Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Dennis Lazaro Londo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mikumi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami pia niungane na wenzangu ambao wamenitangulia kuipongeza Serikali yetu kwa kuonesha seriousness kwenye suala zima la kilimo ambapo tumezoea kusema kwamba ni uti wa mgongo. Tunasema kilimo ni uti wa mgongo kwa sababu ndiyo eneo ambalo linatuhakikishia ajira za watu wengi wa Tanzania. Katika hili, ongezeko la bajeti kwenye Wizara hii ni jambo ambalo linatuonesha na linatufariji sana sisi wawakilishi wa wananchi kuona kwamba kuna mkazo ambao unawekwa kwenye eneo la kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kumpongeza Rais wetu, Mama yetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ambayo anaifanya kuhakikisha kwamba Taifa liko salama kwa sababu ya usalama wa chakula. Nawapongeza wasaidizi wake wakiongozwa na Mheshimiwa Waziri Bashe; Naibu Waziri Mheshimiwa Silinde; Katibu Mkuu, ndugu yetu Gerald Mweli na watendaji wengine wa taasisi mbalimbali ambazo ziko chini ya Wizara ya Kilimo, ambao wamepewa jukumu la kuhakikisha kwamba Taifa letu liko salama katika sekta nzima ya chakula, lakini ajira kwa maana ya kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikirejea mpango wa bajeti ambao uliwasilishwa mbele ya Bunge lako miezi mitatu iliyopita, ulijikita sana kwenye sekta ya kilimo kama eneo muhimu la kutuhakikishia ongezeko la pato la Taifa, ajira na chanzo cha ku-stabilise thamani ya pesa yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, projection ya kilimo ni kwamba tunategemea ongezeko kubwa la kilimo. Ni matumaini yangu kwamba tutafikia malengo hayo iwapo baadhi mambo tutayazingatia, kwa sababu mchango wa sekta ya kilimo ni mkubwa kwenye uchumi wa nchi yetu. Tunaweza kuona kwamba pato la Taifa kwenye ajira peke yake, 26% inatokana na kilimo kwa Watanzania, na 65% mpaka 70% ya Watanzania wameajiriwa katika sekta ya kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaona mchango wa kilimo ni zaidi ya 65% kwa maana nzima ya uchumi wa viwanda kwa maana ya malighafi, na tunaweza kuona kwamba zaidi ya kaya milioni nane za Watanzania wameajiriwa aidha moja kwa moja ama indirectly katika sekta ya kilimo, wakati kaya milioni nne zinategemea mauzo ya chakula kama chanzo kikuu cha mapato. Kwa hiyo, siyo eneo la kulifanyia mzaha kwa sababu limebeba hatma na stability ya nchi yetu na usalama wa watu wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naweza kuona kwamba hapa kuna ongezeko kubwa la bajeti. Ndani ya mwaka 2021/2022 tulikuwa na shilingi bilioni 294 lakini mwaka 2022/2023 ikapanda mpaka shilingi bilioni 751; na mwaka 2023/2024 Bajeti ya Kilimo imepanda mpaka shilingi bilioni 970 ambayo ni zaidi ya ongezeko la 29%, na leo hii tunazungumzia over one trillion. Siyo jambo dogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa kuliko yote ambayo tunaweza kuzungumzia, upandishaji wa bajeti hii, tunategemea kwamba uende ukaongeze uzalishaji. Ongezeko la uzalishaji tunategemea kwamba utaweka ziada kubwa zaidi katika eneo la chakula ambalo linaenda kupunguza gharama ya uzalishaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaona kuna mfumuko wa bei katika mazao hasa ya chakula. Kwa hiyo, ziada ambayo tunazalisha kupitia kilimo haijampa nafuu mkulima au mwananchi mmoja mmoja kwa sababu bado tuna experience mfumuko wa bei ya vyakula. Kwa hiyo, maeneo ambayo nitajielekeza katika mchango wangu ni nini tufanye ili tupunguze mfumuko wa bei ya vyakula ili ongezeko la mavuno liwe na tija kwa Mtanzania mmoja mmoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hilo nina ombi, huu mfumuko wa bei kwa mfano mwaka 2023, tulikuwa na zaidi ya asilimia tisa ukilinganisha na mwaka juzi ambayo tulikuwa na asilimia sita, inayotokana na gharama za uzalishaji. Gharama kubwa ya uzalishaji inasababisha mkulima akose uwezo wa kuweka akiba. Kwa hiyo, jitihada za kujiondoa kwenye umaskini kupitia kilimo bado zinakwazwa na ongezeko la bei katika uzalishaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nategemea bajeti ya kilimo mwaka huu ije kitofauti kabisa na bajeti zilizotangulia. Kivipi? Kwa sababu mwaka huu tuna-experience hali ambayo siyo ya kawaida katika nchi yetu; uharibifu mkubwa wa barabara, madaraja na vivuko ni ndwele ambazo zinaashiria hali ngumu zaidi huko mbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tunazungumzia 70% ya Watanzania waliojiajiri kupitia kilimo, maana yake wako vijijini. Kama tunazungumzia kwamba barabara za TARURA hazipitiki huko vijijini, maana yake tunazungumza kwamba hatuwezi kusafirisha pembejeo kwa bei ile ile ambayo tumeizoea. Kama hatuwezi kusafirisha pembejeo kwa bei ambayo tumezoea, maana yake inaenda kuongeza gharama ya uzalishaji kwa mkulima. Maana yake inaenda ku-compromise ongezeko la chakula na usalama wa chakula kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilitegemea bajeti hii ijikite kwenye suala zima la restoration ya miundombinu. Wakati wa majumuisho, napenda kuona Serikali kwa pamoja; Wizara ya Kilimo, TARURA, TANROADS na Viwanda na Biashara, wanakuja na mkakati wa kuokoa kilimo na mkulima katika maeneo ya vijijini na pembezoni, kwa sababu bajeti hii bado naona ni ya kawaida ukilinganisha na ya mwaka 2024. Ni bajeti ya kawaida katika kipindi ambacho siyo cha kawaida. Hivyo, tunategemea Serikali ichukue maamuzi yasiyokuwa ya kawaida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maamuzi yasiyokuwa ya kawaida sasa hivi ni kumhakikishia mkulima anakuwa na uhakika wa kupata mbegu na pembejeo zote kwa wakati na uhakika wa kusafirisha mazao yake kwa wakati. Hivi ninavyozungumza, pale jimboni kwangu kuna shamba la ASA Kilangali, wameshindwa kusafirisha mbegu kwa sababu barabara haipitiki. Kama hatuwezi kusafirisha mbegu kwa sababu barabara haipitiki hatima ya uzalishaji katika kilimo ni nini? Ni maeneo ambayo tunapaswa tuyaangalie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna hali mbaya ya barabara. Wananchi wangu 90% ni wakulima, lakini Kata ya Ulaya kwenda Kisanga mpaka Malolo hapapitiki; kutoka Malolo mpaka Uleling’ombe ambapo wanategemea kilimo haipitiki; kutoka Kidodi – Ruhembe – Kidogobasi - Kihelezo mpaka Ilundo hakupitiki, na hilo lote ni bonde la mpunga na bonde la kilimo cha miwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pale Masanze kwenda Kilangali, Mbamba mpaka Kiduhi hakupitiki na kuna Shamba la ASA ambalo linazalisha mbegu, lakini Zombo, Nyali na Nyameni hakupitiki kwa barabara. Mikumi - Kisanga kwenda Msolwa- Madizini ambao ndiyo wazalishaji wakubwa wa mboga mboga hapapitiki. Mabwerebwere - Tindiga ni sehemu ambazo zina tija kubwa ya kilimo, barabara hazipitiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunapozungumzia hatima ya wakulima katika jimbo ambalo 90% ni wakulima, haliwezi kufikika katika barabara zake zote kwa sababu ya kukatika kwa miundombinu. Tunaweka wapi kilimo cha nchi yetu? Hilo tunapaswa tuli-discuss kama suala la dharura na pia tunapaswa tuli-discuss kama mpango maalum wa Bunge lako kuokoa wakulima wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepitia hotuba ya Wizara ya Kilimo, tunazungumzia uharibifu wa miundombinu yote ya barabara na nini, lakini hatujazungumzia uharibifu wa skimu za umwagiliaji. Tunazungumzia skimu mpya, hatuzungumzii uharibifu wa skimu za kienyeji za wananchi. Tuna mpango gani kwanza wa kuokoa skimu za kienyeji za wananchi? Tuna mpango gani wa kuokoa skimu ambazo zimeharibika ambazo tumeshawekeza fedha? Tuna mpango gani wa kuanzisha skimu mpya ambazo zinaenda kutuhakikishia ongezeko la uzalishaji?

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, zao la miwa limesahaulika. Tunazungumzia ruzuku ya mbegu kwenye maeneo mengine lakini mkulima wa miwa amesahaulika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja na ninaunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)