Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, wewe Mheshimiwa Mwantum Dau nyamaza hapo. Ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia hotuba hii ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya mwaka 2024/2025.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza kumpongeza sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa juhudi zake za kimaendeleo kwa Nchi yetu ya Tanzania. Napongeza sana kwa kuridhia bajeti hii ambayo ina mchango mkubwa kwa usalama wa wananchi, mali zetu na utulivu ambayo ni chachu ya maendeleo kwa nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri, Engineer Hamad Masauni, ambaye ameimudu vyema Wizara hii na sisi wana-Jimbo la Kikwajuni na dada zake ametuheshimisha sana. Vilevile, nampongeza sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa jinsi anavyofuata nyayo na mambo kule Wizara ya Mambo ya Ndani yanakwenda bila shida. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza timu nzima ya Wizara kuanzia Makatibu Wakuu, Wakuu wa Vyombo vya Wizara hii na watendaji wote kwa sababu, mara hii mambo yenu yamekuwa mazuri hata malalamiko yamepungua sana. Kwa hiyo, mnaupiga mwingi pokeeni maua yenu Wakuu wa Vyombo na Watendaji wote wa Wizara ya Mambo ya Ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba nianze mchango wangu kwa taasisi hii ya Magereza. Nimeona hapa kumependekezwa kiasi kikubwa cha pesa kama shilingi 990, 000,104 kwa ajili ya kuandaa mitandao ya biogas (gesi vivunde) kwa kushirikiana na Taifa Gas na REA. Hata hivyo, ninapendekeza kwamba, waweze kutumia njia ya vinyesi vya watu na wanyama. Kwa kuwa, magereza mengi yana mifugo mingi, hivyo ni wakati mzuri wa kwenda na maelekezo ya Mheshimiwa Rais wetu ambaye amekuwa katika harakati kubwa za kuwezesha kuwa na matumizi endelevu ya hii nishati bila kukata miti na hivyo, kutunza mazingira. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, magereza yetu ni hazina kubwa ya kuonesha mfano wa matumizi ya nishati endelevu ya gesi ya kinyesi cha wafungwa na ng’ombe. Mifano ya matumizi ya kinyesi hiki ipo katika nchi jirani, unaweza kwenda kusoma kule Rwanda ambako shughuli zote za kimagereza zinatumia nishati hii. Kwa kutumia hii nishati ya vinyesi itapunguza gharama ambazo mtaingia katika mikataba mtakayoiweka baina ya REA na hiyo taasisi nyingine. Kwa kufanya hivi pia, itasaidia kuhifadhi mazingira katika zile sehemu za magereza kwa kupata nishati ya kutosha, kwa ajili ya matumizi mengine kama vile kuchemsha maji na kupikia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mavi ya ng’ombe au kinyesi cha ng’ombe, kama nilivyosema kwa vile magereza mengi yana mifugo kwa hiyo, ni kupata tu hii teknolojia ambayo ina msaada mkubwa na itapunguza gharama nyingi. Mitambo ya kuchakata gesi hii inapatikana kwa bei nafuu hapa nchini. Kwa mfano, hata sisi wenyewe kwenye shamba letu, Msonge Farm, tuna ng’ombe sita na tunapata gesi ya kutosha ya kutumia kwenye mambo yetu, kuwashia taa na kufanya mambo yote yanayohitaji gesi. Kwa hivyo, kwa magereza jambo hili litakuwa zuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ninalo kuhusu magereza ni kwamba, hawa watu wanafanya kazi kubwa sana, lakini mazingira yao wanayokaa ni hafifu na masilahi yao pia, ni madogo. Kwa hiyo, ninapendekeza wale askari wa magereza waboreshewe masilahi yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ni kuhusu magereza. Magereza mengi huko wilayani yamechoka sana mpaka yanavunja moyo, kwa mfano Gereza la Lushoto. Ninaiomba Serikali ifanye mapitio na kuyajenga upya magereza yote nchi nzima, ili kidogo yawe na sura ya kuwafanya wahalifu wasipende kuja kufungwa kwenye magereza kama yale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wangu naomba niwe na hayo tu, lakini napongeza sana mambo ambayo yanafanywa na Wizara hii. Kwa kweli, mnaupiga mwingi, pokeeni maua yenu. Naunga mkono hoja, ahsanteni.