Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Kunti Yusuph Majala

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru nami kunipatia nafasi ili niweze kutoa mchango wangu kwenye bajeti kuu ya mwaka 2022/2023. Natambua jitihada kubwa zinazofanywa na Serikali kwa ajili ya kwenda kumtua mama ndoo kichwani; na pili, ni kwenye sekta nzima ya Afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na miradi mingi sasa hivi ya mabilioni ya fedha ambayo inazinduliwa kwa ajili ya kuwapatia wananchi huduma ya maji safi na salama na yanayopatikana kwa urahisi. Miradi hii ni ya gharama kubwa, lakini kwenye hizo gharama zote anayekwenda kuzilipa ni mlaji wa mwisho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mitambo ya maji inayoagizwa kutoka nje inalipiwa VAT; pili, watu hawa kwenye mamlaka za maji bado wanalipa service levy; tatu, kwenye suala la gharama za umeme, kwakuwa mitambo hii ni mikubwa, unakuta mitambo hii au mamlaka hizi zinalipa gharama kubwa sana za umeme kwa ajili ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma. Gharama hizo mwisho wa siku anayekwenda kuzilipa ni mlaji wa mwisho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, badala ya kumsaidia mwananchi kupata maji safi na salama na kwa bei rahisi, kutokana na hizo gharama anaendelea kupewa mzigo mkubwa wa kulipia ilhali Serikali ni moja, na wanaweza kufanya namna bora.

Mhshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, kwenye fedha za UVIKO zimepelekwa kwenye maji, vifaa vyote ambavyo vimekwenda kutekeleza mradi wa UVIKO vimetolewa kodi, havijalipiwa VAT. Kwa nini Serikali isiendelee na mfumo huo wa vifaa vyote vya maji na mitambo yake inapoingia nchini visilipiwe VAT ili tuweze kumpunguzia mwananchi gharama kwenye suala zima la maji? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye suala la umeme, naiomba Serikali. Serikali hii ni moja na hawa tunaowahudumia ni wananchi wa Taifa hili la Tanzania, twende sasa kwenye taasisi zetu za maji wapewe tariff yao peke yao itakayokuwa na punguzo ambalo litakwenda kupunguza gharama za uzalishaji maji ili wananchi wetu waweze kupata maji kwa gharama watakayoweza kuimudu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, keshokutwa tunatarajia kupokea mitambo ya kuchimba visima. Mitambo ile naomba pia, Mheshimiwa Waziri nenda ukaangalie namna ya kuitolea VAT ili iingie kwa bei rahisi na wananchi waweze kuchimba maji kwenye maeneo yao na tuachane na suala zima la kuzungumzia maji kila siku tunapoingia ndani ya Bunge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niende kwenye barabara ya Kibirashi, Chemba hadi kwa Mtoro. Barabara hii nimekuwa nikiimba tangu nimeingia Bunge hili. Imekuwa ikiandikwa kwenye vitabu vya Waziri wa Ujenzi na vya Waziri wa Fedha. Mheshimiwa Dkt. Mwigulu nakuomba sana, hebu hii barabara safari hii tunakuomba, biashara ya kilometa 20 mnazokwenda kuanza navyo, niliwaambia mkitaka kufanya kwa biashara ya kilometa ishirini ishirini, mnahitaji miaka zaidi ya 40 muweze kujenga ile barabara ya kilometa 460. Hivi mnashindwa nini kujenga ile barabara?

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Serikali mmekwenda kuutambua Mkoa wa Dodoma kwenye Kilimo cha Alizeti ambacho kinakwenda kutatua changamoto kubwa ya uagizaji wa mafuta nje ya nchi, sasa kama barabara ile ya Kibirashi hamtaki kuijenga, mazao yale yanafikaje sokoni? Mwisho wa siku yale mazao yataendelea kuozea kule shambani. Hizo jitihada mnazozifanya za kwenda kupunguza crisis ya mafuta nchini haitaweza kutoweka, mwisho wa siku tutabaki hapo hapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba barabara hii iweze kufanyiwa kazi na tuache kuizungumza humu ndani, nasi tuonekane kwamba ni watu ambao tupo ndani ya nchi hii. Tunajiona kama tumetengwa kanda ya kati hususan Mkoa wa Dodoma. Kwa hiyo, naomba sana Mheshimiwa Waziri aliangalie hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie pia mapori mawili; Mkungunero na Swagaswaga. Nimekuwa nikizungumza humu ndani pia suala zima la Mkungunero na Swagaswaga kwa mateso ya Maaskaripori waliopo kwenye zile hifadhi wanavyowatesa wananchi wetu kule. Sasa leo nimekuja kuona Serikali, kumbe ina uwezo wa kuwatafutia wananchi mahali ambapo watakuwa salama, hawatabughudhiwa na taasisi zao za Serikali! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, kama mmeweza kuwaondoa watu wa Loliondo, kwanini hamtaki kutuondoa na sisi mkatutafutia maeneo watu wa pori la Swagaswaga pamoja na Mkungunero? Tunaomba na sisi, wananchi wa Mkungunero wamechoka kuchapwa viboko, tumechoka kupigwa risasi, tumechoka kuibiwa mifugo yetu! Tunaomba na sisi suala la wananchi wa Mkungunero na Swagaswaga tupeni maeneo, tufanyieni kama watu wa Loliondo, Ngorongoro, nasi mtujengee hizo nyumba, mtukabidhi tuweze kuishi kwa amani na utulivu, tule matunda mema ya Taifa letu hili la Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu Bunge lililopita la Kumi na Moja, tumekuwa tukiomba Bima ya Afya. Bima ya Afya Waheshimiwa Wabunge tunaiomba kwa sababu, leo matibabu gharama zake ni kubwa sana. Kipimo cha MRI ni zaidi ya shilingi 500,000, CT-Scan ni shilingi 200,000 mpaka shilingi 300,000; X-Ray, Ultrasound, mashine hizi zote matibabu yake ni ya gharama. Tukileta Bima ya Afya kwa pamoja, itasaidia kumwondolea mwananchi mzigo huu mkubwa anaolipia gharama hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, Serikali mtakuwa na uwezo sasa wa kuona namna gani mnadhibiti na kusimamia miundombinu ambayo mtakuwa mmeifunga kwenye hizi hospitali zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba na ninasisitiza, Bima ya Afya tuombe tarehe 1/7/2022 tunapoanza mwaka mpya wa fedha, tunaomba tuanze Bima ya Afya ya pamoja ili tuweze kuwasaidia Watanzania wetu. Watanzania wengi waliopo vijijini na wenye uchumi wa chini, wanashindwa kugharamia matibabu kwa sababu ya gharama kubwa za matibabu katika hospitali zetu. Kwa hiyo, naomba sana hilo pia liweze kufanyiwa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Dkt. Mwigulu, Ranchi ya Kongwa aachane nayo. Mna maeneo mengi sana ambayo yanaweza kwenda kulima alizeti. Wilaya ya Chemba kule tuna mapori, yapo, njooni mchukue, lakini Ranchi ya Kongwa tunaomba muiache ili iweze kuhudumia mifugo ya Mkoa wa Dodoma na wawekezaji wengine tuweze kukuza uchumi wa Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, TBS kazi yao ni kukagua ubora wa bidhaa. Sasa nashangaa Mheshimiwa Dkt. Mwigulu, TBS wanataka waende wakakague ubora wa mawasiliano. Wallah, tutakuwa tunapata mawasiliano ya Kenya, Burundi na Uganda. TBS leo wameshindwa hata kukagua viuatilifu tu ambavyo vinasaidia wakulima wetu kule. Viuatilifu feki vimeingia nchini na wananchi ndio wanaokula hasara, bado mnataka mkamwongezee mzigo TBS aende akakague ubora wa mawasiliano! Hiki kitu hakiwezekani. Nakuomba kaka yangu pia hilo uweze kuliondoa na lisiwepo kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni matumizi mengineyo kwa ma-OCD nchi nzima. Tunafahamu kila sekta ina haya matumizi mengineyo kwa maana ya OC, lakini OCD wa nchi hii, wa Wilaya yoyote ile, anaambiwa matumizi yake mengineyo ayapate kwa Mkuu wake wa Polisi wa Mkoa, kwa maana ya RPC. Hivi kwanini Mkurugenzi mnampa OC? Kwanini DC anapewa moja kwa moja OC yake? Kwanini taasisi nyingine zote zinatengewa OC yao? Kwanini huyu OCD ambaye ndiye ana-deal na wahalifu na kila kitu kule chini mnamwambia yeye OC yake akaipate kwa RPC? Mna uhakika gani ma-RPC wetu wanafikisha hizo OC kule chini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati tunatumia karatasi kwa ajili ya Order Paper hapa, vituo vya Mkoa wa Dodoma vya Polisi walikuwa wanatumia Order Paper za Bunge kuandika maelezo ya watuhumiwa kwenye vituo vya Polisi. Leo mtuhumiwa akipelekwa kituo chochote cha Polisi, anaambiwa ndugu yake au mtu wake yeyote haandiki maelezo, matokeo yake ndugu yake akienda kumdhamini, anaambiwa akanunue karatasi aje wamwandikie ndugu yake maelezo. Kwa hiyo, naomba ma-OCD nchini, OC zao zipelekwe moja kwa moja bila kupita mahali popote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ni suala zima la ukuaji wa uchumi au uchangiaji wa pato la Taifa kwenye Wizara zetu za uzalishaji. Tunajua maliasili kwamba ndiyo sekta muhimu na tunaitegemea sana kwa ajili ya kuongeza pato la Taifa la nchi yetu. Ila kutokana na janga la Corona, maliasili imeshuka. Mpaka mwaka 2021 maliasili imechangia kwenye pato la Taifa wastani wa asilimia 1.1. Sasa naomba, ili tuweze kuondokana na hizi changamoto za ukuaji wa uchumi katika Taifa letu, naomba Wizara ya Fedha, kitu pekee au Wizara pekee itakayoweza kutusaidia kukuza uchumi wa Taifa letu, ni kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru sana Serikali na Mheshimiwa Rais kwamba ameona mbali na kuhakikisha kwamba Wizara ya Kilimo inakwenda kupata fedha za kutosha. Shilingi bilioni 900 siyo haba, japokuwa Kamati tulitamani sana tupate shilingi trilioni mbili angalau ingeweza kusogeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Dkt. Mwigulu, fedha hizi ziweze kutolewa; moja, kwa wakati; na pili, zitoke zote ili ziweze kusaidia uchumi katika Taifa letu, tuweze kupata lishe bora na kujenga uchumi wa Taifa letu. Kwa kuwa kilimo leo ndiyo kinaokoa, pamoja na changamoto kubwa ya COVID-19, bado kilimo kimechangia kwenye pato la Taifa asilimia 27. Kwa hiyo, tunaona ni kwa namna gani, pamoja na changamoto zozote zitakazotokea, kama kilimo kitakuwa kimesimama vizuri, nina uhakika kwamba Taifa letu halitaweza kuyumba kwa chakula, na pili, halitaweza kuyumba…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Kunti.

MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.