Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa roho safi tu nitambue ongezeko la mshahara kwa Watumishi wa Umma ambao wamekaa kwa miaka mitano. Naona dada yangu pale anapiga makofi; nitambue kwa roho safi ongezeko hilo la mshahara, lakini hili ongezeko siyo hisani, ni haki ya watumishi wa Taifa hili. Ila tunatambua nia ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwaongezea mishahara watumishi ambao walikaa zaidi ya miaka mitano. Natambua hilo, kwa sababu nililipigia sana kelele. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimesoma kitabu cha Mheshimiwa Waziri cha bajeti, sijaona ile ahadi yake ya kutenga tena Shilingi trilioni mbili kwa ajili ya kulipia deni kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii. Wakati Mheshimiwa Naibu Waziri anajibu swali la Mheshimiwa Halima Mdee, kwenye majibu yake ya msingi alisema kiasi hicho kitakuwepo kwenye bajeti hii, mbali ya kwamba inalipwa kupitia hati fungani ya muda mrefu, lakini hii mifuko inahitaji fedha zao zilipwe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa nasema hapa, kwa sababu hamlipi madeni kwa wakati, ndiyo maana mmeleta sheria ya kikokotoo cha kuwaminya Watumishi wa Umma. Siyo sawa. Tuliambiwa hapa tusubiri, mnakutana na wadau. Mmekutana na wadau yes, mmeleta asilimia 33 halafu mnajisifia wakati cha mwanzo kile kabla ya asilimia 25, ninyi wenyewe ndio mlikibadilisha. Siyo sawa.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi kwanini mnataka muwape asilimia 33 halafu mbaki na fedha yao nyingi watumishi ambao wanapata mishahara midogo; watumishi ambao kama hakuna Rais mwenye huruma, wanaweza kukaa miaka mitano bila kuongezewa mishahara; mtumishi ambaye hajajenga; mtumishi ambaye hajaanzisha biashara; halafu unamlipa asilimia 33 useme nyingine utalimpa taratibu, na huko kwenye kumlipa umempunguzia miaka ya kumlipa baada ya kustaafu. Siyo sawa! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika na Waheshimiwa Wabunge, hivi kwa mfano mtumishi wa daraja la TGTS F1 anayepata mshahara wa Shilingi 1,235,000/= kwa kikokoto cha asilimia 33, kiinua mgongo chake kitakuwa Shilingi milioni 47. Tujiulize hapa, nyumba ya kawaida ya mtumishi wa mshahara mdogo, anajenga saa ngapi? Anaanzisha biashara saa ngapi? Ila kwa kikokotoo cha 1/540 ambacho nacho siyo rafiki, kile kilichokuwepo mwanzo kwa mshahara huu, at least angestaafu kwa kuchukua asilimia 50, angelipwa Shilingi milioni 95 na angebaki na shilingi 500,000 ya kama pension. Vilevile angeweza kulipwa kwa miaka 15. Mmepunguza!
Mheshimiwa Naibu Spika, yaani mnamtengenezea mazingira magumu na bado mnamkadiria afe haraka, kwa sababu mnajua mazingira mliyoyatengeneza siyo rafiki kwa wafanyakazi. Siyo sawa! Hawa wafanyakazi ndio wanatekeleza hii mipango jamani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi najua Mheshimiwa Waziri...
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WATU WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.
NAIBU SPIKA: Taarifa Mheshimiwa Waziri.
T A A R I F A
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WATU WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa nataka tu kumpa taarifa dada yangu, Mheshimiwa Ester Bulaya ambaye anachangia kwamba huo umri ambao umewekwa kwenye kikokotoo miaka 12.5, mtumishi ambaye Mungu atamjalia neema akaishi hata miaka 30 baada ya kustaafu ataendelea kupata mafao.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa nataka tu kumpa hiyo taarifa.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Bulaya, taarifa hiyo.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, mimi siipokei. Kwanini mliweka sasa huu umri wa miaka 12 na mkatoa ule wa 15? Mnafanya hivi kwa sababu mnajua mifuko ya hifadhi ya jamii mmeikopa sana, hamna fedha ya kuwalipa huu muda. Halafu mbaya zaidi, hata formula ya kukokotoa ile, wadau wanawaambia mtumie mshahara wao wa mwisho. Nyie mnasema mnatumia mshahara bora ndani ya miaka mitatu kwenye kipindi cha miaka 10. Watumishi hawa ambao wanaweza kukaa miaka mitano hawajaongezewa mishahara. Siyo sawa! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hawa watumishi wanashindwa kusema kwa sababu mliwabana wawakilishi wao kwenye vikao ndiyo maana leo Vyama vya Wafanyakazi havina guts ya kutoka vimekaa kimya. Nawaambia acheni kuwasaliti watumishi wa Taifa hili, ndiyo wanaoenda kutekeleza hii mipango. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, najua hii kanuni siyo Msahafu, waende wakakae nao wawabadilishie. Halafu hawa ni watu wazima, wewe unampangiaje eti nakupa asilimia 33. Unampangia nini? Mpe asilimia 50, 50 baki nayo ili kama hajajenga aweze kujenga, kama hajaanzisha biashara aweze kuanzisha biashara, aweze kusomesha watoto wake, lakini wanampa asilimia 33, 67 wanabaki nayo. Tunajua hawawezi kuwalipa wastaafu wengi kwa sababu Mifuko iko hohehahe. Wataweza kufanya hivi wakiweza kulipa madeni ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ikawa na uwezo wa kulipa wastaafu vizuri. (Makofi)
NAIBU SPIKA: Taarifa Mheshimiwa Waziri.
T A A R I F A
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tu nimpe taarifa Mheshimiwa Ester Bulaya kwamba katika mchakato wa kufikia maamuzi ya kikokotoo siyo kweli, nadhani tuliweke sawa kwamba eti Serikali ilivibana Vyama vya Wafanyakazi wasizungumze jambo lolote.
Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani tunakumbuka wote hata wakati wa Mei Mosi, risala ya Vyama vya Wafanyakazi iliiomba Serikali kufanya nini kuhusu suala hili la kikokotoo na waliweka wazi kabisa mchakato mzima na walikubaliana na Serikali kwamba ilikuwa ni mchakato shirikishi na wala haikuwa mchakato wa Serikali, Vyama vya Wafanyakazi vilikuwa peke yake. Kwa hiyo, naomba aende kwenye risala ya Mei Mosi ya Vyama vya Wafanyakazi hapo ndipo atakapoona kama walibanwa ama walishirikishwa kwenye jambo hili.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Bulaya.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani unajua hili suala mimi nalijua vizuri, mimi sina haja ya kwenda kwenye risala. Naongea kitu fact ambacho wafanyakazi wameniletea mezani. Hili jambo very serious, leo naongea nikiwa mpole kabisa, najua tunagusa hatma ya watu wanaoenda kutekeleza hii mipango. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba suala hili la kikokotoo, suala la haki ya watumishi wa umma tusilifanyie mchezo. Tuwape asilimia 50 na Waziri anajua, ingekuwa haki bin haki hapa hata hiki kikokotoo kingekuwa 1/480 wala siyo 1/540. Nayafanya haya kwa sababu nalipenda Taifa langu, napenda wafanyakazi wa Taifa hili wafanye kazi wakiwa na morale. Siyo sawa, halafu wanakuja wanajisifia wameweka asilimia 33, wenyewe ndiyo walitoa asilimia 50 wakaleta 25 ikazua mjadala. Mungu amrehemu Rais wa Awamu ya Tano akakisimamisha. Leo wanaleta asilimia 33, kweli? Halafu wanataka tunyamaze kwa watu ambao mipango tunayoipitisha hapa ndiyo wanaitekeleza? Naomba Mheshimiwa Waziri aliangalie hili lakini walipe na madeni. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo napenda kulizungumzia, katika nchi yetu Mungu ametujalia vitu vingi sana, lakini kitu pekee tunachokwama mipango ya muda mrefu bila utekelezaji. Leo Rais Samia kwa huruma yake ametoa ruzuku kwenye mafuta, leo wala asingeweza kutoa hiyo ruzuku kama tungeliwezesha Shirika letu la TPDC likawa na uwezo, lika-supply nishati mbadala ya gesi, likaunganisha mfumo wa gesi kwenye magari, likaunganisha mfumo wa gesi kwenye viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo tunalazimika Rais atoe Shilingi Bilioni 100 kila mwezi kuweka kwenye ruzuku ya mafuta kwa sababu Mungu alitupa gesi tukashindwa kutekeleza mipango ya TPDC tangu 2009, kuhakikisha kwenye viwanda, magari na maeneo mbalimbali tunakuwa na nishati mbadala. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ku-¬invest kwenye kisima kimoja cha gesi wanatakiwa wawe na shilingi bilioni 100. Leo tungeweza kutenga zile shilingi bilioni mia mia ambazo Mheshimiwa Rais atagharimu kutoa karibu shilingi bilioni 700 zingejenga visima saba vya gesi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mbali na hilo, hili shirika nyie wenyewe mna madeni, mnadaiwa shilingi bilioni 412 TPDC. Tunazungumzia visima vinne na ukienda kwenye report mbalimbali, maeneo yanayotumia mafuta ya petrol kwa wingi, viwanda pamoja na kilimo ni asilimia 49 na usafirishaji ni asilimia 42, yaani leo tungeliwezesha TPDC inge-cover maeneo yote, tusingekuwa tunazungumzia vita ya Ukraine na Russia kwa sababu tungeweza ku-invest kwenye TPDC, Shirika letu la Serikali lenye jukumu la kuhudumia nishati ya gesi lakini na kufanya utafiti wa mafuta. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo mikakati ya TPDC walikuwa wamejiwekea at least wawe wameshaunganisha magari 10,000, lakini kwa sababu hatuwapi fedha, tangu 2009 wamefanikiwa magari 1,000. Kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri kwenye hotuba yako sijui ulikuwa na mpango wa magari 100. Tungeliwawezesha hawa wangefanya yote. Kwa hiyo, tujifunze kufanya maamuzi sahihi, kwa wakati sahihi ili crisis yoyote duniani ikitokea tuwe tuna uwezo wa ku-manage kama Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo kwa mfano haya tunayasema na kwenye mafuta ya kula hivyo hivyo. Nimpongeze Mheshimiwa Bashe kwa kazi nzuri anayoifanya na mimi pia vilevile nasisitiza kwenye hili suala la ruzuku ya mbolea afanye hivyohivyo. Crisis hii iliyotokea mbolea duniani kote imepanda, Mheshimiwa Waziri ndiye amepewa hii dhamana. Akicheza na miluzi ya watu tutakuja kumbana hapa mwakani, atimize wajibu wake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo mahitaji ya asilimia 61 ya ngano tunaagiza kutoka nje. Natambua kwamba tumejiwekea fedha nyingi Wizara ya Kilimo, lakini leo tusingekuwa tunatumia fedha nyingi ya kuagiza ngano takribani Shilingi Bilioni 673, tusingeweza kutumia hizo fedha. Mafuta tunaagiza kutoka nje tunatumia Shilingi Bilioni 582…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tungewezesha wakulima wetu yale mambo tungeweza kuyafanya hapa kama nchi, tusisubiri mpaka vita…. (Makofi)