Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kilolo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi hii. Awali ya yote, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa nafasi aliyoitoa ili niweze kuchangia katika Wizara hii ya Viwanda na Biashara. Pia natoa shukrani zangu kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa jinsi anavyowajibika katika sekta zote, hasa kwa Jimbo langu la Kilolo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi tunavyozungumza Mheshimiwa Rais ameshatoa fedha shilingi milioni 700 kwa ajili ya kununua mitambo ya kusimika kwenye sehemu ya kiwanda cha chai pale Kidabaga. Tayari Bodi ya Chai wamepokea fedha hizo na wapo katika hatua za manunuzi ili kiwanda kile kiweze kufungwa. Hii ni historia wa sababu, kiwanda hiki kina zaidi ya miaka 30 kikiwa gofu, lakini leo kwa juhudi za Mheshimiwa Rais, tunaona mapinduzi makubwa na kiwanda hiki kinaenda kuanza kufanya kazi muda siyo mrefu ujao. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua fursa hii kuwashukuru sana Mheshimiwa Waziri pamoja na Mheshimiwa Naibu Waziri wa Wizara hii kwa ushirikiano wanautoa katika mambo mbalimbali. Hapa nataja jambo moja, tumekuwa na mazungumzo na majadiliano kuhusu ujenzi wa Chuo cha CBE katika eneo la Kata ya Lugalo, pale Mbigili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ujenzi huo kwa sasa tayari ile hati ipo tayari ni Wizara tu kwenda kuichukua. Sisi, kama Halmashauri tumelipia kabisa kwa hiyo, Wizara ni kutia saini tu na kuondoka na hati yao. Namwomba waje tuwakabidhi eneo, ili waanze kujenga chuo kwa sababu, ni muda mrefu tangu mazungumzo haya yameanza.
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.
MWENYEKITI: Taarifa, Mheshimiwa Jesca.
TAARIFA
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba nimpe taarifa mzungumzaji kwamba hicho Chuo cha CBE na RCC ya Iringa inakisubiri kwa hamu na tulibariki kwamba kikajengwe hapo. Tunaomba tafadhali.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Justin.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa hiyo, kwa sababu, najua Mheshimiwa Waziri ni msikivu, nina uhakika watakuja ili tuwakabidhi eneo. Sisi tupo tayari kuwakabidhi, hamlipi hata kitu kama Wizara, vyote vinafanywa na Kilolo. Kilolo tumejipanga na tupo tayari kupokea chuo hicho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutoka pale mpaka Iringa Mjini ni kilomita 30 tu kwa hiyo, tumetenga eneo zuri ambalo hata Waziri mwenyewe hapati usumbufu kufika pale. Baada ya kusema hilo narudia tena kuwashukuru kwa sababu, wameonesha ushirikiano mkubwa sana kwenye suala hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo mambo machache ambayo bado nayadai kwenye Wizara hii; Mheshimiwa Waziri pamoja na Ofisi yake. Tumekuwa na mazungumzo kuhusu kiwanda kidogo cha sukari, hapa mimi naomba nizungumze. Nimesoma kwenye taarifa yao na nimeona hapa wameandika kwamba, kuna kiwanda kidogo cha sukari kinatengenezwa na kikikamilika kitatoa ajira kwa zaidi ya watu 2000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo tupo tayari, kwanza AMCOS ya sukari ipo pale. Wale wameunda AMCOS na wameandaa mashamba. Mimi nipo tayari kwenda hapo Wizarani ili tupate mbegu na vitu vingine, kwa ajili ya kupanda miwa. Hilo wala siyo tatizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri afanye jambo moja tu. Sisi kama halmashauri tutatafuta fedha, tutaandika hata nusu, shilingi milioni 800. Si ni shilingi bilioni 1.6 hapa, tutaandika tu hata kwa Mheshimiwa Rais, tuna zile 10% nyingi tu zimewekwa pale. Tutaomba watupatie shilingi milioni 800 kwa sababu, watakaotumika kwenye viwanda hivi watakuwa ni vijana, watakuwepo wanawake na hata wenye ulemavu watapewa nafasi. Tutaomba shilingi milioni 800.
Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu Wizara ya Kilimo tutaendanao, tutaomba labda shilingi milioni 400 na wao watupatie 400 tujenge hicho kiwanda pale Kilolo. Ni kazi rahisi na hapo mimi nimetoa zaidi ya nusu. Mheshimiwa Waziri hivi kweli, atakataa ofa nzuri namna hii ambayo haijatolewa na Mheshimiwa Mbunge yeyote tangu tumeanza asubuhi hapa! Mheshimiwa Waziri nakuomba sana kiwanda hicho kijengwe, kiwekwe pale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ninavyosema, nimeshajadiliana na Halmashauri yangu na tupo tayari kufanya hilo kwa sababu, Wananchi wa Kata ya Mahenge, Kijiji cha Magana na Kijiji cha Ilindi wana mashamba katika lile bonde lote. Kata ya Mahenge, pale Mgowelo mpaka Nyanzo yenyewe kuna mashamba, lakini hata pale Ruaha Mbuyuni kuna mashamba yameshapimwa na yanafaa, kwa ajili ya kiwanda cha sukari na unajua kuna upungufu wa sukari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nakupa hiyo deal, na kuwekea mezani Mheshimiwa Waziri, naomba tujadiliane tuikamilishe ili hata mwakani tu tuanze kutoa sukari pale Kilolo. Naamini tutakuwa tumewatendea haki wananchi wa Kilolo kwa kiwango kikubwa sana. Kwa hiyo, hilo lilikuwa jambo langu la pili ambalo naliomba ili kwa kweli tuweze kuona kwamba na sisi tumetendewa haki pale Kilolo kwa sababu, ni sehemu ambayo inaweza kustawisha miwa kwa ajili ya sukari na tayari tafiti zote zimethibitisha hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, yanayohusu Kilolo ni hayo na la mwisho ni hili la vipimo. Sisi tunauza mazao ya kilimo, mahindi, viazi, njegere, pamoja na mazao mengine, lakini sasa hivi kumekuja huu uuzaji wa kutumia mifuko. Kuna mbinu nyingi sana sasa hivi, kuna mifuko ambayo ni elastic, yaani inapanuka, ukijaza inapanuka, kwa hiyo, ukiweka mahindi badala ya kuwa madebe saba sasa hivi ni madebe nane, lakini bei bado inakuwa ni ya gunia kwa sababu, nchi yetu bado inatumia vipimo vya vifungashio badala ya mizani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la kutumia vipimo vya vifungashio ni la muda mrefu na sisi tunaotoka kwenye maeneo ya kilimo, wengi tumelalamika muda mrefu, lakini bado tatizo hili lipo na limesababisha kero kubwa sana kwa wananchi. Hivi karibuni nimekuwa nikitumiwa picha za hiyo mifuko ambayo inapanuka, unaona kabisa gunia limekuwa nene kuliko ule unene wa kawaida, lakini wale wafanyabiashara ni mbinu ambayo wameibuni kuepuka lumbesa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, sasa hivi siyo lumbesa tena ni ule mfuko tu wenyewe unakuwa elastic, unanenepa, badala ya lumbesa. Kwa hiyo, hutaona kwamba ni lumbesa, lakini kimsingi ukiliangalia lile gunia unajua kabisa hili siyo gunia la kawaida. Sasa wakipita kwenye mizani wanasema hii siyo lumbesa, lakini kimsingi bado tatizo hilo lipo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi najiuliza, hii nchi tumeshindwa nini kuweka utaratibu wa kutumia vipimo katika kuuza bidhaa zetu? Kwa sababu, huo ndiyo ukombozi wa wakulima. Kama kilo ni shilingi 300, basi ni shilingi 300, au kama ni shilingi 500 basi ni shilingi 500, lakini kutumia ujazo haijawahi kuwa kawaida. Ninyi mnanunua vitunguu huko njiani, mnaona zile ndoo, unamimina, inabidi uchungulie kule chini kwa sababu lazima pale kumewekwa angalau kisimenti kidogo ili vitunguu viwe vichache kwa sababu, tunatumia hivi vipimo ambavyo ni vipimo vya vifungashio badala ya kutumia vipimo vya mizani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri ni wakati wa kuleta mapinduzi katika nchi yetu, kwamba, utaratibu tunaokuwanao uwe ni ule wa kutumia vipimo vya uzito badala ya vipimo ambavyo vinamnyonya mkulima, vinamuumiza mkulima, vipimo ambavyo havimpi faida mkulima ambaye anakuwa ameteseka kwa muda mrefu katika kuhakikisha anapata faida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ni kuhusu ubunifu unaofanywa na muunganiko. Tumeona hapa kwamba, TEMDO wanatengeneza vifaatiba, vitanda kwa ajili ya maternity vinatengenezwa pale. Nadhani changamoto ni kwamba, wakishatengeneza kwanza mtaji ni mdogo, kwa hiyo, utengenezaji wao ni vitanda viwili, vitatu na tumeona sehemu vinakoenda, tunashukuru na tunapongeza ubunifu huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri sasa ni wakati muafaka wa kutafuta namna bora ya ku-mobilize viwanda. Hapa, nimerudi kule, tuzungumze kwenye kuona je, hakuna Halamshauri yenye kipato kikubwa inayoweza kuwekeza kwenye viwanda kwa kutumia hizi 10% kwa mfano, lakini tuone pia, ni jinsi gani tunaweza tukawavutia wawekezaji?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuvutia wawekezaji kutakuja hivi, hawezi kuchukua hii teknolojia ya TEMDO kama hana uhakika wa soko. Kwa hiyo, inabidi Wizara ya Afya iingie mkataba na huyu mwekezaji kwamba, vitu vitakavyotengenezwa atavinunua ili viweze kuzalishwa ndani na awe na uhakika wa lile soko.
Kwa hiyo, naomba hapo tusije tukaishia kwenye kutengeneza vitanda au bidhaa mbili tatu, tutafute namna ya kufanya scale up ambayo nina uhakika TEMDO hawezi kufanya. Ni lazima ile teknolojia ihamie kwenye viwanda ili vile viwanda viweze kuzalisha, tuweze kupata bidhaa nyingi za ndani ambazo sasa tukizitumia tutaona tunapata tija.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi sina mengi, nina uhakika Wizara imesikia, maombi yangu siyo mengi. Chuo chetu cha CBE kijengwe, lakini pia, ofa yangu ya kiwanda cha sukari imesikika na Bunge zima na nimeona kabisa kwamba, Wizara imepokea. Nina hakika wakati wa majibu pengine nitajibiwa kabisa kwamba, hicho tayari kimeshapelekwa Kilolo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naunga mkono hoja. (Makofi)