Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Maryam Omar Said

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Pandani

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. MARYAM OMAR SAID: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi niweze kusema neno katika hoja hii iliyoko mezani. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri kwa kadri wanavyofanya kazi, lakini uongozi mzima wa Wizara hii ikiwemo Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina shida mbili au tatu katika Wizara hii, mojawapo, ni mara nyingi sana huwa nasimama hapa na Mheshimiwa Naibu Waziri ni shahidi, nikiulizia either vituo vya polisi ama majengo ya askari wetu Mkoa wa Kaskazini Pemba. Kwa asilimia kubwa kila atakayesimama hapa kuchangia basi hoja kubwa itakuwa ni vituo vya polisi, majengo ya makazi, askari wetu hali haziridhishi. Mkoa wa Kaskazini Pemba tuna vituo vitatu vya polisi, kituo kimoja kinabeba Makao Makuu ya Jeshi la Polisi, Mkoa wa Kaskazini Pemba, kituo kiko Wete pale. Hali ya lile jengo ni mbaya hairidhishi na mara zote tukisimama hapa kuuliza unaambiwa tunafuatilia tunasubiri fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, fedha ndio kama hizi hakuna fedha nyingine itakayokuja ikawa mahususi, hebu tunakuomba na sisi Mkoa wa Kaskazini tuone, tena tuone kwa jicho la huruma. Kwa mfano, kuna nyumba inayokaliwa na familia karibia 12 na zaidi ya Jeshi la Polisi. Askari Polisi hawa wanakaa katika mazingira magumu. Jengo ni bovu ninavyokwambia kipindi hiki cha mvua ni kama chujio, bora ukakae kwenye mwembe kama ile nyumba wanayoishi. Hili ni Jengo linaitwa Like Kilimanjaro liko karibu Uzunguni kule Wete Pemba, hili jengo haliridhishi, hali ni mbaya mno. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo hapo ukija kwenye utendaji wa Jeshi la Polisi, tukija kwenye usafiri wa magari, Mkoa wa Kaskazini pale Makao Makuu kuna gari moja tu la OCD, gari moja la OCD, hebu niambie Mheshimiwa Waziri gari hili moja litafanya kazi vipi, kule mhalifu ameshaiba, huku huyu ameshalawitiwa, gari hilo moja litafanya kazi vipi. Nimwombe Mheshimiwa Waziri katika haya magari ambayo nimesikia hapa akiyataja, hebu na siye atuangalie kwa jicho la huruma, atupatie angalau gari moja watuongezee angalau gari moja tuwe na mawili. Badala ya gari moja, hakuna hata pikipiki moja inayofanya kazi. Angalau hata ikitokea emergency ukaambiwa askari yule atafika kwa pikipiki, hakuna. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo niingie katika usalama barabarani. Mheshimiwa aliyenitangulia amezungumzia sana bodaboda. Bodaboda ni vijana wetu, tunawapenda sana na sisi wengi hapa, mtu anakujia Mheshimiwa naomba unipatie bodaboda ili nijiwezeshe kimaisha sawa, lakini sasa imekuwa ni changamoto kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaambie, wenzetu Rwanda walipoanzisha bodaboda walikuja kujifunza kwetu Tanzania, twende Rwanda tukaangalie, bodaboda anavaa helmet pamoja na abiria wake, bodaboda anavaa uniform pamoja na abiria wake wana kile kikoti cha blue, bodaboda hazidishi abiria zaidi ya abiria wake mmoja, bodaboda anasimama kwenye mataa mpaka taa imruhusu, sisi tunashindwa wapi? Wapi sisi tunashindwa? Kama wale walikuja kusoma kwetu wakaenda kuboresha kule kwao sisi tuliosomesha kipi tunashindwa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapoteza vijana wengi, juzi hapa tulisikia kati ya watu wengi ambao wanahatarisha maisha yao wanakuwa katika hali ngumu kule MOI wodini ni bodaboda. Hawa hawana bima, asilimia kubwa hawana bima na ukizingatia hao hao bodaboda asilimia kubwa hawana leseni. Niwaulize watu wa usalama barabarani wanafanya kazi gani? Ni sheria gani inayomruhusu mtu aendeshe chombo barabarani akiwa hana leseni? Hii sheria tumeitoa wapi? Namwomba Mheshimiwa Waziri, hiki Kitengo cha Usalama Barabarani hebu kiangaliwe sana bado kuna mapungufu makubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na muda nataka nilisemee kidogo suala la kitambulisho cha Taifa pale migration.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mariam, bahati mbaya muda wako umeisha.

MHE. MARYAM OMAR SAID: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Kicheko)