Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa fursa ya kuchangia Bajeti ya Wizara hii ya Uchukuzi. Nami napenda kuanza kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa wa tija ambao umefanyika kwenye sekta hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kurejea tarehe 17 Novemba, 2022, niliiomba Serikali ichukulie kwa uzito mkubwa suala la uboreshaji wa airport yetu ya Bukoba Mjini ikiwemo na kutujengea airport mpya ya Kajunguti. Mnamo tarehe 19 Novemba, mwaka huo huo 2022 Serikali ilikiri kwamba airport yetu ya Bukoba Mjini ina mapungufu na itafanya uwekezaji kwa ajili ya kuboresha pamoja na kuanza taratibu za kujenga airport mpya ya Kajunguti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe 24 Juni, 2023 kwa maana ya mwaka jana, nilisimama hapa Bungeni nikikumbushia lini airport yetu ya Bukoba Mjini itajengewa control tower, jambo ambalo nilipata ahadi kutoka Serikalini kwamba itafanya, lakini isivyo bahati kwenye bajeti ya 2023/2024 haikufanyika hivyo. Halikadhalika tarehe 6 Februari, 2024 nilikumbushia tena hapa Bungeni kupata uhakika kutoka kwa Serikali, kwamba ni lini Serikali itaanza mpango wa kutujengea Airport mpya Kajunguti iliyopo Wilayani Missenyi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe 15 Mei, 2024, kupitia Ripoti ya CAG alikiri yeye mwenyewe kupitia tafiti aliyoifanya kwamba airport yetu ya Bukoba Mjini inahitaji uboreshaji wa haraka, kwa sababu ndege zinazotua Bukoba, rubani anapata maelekezo kwa kutumia simu kupitia control tower ya Mwanza na siyo ya Bukoba. Jambo ambalo ni kinyume na sheria na kuhatarisha maisha ya abiria. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kipekee sana naomba niishukuru Serikali chini ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan na nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri, Profesa Mbarawa; Mheshimiwa Naibu Waziri, Kihenzile pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Masuala ya Ndege (TAA), kaka yangu Mussa kwa kazi kubwa ambayo amefanya na kwa ushirikiano mkubwa ambao ameendelea kunipa kwa kipindi chote hiki tokea tarehe 17 Novemba, 2022 mpaka hivi leo ambapo nimekuwa nikiendelea kufuatilia uboreshaji wa Airport yetu ya Bukoba Mjini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa furaha kubwa sana nimefarijika kuona katika Bajeti hii ya Mwaka wa Fedha 2024/2025, Airport yetu ya Bukoba Mjini inakwenda kufanyiwa uboreshaji. Kupitia katika uboreshaji huo tunakwenda kujengewa control tower Airport ya Bukoba Mjini. Hali kadhalika tunakwenda kuwekewa taa za kuongoza ndege katika Airport yetu ya Bukoba Mjini kwa maana ya Airport Ground Light (AGL). Vilevile tunakwenda kuwekewa vifaa ambavyo vitamwezesha na kumwongoza rubani kuweza kutua katika airport yetu kwa maana ya instrument landing system. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya wananchi wa Bukoba pamoja na Mkoa mzima wa Kagera, napenda kutoa shukrani zangu za dhati kabisa kuona namna ambavyo Serikali yetu sikivu chini ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, inapokea maoni ya Wabunge na inayafanyia kazi kama ambavyo tunaona sasa kwenye Bajeti ya 2024/2025, jambo hili linakwenda kufanyiwa kazi na airport yetu inakwenda kuboreshwa. Kupitia uamuzi huo na namna ambavyo Serikali inafanyia kazi mawazo yetu Wabunge, inatupa sisi nguvu na kutuwezesha kuendelea kuishauri Serikali kwa tija, kwa maslahi mapana ya maendeleo ya maeneo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi hizi naomba pia kuishukuru sana Serikali, nimeona katika Taarifa hii ya Bajeti ya Wizara kwamba Wizara imetenga bajeti kwa ajili ya kufanya tathmini katika eneo la kujenga airport ya Kajunguti katika Bajeti hii ya Mwaka wa Fedha 2024/2025. Nimwombe sana Mheshimiwa Profesa Mbarawa atakapohitimisha hoja yake, atueleze bayana hii bajeti iliyotengwa ni kwa ajili ya tathmini tu au pamoja na kuanza mchakato wa kulipa fidia? Maana miaka iliyopita tayari airport ilishafanyiwa tathmini na bajeti ilishajulikana kwamba ni takribani bilioni tisa za fidia. Hivyo nimwombe sana Mheshimiwa Profesa Mbarawa…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante.
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: …atakapohitimisha hoja yake atueleze kinagaubaga nini kinakwenda kufanyika kuhusu airport mpya, maana Mkoa wetu wa Kagera unaweza kuwa economic hub kwa ajili ya Afrika Mashariki. Ahsante. (Makofi)