Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Haji Amour Haji

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makunduchi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. HAJI AMOUR HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kuniona na mimi niweze kuchangia bajeti hii ambayo ni bajeti ya kitaifa na ni bajeti ambayo imepangika vizuri sana. Pili namshukuru kwa kumpongeza ndugu yetu aliyetulea bajeti hii, Waziri wetu wa Fedha pamoja na timu yake nzima kwa kuweza kutuandalia bajeti iliyo na mwelekeo ambao kwa kisura maana yake inaweza ikaleta manufaa kwa wananchi wa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, nampongeza Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi yake nzuri na kwa ushauri wake aliouleta katika bajeti hii ambayo tunayoijadili sasa hivi ni bajeti ambayo itakayoweza kumfanya mwananchi wa Tanzania kuondokana na umaskini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije katika upande wa bajeti. Bajeti yetu hii kwa kweli imekuja na mambo matatu makuu, muonekano wa hii bajeti. Bajeti hii imekuja na maelekezo ya Rais ambayo ukiyaangalia kitu cha mwanzo katika bajeti hii kuna maelekezo ya Rais, katika hii bajeti kuna maagizo ya Rais, kwenye bajeti hii kuna mapendekezo ya Waziri. Sasa sisi Waheshimiwa Wabunge baada ya kuiangalia bajeti hii tuangalie suala agizo lolote la Rais ambalo hatuna namna pengine ya kulikataa kama ni Wabunge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na kuna maelekezo ambayo kaielekeza bajeti hii kuhusu namna ya Kwenda vizuri katika mwelekeo mzuri utakaoweza kuwafanya wananchi wa Tanzania kuwa na uchumi ambao pengine utaweza kupunguza ile hali ngumu ya uchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi labda nije kenye mapendekezo ambayo yamekuja kutokupitia kwa Mheshimiwa Waziri. Moja ya pendekezo ambalo kaja nalo katika bajeti ile ni kuhusu suala la mashirika ya umma. Kwenye suala la mashirika ya umma kuna mambo ambayo amependekeza hasa katika suala la uteuzi wa viongozi katika mashirika ya umma, hasa wale top leader. Tukiangalia katika ile management hasa upande wa directors pamoja na bodi, Mheshimiwa Waziri amependekeza maana yake nitasema kwamba kwenye bajeti hii Mheshimiwa Waziri akapendekeza kwenye viongozi hao wa juu katika mashirika yetu ya umma wawe wanafanyiwa interview, au anakusudia kwamba wawe wanapimwa kuliko kuteuliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachotafuta ni ule ufanisi pamoja na tija katika yale mashirika. inaonekana dhahiri kwamba katika kupitapita kwetu na katika yale mashirika mengi ambayo tulikuwa nayo, tunakuwa na bodi ambazo kama alivyozungumza yeye Mheshimiwa Waziri; kwamba zinakuwa ni bodi ambazo zinazotengeneza urafiki sana pamoja na management.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati mwingine unakuta pengine katika mashirika hayo anakaa muda mrefu sana hata hizo bodi zenyewe zinakuwa hazipo. Sasa ni suala ambalo wakati mwingine tukiangalia suala la ufanisi na tija inakuwa kwamba ni kitu ambacho kina kuwa kinakosekana sisi tunataka kwenda mbele tunataka kusonga mbele kama ni nchi. Ikiwa kwa mfano kama kuna mashirika ya umma ambayo hayaleti tija wala ufanisi katika uendeshaji wake mashirika hayo, kama walivyopendekeza wenzangu, kuna haja ya kuyafuta au kuyaangalia upya katika utendaji wao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumetolewa mifano miwili mitatu humu kwa baadhi ya mashirika hayo ingawa kuna mashirika mengine kuyafuta inakuwa shida kwa sababu ni mashirika ambayo yanatusaidia sisi katika uendeshaji wetu na katika kuyatumia kwa shughuli zetu za kijamii. Kwa mfano shirika kama la ATCL, kuna wengine wanasema kwamba lifutwe, lakini miongoni mwa mashirika ambayo mimi mwenyewe sitakubaliana kwamba lifutwe ni hilo shirika la ATC. Kwa sababu tusiliangalie katika mtindo wa kibiashara tuliangalie pia katika mtindo wa kusaidia jamii zetu katika kuwasafirisha huku na huku. Haiwezekani kwamba shirika muhimu kama lile likafutwa; ila pengine tulifanyie kama alivyopendekeza Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwamba labda tuangalie watendaji pamoja na zile bodi, kwamba je, kweli zina efficiency, na ni kweli kutakuwa na tija kwa wale watendaji? Tukiangalia hapo labda pengine tunaweza tukafika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo pia nije kwa upande wa manunuzi ya umma. Ni kweli imezungumzwa hapa kwamba tuachane na ule wa mfumo ambao kwa sasa hivi pengine unatia hasara Serikali. Lakini katika upande huu wa manunuzi ya umma kuna pande mbili. Kuna pande za hawa watu wanaotoa huduma za kawaida kama vile za usafi na kadhalika, na kuna hawa watu tunaowaita tenderers ambao hutoa huduma kama vifaa vya ujenzi na kadhalika. Sasa tujaribu kuliangalia suala hilo kwa hawa watu ambao wanaomba tena.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa watu wa huduma za kawaida kuwapangia bei kunahitaji ufundi mkubwa sana. Kwa sababu kumpangia bei mtu ambaye anatoa huduma, kwa mfano kama usafi au ulinzi, inabidi uangalie vitu vingi. Uangalie kuanzia mishahara, malipo ya kodi na kadhalika; otherwise tutakuja kuwabinya katika makubaliano ya kikodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwa upande wa mfuko wa jimbo. Nimeiona katika bajeti hii kwa upande wa kifungu cha Bunge, kwamba kutakuwa na ongezeko la mfuko wa jimbo kwa mwaka huu. Sasa mimi ningeligusia tu kwa upande wa Zanzibar, kama vile inavyozungumza sheria. Kwamba kwa mujibu wa kifungu Na. 4 (2) cha sheria kimeweka utaratibu wa usimamizi wa fedha zifuatazo, waziri mwenye dhamana ya Serikali za Mitaa atakuwa mratibu wa mgao wa fedha za mfuko wa jimbo zinazoelekeza katika majimbo yaliyopo Tanzania Bara. Kwa upande wa Zanzibar waziri mwenye dhamana ya masuala ya muungano atakuwa mratibu wa mgao wa fedha za mfuko wa jimbo zinaelekezwa katika majimbo yaliyopo Zanzibar.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati huo huo kuna kifungu Na. 7 (3) cha sheria kimetoa utaratibu wa malipo katika kila Mfuko wa Jimbo. Tatizo ambalo lililopo upande wa mifuko ya jimbo huu utaratibu hatusemi kwamba ni utaratibu mbaya, lakini kwa kweli kwa upande wa Zanzibar utaratibu huu unachelewesha sana zile fedha kuzipata au kufikia upande wa jimbo. Kwa mfano fedha ile inatoka Ofisi ya Makamu wa Rais kwenda Wizara ya Fedha, halafu ije Ofisi ya Makamu wa pili wa Rais. Ofisi ya Makamu wa pili wa Rais fedha hiyohiyo iende kwenye halmashauri zetu. Fedha zile zitakuwa zinatumika bila wakati maalum ambao unakusudiwa kutumika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano kama fedha itakayotolewa kipindi hiki inaweza ikatumika mwakani, kwa mujibu wa huu utaratibu ambao upo. Sasa sheria iko wazi, waratibu maana yake wanajulikana kisheria. Lakini shida iliyopo ni kwamba suala hili niliwahi kuliuliza katika suala la Kibunge; kwamba utaratibu huu ukoje nikajibiwa kwamba uratibu wa fedha za jimbo upande wa Zanzibar zinasimamiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais. Sasa mimi shida yangu mimi iko hapa; kwamba kwa nini mratibu, anamratibisha mtu wa pili?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nadhani ni vizuri zaidi mratibu huyu akabeba dhamana ile ili kutokuchelewesha zile fedha za mfuko. Pili, mimi ningependekeza sheria ya Mfuko wa Jimbo kwa sasa hivi nadhani kuna haja ya kufanyiwa marekebisho kwa sababu ni ya muda mrefu. Pia shida yenyewe kwa Sheria hii ya Mfuko wa Jimbo imeundiwa utaratibu tu lakini kwa kipindi hicho hiko hakuna kanuni za Mfuko wa Jimbo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naomba kuunga mkono hoja ahsante sana.