Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mufindi Kusini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuwa mchangiaji wa eneo hili la Wizara yetu ya Uchukuzi. Kwanza na-declare interest kwamba, mimi ni mfanyabiashara wa usafirishaji kwa hiyo, leo nitajikita sana kwenye usafirishaji.
Mheshimiwa Spika, nimeona Wabunge wengi wanazungumzia habari ya ndege, reli na viwanja vya ndege, nataka niseme kwamba, hivi vyote tunavyovizungumza kwa sasa tunaweza tukaviona kwa kuwa, tuko kwenye wakati mzuri na tunaenda vizuri, lakini vinaweza visichukue muda vikawa historia. Ndege zikawa history, treni zikawa history na kila kitu kikawa history. Nimewahi kuzungumza kwamba, Shirika la Ndege na Shirika la Reli yaachiwe uhuru yajiendeshe kibiashara, ili yaweze kujiendesha, lakini naona hilo halipo.
Mheshimiwa Spika, niko kwenye Kamati ya Miundombinu. Shirika la Reli kwenye upande wa abiria kwa miaka mitatu limepata hasara ya shilingi bilioni 25. Ukiangalia hiyo hasara yenyewe siyo kwamba, limeipata kwa sababu kuna uongozi mbaya, hapana, ni simple tu, kuna mamlaka nyingine na Serikali yenyewe inachangia kuingilia uendeshaji wa shirika. Kwa hiyo, ukiangalia kwa mtazamo wa juu au wa nje unaweza ukajua labda waliomo mle siyo wafanyakazi wazuri, lakini ni kwa sababu ya uingiliaji, hawajipangii mambo yao, mambo mengine wanapangiwa kwa hiyo, mwisho wake wanapata hasara.
Mheshimiwa Spika, naona Wabunge wengi wanaongelea viwanja vya ndege. Morogoro kuna Mikumi sasa hivi wazungu wengi wanatua. Yule ndugu yangu Mussa Mbura, Mkurugenzi wa Viwanja vya Ndege, anafanya kazi nzuri sana. Ni kijana mchapakazi na anafanya kazi nzuri sana. Naomba aangalie pale Morogoro, sasa hivi wana-assemble ndege, hata Wabunge wakitaka ndege pale zinauzwa za watu wawili, watapakiana na mkewe, wanakaa huku nyuma, ziko pale Airport ya Morogoro. Kwa hiyo, tunaomba uwanja wa ndege, siyo tu wanapeleka Njombe, maana nimesikia Njombe unakwenda uwanja. Sasa jamani Morogoro hakuna uwanja, naomba uwanja. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa najikita kwenye eneo la usafirishaji. Juzi bodaboda wamekuja kwangu wanalalamika, najua Mkurugenzi wa LATRA pamoja na wafanyakazi wengi ni wapya, lakini naomba wasichukue mawazo yaliyopita ya wale waliowatangulia. Wakichukua mawazo ya waliotangulia wanaleta mizozo, kazi ya LATRA ni kusimamia udhibiti wa nchi kavu. Tukizungumza hivyo ina maana tuna maguta, bodaboda, magari, treni na kila kitu.
Mheshimiwa Spika, leo hii nimeona pale Gairo LATRA wanachukua kwa bodaboda shilingi 17,000 kwa mwaka. Hata hivyo, ukiangalia hawawapangii route, route anatafuta mwenyewe, usiku kucha anahangaika yeye mwenyewe, wao wanachukua shilingi 17,000 tena pamoja na polisi, lakini ukiangalia hawawasaidii chochote. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hivi ngoja niwaulize, wao wameshindwa kuiambia Serikali na kuitetea taasisi yao kwamba, leseni ya bodaboda ya kuendesha pikipiki ni shilingi 70,000 ili apate leseni ni lazima aende chuo akasome kwa shilingi 50,000 kwa hiyo, bodaboda alipe shilingi 110,000 ndiyo apate leseni? Halafu dereva wa basi na dereva wa lori naye hivyo hivyo, kwa hiyo, gari la miguu minne na ile pikipiki ya miguu miwili thamani ya leseni yake ni moja shilingi 70,000, inawezekana wapi hii? Hiki ni kitu ambacho hakiwezekani. Mheshimiwa Waziri wa Fedha yuko hapa, hivi ni kweli wanachukua shilingi 70,000 kwa dereva wa basi, dereva wa lori na kwenye bodaboda?
Mheshimiwa Spika, mpaka leo 95% ya madereva wa bodaboda hawana leseni, kwa hiyo, wanakosa mapato kwa sababu, wanatunga sheria na utaratibu ambao hautekelezeki. Bodaboda alitakiwa leseni yake isizidi shilingi 25,000 au shilingi 30,000. Ndiyo maana Waheshimiwa Wabunge waliona hapa na wakaishauri Wizara ya Mambo ya Ndani ikakubali kwamba, faini ya gari ni shilingi 30,000, lakini faini ya bodaboda ni shilingi 10,000. Leo wanafurahia kumgonga bodaboda leseni shilingi 70,000 na aende akasome kwa shilingi 50,000, lakini wamesahau kwamba, wanakosa mapato, wanawapa tu shida polisi ya kuwakamata kila siku. 95% ya bodaboda hawana leseni, kwa hiyo, naomba walifikirie hilo, washushe, wasiweke sheria ambayo watu wataivunja. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ukiweka kiasi kikubwa mtu anavunja sheria kwa sababu, hana hicho kiasi halafu unamwambia mpaka akasome. Nasema hapa kama kuna asilimia tano ya bodaboda wamesoma, wenye vyeti, najiuzulu Ubunge. Wanaenda wanawahonga wale wenye vyuo wanawapa shilingi 50,000 anaandika cheti na jamaa hajasoma chochote. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tuna polisi kata, ma-inspector, IGP amewaweka kila kata. Kwa nini wasiwatumie hawa watoe semina na vibali watu wapewe leseni, kuliko kwenda kusumbua watu kwa kutumia hizo shilingi 50,000? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kitu kingine, LATRA wasiwe TRA. Wasiwe wanapanga mbinu za kupata pesa tu, kwenye bodaboda wachukue shilingi 17000, kwenye mabasi wanakataa wapiga debe wa stendi, halafu LATRA wanaingia wanakuwa wapiga debe wa mtandao. Sasa sielewi hapa, maana wameongeza nauli shilingi 3000, halafu gari likitoka Bukoba mpaka Dar es Salaam wanachukua shilingi 3000, tena wanapiga juu kwa juu kwenye ile tiketi mtandao. Wanakata hela wanasema huyu agent wa tiketi mtandao (vender) amechukua, lakini yule vender hana shida ya aina yoyote. Basi, wamuunganishe vender na TRA, lakini vender hana shida kwa sababu, anachukua shilingi 200 tu. Unakuta kwenye basi abiria mmoja anachukuliwa shilingi 3000 na inakatwa juu kwa juu kwenye tiketi mtandao, sasa hawa wamekuwa TRA badala ya kudhibiti watu? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, waangalie bodaboda, kuna dada yangu mmoja pale amesema wawaangalie bodaboda wawape semina. Sasa wao wamekuwa wakusanya mapato tu. Kitu kama hicho hakiwezekani! Ni lazima wajitafakari, hasa Mkurugenzi mpya, asije akaleta mzozo wa watu wenye mabasi wakagoma halafu baadaye akaanza, maana siku hizi kuna tabia ambayo imeanza hasa kwa wenzetu wa huko mbele, watu wakigoma unasikia wanampinga mama, wanawapakazia, wanampinga mama. Wao ndiyo wanaoleta sheria na vitu ambavyo havitekelezeki, watu wakigoma au wakifanya hivi kwenye haki zao za msingi unasikia hawa wanampinga mama. Wao ndiyo wanaompinga mama, wanaweka mavitu ya hovyo hovyo. Wao ni wapingaji wa mama. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nataka hata mama anisikie huko aliko kwamba, wapingaji wako kwake na taasisi zake. Hawa ndiyo wapingaji wakuu, wanaweka vitu ambavyo havitekelezeki. Huo ndio ukweli, maana sasa hivi kila mtu anataka akusanye pesa ili azitwange. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, semeni tu leo, Bunge tuamue hapa, pesa zote, taasisi zote na hizi authority zote, mamlaka zote zinazokusanya pesa ziingie kwanza Benki Kuu halafu wapewe kidogo kidogo, kama tutaona hizi sheria zinakuja. Sasa hivi si anakusanya halafu anapanga plan za kutandika. Sisi Wabunge hapa ndio tukipata vimshahara kidogo watu wanapiga kelele eeh! eeh! Eeh! hela yenyewe iko wapi? Watu wanatangwa huku hela siyo mchezo. Huo ndio ukweli. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa sababu, hizi sheria zote zinazoletwa zilikuja mwaka 2019 kwenye Awamu ya Tano. Watu walitaka kugoma, tumshukuru Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa, aliwaita wasafirishaji wote na haya yote yakafutwa, yakatulia. Sasa wamemwona mama amekuja wanaanza, ukiangalia kila taasisi wanaanza kuleta vichokonoko-chokonoko. Labda sijui ni kwa sababu, wanamwona mama ni mpole au mama hajui, mama anafahamu. Sisi ndiyo tunamwambia hapa kwenye spika ili atusikie.
Mheshimiwa Spika, Waziri Mkuu aliliondoa watu wakatulia. Walikuwa wanataka kugoma, Waziri Mkuu akatuliza mgomo. Sasa tena wameyarudisha yale yale ambayo Waziri Mkuu aliyamaliza. Sasa, sijui ni nani mkubwa kati ya Waziri Mkuu na wao? Naomba wajitafakari kwa kina.
Mheshimiwa Spika, ukiangalia basi, maana mimi ni mfanyabiashara wa mabasi na nisipozungumza mambo ya mabasi halafu nimo humu ndani, basi nitakuwa mwendawazimu. Kwenye basi LATRA wanatoa license kwa shilingi 180,000 halafu kwenye tiketi wana-charge tena pesa kwa kila abiria. Ukija kwenye malori ni shilingi 180,000, lakini kwenye mzigo hawa-charge pesa kwa sababu, ule mzigo wakati mwingine si unalipwa baada ya mwezi, ila huku kuna cash wanaipata chap chap ndiyo maana kila siku wanatamani wakusanye ile pesa. Sasa hiyo siyo haki.
Mheshimiwa Spika, ukiangalia lori linapewa exemption. Unaweza ukaingiza lori ukalipa shilingi milioni 15, ukiingiza basi moja jipya, ushuru wa TRA peke yake bila wharfage na bila port charge ni shilingi shilingi milioni 102. Ushuru peke yake kwa basi moja ni shilingi milioni 102, halipati exemption wala halipati chochote. Sasa wajitafakari kwenye hilo.
Mheshimiwa Spika, lingine wajitafakari kwenye school bus. Mabasi ya shule ni mabovu, madereva ni wabovu, wao wameng’ang’ania tu kwenye pesa. Juzi hapa Arusha yameua, sasa ni mara ya pili, Dar es Salaam huko ni kila siku, kila sehemu.
Mheshimiwa Spika, ukipishana na vile vibasi kinaenda upande, dereva mwenyewe kasuka rasta, yaani yule dereva hata haeleweki anatoka wapi, lakini sijawahi kusikia LATRA wanasimamia habari ya abiria wa school bus, wameng’ang’ania tu kwenye sehemu wanazopata pesa. Kule kwenye sehemu ambazo hakuna pesa wao hawapo. Dereva wa basi haendeshi mpaka apimwe kama amelewa na aweke fingerprint kwamba ametambulika, kwenye mabasi wanafanyaje?
Mheshimiwa Spika, kwanza, Sheria ya Mabasi yanayosafirisha duniani watoto wadogo wa chekechea ni haya? Sheria ya Mabasi yoyote inayosafirisha watoto wadogo wa chekechekea lazima iwe na pua mbele engine inakaa mbele dereva anakaa nyuma ili hata ikitokea kugonga inaumia ile engine kule mbele, abiria huku wanakuwa salama lakini sasa hivi dereva yupo hapa na mtoto naye chezacheza anachungulia nje hata akigonga ng’ombe mtoto anaumia. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa…
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Spika, hata mkiingia kwenye google hapo…
SPIKA: Mheshimiwa Shabiby, kengele ya pili imeshagonga.
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Spika, mimi si ndio mtu wa mwisho au bado? Mama inatosha. Ahsante sana na naunga mkono hoja. (Makofi/Kicheko)