Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mbinga Vijijini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Naanza kwa kukupongeza wewe Mwenyekiti pamoja na Mheshimiwa Mwanyika kwa kuchaguliwa kwa kura nyingi sana ndani ya Bunge hili kuwa Wenyeviti wetu, hongereni sana. Nampongeza Waziri Mkuu, Naibu Waziri Mkuu na Mawaziri, Mheshimiwa Jenista na sasa kaingia Mheshimiwa Deogratius na Naibu Mawaziri. Kwa kweli, tunawapongeza kwa kazi zenu nzuri, mnafanya vizuri sana katika kuitumikia nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza mchango wangu kwa kuijadili hotuba ya Waziri Mkuu kwenye eneo hili la kilimo. Sisi Mbinga Vijijini kama tunavyoitwa vijijini, ni wakulima. Tunalima vizuri kahawa, mahindi, maharage, ngano na mazao mengine. Katika kipindi hiki tunamshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa sababu mvua imenyesha vizuri, tumelima vizuri na mazao yameota vizuri. Pamoja na kwamba mvua imekuwa kubwa na uharibifu mwingine uliotokea kwenye miundombinu, lakini kwa upande huu wa mazao, tunamshukuru sana Mwenyezii Mungu kwa mvua hizi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaishukuru pia Serikali kwa mpango ule wa mbolea za ruzuku. Sisi wananchi wa Mbinga hatulimi bila mbolea. Mbolea ndiyo muafaka kabisa, ndiyo mwarobaini katika kilimo chetu. Tunaishukuru Serikali kwamba mpango huu umekuwa endelevu. Mwaka uliopita 2023 na mwaka huu 2024, tumepata mbolea za ruzuku bila usumbufu wowote. Sasa mazao yanaonekana mashambani, kiasi kwamba inasababisha hali ya hofu kwa wananchi. Kwenye zao hili la mahindi hapa karibuni pameibuka hofu kubwa sana kwa sababu mpaka leo ninavyoongea, bado wananchi wana mazao ya mahindi ya mwaka uliopita. Naongelea nini hapa? Kuna shida kubwa ya soko la mahindi ndani ya nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mahindi ya mwaka 2023 bado hayajaisha na sasa tunakaribia mavuno. Kwa namna ilivyo, tutakuwa na mavuno mengi sana katika Jimbo langu la Mbinga Vijijini na hata Mkoa wa Ruvuma kwa ujumla. Wananchi wamenituma, wanaishukuru Serikali kwa kutoa mbolea, lakini wanaitaka Serikali itafute soko hili la mahindi. Kwa namna ilivyo, kwa mazao yaliyopo mashambani mwaka huu, inawezekana tukawa na shida kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wewe unajua, wananchi wetu hawa wasipopata soko lenye uhakika wanaacha kulima. Wakiacha kulima, nchi yetu itapata shida, itaingia kwenye majanga ya njaa. Kwa hiyo, naiomba sana Wizara ya Kilimo, imefanya vizuri sana kwenye mambo haya ya input, sasa ifanye vizuri ili baada ya mazao haya tupate masoko. Ipo hofu kwa wakulima hawa kwamba tumefunga mipaka, lakini nina uhakika mipaka haijafungwa. Kwa hiyo, naomba Wizara hii ipite, iwahakikishie wakulima kwamba awamu hii mazao yao yatapata soko, kwani mazao ni mengi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu nyingine ambayo nataka kuizungumzia, ni eneo la ukubwa wa haya maeneo ya kiutawala. Maeneo haya tumezungumza hapa mara kadhaa kwamba yapo maeneo makubwa sana. Juzi wakati Mheshimiwa Kakunda anaongea Mheshimiwa Spika alisema, lakini yako maeneo pia madogo sana. Sasa ombi langu hapa haraka haraka, haya maeneo makubwa tuyaangalie kwa jicho la kipekee. Haiwezekani Halmashauri ya Mbinga au Jimbo la Mbinga Vijijini lenye eneo kubwa sana, kata 29, tarafa tano, leo hii magari ya ambulance yako mawili tu. Hivi yatahudumia wapi? Yatatoa huduma gani? Lazima tuangalie namna tunavyopeleka hizi huduma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeelewa kwamba sasa hivi Serikali inaboresha miundombinu kwenye maeneo haya, kwa hiyo, haipendi sana kuelekea kwenye kugawa, lakini sasa tutoe kipaumbele. Tupeleke hizi huduma kwa namna ya ukubwa wa yale maeneo, ikibidi hata mishahara mimi mwenye Jimbo kubwa, basi nipate mshahara mkubwa ili niweze kufika haraka kwenye huduma hizo kuwahudumia hao wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, natoa ushauri tu, ikibidi kwenye kupeleka hivi vituo vya afya, basi maeneo haya yenye ukubwa yasiende jumla jumla. Hata kwenye ule Mfuko wa Jimbo najua kigezo kinakuwa labda idadi ya watu, lakini twende mbele zaidi, tuangalie siyo kwa idadi ya watu tu, bali hata ukubwa wa maeneo haya kiwe kigezo. Kwa sababu mwenzako atatumia tenki moja kuifikia jamii lakini wewe ili umalize Jimbo unatumia tenki kumi. Kwanini usipewe kipaumbele wewe kuongezewa hata mshahara, kuongezewa huo mfuko wa Jimbo, kuongezewa Jimbo Allowance, ili ufanye kazi hizi na wananchi hawa wafurahie? Watu hawa sehemu nyingine unaona wanasema mtu huyu haonekani, haonekani, ni kwa sababu kuwafikia inakuwa ngumu. Ukiongeza huu mshahara, ukaongeza na Jimbo Allowance, huyu mtu atafika kirahisi sana na wananchi wataona Serikali inafanya kazi vizuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo nataka kulisema haraka haraka ni hili eneo la kikokotoo…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba dakika moja tu nimalizie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kikokotoo kimezungumzwa vizuri sana na Mheshimiwa Gambo na hapa ndani tuliaminishwa kwamba formula hii mpya itawanufaisha hawa watakaopata kikokotoo hiki kipya…
MWENYEKITI: Mheshimiwa Benaya naomba hitimisha tafadhali, hatuna muda.
MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nahitimisha. Hapa nina mifano ya watu wa level moja, aliye…
MWENYEKITI: Mheshimiwa Benaya naomba tafadhali hitimisha hoja yako.
MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, nitaizungumza wakati mwingine. Naunga mkono hoja. (Makofi)