Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Lindi Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa kazi kubwa nzuri anayoifanya pamoja na timu yake katika kuhakikisha kwamba wanaendelea kuleta mapinduzi makubwa katika Sekta hii ya Ulinzi na Usalama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana nchi yetu sasa imendelea kuwa na amani utulivu wa kutosha na hatimaye hata waganga njaa mitaani wameendelea kufanya mikutano kwa amani kubwa. Japokuwa wameendelea kumtukana Mheshimiwa Rais wetu, lakini sisi wenye akili timamu tuko vizuri kuhakikisha kwamba tunaendelea kumlinda Mheshimiwa Rais wetu na kuhakikisha kwamba mwaka 2025 mpaka 2030 tutaendelea kuwa naye. Niendelee kumpongeza Mheshimiwa Rais, amekuwa mtulivu sana hatujawahi kusikia hata siku moja akitoa majibu kwa watu ambao hawajitambui. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la Magereza – Lindi, kwa sababu muda hautoshi, lakini niseme tu kwamba kwanza jambo la kwanza nimwombe Mheshimiwa Waziri ama Naibu Waziri kuja Lindi kufanya ziara maalum ya kutembelea majengo ya Magereza pamoja na nyumba za watumishi wa Magereza na nyumba za watumishi wa Polisi. Maana yake yawezekana mimi nikisema hapa Mheshimiwa Waziri hatonielewa, kwa hiyo nimwombe afanye ziara rasmi ya kuja Lindi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri, bajeti ya 2023/2024 walitenga fedha milioni 800 kujenga majengo ya utawala ya ofisi za Magereza katika mikoa mitano ikiwepo Lindi. Sasa tuko robo ya mwisho wa mwaka, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri kuhakikisha kwamba fedha hizi zinakuja ili tuboreshe kujenga ofisi ya Magereza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini magereza ya Lindi ni magereza kuu. Magereza ambayo wale wafungwa waliohukumiwa kunyongwa maana yake wanakaa pale kusubiria. Wafungwa walioshindikana katika maeneo mengine wanaletwa pale, wafungwa wa muda mrefu, wanaletwa pale Lindi lakini hali ya magereza ya Lindi ni mbaya sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mabati yametoboka, jua likiwaka wanalo kwenye mabweni, mvua zikinyesha wanaendelea kutaabika wafungwa hawa. Kwa hiyo, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri kuhakikisha tunapata fedha kwenda kukarabati ili kuweka hali salama. Pia Magereza ile haina uzio maana yake mabwenini mtu akichomoka akapanda juu ya ukuta anaondoka zake. Ndiyo magereza ya kwanza ya aina hiyo, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri aje Lindi athibitishe hayo na aone namna ya kutusaidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wake za Polisi pamoja na Polisi wanawake wameniomba kwamba, tunaomba tupate hali ya utulivu, amani kuhakikisha kwamba tunapata nyumba safi na salama ili waweze kuishi vizuri na familia zao. Najua kwamba kuna changamoto nchi nzima Tanzania, kila kona nyumba za Polisi ni mgogoro, nyumba zilizokuwepo ni za muda mrefu zimepitwa na wakati. Mheshimiwa Masauni ana kazi kubwa sana ya kuhakikisha kwamba anatafuta fedha ili kuboresha nyumba za maaskari wetu waweze kukaa salama na wapate utulivu wa kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri wametupatia fedha zaidi ya bilioni moja kujenga Kituo cha Polisi Daraja A na ni kituo cha mfano Kanda ya Kusini ambacho kimekamilika. Changamoto iliyopo furniture za kisasa hatuna na jengo limeshakamilika, ni Mheshimiwa Masauni kujiandaa kuja kufanya uzinduzi kuhakikisha jengo lile akishatupatia furniture linaanza kutumika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto kubwa nyingine, tumejenga majengo ya Mahakama ya kisasa ya watoto ya wilaya na mkoa, tumejenga jengo la uhamiaji, tuna ofisi za TAKUKURU nzuri za kisasa, lakini changamoto kubwa ni vitendea kazi, hawana magari wale wenzetu wa TAKUKURU, wengi wana magari yao binafsi, kwa hiyo, wanatumia hayo, lakini Maafisa Uhamiaji ni changamoto hawana magari, Zimamoto changamoto hawana magari, hawana majengo ya ofisi wala vifaa vya uokoaji. Sisi tuliokuwa kanda ya pwani ya bahari ni changamoto, tunapata na kunatokea matukio mengi ya ajali. Kwa hiyo, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri kuhakikisha kwamba maeneo hayo anayatazama kwa jicho la huruma kuhakikisha vifaa hivi vinapatikana ili maafisa wetu wajisikie amani kuwa na vyombo vya usafiri ili waweze kufanya kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Afisa Uhamiaji anapotoka kwenda wilayani kuangalia maendeleo ya kazi zake ni mbaya sana kuona anakwenda stendi kupanda basi ili asafiri, ni changamoto. Kwa hiyo, hebu tuwape heshima zao maafisa hawa wapate magari ili waweze kusimamia kazi zao vizuri ili wajisikie amani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kumshukuru sana Mheshimiwa Waziri na timu yake, najua kwamba wameendelea kufanya kazi nzuri, bajeti yao ina mambo mengi, mambo ya maendeleo, mambo makubwa ya mapinduzi katika nchi yetu. Niendelee kuwapongeza sana maaskari wetu wa Jeshi la Ulinzi na Usalama, wanaendelea kutufanyia kazi nzuri, ni wazalendo wa kweli japokuwa mazingira yao ya kazi siyo salama sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja na ahsante sana. (Makofi)