Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Ritta Enespher Kabati

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niwe mchangiaji jioni ya leo. Naomba kumtanguliza Mwenyezi Mungu katika mchango wangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa pongezi kubwa sana kwa Mheshimiwa Rais wetu ambaye ni Amiri Jeshi Mkuu, naomba tu nipige saluti kwake, kwamba amefanya kazi nzuri sana katika kuiongoza nchi hii na kuhakikisha kwamba usalama unapatikana katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri wetu Masauni kwa kazi nzuri, lakini pia nampongeza Naibu Waziri Mheshimiwa Sillo kwa kuteuliwa kuingia katika Wizara hii, tunajua wameitendea haki. Pia nawapongeza wakuu wote wa vyombo vya usalama bila kumsahau Commissioner General dada yetu Dkt. Anna Makakala ambaye anatuwakilisha sisi wanawake hapo juu kabisa katika jeshi, anatenda haki. Sasa hivi pasipoti zinapatikana kwa haraka sana, hongera sana, lakini pia hatugongi tena mihuri airport, kwa hiyo ni big up kabisa katika kazi yake. Pia nampongeza RPC wetu wa Mkoa wa Iringa kwa kazi nzuri na askari wote wa Mkoa wetu wa Iringa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna changamoto nyingi katika Mkoa wa Iringa. Kwanza kuna uhaba mkubwa sana wa askari katika vituo vya polisi, lakini pia kuna uhaba wa magari katika mkoa wetu, pia hawana hata fedha kwa ajili ya mafuta na kwa hiyo wanapata shida sana. Tuna magari ambayo hayatengenezeki kwa sababu hawana OC za kutengeneza magari, kwa hiyo magari yanachukua muda mchache sana kuharibika kwa sababu hayafanyiwi ukarabati mkubwa. Tunaomba Mkoa wa Iringa uletewe pesa za kutosha. Pia makazi ya askari, kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Mjini, kwa kweli ni changamoto kubwa sana. Tunaomba Mkoa wa Iringa tuangaliwe, nyumba nyingi zijengwe kwa sababu askari wengi wanaishi uraiani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja sasa katika Jeshi la Magereza, pia waangaliwe posho zao na makazi yao. Naomba sasa Serikali iangalie uwezekano wa kuhamisha Gereza la Kihesa Mgagao. Hili gereza libadilishiwe matumizi kwa sababu Tanzania tuna dhana kubwa sana ya kulinda historia za wenzetu. Pale kulikuwa ni kambi ya wakimbizi, kuna Waheshimiwa Marais ambao walitetea nchi zao, kwa mfano Nelson Mandela na Walter Sisulu walikaa pale. Sasa hivi tunaomba lile gereza liondoke ili tuweke historia. Kuna makaburi pale. Tayari Waheshimiwa Wabunge waliopita wote walikuwa wameomba kwamba lile gereza lihamishwe na wakakubaliana kwamba litafutwe eneo ili wale mahabusu, kwa sababu pale kuna mahabusu tu, waondolewe ili pale tuendelee kutengeneza historia za wenzetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna nchi zinataka kuja kutembelea katika kile kituo ambacho waliishi, wanashindwa kuja kwa sababu kuna gereza. Kwa hiyo naomba na ikiwezekana Mheshimiwa Waziri aje Kihesa Mgagao aje aone ili tufanye utaratibu wa kuhamisha lile gereza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tuna tatizo hilohilo la magereza. Kuna mwingiliano mkubwa sana katika gereza la mkoa, pia kuna mwingiliano katika hospitali ya mkoa, kuna changamoto kubwa sana. Sasa hivi, hakuna nyumba za madaktari lakini kunatakiwa majengo mengi yawepo katika hospitali yetu ya mkoa. Kutokana na ule mwingiliano unaweza ukakuta wafungwa wanatolewa kwenye gereza upande mwingine na ambulance inaingia hospitali. Kwa hiyo kunakuwa kuna shida sana, kuna wagonjwa wanapata matatizo makubwa. Iringa kuna eneo kubwa kule Mlolo, naomba ikiwezekana Serikali itoe pesa. Tayari tulishaanza huo mchakato, gereza lihamie Mlolo, kuna eneo kubwa kule ili kupisha uendelezaji wa Hospitali ya Iringa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia kupongeza sana Serikali kwa ujenzi wa Jengo la Polisi Kilolo. Naomba sasa waongezee zahanati za polisi na magereza ambazo zinasaidia sana huduma kwa wananchi. Basi nao wapewe dawa na vifaa vya matibabu ili waendelee kuwasaidia raia ambao wapo karibu na kambi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Jeshi la Zimamoto, nawapongeza sana. Napongeza kwamba wamepatiwa magari ya zimamoto. Naomba Mkoa wa Iringa uangaliwe katika hayo magari. Tunayo mazao ya misitu katika Wilaya za Kilolo na Mufindi ambako moto unatokea kila wakati. Wananchi na hata Serikali wanapata hasara kwa sababu ya moto wa kila wakati. Kwa hiyo naomba kila wilaya kuwepo na gari la zimamoto ili inapotokea moto wowote iweze kusaidiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na ajali nyingi sana katika Mito ya Ruaha na Lukosi, watoto wamekuwa wakipata tatizo kubwa. Hakuna vyombo vya uokozi katika Jeshi la Zimamoto. Juzi tu pale Mahenge kuna mtoto wa miaka 15 amezama kwenye maji na wameshindwa kumuokoa kwa sababu hakuna vifaa. Kwa hiyo naomba hili liangaliwe, tuletewe vifaa vya uokozi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia kuendelea kulipongeza Jeshi la Polisi, lakini naomba sasa hivi tujengewe vituo vingi vya polisi kwani vimechakaa sana. Tunaomba tuletewe gari pia katika Kituo cha Polisi ya Ruaha Mbuyuni, kimekuwa kikifanya kazi kubwa sana lakini hakuna gari la polisi. Kuna ajali nyingi zinatokea pale katika Mlima Kitonga. Pia imekuwa ikisaidia mpaka Jimbo la Mikumi pamoja na Jimbo la Kibakwe. Kwa hiyo naomba sana gari la polisi katika Kituo cha Ruaha Mbuyuni…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante.

MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)