Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Josephat Sinkamba Kandege

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kalambo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami niwe miongoni mwa wanaochangia jioni ya leo. Kwanza naomba nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema kwa kunijalia uhai ili niweze kusimama leo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niungane na wenzangu waliokupongeza kwa nafasi ambayo hakika Kiti kimetulia, umeenea ipasavyo, Mungu akubariki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kipekee nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa jinsi ambavyo anawatumikia Watanzania. Hakika sisi sote na majirani wanajua jinsi ambavyo Mheshimiwa Rais amejitoa katika kuwaletea maendeleo Watanzania. Naomba niungane na wenzangu wote ambao wamempongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na wasaidizi wake wote; Mawaziri, na Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu. Hakika kazi mnaichapa, Mwenyezi Mungu azidi kuwajalia afya ili mwatumikie Watanzania, kwani wana matarajio na matumaini makubwa sana kwenu ninyi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba mchango wangu nijielekeze kuonesha jinsi ambavyo Serikali hii ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Serikali ya CCM ambayo yeye ndio Mwenyekiti wa Chama chetu cha Mapinduzi, amefanya mapinduzi makubwa katika suala zima la elimu. Sote ni mashuhuda jinsi ambavyo yamefanyika maboresho makubwa sana katika utoaji wa elimu baada ya hamasa ya elimu bila ada, jinsi ambavyo bajeti imekuwa ikiongezeka ya elimu ya kati na elimu ya juu na hivi karibuni sote tunakumbuka jinsi ambavyo vijana wetu waliongezewa posho ambayo ni maarufu kwa jina la boom kufika shilingi 10,000. Hakika Mheshimiwa Rais Mungu azidi kukubariki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maboresho haya, hakika vijana wengi wa kitanzania wameweza kupata fursa ya kujipatia elimu. Tafsiri yake ni kwamba, ukienda sokoni wamejaa vijana wengi ambao wana matumaini ya kuweza kupata ajira. Ajira zinategemewa kutoka katika Serikali na kutoka kwenye sekta binafsi na kwa mantiki hiyo, pamoja na kwamba Serikali imejitahidi kuajiri walimu, imeajiri kwenye sekta ya afya, lakini bado ukienda mtaani wenye matumaini ya kupata ajira bado idadi ni kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nini ambacho nashauri? Kwanza ni vizuri Serikali wakafuatilia, kwani yapo malalamiko mtaani ambayo yanatokea na hasa upande wa walimu wanaoajiriwa. Tunapata malalamiko kwa vijana pale ambapo yule ambaye alihitimu mwaka 2015 hajaajiriwa lakini mwenzake ambaye wako kwenye kada hiyo hiyo arts amemaliza 2020 amepata ajira. Wanajiuliza, ni criteria ipi ambayo inatumika kiasi kwamba huyu ambaye amemaliza shule hivi karibuni anapata ajira na anaachwa yule aliyetangulia kumaliza? Ni vizuri Serikali mkafuatilia ili tusije kulaumiwa, ikaonekana kuna namna mtu ambaye anafahamiana na mtu mwingine ama godfather hao ndio wanapata nafasi ya kajiriwa. Hayo mambo yanaleta malalamiko sana kwa vijana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyoseama, anayetegemewa kutoa ajira ni Serikali na Sekta Binafsi, naiomba Serikali na hili naomba niungane na maoni ya Kamati ambao wamepongeza Serikali kwa kuendelea kutiliana mikataba na nchi ambazo zina nafasi za kutoa ajira. Fursa hii ni vizuri tukaitumia kwa sababu tunao vijana wetu ambao tungependa waajiriwe, lakini nini ambacho tunatakiwa kufanya ili vijana wetu waajiriwe, ambao wataenda kufanya kazi zenye staha? Isije ikawa ilimradi kufanya kazi. Wewe umekuwa ukisikiliza, kuna kipindi tunapata malalamiko, vijana wetu wanaenda kufanya kazi ughaibuni huko, lakini wanakuwa wanatwezwa. Jambo hili halina afya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri tukaiga mfano kwa jirani zetu wa Kenya. Kuna kampuni ambazo zimeanzishwa kwa kushirikiana na Serikali ambao wanakuwa wanatafuta ajira kwa ajili ya vijana wao. Pia, wanakuwa na jukumu la kuhakikisha wanawafuatilia kujua kwamba je, katika mikataba ambayo wameingia, zile kazi ambazo waliahidiwa ndiyo hizo ambazo wanazifanya? Pale ambapo kunakuwa na malalamiko, inakuwa ni rahisi wao kujua chombo gani wakifikie ili kuweza kupeleka malalamiko yao. Jambo kama hilo tunaweza tukafanya kama Taifa. Unajua zimetangazwa ajira duniani kwa ajili ya kufundisha Kiswahili. Hebu tuambizane kwa jitihada za makusudi, ni chombo gani ambacho kimefanya uratibu kuhakikisha Watanzania hawa ambao wana uwezo wa kwenda kufundisha Kiswahili wametafutiwa ajira wakaenda kufanya kazi na tukapata remittance hapa kama Taifa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri na ni wakati mwafaka kama Taifa tutumie fursa hizi kwa sababu siyo rahisi kwamba wote wataajiriwa Tanzania. Pia ni vizuri Serikali ikaweka mazingira kwa sekta binafsi ambayo ndiyo inaweza ikawa na uwezo wa kuajiri Watanzania walio wengi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuchangia upande huo, naomba nitumie fursa hii kumshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu. Personally, alifika mwaka 2020 katika Wilaya ya Kalambo kwenye ziara yake. Wananchi wa Kalambo hususan eneo la Kasanga, wamenituma nimkumbushe maana muungwana akiahidi huwa ni deni. Aliahidi ujenzi wa Kituo cha Afya katika Tarafa ya Kasanga, Kijiji cha Kasanga na tayari eneo lishatengwa, tunasubiri na ninaamini Serikali wakati mnahitimisha Ofisi ya Waziri Mkuu, itoe tamko lini ujenzi wa kituo cha afya utaanza Tarafa ya Kasanga katika Kijiji cha Kasanga?

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo, tuna uhitaji mkubwa wa Kituo cha Afya cha Mkakati katika eneo la Katete, Kata ya Katete ambayo inapakana na nchi ya Zambia. Ni hitaji kubwa na tulivyopata fursa ya Wabunge kuandika maeneo ya kujenga vituo vya mkakati, nimeandika Katete. Kwa hiyo, naamini Serikali safari hii mtaanza kutenga fedha ili tuanze kujenga hivyo vituo vya afya ambavyo ni hitaji kubwa sana la wananchi wa Kalambo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali kwa jitihada zake, naona kuna mapitio ya maboresho kwa ajili ya reli yetu ya TAZARA, ni jambo jema sana. Naomba niikumbushe Serikali tutumie fursa hii wakati maboresho yanafanyika juu ya reli yetu ya TAZARA, ni wakati muafaka wa kutazama njia pacha kutoka Tunduma kwenda Border ya Kasanga kwa sababu tayari tuna bandari. Sisi kama Mkoa, tutakuwa tumepata kiunganisho kizuri, na mbele ya safari na wewe umekuwa ukiniombea ili kama nchi tuweze ku-access Kongo DRC kwenda Lubumbashi kwa kupitia Kasanga. Hakika kwa ndoto hii ya sasa hivi, kwa maono makubwa ya Serikali, naamini ndoto yangu itakuja kufanikiwa ili tuweze ku-access kwenda DRC kwa kwenda Lubumbashi bila kupita Zambia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa heshima kubwa, naunga mkono hoja, ahsante sana.