Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mtera
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili nitoe mchango wangu kwa Wizara ya Kilimo. Awali ya yote, nataka nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, pamoja na timu yake nzima kwa kazi kubwa ambayo wanafanya. Vilevile nataka nimtahadharishe kwa sababu najua kuna wengine hawajamzoea sura aliyoingia nayo leo, watu wengi hawajaitafsiri.
Mheshimiwa Spika, chama kinachotawala nchi hii ni Chama cha Wakulima na Wafanyakazi, kwa hiyo seriousness yake kwa jioni ya leo inazingatia hilo kwamba, hii bajeti ya leo tunaijadili ni bajeti ya wananchi wa Tanzania karibu 90%. Kwa hiyo, wawe makini sana Mheshimiwa Waziri Bashe na Mheshimiwa Naibu Waziri Silinde, wanaweza wakapotea ghafla hapo kama hawatasikiliza kwa makini mambo yanayozungumzwa hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais amepanga safu kwenye Wizara hii ambayo siyo tu imekuja kuchangamsha, bali imewafanya vijana wengi na Watanzania kutamani sasa kuingia kwenye kilimo. Imegeuza fikra kabisa kwamba, hata maeneo makavu kama Mkoa wa Dodoma, imeonekana wazi kwamba ukame wa Dodoma haukuwa ukame wa ardhi bali ulikuwa ukame kwenye vichwa, kwa maana kumbe tukiweza kuchimba maji chini ya ardhi tukapata mabwawa ya kutosha ukame itakuwa ni hadithi, hatutazungumzia habari ya ukame. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tumpongeze Mkuu wa Nchi kwa namna anavyoshusha pesa kwenye Wizara hii na vision yake. Tumeona akitoa usafiri nchi nzima kwa ajili ya wataalam wetu mbalimbali waweze kufika shamba. Tumeona zikinunuliwa mashine mbalimbali za kupima udongo, lakini shida yangu kubwa ni namna Wizara itawezesha vile vyombo kuweza kutembea. Sijui OC, mafuta yanapatikanaje ili pikipiki ziweze kufika kwenye mashamba ya wakulima badala ya watu kurandaranda nazo pale Mjini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa Mkoa wa Dodoma sisi, naomba ku-declare na mimi sasa hivi ni mwekezaji mdogo wa Kiwanda cha Mchuzi wa Zabibu, tunatengeneza wine, kwa hiyo, tumejifunza mengi sana kutokana na zao la zabibu. Zao la zabibu ni zao la matunda na halitunziki kirahisi, ni lazima uchakate mchuzi na uweze kutunza ule mchuzi. Vyombo ya kutunzia mchuzi ni ghali sana. Kwa hiyo, tungemwomba Mheshimiwa Waziri, Serikali ijaribu kuwaangalia wasindikaji wadogo wadogo iwasaidie hata kupata vyombo vya kutunzia huo mchuzi kwa kipindi kirefu ili waweze kumudu, waweze kutunza mchuzi na baadaye wakulima waweze kupata tija. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo ni lazima kutambua ardhi, siyo Mkoa mzima wa Dodoma unalima zabibu, kuna maeneo zabibu hazikubali. Ardhi inayolima zabibu ni ndogo sana. Kwa hiyo, ni vyema Wizara ikaitambua hiyo ardhi ikapimwa wakulima wakapata hati na tukalinda eneo hilo, kwa sababu kuna uwezekano mkubwa eneo hilo likapangiwa matumizi mengine, basi itakuwa hadithi ya kusikia kwamba, Dodoma tunalima zabibu.
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo ni vema Serikali sasa ikajikita kwenye kutafuta masoko ya mazao. Masoko yamekuwa tatizo, wakati wa mavuno chakula kinakuwa kingi ndani ya nchi, kuna baadhi ya maeneo kinashuka sana bei na maeneo mengine kinakuwa kimepanda sana. Kwa hiyo, utakuta mkulima hanufaiki chochote isipokuwa mfanyabiashara wa mwisho ndiyo anayenufaika na mazao ya mkulima, hii sasa si sawa! Ni lazima tuangalie namna ya ku-balance ili mkulima aweze kuinuka pale alipo.
Mheshimiwa Spika, Mradi wa BBT, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais, namna alivyotutengenezea kitu kizuri, Jimbo letu la Mvumi tumepata huu mradi zaidi ya hekari 11,000 zinalimwa pale, ni rai yangu kwa Mheshimiwa Waziri kututengenezea barabara, kwa sababu huku kote barabara tumeweza kuitengeneza, lakini kutoka Kijiji cha Ndogowe kupita kwenye ule mlima kuelekea Ihimbwa, kushuka Mlazo kwenda kwenye mradi, pale pamekuwa pana tatizo kubwa sana pale mlimani. Kwa hiyo, niiombe Serikali, kwa sababu ipo siku Mheshimiwa Rais, atatamani kwenda kule, hivi watampitisha na helikopta wakati barabara ipo? Kwa hiyo, ni vema wakatutengenezea kile kipande cha kilomita kama nane hivi au kilomita tano wakaweka concrete zege pale kwenye mlima. Hii itasaidia hata magari makubwa na mitambo kupita kuelekea kule kwenye mradi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunawashukuru sana Wizara kwa namna ambavyo wanafanya kazi. Mkoa wa Dodoma hauna mito inayotiririka maji msimu mzima. Sasa hivi ukitembea huwezi kukuta mto unatiririka maji pamoja na mvua kubwa ambayo imenyesha mwaka huu. Kwa hiyo, ni rai yangu kuwaomba, hatuwezi kulima bila mabwawa. Sisi hapa ili tuweze kupata kilimo cha umwagiliaji ni rai yetu kwa Serikali ituchimbie mabwawa makubwa ambayo yatatunza maji, hayo maji tuyatumie kwa ajili ya mifugo na tuyatumie kwa ajili ya kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tumeona Eng. Mndolwa, akitupatia Eng. Salehe, tumezunguka naye Jimbo zima, ameainisha baadhi ya maeneo ambayo yanafaa kuziba tu. Kuna baadhi ya maeneo ukiziba unapata bwawa kubwa. Ni vema wataalam wetu, ukipita hii barabara kubwa ya kwenda Dar es Salaam, ukifika Mtanana na Kibaigwa Waheshimiwa Wabunge, wakati mwingine unakuta kuna kibao pale kimeandikwa taratibu maji yanakata barabara. Lile eneo mimi huwa naona ni bwawa kubwa. Ni bwawa kubwa ambalo unaweza kuziba tu ile barabara ukaihamisha ikapita sehemu nyingine ukapata bwawa kubwa Kibaigwa na ukapata maji mengi.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, wataalam wetu wakati mwingine wajielekeza kugundua maeneo ambayo unaweza ukaziba kidogo halafu ukapata maji mengi ambayo yanaweza kufaa vitu vingi. Yanaweza kufaa kufuga samaki, yanaweza kufaa humo kwa umwagiliaji, yanaweza kufaa vitu vingi hata kuongeza nguvu katika uzalishaji wa umeme.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba sana Serikali katika kuboresha kilimo, badala ya kuwatambua vijana kupitia JKT pekee yake, wapo vijana ambao hawapo JKT, lakini nao wanataka kulima, wanajibidiisha na kilimo, hawa nao tuwatambue, tuwape elimu, tuwape uzoefu na tuwape ujuzi ili waende wakafanye kazi na zaidi sana tuwape vitendea kazi. Tuwakopeshe watu matrekta ili wabadili kutoka kilimo cha mikono kwenda kwenye kilimo ambacho kinafaa. Kilimo cha treka kitatuleta mazao mengi kwa wakati mfupi, kuliko mkulima anashinda shamba anapambana kutwa nzima lakini tija ya uvunaji mazao inakuwa kidogo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja na ahsante sana. (Makofi)