Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Dr. Alice Karungi Kaijage

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. DKT. ALICE K. KAIJAGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami naungana na wenzangu kukupongeza kwa nafasi uliyopata, hongera sana. Nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia Hotuba hii ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa. Pamoja na mambo yote, tunajua hotuba hii inahusu mapitio na mwelekeo wa kazi za Serikali, pamoja na bajeti wanayoiomba, lakini inatuelezea mapitio na mwelekeo wa kazi za Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii Wizara ina mambo mengi sana kwa sababu inaratibu mambo mengi. Nikiwa bado sijajadili sana, kwanza nampongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwasimamia vizuri Mawaziri wetu akiwepo Waziri Mkuu, Naibu Waziri Mkuu, Dada yangu Jenista Mhagama Waziri senior, pamoja na Mheshimiwa Deo Ndejembi na Manaibu wote, Watendaji na Watumishi ambao wamefanya kazi kwa uadilifu mkubwa chini ya Wizara hii mpaka tunaona matokeo haya yote. Ninapongeza hotuba nzuri sana ambayo imesheheni vitu vingi vyenye mantiki kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naenda kutoa ushauri kwa Wizara hii ambao naamini utaisaidia Serikali kuimarisha utekelezaji wa vipaumbele ambavyo vimeainishwa kwenye Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa mwaka huu 2024/2025. Mpango huu ni wa tatu katika ule Mpango Mkuu wa Miaka Mitano ambapo dhima ya mpango huu ni kujenga uchumi shindani na pia viwanda kwa ajili ya maendeleo ya watu, yaani mtu mmoja mmoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika vipaumbele vya ule Mpango wa Miaka Mitano kipaumbele namba tano kinahusu ukuzaji wa ujuzi. Kwa hiyo, ina maana ni watu au rasilimali watu. Pia Wizara ya Mipango inajipambanua kwamba, katika kutekeleza mpango huu wa tatu wa Taifa wa maendeleo itazingatia misingi kumi ambayo itawaongoza kutekeleza mpango huu. Msingi namba saba unasema, kuwa na rasilimali watu ya kutosha, iliyo bora, inayokidhi matakwa ya wakati huu ambao umetawaliwa na teknolojia na ubunifu, lakini msingi mkuu ambao watakuwa wamezingatia Wizara ya Mipango tunawategemea sana, ni kuwa na nidhamu ya utekelezaji wa mipango yao waliyojiwekea. Hii yote inagusa watumishi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Mipango haikuishia hapo, tunaipongeza imeendelea kuboresha mazingira bora ya biashara na sasa imeenda kufungua Idara za Biashara na Uwekezaji katika Halmashauri zote 180. Ina maana, kuna uhitaji wa watumishi lakini siyo hivyo tu, imefungua kwenye hizo Halmashauri vitengo vya mazingira ya biashara, hivyo, kunahitajika watumishi huko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napongeza kwamba Serikali imekuja na mfumo mpya wa tathmini na ufuatiliaji, jambo ambalo Wabunge tumepigia kelele sana. Katika Wizara zote za Kisekta na Taasisi za Serikali zinazojitegemea zilishakuwa na idara hiyo, lakini kwa changamoto. Ina maana kuna utendaji unaohitaji kuingizwa kwa watumishi, yaani uadilifu na uzalendo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi mjadala wangu umejikita katika Ibara ya 146, kuhusu wafanyakazi pamoja na watumishi. Nimebahatika kutembelea mikoa michache na Halmashauri kadhaa. Ukikutana na watumishi, kabla amesimama kuchangia au amekuandikia kwa maandishi, jambo la kwanza utakalokutana nalo, wanampongeza sana Mheshimiwa Rais. Kwanza wanasema amejali maslahi yao; pili, ameboresha mazingira yao ya kufanyia kazi. Kwa hiyo, watu wanaanza na pongezi kwa Mheshimiwa Rais, halafu baadaye ndio wanakuja na changamoto wanazokutana nazo. Kwa hiyo, hii inaonesha kwamba wametambua mchango wa Mheshimiwa Rais ambao tunawapongeza Wizara ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kuendelea kumshauri vizuri Mheshimiwa Rais pamoja na kumpa ushirikiano wa Wizara zote ambazo mnafanya, pamoja na Mheshimiwa Rais mkimsaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna changamoto nyingi sana tunakutana nazo, lakini nitasema chache ambazo natamani jicho la uratibu la Wizara ya Waziri Mkuu liitazame. Kuna suala la elimu na miundo. Wizara ya Utumishi inafanya kazi kubwa sana, nitasema baadaye, lakini watumishi wanakwenda kusoma, wanajisomesha kwa shida, tena wale ambao wako kazini wanaporudi, anapo-submit cheti, kwanza anaogopa aki-submit cheti kwani kuna baadhi ya miundo anashuka Daraja. Kwa baadhi ya miundo hawezi kupanda, matokeo yake wakitoka kusoma wanaficha vyetu vyao, wengine hawavi-submit, wengine hawaoni kwa nini waende kusoma. Naomba jicho la pili la Wizara ya Waziri Mkuu, waende kuangalia wawasaidie kwani wanafanya kazi kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hivyo tu, kuna suala zima la vikao, kuna Mabaraza ya Wafanyakazi kule chini, wanakaa baadhi ya Halmashauri na Taasisi hawakai, wakikaa wanakaa Baraza moja na Baraza hilo wana nia ya kupitisha bajeti yao, nasi tunajua kabisa Mabaraza yale hawakai watumishi wote, wanakaa wawakilishi. Baadhi ya wawakilishi ni wale wanaolalamikiwa na watumishi wa kawaida. Kwa hiyo, jicho la Waziri Mkuu liangalie sehemu hiyo wakisaidiana na vyama vya wafanyakazi. Mabaraza yakae kwa wakati na waende watu ambao wanaaminiwa kushiriki kuwasilisha mawazo yao kwenye Mabaraza hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli hakuna haki bila wajibu, lakini watumishi wakifanya wajibu wao walipwe kwa wakati. Kuna baadhi ya Halmashauri unakuta mtumishi, labda ni Mtendaji Kata amefanya kazi kwa miezi saba, anakwenda na kurudi lakini hajawahi kulipwa posho yake. Wapo wengi wa namna hiyo ambao masilahi yao wanategemea mapato ya Halmashauri. Kuna Halmashauri hazina uwezo, tunakubali, alikuwa anasema Mchangiaji wa Kilolo kwamba Halmashauri ambazo zina njia nyingine za ubunifu tuwasaidie, hatuwezi kulipwa na Serikali Kuu vyote, haiwezekani. Kwa hiyo, ni vizuri sana kama kuna haki na wajibu, basi mtumishi wa Tanzania baada ya kutekeleza wajibu wake, apate haki yake kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza sana Ofisi ya Waziri Mkuu, wamekuja na Tume inayotembea, Tume ya Kurekebisha Matatizo ya Wafanyakazi mahali pa kazi. Napongeza, lakini ina kazi kubwa ya kufanya, kuna mambo mengi sana kwenye Halmashauri zetu na Taasisi kule chini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mambo mengi ya kusema, lakini ngoja sasa niongee kuhusu kikokotoo. Katika Awamu hii ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ndani ya miaka mitatu almost, kuanzia Machi, 2021 mpaka Septemba kwa nini watumishi wanamsifu? Ameweza kupandisha vyeo na madaraja zaidi ya watumishi 455,000 ambayo imeigharimu Serikali 1,011,000,000,000/= ndani ya miaka yake mitatu. Siyo hivyo tu, amebadilisha kada na miundo ya watumishi 30,000 na zaidi ambayo imeigharimu Serikali shilingi bilioni 2.5. Hakuishia hapo, kilio cha kulipwa malimbikizo ya mishahara Mheshimiwa Rais ndani ya miaka mitatu anapata keki ndogo, lakini watumishi hajawasahau, amebadilisha madaraja amelipa malimbikizo ya watumishi watumishi 130,000. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. DKT. ALICE K. KAIJAGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba dakika moja nimalizie. Kwa hiyo, kwa yote aliyofanya, haya ajira za kutosha zaidi ya ajira 150,000 na bado tumeona juzi walitoa ajira 8,900 kwenye Idara ya Afya. Vilevile tulimwona Mheshimiwa Rais akiongea na ndugu zetu Askari akasema, ndugu zangu suala la kikokotoo nimelisikia. Sasa mtu mzima akisema hivyo, tumpe nafasi, tumwombee kwa Mungu, suala la kikokotoo aweze kufanya maamuzi yaliyo na tija. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja, ahsante. (Makofi)