Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Katani Ahmadi Katani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tandahimba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. KATANI A. KATANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nachukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya pekee kabisa nampongeza sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Kwa sisi wakulima wa korosho, mimi nimezaliwa kwenye korosho. Transformation ya zao la korosho nimeanza kukua nayo nikianza kutambaa mpaka natembea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunapozungumza, Mheshimiwa Rais ameendelea kutoa pembejeo za korosho bure. Leo tunapozungumza, Mheshimiwa Rais amekubali kurejesha fedha ya export levy, yote irudi kwenye Tasnia ya Korosho. Leo tunapozungumza, Mheshimiwa Rais ametoa fedha zaidi ya shilingi bilioni 10 kwenda kutengeneza kongamano ya viwanda pale Maranje, Nanyamba. Kwa sisi wakulima wa korosho hakuna tunachoweza kumwahidi Mheshimiwa Rais zaidi ya kuendelea kumtafutia kura za mwaka 2025. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana ya sekta ya kilimo, lakini napata mashaka makubwa sana tunaposema leo bajeti ya Wizara ya Kilimo imeongezeka kutoka shilingi bilioni 970, kwenda shilingi trilioni 1.2.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunapozungumza, ukisoma taarifa ya bajeti ya Wizara ya Kilimo, wamepokea 53.8% ya bajeti ya msimu uliopita mwaka 2023/2024. Tumebakiza mwezi mmoja tu tunakwenda mwaka mpya wa fedha. Maana yake ni kwamba 46.2% hawajapata fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tutashindwa kuwapima watu hawa kwa mission na vision walizokuwanazo kwa sababu fedha wanayoiomba na kinachokwenda ni tofauti. Tutakapofika tarehe 13 Juni, hii bajeti tuliyoizungumza mwaka 2023/2024 inakwenda ukingoni. Leo tunapozungumza, wamepata shilingi bilioni 522. Sioni uwezekano wa kupata shilingi bilioni 448 kwa kipindi kilichobaki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sekta ya Kilimo kwenye Taifa hili, ndiyo inaajiri watu wengi. Sekta ya Kilimo kwenye Taifa hili ndiyo inayofanya, leo wanafunzi wana shida ya vyoo, kwa sababu uzalishaji unaongezeka, watu wanazaliana ndiyo maana shuleni kunatakiwa vyoo. Kunatakiwa watoto wapate chakula. Leo kama kuna shilingi bilioni 448, haijaenda na tumebakiza mwezi mmoja, tutashindwa kuwapima Waheshimiwa Mawaziri hawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata ukiitazama Bajeti ya Wizara ya Maji, fedha zilizokwenda na kilichopangwa, havilingani. Tutapata shida ya kuwapima watu hawa. Dhamira ya Mheshimiwa Waziri ni njema sana, lakini kwa uendeshaji huu wa fedha ya upatikanaji wa fedha huu, tutashindwa kukaa sehemu salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi wakulima wa korosho, tunampongeza Mheshimiwa Waziri kwanza, kwa kutoa ule ulazaji wa box kwenda kwenye TMX na kwenye jambo hili awe na comfort. Nimesema mimi nimezaliwa kwenye korosho, transformation hii aliyoifanya, mwaka 1998/1999 mimi nilikuwa mpimaji wa korosho godown. Hiki alichokifanya Mheshimiwa Waziri cha kwenda kwenye TMX, tulikuwa tunafanya nyuma kwa namna nyingine. Wahindi wanakuja kwenye Chama cha Msingi, huyu anaweka bei yake na mwingine anaweka bei yake, anayeweka bei ya juu ndiyo tunamuuzia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri amefanya transformation ya kisasa. Tunakwenda kwenye computerization huko lakini kilishafanyika nyuma. Usipate shida na maneno ya kwenye mitandao, ukiona umerusha jiwe msituni ukasikia mtu analia, ameshatandikwa huyo. Haya yanayozungumzwa kwenye mitandao, kuna wadau wa korosho nimewaona kwenye mitandao. Impe comfort Mheshimiwa Waziri, sisi wawakilishi wa wananchi tunajua anachokifanya. Tunajua dhamira yake ya kumsaidia Mheshimiwa Rais. Fanya kazi yako vizuri Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo maneno kwamba unaingilia Tasnia ya Korosho, unaingilia vyama vya ushirika. Wewe ni Waziri mwenye dhamana ya Kilimo, usipate hofu na maneno. Usipomsaidia mlaji, au usipomsaidia mkulima, hali itakuwa mbaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo pembejeo hizi ambazo Wizara inatoa bure ni zaidi ya shilingi 66,000 mfuko mmoja, lakini pembejeo hizo ukisema Serikali msiingie, zinaweza kuuzwa bei yoyote. Mwaka 2023 tumeona wakati Mheshimiwa Waziri anarudisha bei ya mbolea, zilishafika shilingi 100,000 na kidogo, akajaribu kusimama, akahakikisha mkulima anapata mbolea kwa bei nafuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo akitokea mdau akasema yeye ni mdau, akaandika huko; “Ogopa Waziri ku-intervene”, wakulima wa Taifa hili wataumia. Ipo shida kwenye Sheria zenu za Ushirika, kuna wakati mnasema wanasiasa wasiingie kwenye ushirika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani hii ndiyo wanapokosea bila kufahamu ushirika wenyewe ni Sera na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ambayo Waziri wake ni wewe. Sasa usikae ukawa na uoga uoga. Fanya intervention kwenye Sekta ya Kilimo, popote unapoona hapa mlaji, mkulima anakwenda kuathirika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzetu wanaolima ufuta na mbaazi, Serikali mmefanya intervention. Wameshaingia makubaliano ya mikataba na nchi zinazonunua mbaazi na ufuta. Mimi nashauri sana, tunapokwenda kwenye msimu wa korosho wa mwaka huu, tuweke bei dira, wakulima wajue bei dira ya korosho ili mnunuzi yeyote anayekuja, asinunue korosho chini ya bei dira ambayo Serikali mtaitangaza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tutakapokwenda kwenye minada, kama mnunuzi hafiki bei hiyo, tusiuze korosho, na jambo hili mnaliweza. Kama leo mnaweza kununua mahindi NFRA mnayahifadhi, sidhani kama kuna mahali mtashindwa ikitokea kwamba bei dira ambayo mtaiweka indicative price kuna watu wanaweza kuchezesha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuliwahi kukaa kwenye kikao cha tathmini ya korosho. Tukiwa kwenye kikao kile miongoni mwa mambo makubwa aliyoyafanya ni kuunda Tume ambayo ilikuwa huru na 98% ya maoni yaliyotolewa na Tume ni maoni sahihi yanayotoka kwa wananchi. Bodi yake ya Korosho ina madudu, ameyaona, watumishi wa Bodi ya Korosho amesikia madudu wanayoyafanya. Kama mtumishi mmoja anaweza kusaini documents za vibali akiwa meneja tu wa sehemu fulani na bado wakawa naye, maana yake Serikali iko kimya, wanashiriki wizi na hujuma hizo, yaani Mheshimiwa Waziri na Bodi yake wanashiriki hujuma hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ripoti iko wazi, mtu anasaini document, siyo afisa masoko wa bodi tena akiwa sehemu nyingine na wamekaa kimya mpaka leo na siyo kwamba hawajui. Ripoti inaeleza, mtu amechukua fedha za wakulima huko Katavi ili aagize mabomba sijui vitu gani; ilhali wakulima hawajapewa na ni mtumishi wa Serikali. Ripoti inaeleza mtu kuwa amechukua korosho bila vibali, korosho zinakamatwa, kuna ushahidi, kuna voice note wakitaka tutawapa, hizo document tunazo kama hawana ushahidi; lakini bado wanaendelea kukaa na mtu huyo kwenye tasnia ya korosho. Itakuwa ni Serikali ya ajabu sana, itakuwa ni Bodi ya Korosho ya ajabu sana; hujuma zinafanywa, conflict of interests inaonekana na bado wanakaa bila kuchukua hatua, ni Serikali ya aina gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu yuko kwenye tasnia, wakulima wanaumia. Ukisoma sheria waliyoitengeneza wenyewe Bodi ya Korosho, kwamba, kama unakamata korosho ambazo hazina documents zimepelekwa mahali kinyume na utaratibu faini ni kati ya milioni tano mpaka milioni 500

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Katani, muda wako umekwisha kabisa…

MHE. KATANI A. KATANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.