Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. George Natany Malima

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mpwapwa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. GEORGE N. MALIMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia Hotuba ya Wizara hii ya Kilimo. Kwanza naanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye anaendelea kutulinda, kututunza na kutufanya tuendelee na shughuli zetu kama kawaida. Pili, nampongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amefanya kazi nyingi sana katika Wizara hii ya Kilimo. Sisi kule Mpwapwa tumepata bwawa kubwa sana la umwagiliaji lenye thamani ya shilingi bilioni 27.8 ambalo ujenzi wake unaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, namshukuru Waziri wa Kilimo, Mheshimiwa Bashe. Yeye anajua jinsi nilivyofuatilia na hatimaye akakubali na sisi watu wa Mpwapwa tupate bwawa hili. Nakushukuru sana Naibu Waziri, Mheshimiwa Silinde, nawapongeza kwa kazi nzuri.

Mheshimiwa Spika, nianze kwa kuchangia bajeti ya Wizara hii. Mheshimiwa Waziri ameanza kueleza hali ya kilimo katika nchi yetu ya Tanzania. Ameeleza kwamba, kuna ukuaji wa Sekta hii ya Kilimo kwa 0.9% na kwamba, kulikuwa na ukuaji wa 3.3% mwaka 2022, lakini kwa ujumla mwaka 2023 kumekuwa na ukuaji wa 4.2%.

Mheshimiwa Spika, nawapongeza sana kwa jitihada hizi, lakini naamini kabisa nchi yetu inaweza kukua zaidi ya hapa. Ukuaji huu ni mdogo ukilinganisha na maeneo ya kilimo tuliyonayo katika nchi yetu, tunaona kwamba tungeweza kufika katika asilimia kubwa kuliko hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napenda niongelee kwenye eneo la umwagiliaji. Umwagiliaji ndicho kilimo cha uhakika kuliko kilimo kingine chochote na ripoti au bajeti imeeleza kwamba, mpaka sasa hivi nchi yetu ina hekta 727,000.3, ndilo eneo ambalo linafanyiwa kilimo cha umwagiliaji. Ukiangalia nchi yetu ni kubwa na pia maeneo ni mengi ambayo kama yangeweza kutambuliwa, kujengwa mabwawa na kuwekewa miundombinu ya umwagiliaji, ukuaji wa sekta hii ya kilimo ungeweza kuwa mkubwa sana.

Mheshimiwa Spika, hata ukiangalia mchango wa Sekta ya Kilimo kwenye pato la Taifa bado ni mdogo. Tofauti yake ni ndogo sana, kutoka mwaka 2022 mpaka mwaka 2023 imekua kwa asilimia 0.3, kwa hiyo, bado utaona mchango wake ni mdogo sana. Ni mdogo kwa sababu gani? Eneo tunalolitumia, kwa ajili ya umwagiliaji ni eneo dogo la hekta 727,000 tu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kule Mpwapwa tuna maeneo mengi, lakini naamini hata sehemu nyingine za nchi yetu pia, kuna maeneo mengi ambayo yana sifa ya kufanya kilimo cha umwagiliaji. Kwa mfano, kule Mpwapwa, Kata ya Chitemo kuna eneo zuri, Mlembule kuna eneo zuri, Godegode, ukienda kule Pwaga, ukienda Kitati, ukienda Lumuma, haya maeneo yote kama yangeweza kufanyiwa utafiti na Serikali yakaweza kujengewa miundombinu, kilimo hiki kingeweza kuwa na tija na kingeongeza Pato la Taifa.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo napenda kuchangia ni ukosefu wa mbegu bora. Wakulima wengi wa Kitanzania wana juhudi sana ya kilimo, lakini shida ambayo wanakutana nayo ni kwamba, unapofika msimu wa kilimo wanapokwenda madukani kununua mbegu, wapo wafanyabiashara wengine ambao siyo waaminifu, wanauza mbegu ambazo ni fake. Mbegu ambazo hazijafanyiwa utafiti, hazina sifa ya kuitwa mbegu bora. Kwa hiyo, wakulima wanapokwenda kupanda zile mbegu, matokeo yake hawapati ile tija ambayo walikuwa wanaitarajia. Hili ni tatizo kubwa sana. Naishauri Wizara ya Kilimo, wakati msimu wa kilimo ukikaribia wafanye ufuatiliaji kwenye haya maduka yanayouza mbegu, watakutana na mbegu hizi fake ninazosema. Hii itatusaidia kupunguza athari hizi zinazotokea.

Mheshimiwa Spika, pia, nimeona wanasema wametenga fedha katika sekta hii kama shilingi bilioni 43 hivi. Fedha hizi wanasema kazi yake kubwa ni kujaribu kufanya utafiti ili kupata mbegu bora na kuzisambaza. Basi bajeti hii ingejikita sana kwenye utafiti ili tuwe na mbegu bora na lengo liwe ni kutosheleza nchi yetu yote ya Tanzania. Wananchi wetu wanaoshughulika sana na kilimo waweze kupata mbegu bora kwa wakati na kwa bei ambayo ni affordable ili waweze kuongeza kilimo na ikifika mwakani au angalau hata baada ya miaka miwili tuweze kuona matokeo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Bashe anachakarika sana kujaribu ku-transform kilimo katika nchi yetu, nampongeza sana. Tunaona mikakati mingi anayoifanya, lakini kama hawezi kujikita kwenye upatikanaji wa mbegu bora, juhudi zake zote zinaweza kuwa hewani. Kwa hiyo, naomba sana nimshauri Mheshimiwa Waziri kwamba, mbegu ndiyo kitu muhimu sana katika kilimo. Ni lazima tupate mbegu zilizo bora ambazo watu wetu wanaweza kunufaika nazo. Kama tunavyosema, kilimo ndicho kinachangia asilimia kubwa ya ajira katika nchi yetu, lakini kwa miaka mitatu nimefuatilia hali ya asilimia ya ajira zinazotokana na kilimo iko katika range ya 65 mpaka 70, kwa nini haikui? Ni kwa sababu ya mambo kama haya madogomadogo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwanza, hatuja-utilize eneo letu lote la umwagiliaji, lakini pili, hata wakulima wetu hawatumii mbegu zile ambazo tunadhani ni bora ambazo zinaweza kuleta tija. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri ajaribu kuangalia sana suala la utafiti ili tuwe na mbegu bora.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo pia tunakutana nalo kwenye vijiji, ni wakulima wetu hawana elimu ya kilimo. Tunao Maafisa Ugani, lakini hawatoshelezi. Taarifa yake inasema mpaka sasa hivi tuna asilimia 35 tu ya Maafisa Ugani ambao wako kwenye maeneo yetu, lakini tuna upungufu wa Maafisa Ugani 20,000 na kuendelea, sasa hili ni tatizo. Kata moja inakuwa na Afisa Ugani mmoja, vijiji ni sita, anawezaje kufanya kazi katika mazingira hayo?

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunadhani kwamba, Serikali ni lazima ichukue hatua muhimu na maamuzi magumu kuajiri Maafisa Ugani kwa wingi. Kama tunataka kupata matokeo, kama tunataka kuongeza pato la Taifa kupitia Sekta hii ya Kilimo ni lazima tuwe na wataalam wanaojua ambao watawasaidia wakulima wetu kulima kilimo cha kisasa. Pia, wawe wanaweza kutambua mbegu fake na mbegu bora kwa sababu ya utaalam watakaokuwa nao. Bila hao, wakulima wetu wataendelea kulima kama kawaida, watalima kilimo walichokizoea na matokeo yake hakutakuwa na tija.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo nataka kuchangia na pengine litakuwa la mwisho ni kuhusu uhakika wa masoko kwa mazao yetu ya kilimo. Sasa hivi ukienda vijijini mazao mengi yameiva na yamekomaa, lakini walanguzi wameshavamia kule wananunua kwa bei ya chini kabisa. Kwa hiyo, mkulima anapomaliza msimu wa kilimo anakuwa haoni kitu alichopata. Ameuza mazao yote kwa bei ndogo, wanaofaidi ni wale middlemen wanaokuja kulangua na kwenda kuuza mahali pengine.

Mheshimiwa Spika, Serikali ingekuwa na mfumo wa kuwa na masoko rasmi ambayo mkulima anajua nikilima karanga, nikilima ufuta, nitakwenda kuuza mahali fulani na bei inaweza kuwa imetangazwa inajulikana. Hii itawasaidia kujikwamua kiuchumi, lakini pia, sekta itakuwa na itaongeza pato la Taifa. Kwa hiyo, masoko ni jambo la muhimu. Hatujawa na soko kamili katika nchi hii, wakulima wetu hawajui. Tunajaribu kuhangaika kutumia vyama vya ushirika, lakini bado kuna maeneo mengi vyama hivi havifiki. Kwa mfano, Wilaya yetu ya Mpwapwa, sidhani kama kuna chama cha ushirika pale. Wakulima wetu wanajihangaikia wenyewe, wakishapata mazao walanguzi wanakuja wanachukua mazao yao kwa bei ya chini, wale wanabaki maskini mwaka baada ya mwaka. Kwa hiyo, naomba sana jambo hili lichukuliwe.

Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa, miaka miwili mitatu huko nyuma Kanda ya Kati tulipiga kelele sana juu ya kilimo cha alizeti na zabibu, lakini kuanzia mwaka jana na mwaka huu sisikii kitu. Ni kama hiki kitu kilikuwa ni mbio za sakafuni. Sasa hivi hakuna tena pressure ya kuhimiza watu walime alizeti, walime zabibu. Hii inawezekana ni kwa sababu ya bei za mafuta ambazo hazieleweki, lakini pia soko la zabibu ambazo zinalimwa hapa Dodoma bado halijulikani.

Mheshimiwa Spika, watu wanatengeneza michuzi ya zabibu, lakini mahali pa kuuza hakuna, matokeo yake inaharibika. Kwa hiyo, watu wanaacha wanakata tamaa. Wakulima wanakata tamaa kuendelea na kilimo kwa sababu hakilipi na wala hakijawa na mfumo rasmi wa kuwasaidia wakulima. Kwa hiyo, tukitaka wakulima wetu wafanye vizuri, ni lazima tuwawekee mazingira mazuri kwa maana ya masoko, mbegu na wataalam wawepo, hapo ndipo tutaona kilimo hiki kinakua. Kwa hiyo, Mheshimiwa Bashe naunga mkono hoja, lakini zingatia haya mambo. Kilimo chetu kitakua na wananchi wetu watafaidika. Ahsante sana. (Makofi)