Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Handeni Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kuwa mchangiaji wa kwanza mchana huu kwenye mjadala huu wa Wizara ya Uchukuzi. Natumia nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa sababu anakwenda kuingia kwenye historia ya nchi hii kama Mheshimiwa Rais ambaye alifanya mapinduzi makubwa kwenye eneo la reli. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Serikali ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, inatarajia kutengeneza mtandao wa reli ya kisasa (SGR), unaokaribia kilometa 4,572, hivi sasa mtandao huu wa SGR ambao tunaupambania kwenye central corridor kwa kazi zinazoendelea za kilometa takribani 2,102. Mradi wote huu utagharimu karibu trilioni 20 na sehemu na tayari Serikali ya CCM imekwishalipa trilioni 10 na zaidi kwa ajili ya kazi ambazo zimeshakamilika. Yapo mambo machache ambayo lazima tuyaboreshe wakati tukikaribia kuanza kwa operations za treni ya SGR kutokea Dar es Salaam mpaka Makutupora, wakati huohuo tukiendelea kukamilisha vipande vingine vilivyobaki, haya mambo lazima yaende sambamba na ujenzi wa reli kadri inavyoendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala la kwanza, lazima tuufanye usafiri huu kuwa usafiri wa kisasa, tufanye usafirishaji wa kisasa na njia pekee ya kufanya SGR kuwa usafiri wa kisasa na kufanya usafirishaji wa kisasa ni kuifungamanisha SGR na miundombinu mingine ya usafiri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, zipo taasisi ambazo lazima zifanye kazi usiku na mchana na sisi kama Bunge hapa lazima tulione hili na kwenye bajeti zetu tujaribu kulipa majawabu. Kwa mfano, TANROADS, TARURA, Halmashauri za Miji, ambako reli inapita vilevile bandari, kwenye reli inakopita viko vituo vya SGR ambako ndiyo abiria watakuwa wanashuka na kupakiliwa, ambako ndiyo mizigo itakuwa inashushwa na kupakiliwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, barabara ambazo zinakwenda kwenye vituo hivi vya SGR lazima tuzijenge kwa kiwango hiki cha mradi huu mkubwa wa kitaifa ambao tunajivunia kuwa nao na ambao haupo Afrika Mashariki wala Nchi za Maziwa Makuu na Kusini mwa Afrika, lazima barabara hizi zikajengwe kwa kiwango cha lami. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nitatolea mifano ya vituo kama vitatu hivi ambavyo viko alongside, ambavyo vinajengwa kwa ajili ya kushusha abiria. Kwa mfano, Kituo cha Morogoro, ni lazima kwenye kituo kile cha Morogoro, kwanza tuwe na barabara nzuri ya kufika kwenye kituo ijengwe kwa kiwango cha lami. Pia tujenge miundombinu ya mabasi ili watu wanaoshuka waweze kupanda kwenye usafiri kutoka pale kwenda usafiri mwingine. Vivyo hivyo, kituo cha Kilosa na vituo vingine kama ilivyo pale Ngerengere. Kipande cha barabara kutoka Ngerengere kituo kilipo kwenda barabara kubwa kilometa 16 tupige lami pale, huu mradi lazima tuufananishe na thamani yake ilivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hauwezi ukawa na mradi kama huu halafu kesho tuje tukutane hapa tunajadili fedha za dharura za TARURA kwamba njia ya kwenda SGR haipitiki! Hilo ni jambo la msingi sana lazima tulifanye. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vilevile, wenzetu wa sekta mbalimbali za uzalishaji, lazima SGR tuifungamanishe na Sekta za Uzalishaji kama Kilimo, Mifugo, Madini, Utalii na Viwanda. Tusijenge SGR hii tukitazama mizigo ya nchi jirani peke yake, lazima sisi wenyewe tuishibishe mzigo alongside the way. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri wa Viwanda, Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, Mheshimiwa Waziri wa Madini na Wizara ya Utalii, lazima wakae chini na kuona wataifanyia nini SGR hii ambayo Watanzania tunaweka fedha nyingi. Kila mmoja kwa nafasi yake awaze na aweke mipango ya kuhakikisha kwamba treni yetu hii ya kisasa inapata mzigo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, uwezo wa treni hii kwa mwaka minimum itakuwa na uwezo wa kusafirisha tani milioni 17 na ukibeba maximum itakuwa na uwezo wa kusafirisha tani milioni 25 kwa mwaka. Sasa kama hatukuweka mikakati katika maeneo ya uzalishaji kule inakopita, tutashindwa kuipatia mzigo wa kutosha treni hii na mradi wetu utaishia kuwa a white elephant. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo lingine la kurekebisha na kuwekea mkazo ni uhusiano wa ujenzi wa SGR pamoja na utunzaji wa mazingira. Kwenye ujenzi kuna kitu kinaitwa hard part engineering design, ndiyo hiki ambacho tunaangalia environment impact assessment halafu watu wanajenga reli. Kitu muhimu katika miundombinu ya reli katika dunia ya leo ni soft part engineering design ambayo inahusiana na namna gani tutayatunza mazingira na kuutunza huu mradi ili udumu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nitawatolea mfano, mwaka 2012 pale katikati ya Munisagara na Kilosa, kwenye reli yetu hii ya zamani ya MGR palijengwa daraja pale miaka kama 12 iliyopita. Wakati daraja lile likijengwa, kutoka pale daraja lilipo, kushuka maji ya mto yanapofika ilikuwa ni mita karibu 20. Leo ukienda pale kumefanyika siltation, udongo umetoka milimani, umeshuka kwenye mto, mto umejaa tope na distance ya maji pale imebakia kilometa tatu tu, which means ikinyesha mvua kubwa, lazima maji yata-flood pale, tusiruhusu hiyo ikatokea kwa SGR. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lazima tuweke sera madhubuti za kimazingira na tuweke mpango mzuri wa kulinda miundombinu hii ya SGR, ikiwezekana tuwe na asilimia fulani ambayo inakatwa kutokana na mapato ya SGR iende ikasimamie mazingira ili mradi wetu uweze kudumu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuhusu ukarabati wa Reli ya Ruvu – Tanga na Tanga – Arusha. Reli hii ndiyo reli pekee ambayo iko kwenye Mikoa ya Kaskazini, kwa maana ya Tanga, Arusha, Manyara na Kilimanjaro. Pia, ni reli ambayo imebeba uchumi mkubwa. Ruvu – Tanga (kilometa 268) na Tanga – Arusha (kilometa 438) lakini Serikali haiifanyii ukarabati reli hii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tuna viwanda vya simenti Tanga na ambavyo ukitumia reli kusafirisha simenti, you cut your cost of transportation kwa karibu 40%. Tungeikarabati reli hii leo tusingekuwa tunalia na bei kubwa ya simenti. Ni jambo la ajabu sana, eti ikifika Christmas watu wanaanza kukarabati reli ya kaskazini. Hii ni reli ya mizigo, siyo ya kupeleka watu Christmas. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Spika, tumefanya uwekezaji mkubwa Bandari ya Tanga na sasa tunajenga gati namba tatu pale kwa ajili ya makasha ya kontena, sasa tutayaondoaje haya kama hatukarabati reli hii? Vilevile, tukiikarabati hii reli, ndiyo itatumika kama feeder ya mzigo kwenye SGR. Itakuwa rahisi mzigo kutoka Bandari ya Tanga na ukafika kwenye Bandari ya Kwala kwa urahisi kwa kutumia reli hii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kinachotakiwa hapa ni tukayaimarishe madaraja yaweze kubeba mzigo mkubwa, vilevile, tukaondoe reli ambazo zimechakaa, yale mataluma na tuweke mengine. Kwa kufanya hivyo reli yetu itaweza kutembea angalau kwa speed ya 60 kilometa kwa saa. Hivi sasa inatembea kilometa 20 kwa saa, inatumia masaa 10 mpaka 12 kutoka Tanga kuja Dar es Salaam. Hiki ni kitu cha ajabu kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala la mwisho, bandari yetu kwa maana ya watu wetu wa TPA ni lazima tuwawezeshe. Iko sheria tulitunga hapa, inaitwa The Treasurer Registrar Powers and Functions, ambayo ni Act, Cap. 370. Sheria hii inawapa Hazina kupitia Msajili wa Mashirika, uwezo wa kutoza makusanyo kutoka kwenye mapato ghafi kwenye makampuni na mashirika ya umma 15%, kana kwamba haitoshi kwa mapato ya ziada anapewa Msajili wa Hazina kutoza tena 70%. Hii 15% ya mapato ghafi na 70% ya mapato ya ziada yalikuwa yanatosha kabisa kwa Serikali kuchukua mapato kutoka kwenye mashirika haya.
Mheshimiwa Spika, wharfage wawaachie watu wa bandari, wakusanye wenyewe, lengo watengeneze balance sheet zao vizuri, wakiwa na balance sheet nzuri wataweza kukopa na kuendeleza gati mbalimbali. Kwa kufanya hivyo watakuwa wanawapunguzia mzigo Serikali. (Makofi)
SPIKA: Ahsante sana, kengele ya pili imeshagonga.
MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)