Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda na Biashara kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Sophia Hebron Mwakagenda

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda na Biashara kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru nami kupata nafasi tena ya kuchangia Wizara hii muhimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kimsingi wewe ni msimamizi wa sera, lakini kwenye maamuzi au utekelezaji inakuwia vigumu sana. Nasema hivyo kwa sababu viwanda kuna wakati mwingine vinakwenda kwenye kilimo, leo hii ninapotaka kuzungumzia kiwanda cha chai kilichopo katika Wilaya ya Rungwe kilichofungwa bila kufuata utaratibu na kutokulipa wafanyakazi mafao yao, nikikulaumu wewe Waziri wa Kilimo nae anakisimamia kiwanda hicho.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa sijafahamu tunafanyaje kama Taifa ili tunapokulaumu wewe mwenye kiwanda ujue namna gani utatusaidia. Mheshimiwa Waziri kuna shida hata ya viwanda ambavyo umevionesha katika hotuba yako kwamba kuna viwanda 70, viwanda 100, au 2,000 vimeanzishwa lakini usimamizi wake, wawekezaji wale jinsi ya kuwalipa wafanyakazi mafao yao, masaa yao ya kazi na haki zao, mwisho wa siku tukija kwako tunakwama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba sasa Serikali isomane, Serikali iwe na nia moja, mwekezaji na wewe wa viwanda muwe mnafanya vitu kwa pamoja kuwasaidia Watanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii Mheshimiwa Waziri wewe unasimamia wafanyabiashara, lakini TAMISEMI ndiyo inaweka miundombinu ya wafanyabiashara, sasa wasipoweka sawasawa Mheshimiwa Waziri tunarudi pale pale kupiga kelele zisizotekelezeka. Tunaomba Serikali msomane. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii wawekezaji hawa ambao sisi tunawahitaji, kwa sababu kama Taifa tupo win win, tunataka ajira ipatikane, tunataka watu wetu wapate kipato, tunataka watu wetu wapate fedha na vitu kama hivyo pamoja na kodi, lakini wawekezaji hawa vijana wetu wanapokwenda kufanya kazi kwenye hivyo viwanda ambavyo mmevitoa kwenye ripoti, kijana anaanza kazi saa moja na nusu asubuhi mpaka saa kumi na mbili analipwa chini ya shilingi 5,000/=. Mheshimiwa Waziri hiyo ni ajira au ni mateso? Vitu kama hivyo! (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri tunaamini viwanda vikubwa, uwekezaji mkubwa unaangukia kwa Mheshimiwa Kitila, yeye kama mtu wa uwekezaji. Zamani ilikuwa pamoja labda ilikuwa inawasaidia kufanya kwa pamoja lakini nimesema kwa sababu Serikali inasomana na ni Serikali moja, basi mtafute namna ambayo matatizo haya tunaweza tukayatatua kama Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, bado natoa angalizo la kuangalia wawekezaji na hasa kwenye mafao lakini hatuishii hapo Mheshimiwa, tunafikiri kwamba uwekezaji kama tulivyosema ni faida, basi wale wanaowekeza ni lazima wafuate masharti na kama kiwanda kinaonekana kinafungwa, basi watoe taarifa mapema. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano kwenye masuala ya kilimo, leo hii umefunga Kiwanda cha Chai cha Katumba au umefunga kiwanda cha Chai cha Moo kilichopo pale Rungwe lakini umeacha watu wana chai zao mashambani, umeacha watu vijana ambao ulikuwa umewaajiri bila kuwapa mafao yao au hata kifuta jasho, Mheshimiwa Waziri kama kiongozi na Waziri wa Wizara hii tunaomba sana ulisimamie hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakuja kwenye suala la SIDO, Mheshimiwa Kimei ametoka kueleza hapa, sisi Mbeya tunayo SIDO na tunao uwanja mkubwa sana wa SIDO ambao wafanyabiashara wamepewa kuuza pale. Ninaamini lengo la SIDO sote tunalifahamu, siyo vibanda vya biashara, SIDO ni viwanda vidogo vidogo. Leo hii ndugu zetu, wale wanakodisha maeneo, mtu akija na wazo lake la kibiashara tayari lile eneo limeshakodishwa na yule anayelikodisha anaenda kulipa kodi kwa SIDO. Hivi SIDO huwezi kwenda wewe mwenyewe ukachukue ile fedha badala ya mtu hapo katikati? Naomba ulifuatilie hilo Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru Mungu Waziri ameleta viongozi wake wa SIDO wa Mikoa wapo hapa, tunaomba sana SIDO ifanye kazi ya viwanda vidogo vidogo, ndiyo hasa jukumu la SIDO. SIDO pia ipo kwa ajili ya kusaidia wananchi na hasa hasa wanawake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii SIDO imebahatika kuwa katika Wilaya na Mikoa lakini gharama kubwa sana kwenye vifungashio, kuna wamama wanaojifunza batiki, wananunua dawa kwao, wananunua vifungashio, vimekuwa vina gharama kubwa. Wamekuwa wakitoa semina, nakubali na zinasaidia lakini mwisho wa siku mama mdogo kabisa yule wa chini uwezo huo hana na lengo la Serikali ni kumsaidia mtu wa kawaida kabisa kwamba ainuke atoke pale alipo na kusogea. Naamini kabisa tukiendelea kwa wazo la kwanza la SIDO tutakuwa tumefanya vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bado linarudi Mheshimiwa Waziri kuhusu mavazi na vitendea kazi kwenye viwanda. Kuna buti, kuna vilinda kichwa kwa mfano kofia ngumu, sehemu nyingine watu hawafanyi, wanafanya kazi hatarishi kwenye hivyo viwanda na hivyo vitu hawapewi. Wenzetu wa OSHA wanasimama na wanaenda lakini kwa kuwa wanakuwa wametoa taarifa, basi kuna vifaa vimewekwa kwa ajili ya show off tu na siyo kwamba hawa watu wanavaa kila siku. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, watu wanafanya kazi kwenye mazingira hatarishi sana na kuwafanya kuhatarisha maisha yao ya kila siku. Tunafahamu kuna viwanda ambavyo vinatumia kemikali, wasipokuwa na vitu vya kujikinga hatuwatendei haki Watanzania hawa. Mheshimiwa Waziri, mimi ninaamini kazi yako siyo mbaya, inaendelea vizuri lakini mwisho wa siku nasisitiza kufanya kazi kwa kusomana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu stakabadhi ghalani, kwa mara ya kwanza sisi watu wa Kyela imetusaidia kwenye zao la Cocoa. Safari hii kidogo wakulima wameridhika kutokana na utaratibu mliouleta, lakini bado uboreshaji unatakiwa. Siyo tu kwa Cocoa, tunayo mazao mengine ikiwezekana yaweze kutambulishwa huko. Tunaomba sana wakulima wapate haki yao kwa haraka na speed iongezeke pamoja na kuwasifia, lakini mwisho wa siku tunataka kazi hii iweze kufanyika vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema haya Mheshimiwa Waziri nasisitiza wawekezaji lazima waangaliwe. Najua BRELA ipo chini yako, na jana nimezungumza habari ya BRELA wanafanya kazi vizuri, wamepunguza ile foleni ambayo ilikuwepo zamani kwa kutumia mtandao, lakini staff wao pia wanafanya vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bado najua wawekezaji wanaochukua Watanzania, kwa maana ya kuchukua majina yao ili wasajiliwe, basi mwendelee kuwafuatilia, ikiwezekana mwongeze kijisheria hapo, kama Mtanzania ni mwekezaji, basi kila baada ya miaka mitatu, minne warudi Mezani na kuona je, mahusiano yao ya kwanza yanaendelea au yule mtu alichukuliwa kama bosheni ili leseni ipatikane!

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema haya, naunga mkono hoja kwa mara ya kwanza katika Wizara hii, ahsante. (Makofi)