Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Abeid Ighondo Ramadhani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Singida Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana Mheshimiwa Naibu Spika kwa kunipatia na mimi fursa angalau na mimi nitoe mchango wangu kwenye bajeti yetu hii. Nianze kwanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa uwasilishaji wake mzuri wa hotuba lakini pia na utendaji mzuri akishirikiana na naibu wake pamoja na Wizara kwa jumla.

Mheshimiwa Naibu Spika, labda mimi niseme pia kwa uchache, niipongeze Serikali na Wizara kwa mapendekezo ya kuja na mkakati wa kubana matumizi kwa kuepuka matumizi yasiyo ya lazima ili kuepuka upotevu wa mapato ya Serikali kwenye mambo ambayo hayana msingi. Mathalani kwenye kuachana na ununuzi ule wa transaction or procurement na kuboresha mfumo wa manunuzi wa umma (TANePS). Haya mambo yatasaidia sana Serikali yetu kuepuka upotevu mkubwa wa mapato ambayo yanakwenda kwenye njia ambazo si zenyewe. Pia nipongeze ili hatua ya kutokuinyima halmashauri kwa kosa la hati chafu badala yake tujikite kwenye kushughulikia ama kuchukua hatua kwa wale watumishi ambao wamesababisha hati chafu. Hii inaenda kuwapa haki wananchi wetu ambao walikuwa wanakosa fedha zinazokwenda kwenye miradi ambazo zilikuwa zinanyang’anywa halmashauri ama wananchi wananyang’anywa bila kosa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi niende kwenye jambo lingine la muhimu la force account. Ninataka kushauri, Serikali isije ikaachana mfumo wa force account kwasababu mfumo huu ni wa muhimu sana na umesaidia sana kukamilisha miradi mingi ya Serikali kwa gharama nafuu. Mpango huu umekuwa na uwazi mkubwa kwasababu mradi unapokwenda mahali unakuwa na kamati za wahusika zinazoundwa. Kuna kamati za manunuzi, mapokezi na, matumizi. Zote hizi ni kwa lengo la kuhakikisha tunabana mianya ya upotevu wa fedha ama rasilimali za Serikali. Lakini hapohapo mfumo huu umetusaidia sana kupunguza gharama za bei ambazo zimekuwa kubwa tofauti na ambavyo kama tungeenda kwa wazabuni. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, siku moja alifika Naibu Waziri kule kwenye jimbo langu akakuta sink moja la choo linauzwa shilingi 97,000, ambalo lingeuzwa kwa shilingi 20,000 au 18,000. Lakini ubao mmoja unaotoka kule Mafinga uliuzwa Singida kwa bei kubwa; ubao wa 2/6 uliuzwa shilingi 18,000 badala ya shilingi 4,500. Hii ni kwa sababu ya force account ambayo inatoa ushirikishwaji kwa Serikali, kwa maana ya wananchi, ku-bargain na fundi anayefanyakazi. Lakini pia jambo hili linawaajiri mafundi wetu wadogo wadogo, linatoa ajira kwa mafundi wa kawaida kule vijijini ambao hawawezi kuanzisha kampuni. Kwa maana hiyo unaongeza mzunguko wa fedha vijijini kwa wananchi mtaani lakini. Lakini pia mfumo huu unahamisha ile ownership ya miradi kwa wananchi wetu. Wananchi wanaona hii miradi ni ya kwao badala ya kuja kukuta mradi umeota hawajui umetokea wapi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hivyo, mimi ningeshauri, kuna miradi ambayo wanaweza wakapewa wakandarasi kama hivi tunavyoona kwenye SGR, hapo huwezi kumpa mtu wa force account. Miradi mikubwa ile ya barabara unajenga barabara inatoka Tanga kwenda Singida hiyo lazima umpe mkandarasi mradi wa barabara unaotoka Singida–Hydom kwenye mpaka Simiyu, hiyo huwezi kumpa mtu wa force account, lazima umpe mkandarasi. Kwa hiyo, tusije tukawadharau, tusije tukawapuuza mafundi wetu kwa kupitia hii force account, tutakuwa tumewaumiza sana na tutaiumiza pia Serikali kwa upotevu wa mapato.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, mimi nilitaka nizungumzie pia umuhimu wa kuimarisha sekta za uzalishaji, kilimo, ufugaji na uvuvi ili kuhakikisha tunazalisha ipasavyo kulisha viwanda vyetu vya ndani. Nimeona hapa Mheshimiwa Waziri ameondoa kodi za kuingiza bidhaa kutoka nje. Hii inaenda kuua viwanda vyetu vya ndani. Ingepaswa uongeze kodi, kama ulivyoweka kodi kwenye mawigi ongeza kodi kwenye kucha na kope ili haya mambo yasiletwe kutoka nje unaua viwanda vya ndani, hamasisha uzalishaji wa ndani ili wananchi wetu waweze kujikita.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza viwanda vitaleta ajira na vitaongeza pato la ndani. Huwezi kukusanya kodi kwenye wigi unaacha eneo muhimu la kilimo. Imarisha kilimo, ufugaji na uvuvi; na hapa nchi yetu itapata, kwanza ajira wananchi wetu watapata ajira lakini pia utahamasisha uzalishaji wa zile raw materials zinazotakiwa ziende viwandani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika,tulikuwa tuna viwanda; ningedhani hapa tungejikita kurudisha viwanda vyetu vile vya nyama. Tulikuwa na viwanda vya nyama Shinyanga na Tanganyika Packers. Leo vile viwanda ni maghala na vingine vinatumika kwenye vitu ambavyo siyo kabisa. Ninashangaa sana, sisi badala ya kuhakikisha kama nchi tunajikita kwenye uwekezaji mkubwa tunakimbilia kwenye vitu vidogo vidogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba sana tuisaidie nchi kwa kuhakikisha tunaelekeza uwekezaji mkubwa, tuhamasishe na wawekezaji wakubwa ili tuinue, tuokeo, na tufufue uchumi wetu, tuachane na hivi vitu vidogo vidogo hivi, petty issues, ambavyo kwakweli havitaweza kuisaidia Serikali yetu na nchi yetu. Tutawezaje kujenga miradi mikubwa ambayo tunasema ile inatakiwa itengeneze uchumi wetu kwa kuvipuuza puuza hivi?

Mheshimiwa Naibu Spika, nijikite kushauri sana Serikali, Mheshimiwa Waziri wa Fedha hakikisha unakuwa na eneo diplomasia ya uchumi, uwe na wachumi wazuri, bobezi, watumie wakushauri ni namna gani tunaweza kufufua uchumi wetu na kuachana na haya mambo madogo madogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, nimeona kuna pendekezo la kuongeza kodi kwenye mabasi na kwenye magari makubwa malori kutoka kwenye 2.5 million kwenda 3.5; hapa si sawa, unaenda kuua kabisa wajasiriliamali; hapa unaenda kuwaua wajasiriliamali. Nikuombe sana, wamazungumza Waheshimiwa Wabunge wengine. Naomba na mimi niongeze na nisisitize, usitake kuwaua wajasiriamali hawa ambao wamejikita huku kwenye usafirishaji. Nikuombe hiyo iliyokuwepo ada ile ibaki vilevile, usiipandishe.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikienda kwenye eneo la kuboresha miundombinu ya usafiri na usafirishaji hapa nchini. Sisi tumejikita sana periodic maintenance za barabara. Kila mwaka tunatenga fedha kwa ajili ya kwenda kukarabati barabara zetu. Ningeshauri tuachane na barabara za vumbi twende sasa kwenye barabara za changarawe. Hili jambo limetupotezea fedha nyingi sana kila mwaka. Tunategeneza barabara zilezile kwa fedha nyingi niombe sana tuachane na…

(Hapa kengele ililia kuashiriakwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante kengele ya pili hiyo.

MHE. ABEID R. IGHONDO:… kutengeneza barabara za vumbi twende kwenye barabara ya changarawe.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa na mengi, ninakushukuru kwa nafasi, ninaunga mkono hoja. (Makofi)