Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mufindi Kusini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa fursa anayotujalia ya uhai pamoja na afya njema. Nitumie nafasi hii kwa sababu ni mara yangu ya kwanza kusimama kwenye bajeti kama hii kumshukuru Mheshimiwa Rais wetu kwa imani yake kubwa ya kuniteua na kuniamini kwa nafasi ya Naibu Waziri. Ahadi yangu wakati wote ni unyenyekevu, utii na kumsaidia kwa kadiri ya maelekezo yake. Pia nimshukuru Makamu wa Rais, Waziri Mkuu na Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu kama viongozi wetu wakubwa kwenye nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kipekee nimshukuru Mheshimiwa Waziri wangu, Profesa Makame Mbarawa, Mheshimiwa Waziri amekuwa ni baba, amekuwa ni mlezi, amenipokea, ananifundisha na ananivumilia. Kiongozi huyu mnyenyekevu, mpole na msomi wa daraja la juu ameendelea kuwa mwalimu wetu sote katika Wizara yetu kwa kutupa miongozo na maelekezo ya Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nikushukuru sana wewe umekuwa kiongozi wangu mkuu nilipokuwa Mwenyekiti wako wa Kamati na Mwenyekiti wa Bunge, umenifundisha wakati wote na kunielekeza.
Mheshimiwa Spika, naishukuru Kamati yangu niliyofanya nayo kazi kwa muda mrefu ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo pamoja na Mwenyekiti wake mpya. Naishukuru Kamati yangu inayotusimamia Kamati ya Miundombinu, Kamati ya PAC na PIC na viongozi wake pamoja na watendaji wote Wizarani: kuanzia Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu, Wenyeviti wa Bodi, Watendaji wa Wizarani pamoja na Watendaji wa Taasisi. Aidha, naishukuru familia yangu kwa kuwa nami wakati wote. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kipekee kuwashukuru wananchi wa Jimbo la Mufindi Kusini, kwa kunichagua na kunileta niwe mwakilishi wao katika Bunge hili. Aidha, kama kiongozi mkuu kule Redcross niwashukuru volunteer wenzangu ambao wakati wote wamekuwa wakiniamini na kunisaidia majukumu yangu. Pia, kwa unyenyekevu mkubwa niwashukuru Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nimesikiliza hoja, michango na ushauri, kwa hakika nimejifunza mengi, tunawashukuru sana sana sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, michango ya leo kwa haraka haraka ina taswira tatu; la kwanza inathibitisha nia, dhamira, ushupavu, vipawa na maono ya Rais wetu aliyonayo kwa Taifa letu. Michango hii inadhihirisha kiwango cha juu cha upeo wa Bunge letu (Bunge la Kumi na Mbili) katika kufuatilia, kusimamia lakini zaidi kushauri na kuelekeza Serikali yao. Wametimiza jukumu lao la kikanuni kama Kanuni inavyosema kuanzia 118 mpaka 129 ya kusimamia mchakato mzima wa kibajeti. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hotuba hii ya Wabunge mbalimbali leo imetoa uhakika na usalama wa Taifa letu, leo kesho na hata miaka 100 ijayo chini ya kiongozi wetu shupavu Dkt. Samia Suluhu Hassan, lakini imedhihirisha kwamba kumbe CCM ina uwezo wa kuendelea kuongoza miaka mingine 100 ijayo, kwa sababu mambo inayosimamia ni yanayogusa watu leo, kesho na hata kesho kutwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pamoja na maelezo hayo, nitagusia maeneo machache kama ambavyo tumekubaliana na Mheshimiwa Waziri. Zimejengwa hoja nyingi kuhusiana na uwekezaji kwenye reli, nataka niseme mambo mawili au matatu kwenye reli; nambari moja ni upekee wa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Bara la Afrika anajidhihirisha kwenye reli. Kama alivyosema mchangiaji mmojawapo, ndiye Rais anayejenga reli ndefu kuliko zote Barani Afrika. Reli yetu ina urefu wa zaidi ya kilometa 2,100, ndiye Rais amedhihirisha utekelezaji wa ajenda ya 2023 ya kuunganisha Bara zima na Majiji kwenye Reli ya Kisasa. Nchi inayotufuatia kwa mbali ni Nchi ya Ethiopia yanye urefu wa kilometa 756 na ndugu zetu wa Kenya wana reli ya 592 inayokwenda mpaka Naivasha. Hili ni jambo la kutembea kifua mbele tukijidai na kujivuna. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hata kwenye gharama ama uwekezaji ambao Taifa limefanya wakati Tanzania imewekeza Dola za Kimarekani bilioni 10 mpaka sasa, sawa na shilingi trilioni 25, wenzetu majirani zetu wanatufuata kwa mbali sana. Nikisoma hapa takwimu, wenzetu wa Nigeria wamewekeza dola bilioni sita, wenzetu wa Kenya dola bilioni tano na hawa wengine wa Ethiopia dola bilioni nne, tuko mbali sana. Hii inadhihirisha umadhubuti wa Rais wetu, inadhihirisha dhamira ya dhati ya CCM pamoja na uongozi wake uliopo madarakani kwa sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia reli yetu hii ya Tanzania; kwa sababu ni vyema tukafafanua kwa wananchi wakaifahamu gharama tunazojenga kwa kilometa moja ni dola milioni nne, wenzetu wa Kenya ni dola milioni sita kwa kilometa moja, wakati wenzetu wa Ethiopia ni dola milioni 6.5, lakini reli yetu ni ya umeme yenye uwezo wa kubeba mzigo wa tani 35 kwa excel wakati wenzetu wa Kenya ni ya diesel yenye uwezo wa kubeba mzigo tano 25 kwa excel. Sasa hayo ndiyo mambo ambayo ndiyo upekee wa reli yetu, upekee wa maono ya Rais wetu, ni vyema watu wakalifahamu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nini dhamira yetu kama Wizara kwenye bajeti hii? Nini maono ya Rais wetu? Moja…
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, Taarifa.
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, moja ni kunufaika na uchumi wa kijiografia, lakini pili…
SPIKA: Mheshimiwa David Kihenzile kuna Taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Getere.
TAARIFA
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nataka kumpa sifa nyingine ya reli yetu ni kwamba ina mifumo ya Ulaya ambayo ina milimeta 1,435 ukubwa na upana wake. Kwa hiyo ni standard ile ya Ulaya tumejenga siyo ya Kiafrika.
SPIKA: Mheshimiwa David Kihenzile, unaipokea taarifa hiyo.
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, ndiyo naipokea na namtuma aenende akayaambie mataifa habari hizi njema. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika reli yetu hii tunayoizungumzia dhamira ya Rais wetu ni nini? Ni kuifanya Tanzania kuwa kituo kikubwa cha biashara na huduma katika ukanda wetu wa East Africa na SADC. Yuko mtu mmoja amechangia Mheshimiwa mmoja kwamba nchi yetu ni ya saba katika ufanyaji biashara na Congo, ni kweli kabisa kwa sasa hali yetu ni mbaya lakini tunarekebisha changamoto zilizopo siyo tu tukawe namba moja, tukawe namba moja kwa mbali dhidi ya wengine. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwenye reli naomba nizungumzie jambo lingine dogo la open access kwa sababu ni hoja ambayo inazungumziwa sana. Open access ni nini? Ina faida gani? Kwa nini tunafanya? Huu ni mfumo ambao tunautumia wa Shirika la Reli kuruhusu wawekezaji binafsi kuleta vitendea kazi na mtu mwingine atauliza kwa nini? Ukiangalia reli yetu sisi tuliyoijenga ina uwezo wa chini kabisa wa kubeba mzigo tani milioni 17, uzito wa juu kabisa tani milioni 25.
Mheshimiwa Spika, tumewekeza zaidi ya dola bilioni 10 ili tukatengeneze vitendea kazi, mabehewa na vichwa tunahitaji 10% mpaka 15% tuiwekeze huko. Maana yake leo Bunge lako hapo lipitishe karibu trilioni tatu ili twende tukanunue mabehewa na mabehewa tunayoyahitaji ni zaidi, vichwa vya treni tunavyovihitaji ni zaidi ya vichwa 160; wakati huo kuna mafuriko barabara zinahitajika zikajengwe, tunahitaji vituo vya afya, elimu ya juu na kadhalika. Serikali imeamua ita-control reli itaruhusu watu binafsi kuweka vitendea kazi na jambo hili siyo geni duniani.
Mheshimiwa Spika, wenzetu nchi zifuatazo wanafanya: Cameroon wanafanya; Afrika ya Kusini wanafanya; Japan, Korea, Norway, Sweden, Uingereza, Ufaransa, Canada na nchi nyingine nyingi duniani. Sisi siyo wa kwanza na ni maono mema ya Rais wetu kuona kwamba miundombinu tunayoijenga haibaki bure, itumike kama tunavyojenga Barabara, tunaruhusu malori ya watu binafsi kutumia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia tumepata uzoefu kwenye TAZARA kuanzia mwaka 2018/2019 mpaka mwaka jana tumeweza kusafirisha tani 944,000, hizi ni TAZARA peke yao, lakini tuliporuhusu open access tumeongeza tani 909,000 zingine, jumla 1,800,000 maana yake ni nini? Tusingeruhusu mfumo huu maana yake tusingefika huko. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa kuhitimisha nimalizie hoja ya Mheshimiwa Profesa Palamagamba Kabudi amezungumzia kuhusu Reli ya Kidatu. Huko nyuma tulikuwa tunasafirisha kahawa kutoka Uganda tunaipeleka South Africa, wakati wa Mwalimu Nyerere. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameamua kufufua maono ya Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere. Anatengeneza reli na zaidi ya bilioni moja tumeiwekeza kuunganisha Reli ya Kidatu ambayo alikuwa anaizungumza ili iunganishwe kutoka Uganda ije kwenye meli, ije TRC, iende TAZARA ielekee mpaka South Africa. Haya yanakwenda sambamba na mengine tunayosema ya kuunganisha Atlantic pamoja vitu vingine. Kwa hiyo nimtoe mashaka, tayari maono yameshaanza kutekelezwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa kuhitimisha kuhusu Waziri kutembelea eneo lake tutatembelea, ameshanipa maelekezo hapa. Mwisho mabwawa matatu aliyozungumza Mheshimiwa Profesa Palamagamba Kabudi. Wizara ya Kilimo wapo hatua za mwishoni kuhakikisha kwamba yanajengwa mabwawa matatu ili tukahakikishe kwamba wananchi hao wananufaika na kilimo, uvuvi lakini tuna-control mafuriko. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuhusu Reli ya Mtwara ambayo wote mnaifahamu kwa umuhimu wake Liganga na Mchuchuma inayotoa mzigo Mtwara inaupeleka mpaka Mbamba Bay. Inatoa mzigo Liganga na Mchuchuma kupeleka mpaka Mtwara kuunganika na Kilosa, tutachukua ushauri huo, wataalam watafanyia kazi na kadri itakavyoonekana inafaa tutakwenda kufanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo haya, naomba kuunga mkono hoja na ahsante sana. (Makofi)