Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Condester Michael Sichalwe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Momba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana wewe kwa kunipa nafasi hii adhimu ili niweze kupata nafasi ya kuchangia jioni ya leo. Mwenyezi Mungu akubariki sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nitumie nafasi kuishukuru na kuipongeza sana Serikali ya Chama Cha Mapinduzi, ambayo inaongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuonesha kwa vitendo na dhati wanawajali wakulima wa nchi hii, kwa kuwaongezea bajeti kufika shilingi trilioni 1.2. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niseme kuwa Mheshimiwa Rais ameonesha mapenzi makubwa sana kwa Watanzania kwa bajeti hii ya mkulima, kwa bajeti hii ya Mtanzania, kwa nafasi yake amemaliza kazi yake imebaki kwa watu ambao wamepewa dhamana kwa ajili ya kwenda kuitekeleza bajeti hii iweze kuleta matunda. Niwashukuru timu nzima ya Wizara ya Kilimo wakiongozwa na Mheshimiwa Hussein Bashe, tunawashukuru sana kwa miradi yote ya maendeleo ambayo wametupatia ndani ya Jimbo la Momba. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mchango wangu utajielekeza hapa. Naunga mkono michango yote ya wenzangu ambao wamechangia. Naomba nijielekeze mahali hapa. Mheshimiwa Waziri yeye mwenyewe katika mchango wake akiwa anahitimisha kule mwishoni anakiri kwamba, yapo baadhi ya maeneo ambayo wakulima wa nchi hii wanapitia changamoto. Namnukuu Mheshimiwa Waziri anasema hivi; “Ninawashukuru sana Wakulima wa nchi hii kwa kuendelea kufanya kazi katika mazingira magumu na kuendelea kulinda uchumi wa nchi yetu na usalama wa nchi yetu.” Kwa hiyo, anakiri kwamba, yapo baadhi ya mazingira magumu ambayo wakulima wa nchi hii wanapitia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika hotuba yake Mheshimiwa Waziri mwanzoni kabisa akiwa anamshukuru Mwenyezi Mungu na Mheshimiwa Rais, namnukuu Mheshimiwa Waziri Bashe anasema; “Ninamwahidi Mheshimiwa Rais na Watanzania kuwa, nitatumia uwezo wangu wote kwa uaminifu na uadilifu mkubwa kuhakikisha kuwa, kilimo kinachangia kikamilifu katika kuhakikisha usalama wa chakula na lishe nchini. Kulisha wengine kibiashara, kuongeza ajira na kuinua pato la mkulima ili kupunguza umaskini.” Kwa hiyo, pia yapo baadhi ya maeneo Mheshimiwa Waziri anakiri kwamba, bado kuna maskini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niende mahali ambapo panawafanya wakulima wafanye kazi katika mazingira magumu na Mheshimiwa Waziri anakiri kwamba, ndiyo hayo maeneo yanafanya kuwepo umaskini, mikopo kwa wakulima. Pamoja na ukubwa wa bajeti hii ambayo tunaiona, lakini niseme wakulima wadogo wadogo wa nchi hii bado hawajanufaika kikamilifu na mikopo hii, kuna urasimu mkubwa changamoto nyingi ambazo mkulima wa kawaida wa nchi hii hawezi kupata mkopo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mimi kama Mheshimiwa Mbunge ambaye natoka kijijini, niliamua kujipa jukumu mwenyewe kuunda vikundi vya wakulima kwenda nao mguu kwa mguu kwenda benki kupita Wizarani. Tumepitia changamoto nyingi, kadhia nyingi mpaka sasa hivi kuna vikundi havijapata mkopo. Kwa hiyo, nataka kumwambia nini Mheshimiwa Waziri? Naomba Mheshimiwa Waziri, anisikilize yeye ni Waziri wa wakulima na mimi ndiyo mchangiaji wa mwisho. Tunaomba bajeti hii kubwa ambayo ametuletea sisi hapa Bunge tumpitishie, tunaomba bajeti hii kwenye mikopo iwaguse wakulima wadogo wa chini, ndio ambao wanaumia katika nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, takwimu kubwa ambazo zinasomwa hapa Bungeni kuonesha kwamba wakulima wamepiga hatua ni wale wafanyabiashara wachache ambao wao wanajinasibu huko kwamba, wao ndiyo wakulima ilihali wao wamejisajili kama wakulima tu, lakini wao kazi yao kubwa ni kwenda kuchukua mazao vijijini kwa wakulima, ni kwenda kuchukua mazao kwa bibi zetu, babu zetu ambao mpaka sasa hivi wanalima kwa kutumia jembe la mkono. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hali hii haikubaliki, inaendelea kuwaumiza wakulima na watu wachache ndiyo ambao wanaendelea kunufaika ambao ni madalali wa kilimo. Ndiyo ambao wanaendelea kunufaika na ndiyo ambao wanasomwa kwenye hizi takwimu kubwa za Wizara ya Kilimo. Mimi Mheshimiwa Mbunge ambaye ninatoka kwa watu ambao ni wakulima nakiri kwa kusema zaidi ya 90% hakuna mwananchi ambaye amenufaika na mkopo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika mkopo uliwatangaza pale wadau wageni wake waliokuwa wamekuja CRDB na NMB, tunaomba wanapotoa mikopo kwa wakulima wetu watoe mikopo kwa wakati. (Makofi)

MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

SPIKA: Inatokea wapi Taarifa? Aah! Mheshimiwa Dkt. Thea Medard Ntara.
TAARIFA

MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Mbunge anayeongea sasa hivi. Sasa hivi saa 11.05 nimepokea simu kuna wafanyabiashara wananunua mahindi kwa shilingi 300 pale Peramiho.

SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, nadhani mnajua taarifa inamaanisha nini wakati wa mchango wa Mheshimiwa Mbunge, haya Mheshimiwa Mbunge.

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, napokea taarifa. Naendelea kusisitiza kwamba, wakulima wadogo hawanufaiki, madalali ndiyo wananufaika na ndiyo ambao wanasomwa kwenye hizo takwimu za Wizara ya Kilimo kuonesha kwamba wakulima wanaendelea kunufaika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, CRDB na NMB pamoja ni wadau wa maendeleo tunaomba wawape wakulima wetu mikopo kwa wakati. Wao ndiyo wanafanya wakulima waende wakakope kausha damu. Sisi katika nchi hii, msimu wa kilimo unaanza kuanzia mwezi wa Novemba, wanaenda kumpa mkulima mkopo mwezi Januari, anakuwa ameshakopa tayari kausha damu, anachukua pesa yao ndiyo anakwenda kulipa kule.

Mheshimiwa Spika, wahanga wakubwa wa kausha damu ni wananchi wa Jimbo la Momba, wanateseka sana. Mtu anakopa shilingi 100,000 anakuja kurudisha shilingi 500,000. Mheshimiwa Waziri kama ambavyo amesema amewaahidi Watanzania na Mheshimiwa Rais, kufanya kwa uaminifu na kwa uadilifu, tunaomba katika hili afanye. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni kuhusiana na lumbesa na vipimo vikubwa ambavyo vinawanyonya wakulima. Tunaomba Mheshimiwa Waziri aziandikie waraka Halmashauri zetu nchini kwa kushirikiana na Wizara husika. Jambo hili mtu yeyote ambaye ananunua kipimo kikubwa kumnyonya mkulima, achukuliwe kama mhujumu uchumi kama watu wengine tu. Mbona kuna vitu vidogo watu wanafanya wanachukuliwa hatua? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wakulima wanaendelea kuumia, utakuta ni viazi, gunia linapaswa kuwa kilo 80 mtu anachukua kilo 200 na analipa shilingi 30,000. Kwa mfano, kule kwetu Momba gunia la mpunga linapaswa liwe kilo 100, anaenda kuchukua kilo 250, halafu analipa shilingi 40,000. Huu ni unyonyaji uliopitiliza, ni uuaji na ni wizi kama wezi wengine tu ambao wanaiba huko mtaani. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri, uadilifu na uamini wake ambao amewaahidi Watanzania hapa, tunaomba kuuona. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusu mbolea, mimi ni Mbunge ninayetoka Jimbo ambalo lipo mpakani. Kule Momba tuna Tarafa tatu, tuna Tarafa ya Ndalambo, tarafa hii ipo barabarani na ndiyo Tarafa ambayo inapakana na Zambia. Mawakala wake wote ambao anawatuma wanaishia kuuza mbolea pale kwa sababu wanataka kushirikiana na wafanyabiashara wezi ambao wanavusha mbolea kupeleka Zambia. Katika hili Mheshimiwa Waziri, Ofisi yake inajua vizuri sana namna ambavyo wapo watu wasiokuwa waaminifu wanauza mbolea Zambia. Mheshimiwa Naibu Waziri yupo hapo, analijua sana hili sitaki kuongelea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kipindi kile walijitahidi kwamba, sijui wamechukua hatua, hakuna lolote sasa hivi wamebadilisha mfumo, lakini mbolea kwenda Zambia inaenda. Takwimu zinakuja kubwa, watu wa Mkoa wa Songwe wameingia kwenye orodha kubwa ya kuonekana ni watu ambao wanalima sana kwa kutumia mbolea. Tarafa ya Kamsamba yenye Kata sita za Ivuna, Mkomba, Mkulwe na Chilulumo hawajawahi kupata mbolea. Tarafa nzima ya Msangano ambao ndiyo wanaongoza kwa kulima mpunga pamoja na Chitete kuna skimu ya umwagiliaji hawana mbolea. Mbolea inaenda wapi kwenye takwimu inaonekana ni kubwa, kwamba tumetumia mbolea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunaomba uendelee kuongeza ujuzi wa namna ya kumsaidia mkulima wa kawaida ambaye anaumia, mpaka sasa hivi anayeumia ni mkulima wa kawaida, naamini hata majimbo mengine wenzangu wameongea hapa kwamba, mbolea zinaishia mijini hazifiki vijijini, mkulima wa kawaida na mdogo yupo kijijini hayupo mjini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na masoko Mheshimiwa Waziri bado Wizara yake haijalitendea kikamilifu Soko la DRC - Congo. Soko la DRC Congo, Nchi ya Tanzania hatujalitendea haki hata kidogo, Mheshimiwa Waziri anajua ni kwa kiasi gani ambavyo kuna maghala yalifunguliwa kule yameishia wapi? Huwezi kuwa unaenda kuuza mchele na unga DRC, unatoa unga Iringa, unatoa unga Mwanza katika uchumi, hizo ni biashara gani si utapata hasara? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumeshaiambia Wizara na taasisi yake wanaohusika tumewapa eneo pale Kakozi, ambapo watapata malighafi kwa bei rahisi, mahindi ya kutosha kutoka kwa watu wa Rukwa, watapata mahindi ya kutosha ndani ya Jimbo la Momba lenyewe, kwamba watengeneze kiwanda pale wasindike unga, watengeneze mchele wakauze DRC. Wazambia wanaishia kuchukua mchele wetu wana-brand wanaenda kuuza Congo. Bado hatujaweza kumsaidia mkulima kwenye masoko. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, as we are speaking now, ndani ya Jimbo letu, mahindi sasa hivi yananunuliwa shilingi 35,000 mpaka shilingi 40,000, lakini kama kungekuwa kuna soko zuri, wamefungua kiwanda pale wanasindika, naamini wakulima wengi wangeenda kuuza mazao pale. Hata wale wachuuzi wanaoenda wangenunua vizuri, kwa sababu demand ingekuwa high, kwa vyovyote vile price ingeweza ku-shoot. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na suala la BBT. Mheshimiwa Waziri wazo lake lilikuwa ni jema, lakini jambo hili tunaomba akalifanye jambo hili la BBT kwenye maeneo yetu locally. Hata hayo mashamba ambayo anawatafutia vijana anawapa, mengine yangetumika mashamba yao wao wenyewe. Kwa hiyo, hata gharama za kuendesha hiyo programu ingekuwa chini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wapo kule vijana wanataka kuwezeshwa wapate mbegu na mbolea. Wangefanya hilo zoezi wangesaidia vijana wengi wa Kitanzania. Hatusemi vijana wa Kitanzania wabaguliwe kusaidiwa, la hasha! Vipo vipaumbele, kama hiyo mikoa wanaitambua kwamba inaongoza kwa kuzalisha chakula, tunataka nguvu itumike huko wazalishe ili waweze kuleta tija kwenye nchi hii. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Mheshimiwa Condester kengele ya pili imeshagonga. Sekunde 30 malizia.

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, sekunde 30. Mkoa mzima wa Songwe zaidi ya 70% tunatumia mbegu kutoka Zambia. Shida ipo wapi kwa watu wa Waziri wa utafiti wa TARI na watu wa mbegu? Kwa nini mbegu za kutoka kwenye nchi yetu zisifanywe kwenye Mkoa wa Songwe? Waziri ana kazi ya kufanya, otherwise naunga mkono hoja ya bajeti yake. (Makofi)