Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Muleba kusini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kupata nafasi hii kuchangia hoja ambayo iko mezani kwetu. Nami nichukue fursa hii kumpongeza Rais wetu kwa ziara aliyoifanya Mkoani Kagera ilikuwa ya mafanikio makubwa sana na wananchi wa Kagera wanamshukuru sana kwa ziara hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ninamshukuru ndugu yangu Waziri wa Fedha kwa hotuba yake na niwashukuru wafanyakazi wote wa Wizara hiyo kwa mchango mkubwa walioutoa kufanikisha hotuba hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nitajikia kwenye ukurasa wa 150 paragraph ya 119 kuhusu mamlaka za udhibiti. Nimesoma hiyo para 119, mamlaka za udhibiti zilianzishwa kwa kusudi maalum. Ukiangalia mamlaka za udhibiti tulizonazo tulizianzisha kwa ajili ya kudhibiti sekta maalum. Mamlaka zote za udhibiti bahati nzuri nimefanya kazi kule, kazi yake kubwa mamlaka zote za udhibiti duniani zina kazi kuu Nne.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi ya kwanza ni kutoa leseni na kufuta leseni, kazi ya pili ni kutoa ukomo au bei elekezi kwenye zile sekta ambazo zinaukiritimba wa asili, zile sekta ambazo ni za kimiundombinu, zile sekta ambazo hazina ushindani wa kutosha, kazi ya tatu ni kutoa viwango (standards). Ukiondoa kimoja wapo kati ya hizo tatu hatuna mamlaka za udhibiti. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri ninakuomba tuache chokochoko kwenye mamlaka hizi za udhibiti, tuziache zifanye kazi yake kama sheria ilivyozianzisha. Ukishaondoa suala la standards, nimeona hapa mamlaka zote za udhibiti, umeongelea EWURA, tumeongelea TASAC, tumeongea LATRA, tumeongelea TCRA, hatutakuwa na mamlaka za udhibiti. Kama tunataka na kwenye hizi mamlaka za udhibiti tunapoongelea suala la viwango, hatuongelei viwango hivi vinavyoongelewa na TBS, tunaongelea viwango kwenye zile sekta za kiuchumi ambazo zimelenga kudhibitiwa na hizo mamlaka za udhibiti, kwenye hili, naomba tuziache mamlaka za udhibiti zifanye kazi yake, tukishacheza nazo hatutakuwa na uchumi wa soko (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi mamlaka za udhibiti tumeziunda zimeanza mwaka 2000, 2003 mpaka 2005 tumeunda mamlaka za udhibiti nyingi kwa sababu tumetoka kwenye uchumi hodhi tukaja kwenye uchumi wa soko, siyo uchumi huria wala siyo uchumi sijui wapi ni uchumi wa soko. Tabia ya uchumi wa soko ni kuwa na mamlaka za udhibiti ambazo zinakidhi viwango vya kiudhibiti ambazo zinatolewa na duniani kote utakapokwenda utakuta zina tabia zinazo fanana fanana, tukianza kucheza nazo tunajielekeza pabaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mamlaka ya TBS siyo mamlaka ya udhibiti, ni agency ya Serikali ni lazima tutofautishe, mamlaka ya udhibiti ni tofauti na agency ya Serikali. Sasa kama tunataka kufanya mamlaka zetu za udhibiti kuwa agency za Serikali then tutamke tunafuata uchumi wa aina gani, katika hilo sitakubaliana na hotuba ya Mheshimiwa Waziri ya kuleta chokochoko na kuanza kucheza na hizi mamlaka za udhibiti. Tutakuwa tunafanya janga la kiuchumi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye uchumi wa soko kuna kitu kinaitwa consumer protection. Ukiangalia kwenye nchi yetu na nchi yoyote duniani inapoingia kwenye uchumi wa kati lazima tuwe na mamlaka za kuwalinda watumiaji. Hapa nchini tunayo mabaraza ya kuwalinda watumiaji, tunaita mabaraza ya ushauri, haya mabaraza ya ushauri yameundwa kwenye mfumo wetu wa kiudhibiti tulionao hapa nchini. Tunayo mabaraza kama manne.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia matatizo makubwa tuliyonayo kwenye viwanda, sijui teknolojia yanasababishwa na muundo au mfumo dhaifu wa kuwalinda watumiaji, ndiyo maana ukienda kwenye masoko yetu unakwenda Kariakoo unasikia wanakwambia hii bidhaa ni genuine hii sijui ni aina gani na maisha yanaendelea, kwa sababu tuna mfumo ambao hauakisi matarajio na mahitaji ya watumiaji hapa nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Wizara hasa Wizara ya Viwanda twenda tukaangalie mfumo wetu wa kuwalinda watumiaji na haya mabaraza tulionayo. Chini ya viwanda na biashara tulikuwa na baraza la kuwalinda walaji ilikuwa consumer advocacy council tumeiuwa, sijua kwa maslahi ya nani, matokeo yake tumekuwa tumeyumba na hapa tunaendelea kuyumba, tunaanza kuangalia mamlaka za udhibiti tunataka kuzipokonya mamlaka yake tuyapeleke TBS. Ni kosa kubwa sana ambalo tutakuja kulifanya hapa mbele yako, tuachane nayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na haya mabaraza ya watumiaji tunayo chini ya LATRA, EWURA na TCRA. Hayo mabaraza hayana fedha ya kuyaendesha, tumeachia mamlaka ya kuyapatia fedha chini ya wakurugenzi wa hizi mamlaka. Niwaombe Wizara ya Fedha na wizara zinazohusika tunapokuja kwenye masuala ya bajeti haya mabaraza na yenyewe tuyaangalie kama tunavyoangalia taasisi nyingine za Serikali. Tuyapatie nguvu yaweze kuwasaidia wananchi wetu na yaweze kuanzisha moli ya watumiaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, matatizo mengine tuliyonayo ni kwa sababu tumeachia mambo yanaenda tu holehole. Tunapokuja kwenye kuwalinda watumiaji, kwenye uchumi, tunapokuwa na watumiaji wenye mamlaka wanaoelewa wanachopaswa kukifanya kwenye soko ndiyo njia pekee ya kuamsha hasa innovation, ndiyo namna pekee ya kuleta awareness na ndiyo namna pekee ya kuchangamsha soko. Lakini tukiachia hayo mambo yanaenda tu, leo tunaamkana ili na kesho tunaamka na jingine hatutajenga uchumi wa soko tutabaki tu kuyumbayumba, tutabaki tu leo hili kesho lile. Ni kama yale tuliuokuwa tunasema kuwa na dira ambayo inatuambia ni lipi tulifanye na lipi tuliache.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo niwashukuru Serikali kwa mradi wa Vyuo Vikuu HEET kwa Mkoa wa Kagera niwashukuru kwa kutuletea hiki chuo hiki ambacho kinachotarajiwa kujenga kwa kweli niwashukuru Serikali. Nikuombe Waziri wa Fedha tupatieni fedha hizi tuanze kujenga chuo chetu Kikuu Mkoa wa Kagera, tumekililia kwa muda mrefu sana. Niishukuru Serikali ya Mama Samia ambaye amefanya mageuzi makubwa sana hatutamsahau kwa hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ada ya vijana wa kidato cha tano na cha sita; nishukuru Serikali yangu kwa hili. Hata hivyo tuwaangalie hawa vijana wanaokwenda kwenye hivi vyuo. Serikali imekusudia kujenga vyuo vya VETA, sijui 36, kama alivyosema kwenye bajeti na vyuo vingine vilivyopo. Niwaombe, hawa vijana ambao wanakwenda kwenye hivi vyuo vya VETA, ni wengi sana, na ndio hao wakitoka pale wanakwenda moja kwa moja kwenye ajira; na hao tuwafikirie kuwapunguzia waende bila ada au tuwapatie mikopo kama tunavyofanya kwenye vyuo vikuu na vyuo vingine. Na njia pekee, kama Serikali hatuwezi, tufanye mkakati tuongee na benki hizi benki yziwapatie mikopo; sisi kama Serikali tuangalie namna bora ya kuhakikisha kwamba hii mikopo inaboreshwa kwenye…
(hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante.
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga hoja mkono.