Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Mohammed Said Issa

Sex

Male

Party

ACT

Constituent

Konde

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. MOHAMED SAID ISSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na mimi kunipa nafasi hii niweze kuchangia katika Bajeti Kuu ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu nitajielekeza katika sehemu kuu tatu, kwanza nitakwenda kwenye uchumi wa bluu, lakini pia rushwa, mwisho nitamalizia na sehemu ya mapato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ukurasa wa 75 wa hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha ameelezea suala la uchumi wa bluu. Mimi kwanza nimpongeze kwa sababu sehemu hii ya uchumi wa bluu ni sehemu moja potential sana ambayo inaweza kusaidia kukuza uchumi wa nchi lakini pia uchumi wa wananchi wetu hasa wanaoishi maeneo ya pwani. Kwa maana hiyo, Serikali imeona ni jambo jema sana kulifuatilia suala hili na kulipa kipaumbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nina masikitiko makubwa sana kwamba, Serikali imekuja na jambo jema, lakini bila kuja na mkakati ambao utaleta ufanisi katika jambo hili! Kwa nini nasema hivyo? Nasema hivyo kwa sababu, imefikiria tu zaidi kununua meli na kuwafundisha wale wajasiriamali ama wananchi ili kuwapa uwezo wa ku-deal na hili suala la uchumi wa bluu, lakini kuna mambo mengi katika uchumi wa bluu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la kuwapa elimu, kuandaa viwanda kwa ajili ya yale mapato yanayopatikana kutokana na kule baharini, lakini pia uchumi wa bluu kuna aina nyingi zinazopatikana mle za mazao, kuna Samaki aina ya kamba, samaki aina tofauti, hivi ni vitu ambavyo vinaleta fedha nyingi za kigeni, lakini Serikali haijaandaa wananchi katika kutafuta soko la ndani lakini pia soko la nje. Hili ni suala ambalo bado naona Serikali haijawa sawasawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna suala la kutengeneza gati, kutengeneza freezing depot, pia namna gani zitagawa hizi boti 250 ambazo imeziandaa? Bado hawajatuandalia, kwa hiyo hatujui kwamba keki hii itagawanywa vipi? Tunamwomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa atupe mchakato mzima ambao utafanya zao hili la uchumi wa bluu liwe ni nguzo ya Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lambo la pili nirukie kwenye suala la rushwa. Suala la rushwa kwenye nchi yetu ni gonjwa sugu. Gonjwa ambalo sisi sote kama Wabunge ama nchi tunakubaliana kwamba ndilo linayodumaza maendeleo ya nchi yetu. Umesema katika hotuba yako hapa ukurasa wa 25 kwamba, Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, anakerwa sana na suala la rushwa. Ni kweli Mheshimiwa Rais anakerwa sana na suala hili, lakini pia hata sisi wananchi tunaumia sana kwa sababu maendeleo yanadumaa hatupati stahiki za maisha yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia umeeleza kuanzia mwanzo rushwa inaanzia pale ambapo mpaka ilitungwa Sheria ya Monitoring and Evaluation, lakini kuanzia pale sasa rushwa imeanza, kwa hiyo, mpaka kufikia mwisho huko hakuna kinachofanyika. Ushauri wangu kwa Serikali ni kwamba Serikali inapaswa kutekeleza majukumu yake ili kuondoa rushwa;

(i) Jambo la kwanza, kuwahakikishia wananchi wa Tanzania makazi ya bei nafuu,
(ii) Kuweka public transport ili wananchi wasifikirie kupata mahitaji haya kiziada,
(iii) Ajira ya uhakika,
(iv) Kuwa na bima ya afya,
(v) Elimu bora ya bei nafuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vitu hivi vikipatikana hatutakuwa na shida ya kusema tumuongeze CAG pesa kwa ajili ya kwenda kukagua, hii kuongeza pesa kwa ajili ya kukagua ina maana tuna imani kwamba, rushwa bado itaendelea kukua na hatuna la kuifanya. Mbaya zaidi CAG anaonesha orodha, lakini hakuna hatua hasa ambazo wananchi zinawafurahisha, zinachukuliwa ili kuondosha rushwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napendekeza hayo mambo matano yakifanyiwa uhakiki, yakifanywa sawasawa rushwa katika nchi hii itakuwa ni hadithi. Hivi ndivyo ilivyo katika nchi zilizoendelea. Tukiangalia Marekani, Uingereza, hivi vitu vinapatikana vizuri na ndiyo maana rushwa kule unaisikia, lakini ni ile kwa watu wakubwa siyo watu wa chini. Kwa hiyo, mimi napendekeza mambo hayo yafuatiliwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho nakuja kwenye suala la mapato. Kwa kweli, suala hili la mapato ni suala ambalo kwa kweli, sisi kama wananchi tunaona aibu kuishi kwenye nchi hii. Kwa sababu tuna bahati ya kupata vyanzo vingi vya mapato lakini nchi hii inaonekana kama tumerogwa! Inaonekana kama vile hatufikiri vizuri! Kwa sababu tuna bandari, tuna mipaka, kwa nini tushindwe? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bandari peke yake inaweza kutuendesha katika maisha yetu na kutupa maisha mazuri. Tunashangaa, leo tunafikiria tozo, hii tozo ni kuwauwa tu wananchi, tukiendesha vizuri mambo yetu, hasa kutumia mapato, kwa mfano TRA wanakuja na mifumo ambayo kwa kweli siyo rafiki, kwa mfano inakuja inaleta hii e-filing, e-filing wananchi hawajaandaliwa, hawajui kutumia e-filing, matokeo yake ni kuwaletea ma-penalty ambayo mwisho wa siku wanafunga biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, tumeleta hii EFD machine, ni jambo zuri ni lengo la kukusanya kodi, lakini sasa kwa nini wananchi hawakupewa elimu? Lakini jingine kwa nini sasa EFD machine ukitoa risiti, miezi mitatu tu imefutika, hamna kumbukumbu, eeh? Kwa hiyo, hili suala linahitaji kuboreshwa ili zisifutike risiti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, alichangia hapa Mbunge mwenzangu, mifumo ya TRA inakinzana. Kwa mfano, napenda kuwaambia huu mfumo wa TANCIS kuna mfumo mwingine ambao uliletwa mwaka juzi hapa unaitwa Single Window, mfumo wa TANCIS umefanya vizuri, watu wamefanya kazi vizuri, mapato yamepatikana vizuri hakuna tatizo. Imeletwa Single Window sasa hii Single Window imekuwa balaa wafanyabiashara wa sehemu za nchi za wenzetu wamekimbia kwa sabahu, huu mfumo wa Single Window huu unakutaka uweke requirement zote kabla ya kufanya declaration, sasa container hujalifungua, unapataje kuangalia mionzi? Unapataje kuangalia vitu ubora wake? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kabla ya hapo inapokuja hivi ina maana zile logistic za ku-clear mzigo zinakuwa ngumu, maana yake mtu ambaye anaweza kufanya clearance ni yule mwenye TANCIS, sasa hivi TRA wanalazimisha nenda kwenye Single Window, sijui kuna shida gani kuwalazimisha watu waingie kwenye Single Window wakati TANCIS imefanya vizuri? Mimi nashauri kwamba, huu mfumo haufai huu wa Single Window, turudi kwenye TANCIS ambayo tutapata mapato vizuri na clearance itakuwa nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kwenye suala hili la bandari. Bandari zetu ndiyo ambazo zinaweza kutupa mapato. Kwa mfano, sasa hivi kuna changamoto za wafanyabiashara na wale taasisi nyingine. Mimi nashauri Mheshimiwa Waziri wa Fedha pamoja na Mheshimiwa Waziri wa Mawasiliano wakae pamoja na wadau ambao ni TRA, Clearing, Transporters, TASAC, TICTS, kuziangalia changamoto hizi ili kuangalia hawa watu wanakwama wapi kwenye ku-facilitate huu utoaji wa mizigo na kupata mapato?

Mheshimiwa Mwenyekiti, jingine ni kwamba, hapa tuna shida nyingine, upande wa Zanzibar, Zanzibar mizigo ambayo inakuja kutoka Zanzibar kwa kweli tunasumbuka sana sisi wafanyabiashara wa Zanzibar, mfano mzuri ni kwamba, unapoleta mzigo pale Dar-es-Salaam, umesha-clear mzigo wako, umetoa, umelipia ushuru, huku nje wanakuja TRA wanakufuatilia kwa ajili ya income tax, sasa bandarini kinachokuleta pale ni import duty na VAT na nimelipa. Sasa wewe subiri mfanyabiashara auze, hakutoa risiti, ndiyo utajua kwamba huyu kakwepa kodi. Unakwenda kum-harass mfanyabiashara, hatuwezi tena kuleta mizigo, imekuwa biashara Zanzibar na Dar-es-Salaam ni ngumu, tunaona ni shida, hata wafanyabiashara ambao walipendelea kufanya biashara zao pale imekuwa ni ngumu. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. MOHAMED SAID ISSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini siyo hilo tu suala lingine ni suala la…

MWENYEKITI: Mheshimiwa kengele ya pili imelia.

MHE. MOHAMED SAID ISSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)