Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Martha Festo Mariki

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. MARTHA F. MARIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia nafasi nami niweze kuchangia katika Wizara hii ya Mambo ya Ndani. Kwanza nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunijalia uzima na afya njema, lakini kipekee zaidi nimpongeze sana Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya katika Taifa letu la Tanzania, lakini nimpongeze zaidi kwa jinsi ambavyo ameendelea kuboresha Wizara hii ya Mambo ya Ndani ukizingatia Wizara ya Mambo ya Ndani ndio Wizara ambayo inatusababisha sisi wananchi tuweze kukaa katika hali ya ulinzi na usalama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri pamoja na watendaji wote wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi. Pia, naipongeza sana Kamati inayoshughulikia Wizara ya Mambo ya Ndani kwa jinsi ambavyo wameendelea kuishauri Wizara kuangalia namna nzuri ya kuboresha ili Wizara hii iweze kufanya vizuri katika kuboresha usalama wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuzungumzia suala la gari la zimamoto katika Mkoa wetu wa Katavi. Naishukuru sana Serikali kwa kutenga fedha kwa ajili ya kuleta magari ya zimamoto nchini, lakini katika maeneo mbalimbali. Ni dhahiri kabisa Mkoa wangu wa Katavi ni takribani zaidi ya miaka kumi tumekuwa hatuna gari la zimamoto. Tumekuwa tukitumia gari ambalo ni la airport na unaweza ukaona jinsi gani Mkoa wa Katavi tulivyo katika hali ya hatari pale inapotokea siku ndege inatua katika Mkoa wetu wa Katavi, Wilaya ya Mpanda na inapojitokeza shida ya moto katika Mkoa wetu wa Katavi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, gari tunalolitegemea ni ambalo linatumiwa na airport. Tunaomba sana, Wizara ya Mambo ya Ndani kupitia Mheshimiwa Waziri wetu, katika mgawo wa magari yaliyokuja utupe kipaumbele sisi wananchi wa Mkoa wa Katavi ili tuweze kupata gari la zimamoto. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza sana pia Serikali inayoongozwa na Mama yetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutenga pesa kwa ajili ya ukarabati na ujenzi wa vituo vya polisi nchini pamoja na kujenga Vituo vya Polisi Kata katika maeneo yote nchini. Tunaipongeza sana Serikali kwa hatua hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, tunaiomba sana Serikali, katika Mkoa wangu wa Katavi tunacho Kituo cha Polisi katika Wilaya yangu ya Mpanda. Ni kituo ambacho ni cha miaka mingi na ni chakavu. Naiomba sana Wizara iweze kuangalia namna ya kutenga pesa kwa ajili ya ukarabati wa Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Mpanda, kwani ni kikongwe sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nawapongeza sana Wananchi wa Wilaya yangu ya Tanganyika kwa kuonesha juhudi zao binafsi kwa kutoa nguvu kazi zao, kwa ajili ya kujenga Kituo cha Polisi katika Wilaya ya Tanganyika. Hata hivyo, kwa kuwa, wananchi wameanzisha ujenzi wa Kituo cha Polisi katika Wilaya ya Tanganyika kwa nguvu zao binafsi, naiomba sasa Wizara iweze kutukumbuka sisi wananchi wa Wilaya ya Tanganyika kwa kutenga pesa kwa ajili ya umaliziaji wa Kituo hicho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, tuna changamoto kubwa katika makazi duni ya Polisi katika Mkoa wetu wa Katavi na vilevile, katika maeneo yote nchini. Naiomba Wizara, Polisi wanafanya kazi nzuri sana katika Taifa letu la Tanzania, hata hivyo, ni dhahiri kwamba, wamekuwa wakikaa katika makazi ambayo hayaridhishi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili tuweze kuwapa motisha Polisi hawa, naiomba Serikali, tunajua kwamba, imetenga pesa kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za makazi ya Polisi katika maeneo ya Dodoma, Arusha pamoja na Dar es Salaam, lakini ukiangalia kwa mikoa ya pembezoni makazi yao ni duni sana na hayaridhishi. Mheshimiwa Waziri nakuomba sana tuwakumbuke Polisi, hususani katika mikoa ya pembezoni. Kwa kweli, makazi wanayokaa hayaridhishi, lakini pia, tuwakumbuke Polisi hawa katika maslahi mbalimbali kwa kweli, wanafanya kazi nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaweza tukawalaumu Jeshi la Polisi kwamba, wananingia katika rushwa, ni kwa sababu makazi wanayokaa ni duni na hata maslahi yao pia, ni duni. Naiomba sana Serikali kwa kuwa, Polisi hawa wanatumia nguvu kubwa sana kuhakikisha sisi pamoja na mali zetu tunakuwa salama, basi ni wakati wa kuboresha mazingira yao, ili yaweze kuwa safi na salama, lakini pia, na masilahi yao tuweze kuyaangalia ili Polisi wetu waweze kufanya kazi katika mazingira yaliyo salama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ningependa kulizungumzia ni kuhusiana na suala la Sayansi na Teknolojia katika majeshi yetu yote nchini likiwepo Jeshi la Magereza, Jeshi la Zimamoto pamoja na Jeshi la Uhamiaji. Naiomba sana Wizara, ni muda na wakati sahihi kabisa wa kutenga pesa, kwa ajili ya kuwekeza kwenye Sayansi na Teknolojia katika Jeshi letu hili la Polisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwananchi anapokwenda kutoa malalamiko yake pale anapokuwa amepata shida, badala ya wao kuandika katika makaratasi, basi ziwepo camera na vitendea kazi maalum ambavyo vinarekodi. Rekodi hiyo iweze kutunzwa, ili hata mtu anapokwenda katika hatua ya mahakama, awe na kumbukumbu nzuri na kuepusha ubabaishaji wa kubadili yale maelezo katika makarastasi ambapo mara nyingi watu wanakuwa wanaonewa katika kesi na hawapati haki zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuomba Mheshimiwa Waziri, kuna clip ambayo ilikuwa inasambaa mtandaoni ikionesha mama analalamika kwamba, mtoto wake amelawitiwa, amekwenda kutoa malalamiko yake katika Jeshi la Polisi, lakini Jeshi letu la polisi kwa kweli, halikumtendea haki mama yule. Kama jambo lile lilikuwa ni kweli, naiomba Wizara ya Mambo ya Ndani waweze kufuatilia jambo hilo ili kuhakikisha akinamama hawa ambao ni wahanga wakubwa kwa watoto wao ambao wamekuwa wakilawitiwa waweze kupata haki zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, inasikitisha sana mama anakwenda katika Jeshi letu la Polisi kutoa malalamiko yake, lakini kesi ile inakuwa inapigwa danadana na hapati haki yake. Naomba sana Jeshi la Polisi liweze kushughulikia malalamiko hayo. Pia, katika Mkoa wetu wa Katavi naomba sana tupate Wilaya ya Kipolisi. Tunapata adha kubwa wananchi kwenda katika Wilaya ya Inyonga, ni mbali. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante.

MHE. MARTHA F. MARIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja, lakini ninampongeza sana RPC wangu wa Mkoa wa Katavi, ni mwana mama. Kwa kweli, anaupiga mwingi na anashughulika na vijana wale wa damu chafu. Nakushukuru sana, ahsante. (Makofi)