Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia Hoja hii ya Wizara ya Kilimo. Kwa sababu ya muda naomba kusema kwamba naunga mkono hoja ya Wizara hii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, moja kwa moja naomba tu nimpongeze Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuwashika mkono wakulima wa Tanzania kwa hiki anachokifanya kuendelea kuongeza bajeti ya kilimo. Tulianza na bajeti ya shilingi bilioni 294, msimu uliofuata ika-shoot mpaka 751 na hii tunayoendelea nayo bilioni 970 na sasa, tunamwomba aridhie kutoa trilioni 1.4 ili watu wa kilimo wakafanye kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, uwekezaji mkubwa kwenye kilimo maana yake ni nini? Maana yake ni tutarajie kuona matokeo makubwa sasa kutokana na uwekezaji huu. Matokeo haya makubwa tuangalie kuwasaidia wakulima wadogo, lakini sasa pia, tuelekee kwenye mashamba makubwa. Kwa wakulima wadogo bajeti ijibu changamoto zao, ikiwemo upatikanaji wa pembejeo. Wenzangu wamesema na mimi bado nasema, mbegu ni changamoto kwa wakulima, ni bei ghali na hata upatikanaji wake ni mgumu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa mfano, nchi yetu inahitaji takribani tani 126,650,000 za mbegu bora, lakini kwa msimu uliopita upatikanaji ulikuwa ni tani 64,000 sawasawa na 54%. Kati ya hizo tani 40,000 zilikuwa za mahindi na tani 15 zilitoka nje ya nchi, lakini pamoja na hayo ndiyo tunasema, hizi mbegu ni za wenzetu. Wenzangu wamesema zinatoka Zambia, zinatoka Malawi, ndiyo akina SEEDCO, DK, PANA, PIONEER, ZAMSEED, ambapo pakti la kilo mbili linauzwa mpaka shilingi 17,000 au shilingi 18,000.
Mheshimiwa Spika, mkulima katika eka moja anahitaji pakiti tano ambapo hii inagharimu shilingi 85,000 mpaka shilingi 100,000 kwa ekari moja ambayo ni ghali sana kwa wakulima. Naomba kutoa ushauri kwa Wizara, tunayo taasisi yetu ya utafiti, ina mbegu nyingi za msingi, mbegu mama, ni kwa nini wasipate mbegu zinazoweza kushindana? Tuzalishe mbegu zetu wenyewe ndani ya nchi kwa ruzuku, ili angalau gharama hii ya pakti moja la kilo mbili ishuke kutoka shilingi 17,000 au shilingi 18,000 na ifike shilingi 10,000 na hata chini zaidi ikiwezekana ili kutoa unafuu kwa mkulima.
Mheshimiwa Spika, niseme pia kuhusu mbolea. Naipongeza Serikali kuendelea kutoa ruzuku kwenye mbolea. Kweli, kumekuwa na ongezeko kubwa sana la matumizi ya mbolea ya viwandani baada ya Serikali kutoa ruzuku. Kabla ya Serikali kutoa ruzuku, matumizi ya mbolea yalikuwa ni kati ya tani 400,000 mpaka 600,000. Baada ya Serikali kuendelea kutoa ruzuku, makadirio yalikuwa ni tani 848,884 kwa mwaka, lakini kwa msimu huu hadi kufikia Aprili, tayari matumizi ya mbolea yameshaenda kwenye tani 1,052,000 na kuendelea.
Mheshimiwa Spika, hii maana yake ni nini, kama tuna matumizi makubwa ya mbolea ya viwandani bila kupima udongo wa wananchi hiki kitu ni hatari sana. Kwanza ni hatari kwa gharama, lakini vilevile on future ni lazima itakuja kuwa haina usalama kwa udongo wa wananchi. Hivi kwa mfano, mkulima ardhi yake ina chumvichumvi ya kutosha (salinity) anaendelea kuongeza hii mbolea, mwisho wa siku ile ardhi hataweza kuitumia. Hakuna mmea ambao utaweza kuota hata kidogo. Mbolea ya chumvichumvi ni hatari kwa microorganism walioko kwenye ardhi, ni hatari kwa soil texture na ni hatari kwa kila kitu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba kuishauri Serikali, kwanza kwa sababu, Maafisa Kilimo wamepewa soil tester, hebu iwe ni lazima mkulima apime udongo wake kabla ya kutumia mbolea hii ili aweze kuelekezwa ni nutrients zipi zinakosekana. Pamoja na hayo, Serikali itoe pesa za kutosha kwa TARI Mlingano ambao wao wanapima udongo watupatie soil map ya Tanzania nzima, kwamba, ukanda huu kuna upungufu wa nutrients fulani, upande huu kuna upungufu wa nutrients fulani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vilevile naomba Serikali iendelee kuwekeza kwenye Kiwanda cha Intracom kilichoko hapa kwetu. Kiwanda hiki uzuri wake, kinachanganya mbolea ya samadi ambayo nafikiri ni salama na ina nutrients. Kiwanda kina uwezo kwa kuzalisha tani 800,000 mpaka 1,000,000 kwa mwaka. Kwa sasa hivi kiwanda hiki kinazalisha tani 40. Ni kwa nini tusiwashauri wakulima? Hata kama matokeo yake yanaenda taratibu, pamoja na Kiwanda chetu cha Minjingu, hii ndiyo mbolea ya kuwashauri wakulima kuendelea kuitumia pamoja na samadi na kuendelea kutengeneza mboji. Vinginevyo tunavyokazana kuendelea kutumia mbolea ya viwandani, siku mmoja tutapata changamoto kubwa kwenye ardhi ya wakulima. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lingine ni hili suala la viuatilifu. Tumesema tunapunguza upotevu wa mazao (post-harvest) kwa kuanzia 35% mpaka asilimia tano. Kuna upotevu mkubwa sana wa mazao ya wakulima, hususan mahindi. Mahindi yakiwa stoo upotevu unaweza kufika mpaka 100% kwa sababu, wananchi wanahifadhi kwa kutumia hivi viuatilifu. Pengine kiuatilifu cha kifungashio cha gramu 200 labda mkulima anaambiwa anaweka kwenye magunia manne, lakini wadudu walioko kule hawafi na wengine wanakwepa, hii maana yake ni nini? Badala yake mkulima anatumia sumu kali sana, hizi wanazoita high hazard pesticides, ndiyo zinachanganywa kwenye mahindi, kwenye mazao yaliyoko pale na ambapo athari ya ile sumu ni mbaya sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba na pia naishauri Serikali, hebu kupitia TPHA hawa Wakala wanaoangalia hizi pesticides pamoja na afya ya mimea wavipitie hivi viuatilifu vinavyotumiwa na wakulima kwa sababu, kwa kweli ni hasara kabisa. Ukiweka mahindi yako stoo yakagongwa na wadudu, huwezi kuyauza wala huwezi kufanya kitu kingine na inakuwa ni hasara kubwa sana kwa wakulima. Waendelee kuliangalia hilo.
Mheshimiwa Spika, vilevile Wizara waendelee kukarabati maghala yaliyoko kule kwenye ngazi ya kata kwa sababu, mkulima akishahangaika anatumia dawa fulani ya vidonge. Ile dawa ina conditions zake, lakini wakulima mle nyumbani yanakolala kwenye stoo zao ndiyo wanatumia hivi vidonge ambavyo ni hatari kabisa. Kwa hiyo, basi maghala yakarabatiwe wapeleke mazao kwenye maghala.
Mheshimiwa Spika, vilevile kuna teknolojia ambayo ilikuwa inaenda vizuri. Hii teknolojia ya kutumia mifuko yenye tabaka tatu ni ghali, ule mfuko mmoja ni shilingi 5,000. Mkulima mwenye mahindi yake magunia kadhaa, 20 mpaka 100 hawezi kuendelea kununua hii mifuko. Tunaomba ikiwezekana Serikali kwenye viwanda vinavyozalisha mifuko hii, waweke ruzuku ili angalau hii mifuko iuzwe kwa shilingi 2,000 na kurudi nyuma. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mchango wangu mwingine ni kwenye soko. Naomba niwasemee wakulima wa Manyara ambao ni wakulima wazuri wa mahindi na maharage. Kusema ukweli kwa soko la mazao ya mahindi tunazidi kumrudisha mkulima kwenye umaskini. Kama sasa hivi gunia bado linauzwa shilingi 30,000 mpaka shilingi 40,000, huyu mkulima tunamrudisha kwenye umaskini. Sasa, kama Serikali au Wizara inatoa bei elekezi ya pembejeo ya mbolea, kwa nini isifikie mahali ikasema kwamba, mazao ya mkulima kwa mfano, mahindi kilo isiuzwe chini ya shilingi 800? Wakulima wanahangaika, vinginevyo basi NFRA inunue mazao ya wakulima, itafute masoko ili angalau wakulima waachane na adha ya kuhangaika na mazao huku wakiendelea kuchanganya dawa wakati wakiendelea kusubiri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mchango wangu mwingine ni kwenye mashamba makubwa. Kama tunataka transformation kwenye kilimo, hatuna namna bila kwenda kwenye mashamba makubwa. Tuna potential kubwa katika nchi yetu. Tuna ardhi inayofaa kwa kilimo zaidi ya hekta milioni 44 ambapo tunatumia chini ya 40%.
Mheshimiwa Spika, hivi ni kwa nini sasa hivi pengine Serikali, kupitia Wizara yake, isifahamu kabisa maeneo ya kilimo, hata ikaya-acquire kutoka kwa wananchi, ika-treat afya ya udongo, ikaweka miundombinu ya umwagiliaji ili iwe rahisi kwa wawekezaji? Waje wa-invite wawekezaji watuzalishie hilo gap la mazao muhimu? Kwa mfano, ngano, mbegu za mafuta na hata sukari? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ukishaweka mazingira mazuri ni lazima tutapata wawekezaji. Hata hivyo, mashamba haya ya BBT farm blocks, kutokana na economy for scale nafikiri kwamba, waelekezwe kabisa mazao ya kuzalisha ili nchi yetu tutoke kwenye gap la hayo mazao ambayo ni muhimu kwetu sisi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mchango wangu mwingine na pengine wa mwisho, ni kuhusu kilimo cha umwagiliaji. Kilimo cha umwagiliaji ni kilimo cha uhakika na kutengeneza miundombinu ya umwagiliaji ni gharama kubwa sana, hasa kuchimba mabwawa. Sasa, naiomba Serikali, haya mabwawa kwa kweli, moja linafikia shilingi bilioni na kuendelea. Shilingi bilioni moja, bilioni mbili, lakini bwawa likichimbwa, pengine life span yake ilikuwa iende miaka 50 na kuendelea, lakini haliwezi kufika muda huo pasipo kuwaelemisha wale wanufaika walioko pale, wana-scheme kwa sababu, baada ya muda bwawa linakuwa salted, halifai tena. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa ninafikiri mnavyoenda kwenye kutengeneza miundombinu ya umwagiliaji ni bora mkaingia mkataba na halmashauri au wale wanufaika wa scheme. Wakubaliane kuhusu utunzaji wa miundombinu ya umwagiliaji. Hata hivyo, kuna schemes nyingi sana ambazo Serikali imewekeza hela, lakini bado hazijamaliziwa, pengine ni bwawa tayari, ni spillway tayari, lakini miundombinu mingine bado intake, kuweka line kwenye mifereji pamoja na vitu vingine havijawekwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa, naiomba Serikali, kwa miradi ambayo Serikali imekwishawekeza hela na bado iko nusunusu haijakamilika, kwanza ingeikamilisha miradi hii ya umwagialiaji na ndipo ikaanza kujenga miundombinu mingine. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nakushukuru na naunga mkono hoja. (Makofi)