Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mbogwe
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia kwenye Hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu yenye bajeti ya shilingi 350,988,000,000. Awali ya yote, napenda nimshukuru Mwenyezi Mungu, Muumba wa Mbingu na nchi kwa siku ya leo tena kuweza kupata nafasi ili niweze kuishauri Serikali pamoja na kuwakilisha jimbo langu la Mbogwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kukupongeza wewe kwa kuweza kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti. Mungu akusaidie, akusimamie ili uweze kutuongoza vyema. Namshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa niaba ya wananchi wa Mbogwe, kweli kabisa Mbogwe sasa hivi inaanza kuonekana kwenye ramani ya dunia, mwanzoni ilikuwa haionekani. Namshukuru Mheshimiwa Rais kwa sababu zipo barabara ambazo zilikuwa hazipitiki kabisa, lakini kwa sasa zimeanza kupitika. Pamoja na yote, kuna siku niliwahi kuomba taa za barabarani, nashukuru ninawasiliana na watu wangu waliopo huko Mbogwe wanasema kazi inalendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na shukurani zote, nijikite kwenye kuishauri Serikali kwa sababu muda ni mchache. Kweli Serikali inafanya mambo mengi, inajenga mashule, inatengeneza barabara, inafanya shughuli nyingi kila mtu anaona, lakini unaweza ukafanya mambo mengi ukafeli kwa vitu vidogo. Wapo watu ambao wanamchonganisha Mheshimiwa Rais kwenye hii miradi jinsi inavyotekelezwa. Hii kauli ya kusema kwamba kila mwananchi ahusishwe kuchangia kwenye kila miradi inayotolewa, kwenye jimbo langu imeleta changamoto hasa miradi ya TASAF. Utakuta mwananchi anaambiwa kusomba mawe, kusogeza kokoto, kusogeza moramu; sisi wote huwa tunajenga nyumba, lakini kiuhalisia ukija kuifanya hesabu, pesa zilizotumika unaona kama kuna ujanja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, natumia nafasi hii kuiomba Serikali kwamba huu mfumo wa kuwashirikisha wananchi kusomba mawe, kusomba maji na kufanya shughuli za miradi zinazotolewa na Serikali zinaharibu image ya Serikali na kuonesha kama wananchi wanateswa kwa sababu wanashinda kwenye miradi hasa miradi ya TASAF. Miradi ya TASAF inasumbua sana ndugu zetu, unakuta akina mama wanafanya kazi usiku na mchana na baadaye hata malipo yanakuwa ni shida, mara wanaambiwa uwe na namba ya simu, mara mitandao sijui inagoma, wakati bibi zetu wanashinda wanachonga barabara. Kwa hiyo, ili Serikali ilione la maana sana kuweza kuliondoa, Serikali ifanye mambo yake yenyewe tu na wananchi waweze sasa kustarehe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, inakuwa ni karaha ambapo miradi inakuja kijijini halafu mnaanza kuambiwa kusomba mawe, kusomba matofali halafu unakuta pesa zimetolewa shilingi milioni 450. Kiuhalisia ukija kufanya hesabu, hata kama hujasoma unakuta wananchi wameibiwa. Ifikie wakati sasa Serikali iwapunguzie wananchi mizigo, kwa sababu wananchi wapo tayari kulipa kodi, wapo tayari kulipa tozo, wapo tayari kufanya kila aina ya kazi. Sasa iwapumzishe ili wafanye mambo yao mengine ili kusudi Serikali iendelee kutimiza vizuri miradi kama alivyodhamiria Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni suala la maboma. Juzi niliuliza swali hapa nikaambiwa zimetengwa shilingi bilioni 450, nashukuru lakini kwangu bado sijaziona kwenye Wilaya yangu ya Mbogwe. Tunayo maboma 74 katika Wilaya ya Mbogwe, ambayo ni ya afya, shule za sekondari na maboma ya shule za msingi. Naiomba sana Serikali, kabla hatujaingia kwenye uchaguzi mdogo mwaka 2024/2025, iende ikayaezeke haya maboma kwa sababu wananchi waliumia, waliuza kuku wengine wakajenga haya maboma. Sera ya Serikali ilikuja ili kila Kijiji kiwe na zahanati na wananchi wakajitahidi wakafanya hayo mambo. Kwa hiyo, naiomba sana Serikali yangu iende kukamilisha maboma hayo ili mwaka 2025 tusipate tabu kuomba kura kwa wananchi. Ombi langu kubwa sana ni hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo suala lingine tunashukuru Mungu, mwaka 2023 kweli barabara zilichongwa, lakini kwa neema ya Mungu mvua zimenyesha, barabara zimesombwa zote na maji. Kwenye Wilaya yangu ya Mbogwe kuna njia hazipitiki, ipo Kata ya Ushirika, ipo Kata ya Nanda, kuna Kata ya Ikundigazi, kuna Kata ya Isebya, hali siyo nzuri. Naomba sana Serikali kwenye hizi fedha walizoomba TARURA kwa ajili ya kurekebisha Barabara, itoe haraka iwezekanavyo kabla Bunge hili halijaisha ili kusudi barabara ziende kutengenezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ninaloliomba hapa kwenye Wilaya ya Mbogwe, miradi ya Serikali kutokukamilika kwa wakati. Mwanzoni wakandarasi walikuwa wakifanya kazi, shughuli zilikuwa nzuri, shughuli zilikuwa na ubora. Hizi force account miradi inasimamiwa na wataalam, ni kelele tupu. Tumemwona hapa Mheshimiwa Waziri Mkuu kwenye ziara zake pamoja na Mheshimiwa Makamu wa Rais, unakuta mtu alisomea kilimo, wakati huo anasimamia jengo, ni injinia. Matokeo yake tunatumia pesa nyingi ambapo tunakuwa tunafanya na watu wengine ambao sio professional wa ujenzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tungerudi kwenye miaka ile ya nyuma jinsi walivyokuwa wakitengeneza wakandarasi, ambapo miradi ilikuwa inatengenezwa yenye uimara kuliko ilivyo hivi sasa, kila sehemu ni kelele. Wataalam wanakula fedha, mainjinia wanakula fedha, tunakalia kugombana na kutokufanya shughuli nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine, naiomba Ofisi ya Waziri Mkuu, kwa vile yenyewe sekta zote zinawahusu katika namna ya uendeshaji wa vikao, basi Bunge na vikao vya halmashauri vitengenishwe, kwa sababu muda mwingi Waheshimiwa Wabunge tunakuwa Bungeni, halafu tutakuta mambo yameshafanyika vibaya huko kwenye halmashauri. Mfano, mimi eo ni mwezi wa tatu sijakaa kwenye Baraza la Halmashauri, ukitembea kwa wananchi ukifanya mikutano unakuta kuna kero ambazo zimetengenezwa na wenzangu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria zinasema, ukikuta wenzako wameshamaliza kupitisha jambo, hutakiwi kulipinga. Kwa hiyo, Serikali ione kila namna kuvitofautisha vikao ili wakati wa Bunge uwe wa Bunge tu, ili wakati wa Baraza la Halmashauri kule Waheshimiwa Wabunge tuweze kushiriki ili hata wananchi wanapotuhukumu, watuhukumu katika kweli. Sasa hivi mambo mengi yanafanyika Wabunge hawapo kwenye majimbo yao, matokeo yake ni kupata hati chafu pamoja na kuonekana kwamba labda Mbunge hafai hasa unapokuja ugeni wa kitaifa Mbunge unaanza kuulizwa maswali mengine ambayo unakuta wenzio walishapitisha kitu kingine. Kwa hiyo, Serikali ilione hili suala la umuhimu, kuweza kutofautisha vikao vya Bunge na vikao vya halmashauri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine hapa ni kwa watu wastaafu. vikokotoo, nimepokea kero nyingi sana kutoka kwa watu walioitumikia Serikali. Suala hili la vikokotoo ikiwezekana tuliondoe kabisa kwa sababu, linatengeneza chuki kuanzia kwetu sisi Wabunge tunaotunga Sheria. Kila mstaafu ambaye yuko jimboni kwangu amenifikia kulalamika kwa hiyo, ninaiomba Serikali pamoja na Bunge tulipitie upya suala hili tuliondoe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine, nizungumze kidogo kwa vile huu ni mwaka wa uchaguzi, tumepitisha hapa Sheria ya Vyama vya Siasa pamoja na mambo mengine. Namwombea Mheshimiwa Rais, kwa roho yake ya upendo kabisa, aendelee kusimama na Mungu hivyo hivyo. Nami nasema, tuko tayari kwa mapambano 2024/2025, afe kipa afe refa, lakini cha msingi, wale watakaoteuliwa kusimamia hizi chaguzi, wawe na hofu ya Mungu kama alivyo Mheshimiwa Rais, ili kuhakikisha kiongozi wanayemtaka wananchi huyo ndiye asimame, kusiwepo tena na ujanja wa kubebana. Term hii hakuna kubebana. Naiomba sana Serikali ikae kimya, sisi tulioko majimboni watuache tupambane wenyewe, na kila mtu atatoboa kivyake na tutakutana hapa tena mwaka 2026. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, narudia tena kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa vile anavyoruhusu kila jambo ambalo tunalitaka. Mimi binafsi nimekuwa na maombi mengi, lakini ananisaidia. Kwa hiyo, hili la kisiasa alione ni la maana sana, achague watu…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Mheshimiwa hitimisha hoja yako, uko nje ya muda.
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nahitimisha hoja yangu kwa kumwombea Mheshimiwa Rais ili haki itendeke 2024/2025 na kazi iendelee. Ahsante sana. (Makofi)