Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda na Biashara kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Kilumbe Shabani Ng'enda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigoma Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda na Biashara kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na ninaanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kutujalia afya na uhai.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaka kuanza mchango wangu kwa kuweka falsafa ambayo nafikiri inaweza ikatusaidia sana katika kuona ni nini mwelekeo wa kibiashara. Duniani nchi zote zinapimwa na kuwa na nguvu, kwanza kabisa kwa uchumi. Uchumi una mambo ambayo yanasababisha huo uchumi uwe katika nguvu na uhakika ambao unahitajika kwa mazingira ya sasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiacha nchi ambazo zimejaliwa na Mungu kuwa na maliasili zinazowafanya wawe na nguvu za kiuchumi kama mafuta, gesi, dhahabu, almasi na nyingine, njia nyingine ambayo imezifanya nchi duniani kuwa na uchumi mzuri ni kuelimisha watu wake na kuwa na technology. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo ukiangalia nchi kama Japani na nchi nyingine zote ambao ni ma-giant katika masuala ya viwanda, wanatengeneza magari, wanatengeneza ndege wanatengeneza nini, nao wamekuwa na hali nzuri sana kiuchumi kwa sababu wamewekeza katika elimu na maarifa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ukikosa maeneo yote hayo mawili au ukiwa unapata kidogokidogo katika hayo maeneo mawili, eneo la maliasili una maliasili lakini ambazo siyo muhimu zinazohitajika sana duniani au kama unazo ni kwa kiwango kidogo, una elimu au technology kwa kiwango kidogo, eneo lingine linaloweza kukuokoa ni biashara. Biashara kwa maana ya kufika mahali kuchukua vitu kutoka kwa wazalishaji kupeleka kwa wahitaji na kutengeneza faida. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nimeamua niseme haya kwa sababu Wizara hii ya Biashara bado bado ina kazi kubwa ya kuhakikisha kwamba jambo hili la kuhakikisha Taifa letu linaziba mianya ambayo tunaikosa katika maliasili, tunaikosa katika elimu na maarifa, tuweze kupata kupitia biashara, bado hatujakaa vizuri sana. Ukishakosa hayo yote duniani, kinachofuata wewe ni kuwa nguvukazi tu, mpagazi wa wengine duniani, ukishakosa yote hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi Mungu katujalia maliasili tunayo kiasi, elimu na maarifa tunayo ingawa siyo ya kujivunia sana maana mpaka sasa hatujaweza hata kutengeneza fork lifts za kubeba mizigo yetu bandarini, ila tunaweza kutengeneza mashine za kufyatua tofali. Sasa, hatuwezi kujisifia katika hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa jambo pekee linaloweza kutusaidia kutuongezea hizi nguvu ni biashara. Kwa nini ninasema biashara? Kwa sababu biashara ina vigezo na mihimili yake. Ukishakuwa na bandari, ukishakuwa na barabara, ukishakuwa na reli, halafu huko vinakoelekea yaani majirani zako wana mahitaji ya vitu vinapita kwako, unaweza kufanya biashara vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mpaka sasa ukienda katika takwimu zilizotolewa, nilizitoa hapa na nitarudia kuzitoa; takwimu zilizotolea na Baraza la Biashara la Afrika Mashariki katika mwaka 2019 – 2021, nchi jirani yetu (DRC Congo) ambayo 80% - 85% ya mahitaji yake ya bidhaa mbalimbali wana-import kutoka nje, China ndiyo Taifa la kwanza linalofanya biashara kubwa na Congo. Linalofuata ni South Africa; nchi ya tatu inayofuata ni Zambia, ya nne Kenya, ya tano Rwanda, sisi Tanzania ambao tuna mpaka na DRC Congo ni wa saba. Hatujawa serious, tumeshindwa kufanya biashara pamoja na bandari tuliyonayo na miundombinu na ujirani tulionao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunapofika mahali tukasema dada yangu Mheshimiwa Ashatu na Naibu wako mmekabidhiwa kazi ya kuleta msisimko wa kibiashara ili uchangie katika pato la Taifa, lazima mwende mbele zaidi kujiongeza kuangalia fursa zilizopo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii sasa imefika mahali sisi badala ya kuwapelekea Congo, sasa Congo wameanza kutuletea bidhaa. Kuna Wachina wameanzisha kiwanda cha saruji kinaitwa Great Lakes Cement, kule Kabimba DRC ambao sasa wameanza kuingiza cement pale Kigoma inaitwa GLC.

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.

NAIBU SPIKA: Taarifa.
TAARIFA

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kumwongezea Mheshimiwa Kilumbe kwamba, pamoja na kuwa na bandari zaidi ya saba kwenye Ziwa Tanganyika lakini bado hatuwezi kuifikia Congo moja kwa moja. Wizara ya Uchukuzi pia wana jambo la kufanya. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kilumbe.

MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, naipokea taarifa kwa mikono miwili.

NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri, Taarifa. (Makofi)

TAARIFA

NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, sitaki kuingilia mchango mzuri anaotoa Mheshimiwa Mbunge ambaye ninakubaliana naye, ni kwamba lile neno alilosema kwamba hatuko serious, nataka nimhakikishie kwamba Serikali hii iko serious. Tunajenga reli tuifikie Congo, tunajenga bandari tuifikie Congo, tunajenga meli za kutosha tuifikie Congo. (Makofi)

MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, sina hakika kama ile taarifa nilikuwa napewa mimi. Nafikiri taarifa alikuwa anapewa mtoa taarifa.

WABUNGE FULANI: Ni wewe.

MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Alikuwa ananipa mimi?

WABUNGE FULANI: Ndiyo.

MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Ah, basi tutajadiliana, nafikiri tuna jambo la kujadiliana. (Kicheko)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kilumbe, endelea na mchango wako.

MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ninachokusudia kusema ni kwamba tunatakiwa sisi kama Taifa tuangalie opportunity na kuzitumia kwa wakati. Sasa hivi inaelekea sasa kama tunaanza kuchelewa na hilo soko la Ukanda wa Ziwa Tanganyika kwa sababu mataifa makubwa yanakwenda kuwekeza huko. Hata pale ambapo sisi wenyewe tunaweka mipango kama aliyoisema sasa hivi Mheshimiwa Naibu Waziri kwenye taarifa yake, suala ni kwamba tuna mipango mingi, utekelezaji na wakati ndiyo tatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano pale Kigoma kuna eneo sasa hivi lina zaidi ya miaka saba, linaitwa Kigoma Special Economic Zone. Yaani unaamua kuwa na special economic zone, unatenga ardhi unaacha ina miti, ina magugu, haina barabara, haina maji, haina umeme, unasema hili eneo la uwekezaji. Uwekezaji wa nini? Kufuga ng’ombe! (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hapo ndiyo inaonekana kwamba hatuko serious. Unasema hili eneo ni la uwekezaji, basi eneo hilo la uwekezaji lazima uliwekee miundombinu. Ninyi mmekwenda mpaka Dubai huko kuona maeneo ya uwekezaji, ukifika pale kama ni kiwanda unaweka mitambo yako unafunga unaanza kazi. Yaani mwekezaji aanze kuja kutoa magugu na kung’oa miti na kutengeneza barabara? Kwa hiyo, niseme kwamba lazima tuongeze kasi katika maeneo haya. Tusipoongeza kasi kwa kweli mambo yataendelea kuwa siyo mazuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, siyo hilo tu, mchango wa vyombo vyetu vya fedha katika kusisimua biashara nchini bado ni mdogo sana na ndiyo maana wawekezaji wengi wakubwa wanapofika mahali wakataka kuwekeza nchini, lazima waende kwenye vyombo vya fedha vya nje ili viweze kuwasaidia katika uwekezaji wao. Vinginevyo ikifika mahali wakaamua kutumia benki zetu, riba zetu siyo rafiki. Bado tuna benki haziheshimu tafiti, tuna benki haziheshimu idea, benki zinaheshimu collateral (mali ambayo inaonekana). Yaani huwezi kwenda na andiko na idea ukapewa fedha. Wanakuuliza una nyumba? Una nini? Mambo ya kizamani kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mawazo kama ya Mheshimiwa Prof. Muhongo yale yanazidi nyumba, yanazidi ardhi. Unawekeza kwenye wazo, ilimradi umeita wataalamu wako wamekaa wameona wazo hili litaitoa nchi, litaleta ajira kwa watu, unatoa fedha. Benki zetu bado unafika mahali unakwenda na mradi mkubwa wanakuuliza ehe, sasa dhamana! Yaani wazo hili halitoshi kuwa dhamana? Lazima tubadilike. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimalizie kwa kuomba Serikali iliangalie sana sana eneo la Kigoma. Siyo kwa sababu ni mkoa ninaotoka mimi au kuna jimbo ninalotoka mimi. Iliangalie eneo la Kigoma kama eneo ambalo linaweza likatumika kama hub ya kibiashara baina yetu na nchi za Congo, Burundi na Zambia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. (Makofi)