Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. KHADIJA S. TAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kupata nafasi hii ya kuchangia katika Bajeti Kuu ya Serikali hii. Awali ya yote, naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu, kwa kunifanya kuwa mwenye afya njema, namshukuru sana kusema kweli na sote tunapaswa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa afya njema. Jambo la pili naomba nimshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Rais, kwa jambo zuri alilolifanya, jambo ambalo linaenda kuondoa umaskini katika hii nchi na jambo ambalo linaenda kumwezesha mtoto wa maskini kupata elimu. Hili suala la elimu bure kuanzia darasa la kwanza mpaka form six ni jambo la kiukombozi sana, sana. Watu wengi hawana uwezo wa kujisomesha, lakini leo hii wataweza kusoma bure mpaka form six. Hili ni jambo la kihistoria na ni jambo la kwenda kutangaza na kulisemea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, naomba niishukuru Serikali kwa kuongeza bajeti ya kilimo. Kilimo ni uti wa mgongo, kilimo ndio chenye kuondoa umaskini wetu. Kilimo ndio chachu ya uchumi wa nchi yetu. Sasa leo hii bajeti imeongezwa, inaenda kuongeza ufanisi na ubora katika kilimo chetu ili tuweze hata kuuza nje ya nchi. Naomba nishukuru pia nimshukuru au nimpongeze Mheshimiwa Mwigulu, bajeti hii imelenga hasa katika kubana matumizi. Tunaishukuru sana Serikali, tunawashukuru sana sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii naomba niongelee masuala ya wanawake au makundi maalum. Taasisi ya TWCC au Tanzania Women Chamber of Commerce, wakishirikiana na Trade Mark East Africa wamefanya tafiti ambayo hii tafiti imeonesha wanawake asilimia 40 na vijana asilimia 47 ndio makampuni yaliyosajiliwa katika nchi hii. Tukiangalia Sheria ya Manunuzi ya mwaka 2006, ambayo imekuja kuwa amended mwaka 2011, sheria inataka Serikali katika mapato yake au katika manunuzi yake, asilimia 30 iende kwenye makundi maalum.
Mheshimiwa Mwenyekiti, cha kushangaza, ni asilimia moja tu imeenda kwa wanawake. Tukiangalia kwa tafiti za mwaka 2019/2020 tunaweza kuona kwamba Serikali ilitengeneza au ilitenga kiasi cha shilingi trilioni 25, ambapo asilimia 30 ni sawasawa na trilioni 8.0, katika hizo trilioni 8.0 ni asilimia moja tu, narudia tena asilimia moja tu ndio wanawake wameipata ambayo ni shilingi bilioni 80 tu, ni kiasi kidogo sana cha pesa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tukiachana na hilo juzi kati Naibu Waziri amejibu swali la Mheshimiwa mmojawapo hapa Viti Maalum, amesema kwamba, katika halmashauri 184 ni halmashauri 24 tu zimeweza kutenga vikundi au kuweka vikundi 88, hivi vikundi 88 kwa ajili ya kupata tenda za halmashauri. Vikundi 88 hivi ni vikundi vinne tu vilivyopata tenda za halmashauri na hii asilimia nne ni ya Mkoa wa Dodoma peke yake, ambayo ni Halmashauri ya Dodoma Jiji. Hawa vijana au hawa wanawake ndio wamepata hizi tenda za kupaka rangi, za TEHAMA na kadhalika. Sasa unaweza kuona ni kiasi gani hali ni ngumu katika nchi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii sasa tunaona katika bajeti kwamba wana- plan ya kuondoa asilimia tano iende kwenye kwa hawa machinga, ni wazo zuri sana na sitaki kwamba lisiende, lakini kwa nini tusiongeze? Kwa nini tusiongeze asilimia badala ya kupunguza asilimia ambayo haiwezi kutuwezesha. Ukiangalia katika vikwazo vya hawa watu kutokufikisha ni kwa sababu ya kukosa fedha, kwa sababu ya kukosa uelewa na haya mambo kama kuna hii sheria ipo, lakini pia ukiachana na hayo kuna masuala ya rushwa asilimia 10 ya wale wanunuzi wenzangu masuala ya procurements, lakini ukiachana na hayo kuna sababu nyingi tu ambazo zinakwamisha wanawake kwenye wasipate hizi tenda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Serikali ninachosema hapa ni kwamba asilimia tano, asilimia mbili ya wanawake, asilimia mbili ya vijana, cha kusikitisha zaidi asilimia moja tu ya watu wenye ulemavu. Asilimia moja tu ya watu wenye ulemavu sijui aliyekuwa anafikiria alikuwa anawaza nini? Labda alikuwa anawaza ile asilimia mbili ya watu wenye ulemavu kuna mtu mwenye ulemavu ataenda kwa ajili ya wanawake, ataenda kwa ajili ya vijana, kwa hiyo asilimia moja inawatosha, seriously, hivi ndio tunavyotaka tujenge nchi? Hivi ndivyo tunavyotaka tuinue watu wenye ulemavu? Sio sawa kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba leo niseme sio sawa kabisa na kama wanataka hii aslimia moja wanaweza hata wakachukua basi nayo pia kwa sababu tunakuwa kama vile tunafanyiana favor, asilimia moja ya watu wenye ulemavu? Kila siku napigiwa simu za kuombwa hela za watu wenye ulemavu na sio kwa sababu wanapenda kuomba ni kwa sababu hawana pesa. Sasa leo hii asilimia moja ya halmashauri inawatoshaje? Kwa nini Serikali isiangalie nyanja nyingine au namna nyingine ya kufanya ili wananchi au watu wenye ulemavu waweze kusaidika katika nchii hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali ya Mama Samia Suluhu Hassan, namwomba Rais wetu aliangalie hili kwa jicho la pili. Wabunge wenzangu naamini hili jambo linaweza kwenda kutuondoa huko, tukisema tukubaliane na asilimia tano kukatwa kwa ajili ya kwenda kwa machinga wakati kuna makundi ya bodaboda, wakati kuna makundi ya akinamama ntilie, wanahitaji hizi pesa tunaenda kuumia. Mimi kama mtu mwenye ulemavu leo hii nitawaambia nini wenzangu kwamba nilikuwa Bungeni nilikubali asilimia moja ipitishwe. Sikubaliani na jambo hili! Naomba Serikali iangalie jambo hili kwa mapana ili iweze kusaidia wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiachana na hayo, kuna jambo la asilimia tatu, unaangalia kwenye masuala ya ajira asilimia tatu watu wenye ulemavu wanahitajika ili tu utekelezaji wake imekuwa ni ngumu, tena sio ngumu kidogo, ngumu sana. Sasa leo hii basi, haya mtu huyu hawezi kuajirika, anaamua kujikwamua aende halmashauri aombe mkopo, wanamwambia asilimia moja ya mkopo, tuwe wakweli jamani, tuwe serious na hii kazi. Sijaomba Ubunge kuja hapa kwa ajili ya kuja tu kukaa na kupiga makofi, nimekuja hapa kwa ajili ya kuwasemea wenzangu, lakini kwa asilimia moja nakataa na naomba Wabunge wenzangu waniunge mkono katika hili. Waone namna gani ya kwamba kama tunataka basi asilimia mbili ya watu wenye ulemavu, asilimia nne ya wanawake na asilimia nne ya vijana, halafu tuongeze asilimia tano iwe kwa ajili ya ya nini, kwa ajili ya machinga kwa sababu na wao pia tunawahitaji katika nchi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na naunga mkono hoja. (Makofi)