Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii na mimi kuchangia katika Bajeti Kuu hii ya Serikali. Niungane na Wabunge wenzangu waliopita kumpongeza mkwe wangu Waziri wa Fedha na Mipango.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Kaboyoka nimesema wewe ni dakika kumi waliobaki ndio dakika tano; dakika kumi wewe.
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Ahsante sana kwa hiyo nampongeza Waziri wetu mkwe wangu Dkt. Nchemba kwa kazi nzuri, ambapo tangu nimekaa Bungeni hapa sijaona bajeti ambayo imewekwa vizuri kama hii. Naamini kwamba haya aliyoandika ndiyo atakayoyatenda nashukuru sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hivyo mimi nitachangia katika ukurasa wake wa 28 kifungu cha 35. Pale Waziri anasema mashirika yote ya umma yenye kufanya kazi kwa misingi ya kibiashara yafanye kazi kwa ufanisi na faida, hapo namuunga mkono. Ameendelea kusema kwa nchi zilizoendelea mapato makubwa ya Serikali yanatoka kwenye mashirika yake; nakubaliana naye kabisa. Pia nakubaliana na yeye kwamba yale mashirika mengi ambayo ni mzigo kwa Serikali yafutwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nakuja tatizo; hebu tuangalie Shirika letu la ATCL. Shirika hili muundo wake lilikuwa lifanye biashara na lipate faida lakini matokeo yake tangu lilivyoanzishwa mwaka 2016 lilianza na mtaji hasi. Kwanza umiliki wake uliwekwa chini ya Wakala wa Ndege za Serikali. Ukiangalia utaratibu mzima ni kwa kuliua hili shirika kabla halijaanza kufanyakazi; na sababu iliyokuwa imetolewa labda wakati ule ilikuwa ya msingi, ya kusema kwamba wanaepuka ndege hizi kukamatwa kwa vile kulikuwa ndege hii ya awali ATCL ilikuwa inadaiwa pesa nyingi sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini uzoefu umeonyesha kwamba ndege hizo hata sasa hivi zinakamatwa pamoja na kuziweka katika Wakala wa Ndege za Serikali. Sasa basi tukiangalia pia ATCL wameambiwa wapeleke tozo za kukodisha ndege hizo kwa wakala hawa wa ndege. Wakati 2016/2017 Shirika lilivyoanzishwa tozo zilikuwa zimefika mpaka sasa hivi bilioni 99.7, akiba ya matengenezo imefikia bilioni 59.4 ambazo shirika hili la umma linapeleka kwa Wakala wa Ndege, na yote haya ni mashirika yetu ya umma. Kwa hiyo ukiangalia total, ni jumla ya bilioni 159 ambalo shirika hili la ATCL limepeleka TGFA deni hili liliporithiwa 2016 lilikuwa na bilioni 105.3; lakini kutokana na riba ambayo imekuwa ikilipa kila mwezi sasa hivi inadaiwa bilioni 371.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa utaangalia Shirika hili ambalo limekuwa na mtaji hasi wa ilianza na bilioni 146 lakini kufikia 2021 lina bilioni 240 za mtaji hasi. Sasa ukiangalia hili shirika si tunaliua wenyewe kwa mikono yetu wenyewe? Je Serikali ina nia nzuri na hili Shirika? Maana ingekuwa na nia nzuri ingelipa na madeni haya. Serikali inatakiwa ilipe haya madeni ili liache shirika lifanye kazi kwa ufanisi. Kama kweli unataka kufanya justice unaposema mashirika yanayofanya hasara yafungwe utafunga ATCL? Umenunua ndege kubwa kama Bombardier halafu sasa hivi zinafanya kazi kwa kiwango kidogo sana, maana kati ya viwanja 11 ambavyo vipo Tanzania yetu hii ni viwanja vinne tu ambavyo ndege zetu zinaweza kufanya kazi masaa 24.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa njia hii ni kwamba wenzetu ATCL hawezi kupanga route ambazo zitawaletea manufaa, hawawezi kushirikiana na mashirika ya nje kwa vile hawaaminiki. Wakisema wanunue vipuri wanatakiwa wafanye down payment 100 kwa vile hawaaminiki. Pia ilionekana kwamba fedha ambazo zilipelekwa TGFA kwa ajili ya matengenezo makubwa ya ndege ukifika wakati wa matengenezo fedha ile haipo. Ina maana ATCL itoe tena fedha ipeleke kutengeneza hizi ndege, double payment. Sasa hapo Mheshimiwa Waziri utueleze; hivi kweli hili shirika tunalitakia mema au nia ni mbaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tulikuwa tunataka shirika hili lifanya kazi kiufanisi na kibiashara, kama mwanzo ilionekana kweli kwa kukwepa kulipa deni nikuliweka shirika hili chini ya TGFA; lakini sasa tumeshaona kwamba pamoja na kuliweka chini ya TGFA bado ndege hizi zinakamatwa; kwa nini tusilipe madeni haya ili ndege zetu ziwe huru ziweze kutengeneza faida?
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nafikiri kwamba Serikali ina sababu nyingine ya kufanya kuhusu mpango huu wa kuifanya ATCL ifanye kazi inavyopaswa. Huwezi, mashirika yote mawili ni yako lakini ukafanya shirika moja lilipe tozo kwa shirika lingine halafu liendelee kupata hasara. Ningeshauri kwamba ATCL ikabishiwe ndege zake zote ili iangaliwe utendaji wake. Pia kama kusema mnaweka fedha za akiba TGFA ilhali ATCL wakitaka kutengeneza hizi ndege fedha haipo basi ATCL wafungue escrow account Benki Kuu ili wakati wa matengenezo makubwa yakifika waweze kutengeneza hizi ndege.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ningeshauri Serikali ilipe deni, maana bila kulipa haya madeni kwenye viwanja vya nje ambavyo tunadaiwa na zile ndege zilizokuwa zimekodishwa ambazo hazikulipiwa hela yake ina maana ndege zetu haziwezi kufanya masafa marefu ya masaa 10. Kufanya masafa mafupi ina maana tunazidi kuikwamisha ATCL. Ninashauri Serikali itoe mtaji wa kutosha na iendelee kuboresha viwanja vyake ili viweze kufanya kazi masaa 24; vinginevyo utakuta kwamba hata ule muda wa kuruka unakuwa haupo kwa namna ulivyotakiwa. Kwamba ndege hizi zifanye kazi vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tatizo hili la viwanja vingi kuwa havijafikia ile hadhi au yale matakwa inafanya ndege zetu ziishie labda masaa machache zifanye kazi hadi saa 10:00, saa 12:00 zimefunga kazi. Matokeo yake ni viwanja hivyo vinne tu ambavyo ndiyo vinaweza kufanya kazi vizuri, inasababisha ndege zetu zikose yale masaa ya mruko ambayo ndiyo ingesaidia ndege zetu zikaonesha zinafanya kazi kwa faida. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hili shirika ni kati ya mashirika ambayo yanafanya kazi kwa taabu sana. Angalia TANESCO ina madeni kiasi gani? Inadai na inadaiwa. Angalia TPDC ina madeni kiasi gani? Inadai na inadaiwa. Sasa tutasemaje mashirika yanayofanya hasara yafutwe wakati haya mashirika yetu yote makubwa tunajua hata Serikali yenyewe inadaiwa na haya mashirika? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuomba sana Serikali iliangalie hili. Itakuwa haiwatendei mashirika mengine haki kama itayafunga wakati mashirika haya yanafanya hasara na yanaendelea kuwepo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukija upande wa CAG, mimi nimefurahi kwa jinsi ambavyo nimeona utamwongezea CAG fedha zaidi aendelee kufanya kazi yake kwa ufanisi zaidi. Yule time audit afanye performance audit na technical audit, hili ni wazo zuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona hata Bunge hatuitendei haki Ofisi ya National Audit haki. Inafanya kazi kubwa, inakuwa imepitia miradi mingi na ikaonesha matatizo yaliyopo, lakini Bunge tuna muda mfupi sana wa kukaa na kuangalia ripoti ya CAG. Kwa hiyo, inabidi Bunge lipate muda mrefu wa kupitia ripoti ya CAG. Haiwezekani tunatumia siku moja kwa LAAC na PAC kutoa taarifa na hapo hapo mjadala. Which means kwanza Wabunge hawapati muda wa kujua matatizo kwa urefu; pili, hawapati muda mrefu wa kuchangia, na matokeo yake ni kwamba ripoti hii kubwa ya CAG sehemu kubwa haifanyiwi kazi vizuri. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa.
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba sana Bunge letu liifanyie kazi inayotakiwa ripoti ya CAG. Ahsante sana. (Makofi)