Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Suma Ikenda Fyandomo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia kwenye Wizara hii ya Kilimo. Kwanza kabisa, namshukuru Mwenyezi Mungu wa Mbinguni kwa kunipa uzima na afya njema hatimaye imempendeza siku hii ya leo kusimama kwenye Bunge lako hili Tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Amirijeshi Mkuu. Ninampongeza kwa kazi kubwa na nzuri ambayo ameifanya kwa kuwaona wakulima. Wakulima walikuwa katika kipindi kigumu sana ambapo mbolea ilikuwa na bei kubwa sana, lakini aliweza kutoa fedha za ruzuku kutoka Mfuko wa Mbolea wa kilo 50 ambao ulikuwa unauzwa kwa shilingi 150,000, umeshuka bei mpaka shilingi 60,000 na shilingi 70,000. Pongezi nyingi sana kwa Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza sana Mheshimiwa Bashe ambaye ndiye Waziri wa Kilimo. Mheshimiwa Rais kwa kumteua Mheshimiwa Bashe kuwa Waziri wa Kilimo, naona kabisa jinsi ambavyo Mwenyezi Mungu anamwongoza kumpa macho ya rohoni kwa kumwona Mheshimiwa Bashe anafaa na anastahili sana kwenye Wizara hii ya Kilimo, kwa bajeti hiyo ambayo ameisoma Mheshimiwa Bashe hapa ya shilingi trilioni 1,200 kuomba ipitishwe. Naiunga mkono kwa asilimia mia moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa kwenye ziara kule Kanda ya Ziwa mwezi wa tatu, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri Bashe, aliweza kufanya jambo kubwa sana kwenye Taifa hili la Tanzania mara baada ya kusikia kuna mchele umeingia kutoka Marekani, kwamba mchele ule unakwenda kupelekwa kwenye shule za watoto wetu ambao ni wadogo, ambao ni malaika wa Mungu, mchele ule bila kujua una virutubisho gani na utakwenda kuathiri nini kwenye afya za watoto wetu. Nampongeza sana Mheshimiwa Bashe kwa kusimamia afya za watoto wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Taifa hili la Tanzania tuna maeneo mengi sana. Mikoa mingi inalima mpunga na mpunga huo ambao ndiyo unasababisha mchele, kule Mbeya, Kyela tunalima mpunga, Mbarali mpaka kuna Kapunga Rice, ni mpunga upo kule. Pia kule Kanda ya Ziwa nilipokuwa, kila mkoa ninakopita, ninaona barabarani mchele, ninaona mpunga umeshamiri sana ambapo ndani huko kwenye mashamba yamkini ndiko umeshamiri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo ndani ya Taifa letu hili la Tanzania, kama mpunga mwingi kiasi hicho, kule Rukwa na mahali pengine unalimwa mpunga wa kutosha sana, iweje mchele ukatoka Marekani uje kwenye Taifa letu hili la Tanzania? Wizara ya Kilimo ikiongozwa na Mheshimiwa Waziri Bashe ninawapongeza sana kwa kusimamia hili. Sisi kama viongozi, watetezi na wasimamizi wa wananchi wa Taifa hili la Tanzania, tunampongeza zaidi Mheshimiwa Bashe kwa nafasi hii kwa kuwa anatambua majukumu yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili jambo la kuleta mchele kutoka kwenye nchi ya Marekani, mwaka 2023 pia tuliletewa dawa za meno kwa ajili ya watoto wetu wapelekewe kule mashuleni. Lazima tuogope na tushtuke kwamba hiki kitu kinalenga nini? Sisi kama viongozi ndiyo wasimamizi wa Taifa hili la Tanzania, hasa kwa vizazi vyetu ambavyo ndiyo Taifa la kesho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Mheshimiwa Waziri Bashe anisikilize, Wilaya ya Rungwe wananchi wale wanategemea sana kilimo, wanalima mazao mengi sana, lakini wazazi wengi wanategemea sana chai. Kuna Kiwanda cha Chai cha Chivanje, kile kiwanda kimefungwa. Kuna wananchi wa Kayuki, Nsekela, Katonya, Ruwalisi, Ndende na Kiganga wale wote wamelima chai za kutosha. Wao wanajihimu kuchuma chai wakitegemea watapata fedha mwisho wa mwezi ili waendeleze maisha yao na ndiyo maisha yao siku zote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kufungwa kiwanda kile, namwomba Mheshimiwa Waziri Bashe akawatazame wananchi hawa wa Wilaya ya Rungwe aone namna ambavyo watafanya na kilimo kile cha chai watakifanya nini? Maana kiwanda kimefungwa, wakichuma chai wanaipeleka wapi? Naomba sana Mheshimiwa Waziri Bashe alitazame hili na kuwasimamia hawa wakulima wa chai. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, kuna wakulima wa chai ambao wako kwenye Wilaya hiyo hiyo ya Rungwe, wakulima hawa wanapeleka chai kwenye Kiwanda cha Chai cha Katumba, ambao wako maeneo ya Rungwe, Kapugi, Masege, Segera, Mwakaleli, Mano, Lupa, Itete, Kimo, Suma na Nditi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakulima hao wanafanya vizuri, lakini hawapati fedha kwa wakati. Wanazidishiwa sana muda. Sijajua kwenye hili hawa wakulima wa Mheshimiwa Bashe anawasimamia kwa namna gani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba muda ni mchache sana, naongea kwa sehemu. Mheshimiwa Waziri, kule Mufindi, Mkoa wa Iringa, Serikali iliahidi mwaka 2022 kujenga kiwanda cha kuchakata maparachichi. Eneo lile ambalo mlikuwa mmeomba lipatikane ndipo mjenge kiwanda cha kuchakata maparachichi, limepatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kiwanda hicho cha kuchakata maparachichi ni cha kusaidia wananchi wa Nyanda za Juu Kusini ikiwemo Njombe, Mbeya, Iringa, Songwe na maeneo mengine. Kule Tukuyu Wilaya ya Rungwe, Mkoa wa Songwe wamejitahidi sana kupanda maparachichi baada ya kusikia kauli hii ya Serikali. Hivyo basi, tunaomba sana wakati wa kuja kuwasilisha hapa, Mheshimiwa Waziri atuambie ni lini kiwanda hicho kitaanza kujengwa ili wananchi waweze kupona kwa ajili ya kuendeleza ulimaji huu wa parachichi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa namna ambavyo anaendesha Wizara zote. Katika kumpongeza huko, kule Mbarali na Kyela zilitolewa fedha kiasi cha shilingi bilioni 79 kwa ajili ya skimu za umwagiliaji. Namwomba sana Mheshimiwa Bashe, kule Mkoa wa Mbeya bado kuna Wilaya nyingine ambazo zina uhitaji wa skimu hizo ikiwa ni pamoja na Mbeya DC, Busokelo, Chunya, Mbeya Mjini na pia kuna maeneo pamoja na Rungwe yenyewe, wana uhitaji wa skimu hiyo sana. Wanawake wale pamoja na vijana wanajituma sana kwenye mambo ya mashamba na ndiyo kazi yao kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili jambo la BBT ambalo limeanzishwa ni jambo jema na zuri. Tumeona hapo jinsi ambavyo linafanikiwa. Pongezi nyingi sana kwa Mheshimiwa Waziri kwa namna ambavyo unayaona haya yote kwa ajili ya ajira ya kujiajiri wanawake na vijana. Kwenye hili, Mwenyezi Mungu aendelee kukusimamia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakwenda kumalizia kwamba Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Naomba uhitimishe.

MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Namtia moyo Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa, nzuri anayoifanya. Narudia kwamba, Mwenyezi Mungu anamwongoza, anampa macho ya rohoni hatimaye akamteua Naibu Waziri Mkuu, Mheshimiwa Dkt. Doto Biteko ambaye ana hofu ya Mungu, aendeshe mambo vizuri. Kila kitu kinakwenda sawa, Mawaziri wake wako vizuri, Makatibu Wakuu, Wakuu wa Wilaya, Wakuu wa Mikoa pamoja na Wakurugenzi wako vizuri. Mwenyezi Mungu ambariki sana Mheshimiwa Rais na ninaomba Mwenyezi Mungu aendelee kumpa macho ya rohoni

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)