Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
ACT
Constituent
Konde
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MOHAMED SAID ISSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili na mimi nitie neno kwenye Wizara hii ya Mambo ya Ndani ya Nchi. Sitapoteza muda kwanza nianze kwa Kituo cha Polisi Jimbo la Konde kilichopo pale Konde Mjini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari nimeshapata kuungwa mkono kwa sababu nitashika shilingi na watu wataniunga mkono. Hii ni kwa sababu Mheshimiwa Waziri katika bajeti tatu zilizopita zote ameniahidi kwamba kituo kile kinakwenda kujengwa pamoja na nyumba za makazi wa polisi pale. Kwa hiyo leo nitamshikia shilingi Mheshimiwa Waziri. Sasa nimwombe tu kabla sijashika shilingi leo alielezee Bunge hapa kwamba kituo kile kinakwenda kutengenezwa na isiwe tena ni hadithi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiendelea, mchango wangu wa pili nataka nizungumzie suala zima la ubaguzi. Leo Vyombo vya Ulinzi na Usalama vipo hapa kwa hiyo ningetamani sana kulielezea jambo hili. Sisi Wazanzibar tumekuwa tukibaguliwa kwenye mitandao, kwenye vyombo vya habari, kwenye mikutano hatujui sababu ni nini? Sasa jambo hili nilitamani nilichangie mimi leo ili Vyombo vya Ulinzi na Usalama vijue.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa tumekuwa tukisikia Mheshimiwa Rais akibaguliwa kwa Uzanzibar wake na mwisho anaambiwa kwamba amekopeshwa kutoka kule Zanzibar. Hili jambo si sahihi, mimi kama Mzanzibar kwa sababu siku yoyote naweza kuwa Rais wa nchi hii. Sasa naweza kuja kubaguliwa kama anavyobaguliwa Mheshimiwa Rais jambo hili si sahihi, naomba vyombo vyetu hivi vikemee siyo jambo sawa. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama anavyobaguliwa Mheshimiwa Rais kwa kuambiwa kwamba anatawala nchi ambayo siyo ya kwake, amekopeshwa hivihivi ndio anaweza kubaguliwa na mtu mwingine yoyote. Sasa jambo hili kama Mzanzibar anachaguliwa na hii ni Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania…
MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.
MWENYEKITI: Taarifa Mheshimiwa Anatropia.
TAARIFA
MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Nataka nimpe taarifa mchangiaji anayeongea vizuri sana. Sisi tunaamini ni raia wamoja, ni nchi moja ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lakini katika hali ya kusikitisha Mheshimiwa Mbunge alisimama hapa Bungeni akisema; “Wanaotoka Bara wapatiwe passport ya kwenda Zanzibar.” Sasa nataka kusema sisi ni nchi moja hatuhitaji passport ya kwenda Zanzibar au kuja Tanganyika, hiyo ndiyo taarifa yangu. (Makofi)
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Mohamed.
MHE. MOHAMED SAID ISSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo Taarifa siipokei.
MWENYEKITI: Subiri kwanza sijakuuliza. Unaipokea hiyo taarifa?
MHE. MOHAMED SAID ISSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa hiyo siipokei kwa sababu jambo hilo liko hadharani kila mtu amesikia kuna kikundi cha watu akiwemo Mwenyekiti Mbowe amekuwa akimbagua Rais pamoja na na kikundi chake. Sisemi CHADEMA ndiyo wanaofanya hivyo lakini wako watu hawa wamekuwa wakimbagua Rais pamoja na mimi mwenyewe kwa kuweka hii hoja ya passport…
MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.
MHE. MOHAMED SAID ISSA: … Hii ni hoja yangu mimi Mbunge huku nililetwa kuchangia kwa ajili ya wananchi wa Jimbo la Konde…
MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.
MHE. MOHAMED SAID ISSA: …Wananchi wa Zanzibar lakini na Watanzania sasa jambo hili si sahihi…
MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa
MWENYEKITI: Mheshimiwa Mohamed Issa, kuna Taarifa.
TAARIFA
MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimpe Taarifa Mheshimiwa Mbunge anayezungumza sasa yeye siyo Mzanzibar yeye ni Mtanzania. (Makofi)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Mohamed Issa unaipokea Taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Kunambi?
MHE. MOHAMED SAID ISSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, siipokei, Tanzania ni Muungano wa nchi mbili…
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.
MHE. MOHAMED SAID ISSA: …Zanzibar imeungana na Tanganyika ikiwa ni nchi mbili huru na mimi naamini kwamba ndani ya Tanzania kuna Tanzania bara (Tanganyika) na Zanzibar kwa hiyo siipokei. (Makofi/Kicheko)
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa
MHE. MOHAMED SAID ISSA: …Niacheni niendelee na hili suala la passport naomba mnipe muda niwaelezee vizuri sina nia ya kuvunja Muungano, sina nia ya kero za Muungano.
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.
MHE. MOHAMED SAID ISSA: …jambo hili mnalichukulia kama mzaha…
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.
MHE. MOHAMED SAID ISSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa zinatosha.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Mohamed Issa, kwa mujibu wa Kanuni Taarifa mwisho ni tatu. Taarifa ya mwisho Mheshimiwa Condester.
TAARIFA
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, tunataka kumweleza mwenzetu kwamba sisi Watanganyika na Wazanzibar ni kitu kimoja toka tumepata uhuru na wakati mwingine watu wakikosa hoja wanatafuta hata ambacho hakina sababu kusema. Kwa hiyo yule alikosa hoja na Watanzania wote tunajua alikuwa anasema hayo. Kwa hiyo yeye aridhie kwamba yeye ni Mtanzania mwenzetu hayo mambo yeye atulie tu.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Mohamed Issa unapokea Taarifa hiyo?
MHE. MOHAMED SAID ISSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, siipokei. Kwanza hili suala la kumbagua Rais huyu kwa sababu eti amekuwa Rais kutoka Zanzibar, nataka nitoe mfano mmoja CHADEMA kilimweka mgombea hapa Hayati Edward Lowassa na mgombea mwenza alikuwa ni Babu Juma Duni Haji. Tuseme leo angekuwa Rais Babu Juma Duni Haji wangesema wamemkopa?
MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.
MHE. MOHAMED SAID ISSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, hili jambo siyo sahihi ubaguzi huu hatuutaki na suala hili nililosema la passport nifuateni niwape clarification mtaelewa tu. Sikuwa na nia ya ubaguzi Wazanzibar waingie huku kwa passport Watanzania Bara waingie kule kwa passport na hakuna tatizo ni suala tu la kulinda visiwa. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Mohamed Issa Said muda wako wa kuchangia umekwisha
MHE. MOHAMED SAID ISSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. (Makofi)