndugu yako, ya jamaa yako, ya rafiki yako, kwamba, jambo hili tunaweza tukalitatuaje kwa pamoja?

Mheshimiwa Naibu Spika, Mwanasheria Mkuu na Naibu Waziri wamefafanua maeneo mengi, nawashukuru sana kwa ufafanuzi huo mkubwa, lakini kama nilivyosema awali yako mambo mengine tutaleta kwa maandishi. Tunachukua hoja zote ambazo zimetolewa na maoni ya msingi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala la Serikali kwamba, iendelee kuimarisha mifumo ya utoaji haki ili haki ipatikane kwa wakati kwa watu wote.

Mheshimiwa Naibu Spika, nasema tu kwamba, suala la utoaji haki kwa wote na kwa wakati ni miongoni mwa vipaumbele vyetu. Ndio maana Mheshimiwa Rais ameunda Tume ya Haki Jinai ili ije na maoni ni namna gani haki inaweza kupatikana kwa watu wote na kwa wakati. Kwa hiyo, hii ni miongoni mwa vipaumbele vyetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi karibuni Mheshimiwa Rais ameteua majaji wasiopungua takribani 21. Jana tu, Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesaidia kutupatia watendaji mahiri kabisa, Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka na Mwenyekiti wa Law Reform Commission, Jaji Korosso, wameapishwa jana. Hii yote ni kuhakikisha kwamba, tunapewa nguvu kazi ya kutosha tukachape kazi, tukawafanyie kazi Watanzania ambao wako takriban milioni 61. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika spirit hiyo hiyo ya utoaji haki, ili haki ipatikane kwa watu wote na kwa wakati, Mhimili wa Mahakama umeendelea kupunguza mlundikano wa kesi. Hivi sasa mlundikano unaendelea kupungua, tunayo takribani asilimia tatu tu ya kesi zilizopo ambazo zinaendelea kutatuliwa. Kwa hiyo, naupongeza sana Mhimili wa Mahakama, chini ya Jaji Mkuu Profesa Juma na Mtendaji Mkuu wa Mahakama, ambao wanafanya kazi vizuri sana na wameleta maboresho ya hali ya juu, ikiwa ni pamoja na miundombinu, Mahakama za Mwanzo na za Wilaya zinajengwa katika maeneo mbalimbali. Hapa Waheshimiwa Wabunge wengi wameuliza hili swali na Naibu Waziri amefafanua vizuri sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunao mkakati kabambe kabisa wa kuhakikisha miundombinu hii ya Mahakama inakuwepo katika maeneo yetu kwa sababu, ni chombo muhimu sana cha kutoa haki kwa wananchi. Kadri tunavyozidi kwenda imani kwa Mhimili wa Mahakama inaendelea kuongezeka. Hivi sasa watu wanajua kabisa kwamba, jambo lako linapokuwa halijakaa sawa unapoenda Mahakamani kwa kweli, unapata haki yako. Kwa hiyo, kupitia utafiti wa REPOA unaonesha imani kwa Mhimili wa Mahakama kila siku inazidi kuongezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaishukuru sana Tume ya Haki Jinai ambayo imekuja na maelekezo na maboresho. Sisi kama Wizara, tumeshawasilisha mpango wa utekelezaji na maboresho ya sheria mbalimbali. Kwa hiyo, sheria nyingi tunakwenda kuzirekebisha na nyingine hata sasa tumeshaanza kuzirekebisha. Kwenye kitabu, kama alivyosema Mwanasheria Mkuu, kwenye kiambatanisho namba tano na kiambatanisho namba sita tunaonesha ni miswada mingapi imekuja, sheria ndogo ngapi zimerekebishwa ambapo nyingi ni mapendekezo na maelekezo ya Tume ya Haki Jinai.

Mheshimiwa Naibu Spika, naendelea tu kusema kwamba, pia tumeshauriwa kuanzisha Kituo cha Kimataifa cha Usuluhishi. Tulipokuwa katika Mkutano wa Mawaziri wa Katiba na Sheria wanaotoka Jumuiya ya Madola pale Zanzibar (Commonwealth Ministers of Justice) tumekubaliana kwamba, tunapoweza kutatua migogoro kwa njia mbadala, basi tutumie njia hiyo. Kuna wakati tunakwenda Mahakamani, ni sawa, lakini kama kuna njia mbadala, tunaita alternative dispute resolution, basi njia hiyo ni sahihi, inapunguza muda, inapunguza gharama na pia haki inapatikana. Kwa hiyo, miongoni mwa mikakati iliyopo hivi sasa ni pamoja na kuhakikisha kwamba, tunaanzisha Kituo cha Kimataifa cha Usuluhishi ambacho kinatarajiwa kushughulikia masuala mbalimbali katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kituo hiki kitakuwa na wataalamu wenye ujuzi na ubobezi katika tasnia ya utatuzi wa migogoro. Hivi sasa nchi yetu ina wawekezaji wengi katika sekta mbalimbali, viwanda, maliasili, madini na kadhalika na hawa wote wakati mwingine kunakuwa na migogoro ya aina moja au nyingine. Hivyo, kama kuna mgogoro basi ni wakati sahihi kutumia njia mbadala ya usuluhishi na wakati mwingine inaandikwa kabisa kwenye mkataba kwamba, inapotokea sintofahamu au aina fulani ya mgogoro basi pia, iruhusiwe kutumia alternative dispute resolution.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Mahakama wao katika kesi za madai wana utaratibu wa kuanza na mediation kabla ya kwenda kwenye masuala ya litigation. Hivi sasa kupitia Law School wanatoa mafunzo kuhusiana na namna ya kutatua matatizo na migogoro kwa njia ya usuluhishi, lakini pia, tunazo taasisi mbalimbali nchini ambazo kimsingi zinafanya kazi hii ya kutatua changamoto kwa njia ya alternative dispute resolution.

Mheshimiwa Naibu Spika, nalihakikishia Bunge lako kwamba, tuko imara kuhakikisha, kama ushauri wa Kamati ulivyosema, Serikali iimarishe mifumo ya utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala ikiwa ni pamoja na kuandaa wataalam wenye ujuzi wa sifa zinazotakiwa kimataifa katika utatuzi wa migogoro kwa njia ya majadiliano. Katika taarifa yetu tumesema baadhi ya kesi tulizoshinda kupitia Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali ni zile ambazo tumetumia njia mbadala ya usuluhishi ambako na kwenyewe tumeokoa pesa nyingi sana katika kutatua migogoro hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ni kwamba, napenda kuzungumzia suala zima la sera. Hivi sasa Wizara imeanza maandalizi ya Sera ya Taifa ya Haki Jinai. Sera hiyo itajumuisha masuala mbalimbali katika mnyororo wa haki jinai ikiwemo utolewaji wa taarifa za matukio ya uhalifu, masuala ya ushahidi, uchunguzi, uhalifu, ufunguaji wa hati za mashtaka, uendeshaji wa mashtaka pamoja na utoaji hukumu. Tumesema tuwe na sera mahususi ya masuala ya haki jinai.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia sera hiyo itaangalia usimamizi wa wafungwa magerezani na urejeshwaji wa wafungwa uraiani baada ya kumaliza kifungo au kupata msamaha wa adhabu ya kifungo. Kwa hiyo, haya pia ni maeneo ambayo tunakwenda kuyafanyia kazi. Ni lazima tuwe na sera na tujitahidi kuona namna gani wanaporejeshwa uraiani hawa wahalifu wasirudie tena, maana tusipoweka utaratibu unakuta mwingine anafanya kosa anarudi tena, anafanya kosa. Kuna mtuhumiwa mmoja alipoenda magereza wenzake wanamwambia karibu nyumbani, maana yeye kufanya makosa na kurudi magereza ni vitu vya kawaida. Kwa hiyo, lazima tuwe na sera kuona namna gani masuala haya ya haki jinai yanaweza kuratibiwa na kudhibitiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaendelea pia na suala zima la usajili wa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano kupitia RITA. Jambo hili pia, katika Bunge letu kupitia michango tumewekewa msisitizo wa kutosha. Kwa hiyo, naendelea tu kusema kuwa, ushauri umepokelewa na hivi sasa tunaendelea kuimarisha mifumo ya usajili wa matukio muhimu ya binadamu ikiwemo usajili wa vizazi, hususan usajili wa vizazi kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais ametuelekeza, twende kwa Watanzania tukawasajili watoto walio chini ya umri wa miaka mitano bure, tusiwatoze, hiyo ni gharama ya Serikali, wana haki ya kupata cheti cha kuzaliwa. Anapoenda darasa la kwanza anaulizwa cheti cha kuzaliwa, anapoenda Chuo Kikuu-Loans Board wanahitaji cheti cha kuzaliwa, anapohitaji passport cheti cha kuzaliwa. Kwa hiyo, tunao mfumo maalum kabisa wa kuhakikisha kwamba, tunatoa vyeti vya kuzaliwa kwa Watanzania wote. Natumia nafasi hii kutoa rai kwamba, wazazi wahakikishe watoto wanapozaliwa, iwe ni ndugu au jamaa, wasisahau cheti cha kuzaliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vyeti hivi vipo vya aina mbili, kuna kile cha pink ambacho mara nyingi tunakipata clinic au katika hospitali pale mtoto alipozaliwa na kuna kile ambacho huwa tuna-print certificate kwenye printer. Vyeti hivi vyote vina nguvu sawa, kiwe ni kile cha pink au kile kingine kwa hiyo, nawahakikishia Watanzania kwamba, Serikali iko imara kuhakikisha watoto wanapata vyeti. Tunapopata hizi takwimu ndio zinatuwezesha kujenga madarasa kwa sababu, tunajua ufikapo mwaka fulani watoto wenye umri wa miaka sita wa kwenda darasa la kwanza watakuwa ni watoto kadhaa. Tunaweza kuweka mipango yetu vizuri kabisa.

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu sasa hivi uandikishaji umetoka 13% na sasa hivi tuko 68% ya Watanzania wana vyeti vya kuzaliwa. Tunataka tufike 100%, kila mtoto anayezaliwa awe ana cheti cha kuzaliwa. Wapo wengine wanasahau kuchukua vyeti au wana haraka, lakini sasa hivi sio wengi wanaojifungulia nyumbani, wengi ni kwenye hospitali au dispensary, hivyo niwaombe wachukue vyeti vya watoto. Hiyo, inasaidia sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, naendelea tu kusema tumepata ushauri kwa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka iendelee kuhakikisha kuwa uendeshaji wa mashtaka na usimamizi wa masuala yote ya kesi unafanyika kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu kwa lengo la kuhakikisha kuwa, haki inatendeka kwa wakati. Haya yote ni miongoni mwa vipaumbele vyetu na tutahakikisha yanatekelezeka.

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri mwingine ambao tumeupata ni kwamba, tuangalie ni namna gani tunaweza tuka-prevent zaidi makosa kuliko ku-cure, amesema Mheshimiwa Kakunda. Niseme tu kwamba, tuko imara katika vyombo vyetu vya ulinzi na ndiyo maana Tume ya Kudhibiti Rushwa (PCCB) wao wanajiita Prevention and Combating of Corruption kwa hiyo, hiyo ndio spirit. Ni kweli tusiangalie tu kukinga, lakini tunapoweza kudhibiti kabla ya tukio la uhalifu kutokea na yenyewe ni miongoni mwa vipaumbele vyetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo napenda kusisitiza ni suala zima la Tume ya Utumishi wa Mahakama. Tunayo Tume ya Utumishi wa Mahakama ambayo inaendelea kuratibu masuala ya nidhamu na maadili kwa Watumishi wa Mahakama, ikiwa ni pamoja na kushughulikia kwa haraka mashauri ya kinidhamu dhidi ya watumishi wa Mahakama. Pale inapotokea watumishi wa Mahakama wanatenda shughuli zao pasipo utaratibu, upo utaratibu wa kupokea malalamiko hayo na katika kila wilaya na mkoa kuna Kamati za Maadili. Kwenye Wilaya Mwenyekiti wake ni DC na kwenye Mkoa Mwenyekiti wake ni RC. Kwa hiyo, pale ambapo kuna changamoto ya Watendaji wa Mahakama ni ruksa kutoa taarifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Tume imeimarisha utendaji kazi kwa Kamati za Maadili za Mikoa na Wilaya na kuendelea kutoa miongozo mbalimbali ya uendeshaji wa Kamati hizo. Tumeshatoa mafunzo kwa majukumu ya Kamati hizo za Maadili kwa washiriki takribani 90 na wakati mwingine tunapata maswali hapa Bungeni kwamba, kuna baadhi ya maeneo watumishi wa Mahakama wanafanya ndivyo sivyo. Waheshimiwa Wabunge na Watanzania, nawahakikishia kwamba, tunazo Kamati na vyombo imara kabisa ikiwemo PCCB na Tume ya Utumishi wa Mahakama, hivi ni vyombo ambavyo viko imara kuhakikisha kwamba, utendaji kazi unakwenda vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo pia napenda kulizungumzia ni suala zima la Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora. Maoni yametolewa hapa na Waheshimiwa Wabunge kuhusu Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, tunashukuru na tuseme tu kwamba, tutayazingatia. Maoni mengi ni juu ya kwamba ni namna gani tunaendelea kuiwezesha tume hii? Ni namna gani tunaendelea kuipatia rasilimali watu tume hii?

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba, hii ni tume muhimu sana na ni Tume ya Kikatiba. Kwa hiyo, ushauri umepokelewa na tutahakikisha kwamba, maoni na ushauri wote ambao viongozi Waheshimiwa wameutoa tunaendelea kuuzingatia.

Mheshimiwa Naibu Spika, Tume inaendelea kuwasilisha andiko la mradi la kiasi cha shilingi bilioni 15. Andiko hili limepelekwa Tume ya Mipango ili kuweza kupewa fedha za maendeleo ya ndani. Kwa hiyo, ni lazima tuwe na vyanzo vya ndani na sio vya nje tu. Pia, Tume imepata eneo la ujenzi wa Ofisi ya Makao Makuu, eneo la Chinyoya, Dodoma na kwa sasa inakamilisha hatua za manunuzi kwa ajili ya kuanza ujenzi kama tulivyokubaliana kwamba, Makao Makuu ni Dodoma. Hivyo, Ofisi zote zinapaswa kuwa Makao Makuu Dodoma.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Tume tayari ina kiwanja. Natumia nafasi hii kusema kwamba, mara tutakapopata nafasi ni muhimu Kamati yetu ikapata fursa kwenda kutembelea eneo hili. Pia, Serikali imekuwa ikiongeza idadi ya watumishi mwaka hadi mwaka. Katika Tume hii na kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 ilipatiwa watumishi takribani 23 na kwa mwaka huu tunaokwenda 2024/2025, tume imeidhinishiwa kuajiri watumishi takribani 99. Haya yote ni kutokana na michango mizuri ya Wabunge, tunawashukuru sana kwa maoni waliyotoa, kuisemea Tume hii na kwa kweli, Tume ni miongoni mwa vipaumbele vyetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Bajeti ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora; kwa mwaka 2020 tulipata shilingi bilioni 6.7; mwaka 2021/2022 Tume ilipata shilingi bilioni 6.7; mwaka 2022/2023, Tume ilipata shilingi bilioni 6.7; lakini mwaka huu kutokana na kazi nzuri ya Waheshimiwa Wabunge na Wajumbe wa Kamati ya Katiba na Sheria, Tume imeweza kupata shilingi bilioni 8.1 katika bajeti hii ambayo leo Bunge litakwenda kutuidhinishia, tunawashukuru sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo ningependa kuzungumzia ni eneo la Law School. Tulibadilisha sheria tukasema tuwe na Law School; hiki ni chombo muhimu sana na Law School imekwishafanya mapitio ya mitaala ambayo imejikita katika kutoa mafunzo kwa vitendo na mtaala huo mpya utaanza kutumika kuanzia Julai, 2024. Niishukuru sana kwa maoni ya Waheshimiwa Wabunge, tuone namna ya kuboresha Law School. Pia, Tume ya Mwakyembe ilifanya kazi kubwa na nzuri sana. Kwa hiyo, tunawashukuru sana kwa maoni mazuri na maboresho yanaendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee tu kusema kwamba, kwa mujibu wa Tume iliyofanya tafiti, maoni ambayo yanaendelea kufanyiwa kazi ni kwamba Law School of Tanzania iko kisheria na kwamba mtu yeyote mwenye LLB anaweza kujiunga na Law School. Pia, Law School of Tanzania imekuwa ikiwatumia wataalamu wabobezi katika kutoa mafunzo. Kwa sasa Law School of Tanzania ina kanzidata yenye wabobezi zaidi ya 80 kutoka kwenye maeneo mbalimbali ya kisheria. Baadhi ya wakufunzi ni Majaji ambao wanakwenda kufundisha, Mawakili wa Serikali na Mawakili wa kujitegemea.

Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee tu kusema kwamba mapendekezo mengi ambayo yametolewa na Waheshimiwa Wabunge ikiwa ni pamoja na Kamati, yanaendelea kuzingatiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Sheria ya Ndoa; Sheria hii ni muhimu sana. Hapa Waheshimiwa wamesema tuone namna gani sheria hii inaletwa hapa na kusema kwamba umri wa kuoa au kuolewa uwe miaka 18. Sheria hii ilishawahi kuletwa Bungeni kupitia tangazo namba moja volume 102, tarehe 5 Februari, 2021. Sheria hii ilipofika hapa tukaelekezwa twende tukakusanye maoni. Tumekusanya maoni na tunaendelea kukusanya maoni.

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa kuna different schools of thoughts, wapo wanaoafiki watoto wasiolewe kabla ya miaka 18 (mwiko kuolewa huko chini). Kuna watu wana dini zao, kuna watu wana mila zao, kuna watu wana desturi zao na kuna watu wa haki za binadamu. Wapo wanaosema tuliangalie, baadhi ya mila, desturi, dini kwa kuwa anaweza kwenda shule na sasa hivi tumewarudisha shuleni, hata akiolewa arudi shule…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Waziri, omba pesa. (Kicheko)

WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie kwa kusema tu kwamba, mchakato unaendelea na hivi sasa tuko katika hatua ya kuandaa Muswada.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba sasa Bunge lako liridhie taarifa hii na naomba kutoa hoja.