Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ALEKSIA A. KAMGUNA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi asubuhi ya leo. Awali ya yote sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya uhai na tunamshukuru Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mwanamke wa kwanza kwa kushika nafasi. Tunasema kila siku mwanamke umpe kazi aifanye. Kama tunaweza tukafanya kazi ngumu leo Mheshimiwa Rais amedhihirisha kwamba kweli wanawake tunaweza. Tunaomba huyu mama tuzidi kumuunga mkono hatimaye kazi iwe rahisi siku zote za maisha yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza Wizara, Waheshimiwa Mawaziri pamoja na wafanyakazi wote wa Wizara ya Ulinzi, maana bila ya wao sisi amani Tanzania isingekuwepo, tunawashukuru sana kwa kazi ngumu ambayo wanaifanya katika nchi yetu ya Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunatoa pole kwa Watanzania wote kwa mafuriko ambayo yametupata, hasa Mkoa wa Morogoro. Jamani mafuriko myasikie tu. Katika Tanzania sidhani kama kuna mkoa ambao umeathirika kama Mkoa wa Morogoro, maana hata helikopta zinashindwa kwenda kutua kwa ajili ya kutupelekea misaada. Kwa hiyo tunaomba Serikali hicho kilio wakisikie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuzungumzia kuhusu Jeshi la Zimamoto. Jeshi la Zimamoto ni jeshi ambalo lina msaada mkubwa sana katika nchi yetu lakini ukiliangalia jeshi hili lina changamoto nyingi, japo kwa hivi karibuni tumepata magari 12 ambayo yana uwezo mkubwa sana katika nchi hii. Hata hivyo magari 12 ni machache ukilinganisha na ukubwa wa nchi yetu, lakini si haba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jeshi hili, pamoja na kazi wanayoifanya ya zimamoto na uokoaji bado lina upungufu, halina ofisi, ofisi zao zipo katika hali mbaya. Hivi jamani Serikali, mtu anatoka nyumbani kwakwe anakwenda ofisini, anafanya kazi ngumu halafu anafika kwenye ofisi ambayo haijulikani ilivyo. hali mbaya, huyo mtu si inampunguzia morale ya kazi jamani? Kwa hiyo Serikali tujitahidi tuwaangalie wale watu wapate ofisi nzuri na hatimaye wazidi kuwa na moyo wa utendaji wa kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye jeshi hilo pia kuna tatizo la rasilimali watu. Kwa sasa hivi hapa tunavyoongea kuna wafanyakazi wa zimamoto na uokoaji ambao wapo kazini, hasa upande wa uokoaji kwa njia ya maji wapo 77 tu; ukilinganisha na nchi kubwa ya Tanzania, watu 77 hawatoshi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wanasema kwamba ambao wanategemea kuwaajiri ni 246 na kwamba bado wapo kwenye mpango wa 425, huo ni mpango, hawajui kama wataajiriwa, haijulikani kama hawataajiriwa. Jamani kazi ngumu kama hii kweli bado wanasema kwamba watu 77 ndio waliopo kazini na hao wengine 246 hatuna uhakika kama wote waliopo kwenye mafunzo wataajiriwa au hawataajiriwa. Kwa hiyo naishauri Serikali iajiri hawa watu. Tanzania tuna bahari kubwa ya Hindi, tuna mabwawa, tuna maziwa, yote yanahitaji hawa watu wa uokoaji wa majini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja kuzungumzia matatizo ya barabarani; Jeshi la Polisi kuna shida, kuna zile njia za service, tunaita service roads, unakuta asubuhi kipindi cha kwenda kazini, nachukulia mfano Dar es Salaam au kwenye miji, unakuta kwamba ile njia ya service road, askari wanazuia wanasema watu wasipite katika zile barabara, wakati barabara kubwa ina msongamano mkubwa. Sasa huwa najiuliza hizo barabara za service roads zimewekwa kwa ajili ya watu gani kupita na zinatakiwa watu wapite wakati gani? Labda hilo wangetuelewesha kwamba ni watu gani wanatakiwa kupita, nani wakati gani wanatakiwa kupita ili watu wafahamu kwa sababu usumbufu unaokuwepo ni mkubwa mno bila sababu za msingi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini kwamba mnapoweka service road maana yake zile barabara kuu zimekuwa zimelemewa hatimaye zinajengwa zile za pembeni ziweze kutoa huduma kupunguza msongamano lakini matokeo yake polisi wanawashika na wanawatoza faini watu, sasa sijajua sababu ni zipi na kusudio ni nini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala langu lingine ni la kuhusu bodaboda; katika bodaboda utakuta kwamba bodaboda na bajaji kwenye hizi service roads na hizo barabara kubwa wanapaki yale magari. Kama mtu anaendesha gari hawezi kuona kulia hawezi kuona kushoto na askari yupo pale amesimama anawaona wale watu waliosimama. Sasa najiuliza wale askari wako pale barabarani kwa ajili ya kumwangalia nani? Tunataka ajali itokee ili wao waseme wameona, wakati watu wamesimama pale hawawezi kuwakemea kwamba hizi barabara mtu anatakiwa aangalie kulia na kushoto mbele na nyuma lakini askari wapo. Sasa kazi yake ya kusimama pale barabarani ni nini? Ni kuwaruhusu watu ili wapate matatizo zaidi au kuwasaidia?
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, nataka kuzungumzia suala la bodaboda kupita kwenye taa zinazowaka; bodaboda ni kero, hatusemi kwamba watoto wetu wasiendeshe bodaboda, vijana wetu wanajiajiri lakini askari wako pale bodaboda wanapita wakati taa ni nyekundu. Wale vijana ni nguvu kazi ya Taifa, wale vijana wanagongwa kila siku, tunatumia madawa mengi katika kuwatibia wale vijana na pia, Taifa linapoteza nguvu kazi...
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Matiko, Taarifa.
TAARIFA
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nataka nimpe taarifa mchangiaji anayechangia vizuri kuhusu bodaboda. Bodaboda kwa tafiti ambayo nimeifanya, ninavyokuwa nazunguka na na-drive, bodaboda wengi unakuta wameng’oa zile site mirror zao, kwa hiyo hata ukim-mute lazima ageuke kukuona, by the time anafanya hivyo anapata ajali. Kwa hiyo, ni lazima Jeshi la Polisi liangazie sana na litoe elimu toshelezi kwa bodaboda hawa ili tuweze kunusuru maisha yao lakini na yale ya abiria ambao anakuwa amewabeba.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Aleksia Asia Kamguna, unaipokea taarifa kutoka kwa Mheshimiwa?
MHE. ALEKSIA A. KAMGUNA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea hiyo Taarifa kwa mama yangu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bodaboda hao ukiangalia ni vijana wetu tumewaruhusu, kweli wanapata kibali wafanye ajira, lakini ile ajira sasa inakuwa ni shubiri sio ajira tena kwao kwa sababu wanakufa. Wale Polisi wa Barabarani wanawaangalia hawajali kama kuna mtu amepita kushoto, amepita kulia, wakati wao wana usemi wao unaosema kwamba tii sheria bila shuruti, sasa wale wanapopita kwenye taa je, wale wanatii zile sheria na kwa nini wanawaacha? Sasa hapo tuwaelewe vipi wale askari walioko barabarani, ina maana wale hawawaoni na wale wanaosimama kandokando ya barabara wanazuia barabara hawawaoni? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeshaongea nao mara nyingi, jamani kwa nini wale wanazuia pale barabarani watu hawaoni vizuri ikitokea ajali, wanakwambia mama au Mheshimiwa sisi wale wametushinda. Sasa wanawashindaje wakati sheria zipo? Tunaomba kwa Mheshimiwa Waziri, hili walifanyie kazi wale, wote walioko kandokando ya barabara waondolewe wawekwe kwenye vituo vinavyotakiwa ili hata wale wanaoendesha magari ni haki yao na hata wanaotembea kwa miguu pia ni haki yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu jambo lingine ambalo huwa linanitatiza kwenye hizi barabara zetu kubwa zenye kuanzia barabara mbili na kuendelea yaani barabara za lami, unaweza kukuta kuna malori makubwa, lakini yale malori yaliyoko pale yanapita kushoto na yanapita kulia, kwa hiyo wale wenye magari madogo labda kama ni saloon car au kama ni mabasi ambayo wanataka waende kwa haraka hawawezi wakaenda kwa sababu lori liko kushoto, lori liko kulia kama vile wanafanya kusudi kuzuia watu wasipite.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa unajiuliza mbona nchi za wenzetu kuna utaratibu kwamba kama wewe unajiona mwendo wako ni mdogo au malori wapite kushoto kwa sababu miendo yao ni midogo, wenye magari ya kwenda kasi wapite kulia ili kumfanya kila mmoja afike sehemu yake akafanye kazi. Tunapoteza muda mwingi sana barabarani kwa uzembe na askari wapo. Kwa nini tusipitishe sheria kwamba magari ya mwendo fulani yapite kushoto magari ya mwendo fulani wapite kulia ili yule mwenye haraka aende afanye kazi akazalishe na yule mwenye mwendo mdogo kama wa lori aende taratibu naye afike kwenye safari yake anayokwenda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilishawahi kuuliza hilo swali nikaambiwa hiyo sheria haipo, kwa hiyo tunamsubiri nani aje atuletee hiyo sheria, sio sisi ndio tunatunga hiyo sheria ya Watanzania baada ya kuona tunaenda kwa wakati? Kwa sababu lazima kila jambo linalofanyika tulifanye kufuatana na wakati tulionao. Haiwezekani wewe unatoka nyumbani kwako unajua unaenda kazini, unafika baada ya nusu saa, lakini unafika baada ya masaa matatu eti kwa sababu lori moja liko kushoto moja liko kulia na liko mbele yenu, mnafanyaje mtapita wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani naomba hilo aliangalie ili hatimaye tuweze kufika mapema kwenye sehemu zetu za kazi, tuzalishe badala ya kupoteza muda na kuleta ajali ambazo hazina msingi kwa sababu wengi watajiona kwamba mbona lori linanichelewesha ngoja nijaribu kupita pembeni matokeo yake tunaleta ajali. Askari wapo na kama haliwezekani, kuanzia sasa hivi tutunge sheria na tutoe mafunzo kwa watu ili waelewe. Kama nchi nyingine wanaweza sisi tunashindwa nini? Naomba hili tulifanyie kazi na tulichukue kuanzia sasa hivi ili tupunguze ajali za barabarani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine naomba kuzungumzia kuhusu hizi safari za usiku; safari za usiku ni safari nzuri ambazo vijana wengi wanapenda hasa wafanyabiashara, zinawafikisha kwa wakati, lakini hizi safari zina madhara yake. Madhara ni makubwa kwa sababu kwa usiku ukiangalia barabara zetu hazina taa utakuta ajali zinatokea nyingi. Mchana pia tunaona ajali nyingi, lakini usiku ajali ni nyingi zaidi kwa sababu uwezo wa kuona ni mdogo na pia askari wanakuwa ni wachache, hawapo. Sasa kama mchana tunaona askari ni wengi usiku askari ni wachache, sasa kama hatujajipanga tukafikia hapo, naona hii inasababisha hatari sana kwa Taifa. Tujipange tuweke askari wengi usiku ili kulinda usalama wa watu wanaotembea usiku. Sijasema kwamba watu wa usiku wasitembee la hasha ila tuwe waangalifu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja na ahsante. (Makofi)