Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. AGNES M. MARWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza moja kwa moja kwa kumpongeza sana Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa upendo wake mkubwa aliouonesha kwa vijana wa Kitanzania. Baada tu ya Waziri wetu Mheshimiwa Masauni kumshauri kuwa vijana wanaomba ajira, lakini vigezo vya kwamba mpaka wawe na cheti cha JKT ndicho kikwazo, Mheshimiwa Rais kwa sababu ni msikivu, ni mama na ni mlezi amekubali na sasa vijana wanaomba kazi wakiwa wako huru kabisa. Tunampongeza kwa kweli, tunamshukuu sana Mama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea pia kumpongeza Mheshimiwa Waziri wetu Masauni, pia kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu kwa kutoa pesa nyingi kwa Mkoa wetu wa Mara kwa ajili ya miradi mbalimbali ikiwemo miradi ya ujenzi wa nyumba za askari wetu. Mkoani kwetu Mara, ukija pale Musoma Mjini panang’ara, yaani ukipaangalia ni maghorofa ya polisi ambayo yameng’ara. Kwa kweli nampongeza sana Mheshimiwa Rais wetu. Wanasema kwamba mwenye nacho huongezewa, basi namwomba Mheshimiwa Waziri wetu, hata kwa Askari Magereza atuongezee pia pale maghorofa kusudi Mkoani kwetu Mara paendelee kung’ara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee naomba sasa gereza lijengwe pale Wilaya ya Butiama kwa sababu ni wilaya ya mfano. Taifa zima linajua, ulimwengu mzima unajua kwamba Butiama ndiko alikotokea muasisi wa Taifa hili la Tanzania, Mkombozi wa Taifa la Tanzania na kwa hiyo panapaswa kuwa ni wilaya ya mfano, kwa hiyo ni wilaya ambayo miundombinu yake mbalimbali inapaswa iangaliwe. Kwa kweli hili nimwombe Mheshimiwa Waziri Masauni aliangalie kwa jicho la pili, naamini kabisa mama yetu kipenzi, mama yangu mimi Chifu Hangaya anasikia, atakwenda kufanya mambo katika Wilaya ya Butiama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naungana na wenzangu kuwasemea hawa ndugu zetu wa Jeshi la Polisi, Magereza, Uhamiaji na Zimamoto kwa sababu inajulikana wazi kabisa kwamba mishahara yao kwa kweli ni midogo ukilinganisha na hali halisi ya maisha ya sasa ya Tanzania. Sasa ukiwaongezea tena na kikokotoo mambo yanakuwa siyo shwari. Unaweza ukakuta hata ndoa zao nyingi tunasikia zinavunjika na askari wengine wanajinyonga ni kwa sababu tu ya hali ngumu ya maisha. Kwa hiyo namwomba sana Mheshimiwa Waziri, kwa sababu anapomshauri Mama, Mama huwa anasikia, basi aende akamshauri tena kuhusiana na hili kwamba aliangalie suala la kikokotoo kwa majeshi haya. Tunajua mama analishughulikia na tunajua atafanya jambo. Kuhusiana na masuala ya ongezeko la mishahara na mambo mengine, tunajua kabisa mama ni mlezi, kuna jambo anafanya. Naamini kabisa siku moja mambo yatakuwa vizuri, kwa hiyo wasiwe na wasiwasi kwa hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema kipekee kabisa, kwamba Mkoa wa Mara ni mkoa uliokaa kimkakati, lakini ni mkoa wenye matukio mengi kama inavyojulikana, kwa hiyo ni mkoa ambao tunapaswa kuwa na magari mengi ya kipolisi. Kwa hiyo magari haya ya polisi yatakapokuja basi mimi naomba Mkoa wa Mara uwe ni kati ya mikoa ya mfano na uwe ni mkoa wa upendeleo ambao wataanza kuyapeleka magari haya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia kwenye suala la risiti. nimevuta kidogo nimeshindwa kuliongelea vizuri, suala la risiti, risiti zinakatwa, kwa mfano mimi nikiwa nimepoteza kadi yangu ya benki, nikiwa nimepoteza kadi yangu labda ya gari, kadi mbili, nikienda Kituo cha Polisi, nalipia shilingi 3,000 ya kadi ya benki, nalipia shilingi 3,000 ya kadi na NIDA lakini napewa risiti ya shilingi 1,500 peke yake. Sasa swali langu, zile pesa nyingine zinakwenda wapi? Basi tuangalie kwa wale wenzetu ambao kidogo hawana uaminifu, waangalie hizi pesa ziingie Serikalini kwa sababu tunajiuliza. Labda Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa pia atuelezee kwamba hizo pesa nyingine huwa zinakwenda wapi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee zaidi nampongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa kazi nzuri sana anayoifanya, lakini nampongeza sana RPC wetu wa Mkoa wa Mara kwa kazi nzuri anazozifanya, Mkoa wa Mara umetulia tulii. Nampongeza sana IGP, Tanzania sasa imetulia, ina utulivu wa kutosha na naamini kabisa yeye anafanya kimyakimya, lakini mambo yanakwenda. Nawapongeza sana Jeshi la Polisi na Majeshi mengine kwa ujumla, Mwenyezi Mungu awabariki sana kwa kuleta utulivu Tanzania.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. AGNES M. MARWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)
MWENYEKITI: Ahsante sana. Namwita sasa…
MHE. AGNES M. MARWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)