Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa muda niweze kuchangia. Nitumie nafasi hii kuendelea kumpongeza Mheshimiwa Rais, kwa namna ambavyo anapambana kuweza kuhakikisha analeta fursa mbalimbali katika nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu na mimi nina yangu machache katika Wizara hii. Jambo kubwa kabla sijaenda kuchangia haya mengine ambayo nimedhamiria, kwanza natamani kuiona Wizara hii inautazama Mkoa wa Songwe kwa namna ya tofauti. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Songwe ni Mkoa wa kibiashara, ni Mkoa wa viwanda, ni Mkoa wa uzalishaji na ni Mkoa ambao unazalisha vyakula kwa wingi. Tunazalisha kahawa na madini mbalimbali. Kwa hiyo, natamani kama Wizara wauone kwamba Mkoa wa Songwe ni Mkoa wa kimkakati. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niongelee kwa maana ya Mji wa Tunduma kwamba Wizara naona haijafanya kitu kwa Mji wa Tunduma. Nimekuwa naongea hapa mara nyingi kukumbusha namna ambavyo Wizara hii ya Viwanda na Biashara, iweze kuona Mji wa Tunduma kama ni Mji ambao wanaweza kutengeneza wafanyabiashara wakubwa wengi. Pia, wanaweza kutengeneza viwanda vingi kwa sababu ndiyo mji ambao upo kwenye lango la SADC. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri kwa namna ya tofauti na timu yake waende wakafanye research pale. Ni kwa namna gani Mji wa Tunduma unaweza ukawanufaisha kwa kuanzisha viwanda vikubwa? Pia, kwa kuweza kuanzisha biashara kubwa ambazo zinaweza zikahudumia Ukanda wa SADC. Kwa hiyo, ni namna ambayo wao kama Wizara ya Viwanda na Biashara pamoja na Wizara ya Mipango, wanaweza wakajipanga kufanya kitu kwa ajili ya Mkoa wa Songwe na hususan kwa Mji wa Tunduma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, niungane na wenzangu ambao wameongea kwamba, kama nchi tumeona kumekuwa na changamoto kubwa ya upatikanaji wa dola. Tunapoongelea dola, ni kitu ambacho kama Taifa inaweza ikawa ni fursa kwa kuwa na reserve ya kutosha ya hela za kigeni kwenye nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama Mheshimiwa Mbunge ambaye sio mtaalamu sana wa masuala ya kiuchumi kwa maono yangu tu ya kawaida baada ya kusoma taarifa hii nimeona kwamba Wizara kama Wizara hawana malengo au mkakati maalum wa kulinda fedha za kigeni kwa nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kusema nini? Hii ndiyo Wizara ambayo inaweza kutusaidia kutunza fedha zetu za ndani kwanza zisiondoke nje. Nilikuwa nasoma mahali hapa katika maandiko mbalimbali ambayo yameandikwa nikaona kwamba, kuna kiwango cha samaki ambacho kinaingizwa nchini. Niliwaza tu hiyo ni sample ya product ambayo nimeiona kwamba ni kitu ambacho kama Watanzania hatupaswi kuagiza. Minofu ya samaki imeingizwa yenye thamani ya dola bilioni 6.24 wanaagiza inaingizwa humu nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hiyo fedha tungetumia minofu iliyomo humu humu nchini. Tuna Maziwa ya kutosha tungeweza kuhifadhi hii fedha na tusiwe na uhaba huo wa fedha za kigeni. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hapa naenda kwa mazao ya kilimo ambayo yanaingizwa nchini kama vile ngano. Tunawezaje kuagiza ngano wakati hii ni fursa kwa wananchi wetu kuweza kulima na ku-supply kwa viwanda vyetu ambavyo vipo nchini ambavyo vinaagiza hizo ngano? Kwa hiyo, nataka kusema kwamba hii ndiyo Wizara pekee ambayo inaweza kutusaidia kama nchi kuhifadhi fedha za kigeni. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kusoma taarifa yao, sijaona wao kwamba wana malengo gani ya ku-balance uwiano wa import na export. Nilikuwa najaribu kuangalia kwa biashara waliyofanya kwa hizi Jumuiya za Ulaya, sisi kama Taifa tuliweza ku-import vitu vyenye thamani ya shilingi bilioni 4.05, lakini export ikaenda kwenye shilingi bilioni 3,835. Sasa nawaza, inakuwaje tunaweza tuka-exceed; kwamba sisi tu-import zaidi kuliko ku-export?
Mheshimiwa Naibu Spika, kama Wizara wanafanya mkakati gani wa kuhakikisha kwamba tunakuwa na export nyingi? Kwa sababu tunatengeneza wafanyabiashara, tunatengeneza wajasiriamali wengi na tunatengeneza viwanda. Kama Wizara imejiwekea mkakati wa kutengeneza bidhaa ngapi ambazo ziingie kwenye masoko ya kimataifa? Kwa hiyo, hili nalo sijaliona huku. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Wizara watengeneze mpango kazi ambao utaonesha kwamba wana-balance vipi import na export? Pia wanatengeneza wafanyabiashara wangapi ambao wataweza kuingia soko la Kimataifa kwa ku-export product zao? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nirudi kwa Viwanda vya SIDO. Hii Taasisi ya SIDO ni Taasisi ambayo kama Watanzania tunaitegemea. Nilikuwa nasoma katika taarifa hapa, wananiambia eti nchi nzima SIDO wamekuza wajasiriamali watano tu. Sasa nawaza Mkoa wa Mbeya, Songwe, Morogoro na mikoa yote Tanzania nzima, wakatuambia wamekuza wafanyabiashara watano? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naona ni kitu ambacho kama Taifa Wizara haina mkakati maalum wa kuhakikisha wanatengeneza wajasiriamali wengi zaidi ambao watahakikisha wanakua. Mimi nisiseme mengi, ninashukuru kwa kunipa nafasi. Ahsante sana. (Makofi)