Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Dr. Thea Medard Ntara

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Nami nichukue nafasi hii kuipongeza Serikali kwa kuleta hii Bajeti Kuu, jambo la msingi ni kuisimamia na utekelezaji wa uhakika.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninapongeza sana katika jambo nililofanyika katika kuongeza mikopo, mikopo imekwenda mpaka Bilioni 570 kwa wananafunzi pia benki NMB imetoa Bilioni 200, kwa hiyo sasa hivi kuna karibu Bilioni 770. Niombe mabenki mengine yaige mfano wa NMB, watoe michango hiyo ili taasisi hii iweze kufanya kazi vizuri hasa katika Vyuo Vikuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia bado fedha zinahitajika kazi ya Vyuo Vikuu siyo sawa na sekondari, kule kunahitajika sana research lakini tukijikita tu kutoa fedha ambazo zitawezesha wanafunzi wale kusoma na baadae kupata sijui ada yao na kupata chakula haitoshi, tunahitaji fedha zaidi kwenye eneo la research. Research inaonekana kama kitu cha pembeni, Vyuo Vikuu asipofanya research hawa wanafunzi wakitoka wanakuwa kama wanafunzi tu wa sekondari, yaani Vyuo Vikuu hapa vinaonekana kama ni High secondary school lakini siyo Chuo Kikuu.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ninaiomba sana Serikali iangalie namna ya kupata fedha kutoka kwenye mifuko kama NSSF ili fedha ziongezwe katika eneo la research hasa katika hizi Universities ambazo ni technical zinafanya kazi za mikono zaidi, vitu vinavyohitaji skills bila research tutakuwa tumepotea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaishukuru pia Serikali kwa kuona kwamba walitenga fedha kwa Wahadhiri watakaokuwa wanaandika vitabu au research wapate Milioni Hamsini. Ninawaomba Waheshimiwa Wabunge na Waheshimiwa wengine wanaoweza kuandika vitabu tunahitaji vitabu vya tamthilia, hadithi, mashairi, muandike vitabu na Wizara ihakikishe hawa watu wanapewa fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninasema hivyo kwa sababu gani? Mimi nilisoma kitabu kimoja mpaka leo nakikumbuka nilisoma darasa la nne au darasa la tano kinaitwa Simu ya kifo, nakumbuka Sikonge nilikuwa sijafika, Itigi sijui huko Tabora tulikuwa tunasikia tu, yaani vile vitabu ambavyo vinamfanya mwanafunzi anaweza kufikiri. Mpaka leo nakumbuka lakini Itigi nimeiona nikiwa mtu mzima sasa hivi ndiyo nimeiona Itigi! Kwa hiyo andikeni vitabu Waheshimiwa Wabunge na Waziri atoe fedha kama anavyotoa kwa wale Wahadhiri ambao wanaofanya research. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia niseme kuna hizi fedha za mradi wa HEET, ninaomba hizi fedha za mradi wa HEET zipo kwa ajili ya training ya Wahadhiri Elfu Moja, ninaomba kabisa kwenye kuchambua majina kuna malalamiko, wanaopelekwa kusoma mara nyingi wanatoka chuo kimoja, sasa watakavyofanya huo mchanganuo wahakikishe vyuo vyote vinapata nafasi ya hiyo training, be it Private University or Public University, kwa sababu ni fedha za mkopo hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaishukuru sana Serikali wenzangu wale Wabunge wa Kagera walipiga kelele sana huku na sasa wanapata campus kule Kagera, ninaomba hii iliyoandikwa Ruvuma tupate campus, Ruvuma tupate Public University. Nimeona imeandikwa kwenye vitabu lakini nategemea tutapata hicho chuo muda utakapofika kama mlivyoandika kwenye bajeti hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo jingine ni kwenye fedha zinazotolewa kwenye Wizara ya Maendeleo ya Jamii na Mambo ya Ndani, nalisema hili kwa sababu nililizungumza wakati Fulani, sasa hivi tuna janga la kitaifa, tunalo janga la kitaifa katika maadili na hili janga ili liweze kupungua au kuondoka lazima hii liweze kupungua au kuondoka lazima hii wizara ya Maendeleo ya Jamii na Mambo ya Ndani wawezeshwe zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, siku moja Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano alizungumza kwa huzuni na hisia kali sana kuhusu maadili ya watoto wetu na wananchi kwa ujumla, leo linalonifanya nilizungumze zaidi ni hii kuhusu namna gani Wizara hizi mbili ziweze kulinda watoto katika suala la uzima la ulawiti.

Mheshimiwa Naibu Spika, tafiti iliyofanywa na Dkt. Silvia mwaka huu Januari inaonyesha kwamba kuna watoto wanaolawitiwa na kubakwa ni 3,524, kati ya hawa watoto, watoto wa kiume 567 wanalawitiwa, watoto wa kike 70, hivi baada ya miaka 30 tutakuwa na wanaume kweli nchi hii? Watoto hawa wanafanyiwa vitendo kuanzia Primary, Sekondari mpaka Vyuo Vikuu, tunajenga Taifa la namna gani ikiwa hii imekuwa kama ni kawaida?

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii mzazi anampeleka mtoto shuleni lakini ana wasiwasi tumejielekeza sana kwenye ukatili wa kijinsia kwa watoto wa kike sasa hivi nawaambieni watoto wa kiume ndiyo janga, watoto wa kiume wanalawitiwa kwa kwenda mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mtu mmoja alikuwa ananiambia hapo nje ni juzi tu mtoto wake aliombwa na mwanafunzi mwezake aende akamfanyie vitendo hivyo, mtoto huyo alivyokuwa na akili akaenda kushtaki kwa Mkuu wa Shule, yule mtoto amefukuzwa shule. Waheshimiwa Wabunge niwaambieni hili ni janga na niwaomba hata wazazi watoto wakirudi nyumbani sasa hivi usisema mtoto amekua hebu tujaribu kukaa na watoto, tujaribu kuwacheki wale watoto wadogo hali siyo salama, hali siyo salama nchi hii jamani! (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunajenga majengo yote haya, miradi ni mikubwa, majengo ya shule, zahanati barabara maendeleo haya, hivi maendeleo atakaa nani, maana yake hawa watoto wakianza kulawitiwa hawatakuwa wanaume kabisa!

Mheshimiwa Naibu Spika, madhara ya kalawitiwa tuwaambie watoto ukweli, kwanza sphincter muscles zinaelegea, mtoto anaathirika kisaikolojia, mtoto anapata maambukizi ya magonjwa yote machafu hapa duniani, tunakwenda wapi, ninaomba hizi Wizara wafanye kazi, lakini tukisema tu, kila siku kwenye magazeti lazima ukute mambo ya kulawiti, lakini wanaoathirika zaidi ni hawa Watoto, tutakuwa na mwanaume gani mtu ameshalawitiwa, amefanyiwa vitendo hivyo hawezi kuwa mwanaume rijali hata siku moja!(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wanatembea wanalegea mikono, wanarusha vidole maana yake ni nini? Hili ni jambo linalosikitisha sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine niombe hata hizo Wizara za Mambo ya Ndani, Wizara ya Katiba na Sheria kesi hizi zinachukuwa muda mrefu mpaka ushahidi unakuwa haueleweki! Mtoto amelawitiwa ushahidi upo, mfano ni ile ya Arusha, watoto wamelawitiwa, Mheshimiwa Naibu Spika ukisikia ripoti ya wale watoto Tisa wa Arusha hebu Waziri akachunguze atuambie watoto wale wako salama? Mimi nimesikiasikia tu kwamba wale watoto wameathirika, kati ya watoto Tisa sidhani kama watoto Nane ni salama.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ni taarifa nitamwambia Waziri mhusika baadae. sasa maana yake ni nini mzazi analia lakini tayari watoto wameathirika.(Makofi)