Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi ili niweze kutoa mchango wangu kwenye Wizara hii muhimu. Kwa dakika jinsi zilivyo chache naomba nikimbie mchaka mchaka. Mheshimiwa Waziri tunashukuru Halmashauri ya Wilaya ya Chemba, jengo letu la Kituo cha Polisi cha Wilaya linaelekea ukingoni, lakini tunachoomba ni furniture. Katika bajeti hii tunahitaji furniture ili tuingie kwenye lile jengo na askari wetu wakae sehemu salama, tulivu, yenye hadhi ili waweze kutekeleza wajibu na majukumu yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusu fidia. Mheshimiwa Waziri, eneo lile lilichukuliwa wananchi wakiwa hawajalipwa fidia. Jengo limekamilika na tunakaribia kuingia. Wananchi wa Wilaya ya Chemba waliotoa eneo lile kwa ajili ya jengo la Kituo cha Polisi, Wilaya ya Chemba tunaomba, michakato yote ilishakwisha, sasa akija hapa atuambie fidia ile tunalipa lini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusiana na vituo viwili tulivyonavyo Wilaya ya Chemba. Nimekuwa nikiuliza maswali ya msingi hapa, nimeuliza na maswali ya nyongeza hapa kuhusiana na Kituo cha Kwa Mtoro pamoja na Mrijo. Tuliomba magari, bajeti iliyopita aliniahidi tungepata gari kwenye hivi vituo viwili, lakini mpaka leo hakuna gari. Tuliomba fedha kwa ajili ya kufanya ukarabati wa vituo vile mpaka leo ni kimya. Wananchi tumepambana lakini bado ukarabati wa majengo yale mawili, yaani Kituo cha Mrijo pamoja na Kwa Mtoro, bado vina changamoto kubwa. Kwa hiyo tunahitaji fedha kwa ajili ya kufanya ukarabati wa vituo vile. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna kituo kingine ambacho kimejengwa kwa nguvu za wananchi, Kituo cha Mondo, kiko pale, na tuna askari yuko pale. Watusaidie pia hiki kituo, waongeze fedha hiyo ili tuweze kukamilisha kile kituo na hatimaye tuweze kutoa huduma stahiki kwa wananchi wetu wa Halmashauri ya Wilaya ya Chemba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, naomba kulisemea suala la polisi kata. Tunashukuru Serikali waliliona hilo na wameamua kusogeza huduma ya usalama wa raia na mali zao kwenye maeneo ya wananchi wanakokaa. Hata hivyo watu hawa wa polisi kata hawana vitendeakazi, hawana hata usafiri. Tukio linatokea askari anaambiwa, lakini hana pikipiki wala baiskeli; atembee kwa miguu mpaka aende akafike eneo la tukio mhalifu alishaondoka. Kwa hiyo askari hawa wanashindwa kufanya kazi na wako kule. Mwisho wa siku wananchi wanaona wamekwenda pale si kwa ajili ya kazi kwa sababu wakifika pale wanapoitwa hawafiki kwa wakati. Naomba na kushauri kuwa polisi kata wetu ambao wako kwenye kata zetu kwenye halmashauri zote nchini wapewe usafiri, kwa maana ya pikipiki ili waweze kutimiza wajibu na majukumu yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la posho za safari kwa askari wetu wote na kwa majeshi yote. Posho hizi moja ni kidogo, lakini pili hazitolewi kwa wakati. Kwa mfano tuna Kituo cha Polisi Mrijo na tuna Mahakama ya Mwanzo Mrijo. Mhalifu huyu akikamatwa na akipelekwa Mahakamani, akikutwa na hatia polisi anatakiwa kumchukua huyu mhalifu ampeleke Kondoa Magereza. Anatumia gharama zake, amsafirishe mtuhumiwa ama mshtakiwa yule, ajisafirishe yeye mwenyewe, amlishe na ahakikishe kwamba amemfikisha kwenye mikono salama. Gharama hizi hawa askari wakija kuziomba wanakaa miaka na miaka hawalipwi hizi stahiki zao. Kwa hiyo tunaomba sana Mheshimiwa Waziri, posho za maaskari wetu ziongezwe, lakini pia ziwe zinatolewa kwa wakati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusiana pia na suala la hela za uhamisho. Mimi nina askari kadhaa waliokuwa Wilaya ya Chemba, wamehamishwa wamepelekwa kwenye maeneo mbalimbali, lakini hadi leo hawajalipwa stahiki zao za uhamisho. Tunaomba walipwe hela zao za uhamisho. Kama Serikali haiwezi kulipa fedha za uhamisho, hatuna sababu ya kuwahamisha watu hawa kwa sababu hatuwatendei haki. Wewe umeamua kuniondoa, nipe changu, nisepe tumalizane, lakini watu hawa hawataki kuwalipa, ni kwa nini? Wana miaka minne hadi miaka mitano hawajawalipwa hela zao za uhamisho. Kwa hiyo naomba sana na Mheshimiwa Waziri atakapokuja atuambie kwamba, ni lini watalipa fedha za uhamisho za askari wetu ili na wao waweze kuona kwamba wanapotoa huduma wanathaminiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la OC. Halikadhalika OC hizi zinatolewa flat rate. Haijalishi eneo hili ni kubwa kiasi gani na kwamba anahudumiaje, ni hiyo hiyo moja. Kwa hiyo suala hili nalo pia liangaliwe, hizi OC zinapotolewa, waangalie na maeneo. Leo Halmashauri ya Wilaya ya Chemba ina kata 26, vijiji 114, vitongoji 432, haiwezekani kwenye OC huyu ukampa shilingi milioni na wa Dodoma Mjini ukampa shilingi milioni, sijui na wapi ukampa shilingi milioni, haiwezekani! Watu hawa wana mahitaji makubwa na yanatofautiana. Kwa hiyo tuangalie tunapokwenda kutoa suala zima la OC, tuangalie, tutoke kwenye flat rate twende sasa tukaangalie na ukubwa wa maeneo yao husika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni suala la magereza. Wilaya ya Chemba hatuna gereza. Kama nilivyosema, watuhumiwa wakipatwa na hatia tunatoa kule tunawapeleka Kondoa. Hizo gharama ni kubwa, tunahitaji gereza katika Wilaya ya Chemba ili na sisi watu wetu wanapokutwa na makosa mbalimbali, basi waweze kuhudumiwa kwenye eneo lao husika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, nimwombe Mheshimiwa Waziri, tuna magari mawili pale, la OCD pamoja na OC-CID. Yale magari ni hoi bin taaban. Juzi wamesafiri, wameishia njiani wameshindwa kufika kwenye eneo la tukio, tairi zimepasuka. Hivi hata tairi ya shilingi 250,000, Wizara hawawezi kuwasaidia hawa watu wakapata tairi? Tunawaomba tafadhali tuwatendee haki. Watu hawa wanafanya kazi kubwa na kwenye mazingira magumu, wanalihudumia Taifa lao. Kwa hiyo zile stahiki zao zinazohitajika na vitendea kazi vyao tunaomba wapatiwe ili waweze kutimiza wajibu na majukumu yao wakiwa na roho kunjufu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa muda. (Makofi)