Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bunda
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia Wizara hii. Cha kwanza nampongeza Waziri wa Wizara, Naibu Waziri wake, Katibu Mkuu wake na watendaji wote wa Wizara hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma baadhi ya hotuba za bajeti zilizotoka hapa ndani hii nayo inaweza kuwa hotuba mojawapo nzuri sana ambayo imeletwa na Wizara ya Viwanda na Biashara; na ukiisoma vizuri ni kwamba wamejiandaa sana kwenye hiyo hotuba, wamefanya kazi nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaenda mbali nimpongeze sana Mheshimiwa Rais, wale wakubwa wa hapa Tanzania wanasema big up. Mheshimiwa Rais ametoa shilingi bilioni 15.38 kwa ajili ya kuwalipa fidia watu wa Liganga na Mchuchuma. Heshima kubwa sana. Wale watu wamekuwa na kilio cha muda mrefu mno, wameteseka sana. Mimi nilikuwa Mjumbe wa Kamati hii. Nilikwenda siku moja tukakutana na akina mama wanalia, wanapiga magoti, wanasema mmetunyang’anya ardhi miaka nenda rudi, hatulimi na hatufanyi chochote. Mheshimiwa Rais ameamua kuwapa fidia ya shilingi bilioni 15. Heshima kubwa sana kwa watu wale waliotoa Liganga na Mchuchuma. Hii pia imetoa fursa kuona mradi wetu mkubwa wa Liganga na Mchuchuma sasa unaweza kwenda huko mbele tukapata nafuu ya kutekeleza mradi huu mkubwa sana. Hiyo heshima imekuwa kubwa sana kwa Mheshimiwa Rais kwa kutoa hizo fedha (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wamezungumzia suala la bajeti hapa. Unajua sijui kama mtu anaelewa maana ya viwanda ni nini? Hawa watu wa viwanda huyu Waziri wa Viwanda asipokuwa na fedha za kujenga industrial park kwenye maeneo mbalimbali na hasa kwenye maeneo yenye uzalishaji wa matunda hali ni hatari mno. Unakwendaje kulima parachichi, ukilima, ukitaka kuuza huna mahali pa kuweka at least kupata muda wa siku tano ama nne ili usubiri bei iwe nzuri uuze. Huna uwezo, inaozea hapo. Tunapoteza thamani ya matunda ya maeneo yetu ya mazao kila mahali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lazima bajeti yao iongezeke ili wajenge industrial park ambayo itawawezesha wananchi wa kawaida kwenda kuweka mashine mle ndani. Watuuzie machungwa, maembe, na vitu vingine, hata mahindi na mchele. Kuna mtu anaweza kulima mahindi eka tano lakini hana mahali pa kutunzia. Akiwa ana maeneo ambayo anaweza kuweka samani inaweza ikampa nafasi ya kuuza. Kwa hiyo, nikiri kwamba fedha za Wizara ni lazima ziongezwe ili wapate nafasi ya kujenga industrial park kwenye maeneo mbalimbali ili isaidie wakulima wetu. Nadhani jambo hili ni la msingi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hotuba yenu nimeona kuwa wameunganisha ile TFDA kwenda TBS. Nimeona ubora walioutengeneza sasa hivi. Nawaomba wauongeze kasi kwa sababu sasa hivi wamefikia asilimia 66.4 ya ubora, wamepunguza gharama nyingi. Mimi na-support hili wazo, lakini waongeze kasi ya watumishi, waongeze thamani ya kusajili vyakula salama na vipodozi kwenye maeneo haya. Napongeza sana kwa hatua hii ambayo wamefikia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu ni nchi inayokua sana, nchi yetu ni kubwa mno. Tunahamasisha watu wawe kwenye makazi mbalimbali na sasa tuna kitu kinaitwa climatic change (mabadiliko ya tabianchi). Hali ni mbaya sana kwenye nyumba za kawaida; wananchi wanataka kujenga nyumba za kudumu, bati gharama, cement gharama, nondo gharama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli Mheshimiwa Waziri akija hapa hana mawazo ya kupunguza gharama za vifaa vya ujenzi kwa wananchi wetu, kwa mfano, hii cement wanasema kwamba viwanda vikubwa vipo saba na vinazalisha tani 9.107; na vina nakisi (akiba) ambayo inabaki hapa kama milioni moja hivi wanauza na nje. Leo bati linauzwa shilingi 46,000/=, au shilingi 50,000/= hadi shilingi 60,000/=. Haiwezekani jamani! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali tukubaliane kama ni kupunguza VAT au kama ni kuweka ruzuku, tuweke ili wananchi wetu waweze kujenga. Hata yule Dangote wakisema wanampa mazingira mazuri ya kumpunguzia VAT, anaweza kuuza cement kwa bei nafuu, lakini sasa bei ya vifaa inapanda na wanataka tujenge. Tunajengea nini? Tunajenga bati lipo juu? Siku hizi watu wanataka m-south ambayo bei yake ipo juu, mabati ya kawaida nayo bei ipo juu, nondo bei zipo juu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri aje na mkakati wa Serikali tushinikize tuone namna gani wananchi wetu wanaweza kupunguziwa vifaa vya ujenzi, cement, mabati ili bei iwe nafuu na wananchi wetu waweze kukuza viwango vyao vya ujenzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona kwenye Kamati, wanasema kuwa kuna vijana wetu wanaopata ufundi wanaosoma darasa la saba. Tukumbuke kuwa darasa la saba ni mtihani, ni masomo na Baraza la Mitihani linatambua kiwango cha darasa la saba kwenye nchi yetu; lakini wale vijana wetu wa darasa la saba wanapomaliza wanakwenda kujifunza udereva, wanakwenda kujifunza uanagenzi, wanajifunza na mafundi mchundo (mafundi asanifu) wanajifunza mambo yote. Muda wa kuajiriwa Serikalini wanasema wanahitaji cheti cha Form Four. Lazima walete sheria hapa ya kubadili mfumo huu wa ubaguzi ambao tunao. Hivi kinachoendesha gari ni cheti au ni weledi wa mtu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tukubali wale ambao tumewapeleka kwenye mafunzo ya VETA na maeneo mengine, wa darasa la saba ambao hawakumaliza Form Four wakubalike kuajiriwa na Serikali. Hatuwezi kuwa na ubaguzi wa namna hiyo. Watu wanasoma ufundi mbalimbali, tunataka kwenda viwandani tunakuwa na fundi mchundo, lakini sasa mkienda huko wakitaka kuajiriwa Serikalini mnasema cheti cha Form Four. Lazima mlete sheria tubadili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Kamati, imezungumza vitu vizuri sana hapa vya kubadili suala la hizi sheria ili wananchi wetu waweze kupata nafuu ya kuajiriwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni Wizara mama sana, tunaiomba Serikali kama kuna maelewano, kwa sababu hii ni Wizara mtambuka, ikubaliane na Wizara nyingine zinazohusika, wakae pamoja waangalie hili linafanyika na nani, hili linafanyika na nani ili wawe pamoja. Kuliko kuwa na Wizara ambayo unaipa bajeti ndogo na unakata ishughulike na mambo makubwa ambayo haina uwezo nayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa leo, nilitaka nichangie eneo hili ili niweze kuunga mkono bajeti, lakini mnafanya vizuri sana, ahsanteni sana. (Makofi)