Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tumekuwa tukizungumza sana umuhimu wa kuwa na Uwanja wa Ndege wa Serengeti na Serikali imeahidi mara kadhaa. Mbuga ya Serengeti ni moja kati ya mbuga maarufu sana duniani na imekuwa ikichangia pato kubwa sana kwenye pato la Taifa, lakini napenda kukwambia wewe na Bunge lako Tukufu, wakati wa high season ndege ambazo zinatua kwa siku Hifadhi ya Serengeti ni takribani 200. Ndege hizi zinakuwa na pollution kwa maana ya air pollution na noise pollution ambazo zina-affect ekolojia ya Hifadhi ya Serengeti. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii inachagiza kuona umuhimu wa kujenga Uwanja wa Serengeti pale Mugumu. Nchi jirani tu wana miundombinu wezeshi ambayo wameweka, watalii wanatua Nchi jirani ya Kenya, wanatoka Nairobi wanakuja mpaka Migori wanachukuwa magari kuvuka kuja Mbuga ya Serengeti ambayo hata miundombinu ya barabara siyo rafiki na wale ambao walikuwa wametua KIA pia kutoka Kilimanjaro kule kuja mpaka Mbuga ya Serengeti, ni mbali na miundombinu ya barabara siyo rafiki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapoteza mapato mengi sana. Sasa nikataka nijue mkakati wa Serikali wa kuhakikisha inajenga Uwanja wa Ndege wa Serengeti ambao utakuza uchumi, utakuza na kuendeleza uhifadhi kwa kutoku-affect wale wanyama na ndege kwa ekolojia hiyo ambayo nimeieleza. Pia utarahisisha usafirishaji na usafiri kwa watu ambao wanazunguka kwa upande wa Magharibi, kwa maana ya Mkoa wa Simiyu na Mara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Uwanja huu wa Ndege wa Serengeti ukikamilika na tukizingatia mipango ambayo tupo nayo sasa hivi, ambao tuna mpango mkakati wa kujenga mji wa kisasa wa Mugumu ambao utatoa huduma bora kabisa. Tunaomba Serikali kwa dhamira ya dhati ya Mheshimiwa Rais ya kukuza uchumi uwanja huu wa ndege uweze kukamilika lakini pia Uwanja wa Ndege wa Musoma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Mara ndipo Baba wa Taifa anatoka. Uwanja wa Ndege wa Musoma kila wakati wanauweka kwenye bajeti, unaenda kwa kusuasua. Ulikuwa ukamilike mwaka jana Desemba 2023, hadi sasa hivi hata 60% hazijafika. Tunaomba sana, ni aibu anapotoka Baba wa Taifa, pale kuna kaburi la Baba wa Taifa, watu wakienda kuzuru, inatakiwa wafike Mwanza ndiyo wa-drive kuja kwa Baba wa Taifa, haiwezekani, ni aibu sana. Tunaomba wampe heshima, uwanja huu ukamilike, tuwe na ndege zinazotua kila siku pale Musoma ili pia tuuenzi uwepo wa Baba yetu wa Taifa na kukuza uchumi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pale Musoma tuna mazalia ya Ziwa Victoria, hata ndege za mizigo zikifika pale zitasafirisha. Uchumi wa Mkoa wetu utakua, lakini sasa hivi hatuna ndege ambayo inatua pale. Pia Mkoa wa Mara tunalima mbogamboga na matunda na ndege wamenunua ambazo zinaweza kusafirisha kitu ambacho ni perishable kutoka kule kufika huku. Kwa hiyo tunaomba sana Serikali iweze kukamilisha. Wamemwongezea mkandarasi mwaka mmoja, tunahitaji ule Uwanja wa Ndege wa Musoma ukamilike within time, usiwe na extension nyingine yoyote ili tuweze kuwa na usafiri wa uhakika. Hata wananchi wanaokaa Mwanza ku-drive mpaka Mwanza ili waweze kupata usafiri si haki. Tuweze kukamilishiwa uwanja huu ili wananchi waweze kusafiri kirahisi na pia kwenda kuzuru pale kwa Baba wa Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tuliomba hapa Kivuko cha MV Musoma, wametupatia ila tunaomba watujengee miundombinu ya abiria kukaa upande wa Kinesi ambao una tarafa mbili ambazo wanatumia usafiri wa maji. Wana Tarafa wa Suba ambayo ina kata tano na Tarafa ya Luo-Imbo ambayo ina kata tatu. Hawa wananchi wanapata adha, pale kuna kakibanda tu upande wa Kinesi. Tunaomba waanze ujenzi wa jengo la kusubiriaabiria, kama ambavyo wameanza Musoma Mjini ili sasa hiki Kivuko cha MV Musoma kiweze kuwa na maana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia nimesema ndege zinatua Migori kule. Pale Tarime tuna air strip tu ambazo zipo chini ya halmashauri. Sasa Serikali iangalie kwa kushirikiana, either ipandishe ule uwanja maana sasa hivi zile air strip pamoja na kwamba zinatua ndege mbili, tatu, tano au kumi kwa siku, lakini zile za Migori wenyewe wameweka lami ndege zinatua. Wakati wanasubiria kujenga uwanja wa Serengeti wapandishe hadhi ule Uwanja wa Tarime ili walau waweke lami zile air strips ili ndege ziweze kutua pale, kutoka Tarime kwenda Serengeti ni pafupi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tuna dhamira ya dhati ya kukuza Uchumi, lazima tuwekeze kwenye miundombinu ya hivyo viwanja ambavyo nimevitaja ili kuweza kusaidia utalii kukua Mara na kuweza kusaidia wananchi waweze kusafirisha mazao yao yatokanayo na samaki kuliko kuhangaika na kupunguza gharama ambazo zipo sasa hivi. Tukizingatia hayo yote kwa kweli tutaenda kukuza uchumi wetu na utalii wetu utakua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumalizia hapa, ahsante. (Makofi)