Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa nafasi ya kuchangia. Awali ya yote namshukuru Mungu Mwenye Enzi na Utukufu kwa kuniwezesha kusimama mahali hapa muda na wakati kama huu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niipongeze Serikali kwa hatua mbalimbali inazochukua kuhakikisha Taifa letu linanufaika vema na biashara na mataifa ya nje pamoja na kuongeza tija na kupunguza mfumuko wa bei. Nampongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu wake dada yangu mpendwa sana role modal wangu Mheshimiwa Dkt. Ashatu Kijaji, kwa kazi nzuri, nzuri kabisa anayoifanya kuhakikisha tunafanya biashara vyema na Taifa letu linaongeza nguvu ya uzalishaji na kuhamisha bidhaa zetu nje ya nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimemsikiliza Mheshimiwa Prof. Muhongo na ninaomba kuunganisha nguvu kuanzia pale. Mheshimiwa Prof. Muhongo ametoa kind of a little research, amefanya tafiti na mchango wangu nami unakwenda kuelekea huko. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wote tunakubaliana kwamba, tuna rasilimali za kutosha kuhakikisha Taifa letu linaweza kuuza nje zaidi pamoja na kuhakikisha tunakwenda kufanya biashara bila kuwa na mfumuko wa bei mkubwa. Ninachoamini, mafanikio ya Sekta ya Viwanda na Biashara yatategemea ni kiasi gani kama Taifa tunaibua na kuweka nguvu pamoja katika tafiti (research and development). (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile ni namna gani tunaweza kufanya tafiti ambazo zitaboresha rasilimali zetu na kuhamisha maarifa ya kisayansi katika uzalishaji? Nimeangalia vipaumbele sita vya Bajeti hii ya 2024/2025. Sijaona kipengele ambacho kinazungumzia ni namna gani tunafanya tafiti ya rasilimali zetu ambazo zitaongeza nguvu katika uzalishaji. Hilo sijaliona katika kipaumbele cha bajeti hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia kiuhalisia tunafanya tafiti kwa kutumia fedha za wahisani (DANIDA) na (IFDA). Tunapofanya tafiti, tunapowarudishia wahisani majibu ya tafiti yale, tunawaonesha mianya na gap la kuja kufanya biashara kwetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini kama Taifa tusitenge fedha zetu wenyewe kwenye bajeti tukafanya tafiti zetu ambazo sisi zikatuwezesha kuongeza thamani ya mazao yetu na kwenda kusafirisha nje ya nchi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wahisani wanapotupa fedha tutafanya tafiti kwa mujibu wa wanavyotaka wao. Tukiwapelekea tunawaonesha opportunities na fursa ambazo zipo kwetu na wao wanarudi kwetu kufanya biashara na sisi. Baada ya miaka kadhaa wanatuachia wao wameshanufaika, nchi inabaki bila chochote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana kusisitiza katika eneo hili. Tuna rasilimali za kutosha, tuwekeze zaidi katika tafiti zetu. Kule kwetu Tanga ukiangalia tuna madini ya viwandani. Tuna Mica inayotuwezesha kutengeneza screen hizi za simu zetu. Tuna Graphite inatuwezesha kutengeneza betri za magari. Tuna Quartz, tuna Feldspar, tuna Dolomite na tuna madini lukuki kule Tanga. Mpaka leo sijawahi kusikia kama kuna mkakati mzuri umewekwa kuhakikisha tunanufaika kama Taifa au kama Mkoa kwa madini yale tuliyokuwepo nayo kule Tanga. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Wachina wanachukua Dolomite kutoka kwetu, wanakwenda kutengeneza shanga, wanakuja kutuuzia very expensive. Naiomba sana Wizara hii ya Viwanda na Biashara, itusaidie sana katika kuhakikisha gemstones zilizopo Tanga zinafanyiwa tafiti za kutosha na madini ya viwandani yaliyopo Tanga, yanafanyiwa tafiti za kutosha ili tuone namna gani tunaweza kuongeza thamani na kuweza kusafirisha nje ya nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu Kiwanda chetu cha Tanga Fresh, jamani maziwa ya Tanga Fresh yalikuwa matamu sana kuliko maziwa mengine yaliyokuwepo huko, lakini kiwanda kile kinayumbayumba mpaka sasa. Shida ni nini kwa Tanga Fresh? Kama Tanga Fresh itafanya vizuri, ina maana mwananchi mmoja mmoja anayezalisha maziwa ataweza kununua pale na tutaongeza mzunguko wa fedha katika Mkoa wetu wa Tanga. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, shida ipo wapi ya Tanga Fresh? Kwa nini inayumbayumba? Natamani kusikia kutoka kwa dada yangu mpendwa katika hitimisho lake. Ni namna gani wanatusaidia kuhakikisha Tanga Fresh inakwenda kusimama sawa sawa na tunaona faida ya kiwanda kile cha muda mrefu nchini kwetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile naomba kuzungumzia suala zima la zao la mkonge. Nimesikia vizuri umelizungumza katika bajeti yako, tunashukuru sana kwa hilo. Ili tuweze kutokusafirisha au wakulima wadogo wadogo kuuza ile raw leaf (lile jani lenyewe) wawezeshwe. Vilevile, kupata zile mashine za korona, hiyo ndio shida kubwa inayotukabili Tanga. Mashine za korona kule chini ni kidogo. Wanauza majani badala ya kuuza zile nyuzi ambazo zimeshachakatwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana Serikali katika hili waweke kipaumbele. Hata kutoka kwenye mkonge tunaweza kupata vitu mbalimbali ambavyo tunaweza kusafirisha nje ya nchi, lakini hata tukiusafirisha mkonge wenyewe tuna uwezo wa kupata fedha nyingi za kigeni. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, naomba sana Serikali kwenye mradi uliopo pale Ubungo, issue siyo suala la watu wa Kariakoo kupata maeneo kwenye eneo lile la biashara la Afrika Mashariki. Issue ni namna gani tunaweza kuwa-manage Wachina wasifanye biashara za rejareja ambazo zinaweza kufanywa na Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunawajua Wachina walivyo. Wachina ni watu ambao wanaweza kupenya. Wao ni wazalishaji, wao ni suppliers lakini wakati huo huo wanaweza kuingia mitaani wakauza vitu vile vile ambavyo Mtanzania amenunua kwao kwa bei ya rejareja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaipongeza Serikali, naiona dhamira yake ya kuhakikisha kwamba, Tanzania tuna hubs katika zile nchi ambazo hazina bahari (Landlocked Countries). Ninaamini kupitia mradi ule pale tunaweza sana kuwasafirishia hata huko Congo alikosema kaka yangu Mheshimiwa Kilumbe Ng'enda, lakini that is an issue. Chinese wanajua kupenya kufanya biashara ambazo sisi Watanzania tunaweza kuzifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana mwangalie makubaliano mliyoingia na iwapo itatokea Mchina yeyote anakwenda kuingia mtaani kufanya biashara ambayo Mtanzania anaweza kuifanya, hatua kali zichukuliwe. Hata wale ambao wapo sasa hivi Tanzania wanauza mapazia na maua Kariakoo tuone namna gani ambavyo tunastopisha kwa sababu wapo na siku nyingi tunasema, na sijaona hatua ambazo zinachukuliwa dhidi yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Watanzania na sisi tuna uwezo wa kufanya biashara na tutakua kiuchumi wakati tunatafuta namna ya uzalishaji. Hizi ni hatua muhimu ambazo zinapaswa kuchukuliwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba kuunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)