Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Juma Othman Hija

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tumbatu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. JUMA OTHMAN HIJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi. Niungane na wenzangu jioni hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia kuwepo hapa leo tukiwa hatujambo, Mwenyezi Mungu In Shaa Allah aendelee kutupa afya njema kutekeleza wajibu wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, nami sina budi kuungana na wenzangu kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wetu Mama Samia kwa namna anavyofanya kazi za kutuletea maendeleo katika nchi yetu. Mheshimiwa Rais amekaa muda mfupi lakini mambo ambayo ameyafanya ni mengi sana, sote Watanzania hatuna budi kuendelea kumwombea kheri Mwenyezi Mungu ampe wepesi wa kutekeleza mambo yake haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea pia kumpongeza Mheshimiwa Waziri pamoja na watendaji wake wote kwa namna walivyowasilisha, walivyotayarisha hotuba hii na hatimaye kuiwasilisha kwa ufasaha zaidi. Hotuba ya mara hii ni hotuba ya viwango kabisa. Hotuba yao ya mara hii ina vipaumbele sita, bajeti yao ya mara hii ina vipaumbele sita. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja katika vipaumbele hivyo kipaumbele namba mbili kinasema kwamba nanukuu kukamilisha, kuendeleza ujenzi vituo na makazi ya askari. Kipaumbele hiki ndicho ambacho mimi kwa leo nitakuwa nachangia katika maeneo haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kushukuru sana Serikali yetu hii ya muungano kwa kuendeleza kituo chetu cha Kisiwa cha Tumbatu. Kituo kimefika hatua nzuri kama 60%, sasa hivi kimeshakamilika lakini kituo hiki kama Serikali haitojenga makazi basi ubora wa kituo kile hautaonekana, ni lazima Serikali ijenge makazi kwa wananchi wale. Bila ya makazi kutokana na jiografia ya pale, basi kile kituo kitakuwa kipo tu vilevile, hakina kazi yoyote. Kwa hivyo tunaomba kwamba Serikali ichukue juhudi ya makusudi kujenga makazi katika Kituo cha Polisi cha Tumbatu kwa ajili ya mustakabali wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali kadhalika katika Jimbo langu kuna vituo viwili; kimoja hicho cha Tumbatu ambacho ni kipya lakini pia kuna Kituo cha Mkokotoni ambacho ni cha zamani sana, nacho vilevile hali ya makazi ya pale ni mbovu sana kiasi ambacho inasikitisha sana. Kwa hivyo, kwa dhana ile ile naomba kituo kile nacho kifikiriwe makazi ya askari wetu pale Mkokotoni, wajengewe maslahi mapana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Tumbatu sisi tuna wananchi wa kule tumetenga eneo makusudi la kuwapa askari kama hamna eneo. Kwa sisi tumetenga eneo makusudi kwa ajili ya makazi ya maaskari pale kwa hivyo, hamna haja ya kuja Tumbatu wakanunua eneo, sisi kule maeneo hatuuzi, wao waje tuwakatie wajenge makazi ya maaskari wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania forum zetu za kuelezea maendeleo ya Serikali hii ni sehemu ya pili. Moja hapa Bungeni lakini nyingine ni katika maeneo yetu ya kazi, unapotokezea mradi wa kazi katika eneo lako kwa mfano kama hiki Kituo cha Polisi. Sehemu ile ni sehemu muhimu sana kwa Mbunge kuwepo pale kuelezea na kuisifu Serikali yetu, haipendezi hata kidogo kuona kwamba hii Wizara ya Mambo ya Ndani inakwenda katika sehemu ya mradi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano kama kwangu mie wamekwenda wameweka jiwe la msingi katika Kituo cha Polisi cha Tumbatu, uongozi hauna habari kwa maana ya mimi kama Mbunge sina habari pale. Kitendo kile hakina afya hata kidogo kwa maslahi yetu na maslahi ya Taifa, ni lazima tushirikishwe, tunaambiwa tu kila siku kwamba sisi Wabunge tufuatilie miradi, tusimamie, tuelekeze na hamna wenyeji. Kitendo kile cha kutia jiwe la msingi katika Kituo cha Tumbatu cha Polisi bila kushirikishwa Mbunge na wengine na mambo mengine hakina afya kwa Taifa hili. Kwa hivyo, tunaomba, Mheshimiwa Waziri ni miongoni mwa Mawaziri wazuri, anachapa kazi sana sana. Sasa asiruhusu mambo haya madogo madogo yakamtia doa, jaribu kuyashikilia sana haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo sina mengi, kwa haya yangu machache, naunga mkono hoja. (Makofi)