Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kilombero
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi nami kuchangia Wizara ya Viwanda na Biashara. Kwa kweli, naanza kuishukuru Serikali ya Awamu ya Sita, Serikali ya Chama Cha Mapinduzi, inayoongozwa na Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa anayofanya katika maendeleo ya nchi yetu na mojawapo ikiwa ni katika Wizara hii ya Viwanda na Biashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mara nyingi kwa kweli, tunamwona Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu Waziri, Mheshimiwa Rais na viongozi wengine mbalimbali wakizunguka duniani huko kutafuta fursa za uwekezaji katika kukuza sekta ya Viwanda na Biashara. Nataka kukiri hapa mbele yako kwamba, Mheshimiwa Waziri wetu wa Viwanda na Biashara ni mtu rahimu, mama mzuri kabisa sina nongwa naye, sina shida naye. Amekuja mpaka Kilombero, porini kule kwetu, amefika Mang’ula, amesikiliza hoja yangu ambayo kwa kweli leo nataka kusema hapa, ndiyo miongoni mwa vitu vilivyonisukuma kuchangia kuhusu kufufuliwa kwa Kiwanda cha Mang’ula Machine Tools.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo Mheshimiwa Rais, na Serikali ya Awamu ya Sita amefufua baadhi ya viwanda kikiwemo Kilimanjaro Machine Tools, na sisi Kilombero tulikuwa tuna ajenda ya kufufua Mang’ula Machine Tools. Kiwanda hiki ni muhimu sana katika nchi yetu, wazee wetu wa zamani wanajua umuhimu wa kiwanda hiki katika mchango wa nchi yetu, kwa Taifa, ajira na kadhalika na Mheshimiwa Waziri amefika pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nafikiri Mheshimiwa Waziri kwa urahimu wako huo, baadaye unipe ufafanuzi wa kina wa ni namna gani kiwanda hiki kinafufuliwa na kinafufuliwa lini? Kwa sababu, wataalamu wameshakuja wengi pale na Kamati ya Usalama ya Wilaya chini ya Wakili Msomi Dunstan Kyobya, Mkuu wetu wa Wilaya, tulitembelea pale tukaona baadhi ya vitu vinavyozidi kuharibika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nyumba zilizopo pale zinaharibika mapaa, zimeendelea kuwa magofu. Kuna watu wanakaa mle, hata hatujui ni nani anakusanya kodi. Kuna vyuma vimeharibika, kuna mashine mle hata oil haziwekwi, zinazidi kuharibika, watu wanaondoka na miundombinu. Kuna ulinzi, lakini bado siyo wa kutosha, kuna mapori, nyoka wanafugwa pale, lakini Diwani alituambia kwamba,kuna ubakaji unaendelea pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa kweli, napenda kukiomba Chama changu cha Mapinduzi kinisamehe endapo nitashika shilingi ya Mheshimiwa Waziri. Nilikuwa napima kati ya kura za CCM na Mheshimiwa Rais katika Serikali za Mitaa pale Mwaya na Tarafa ya Mang’ula Kona na kushika shilingi ya Mheshimiwa Waziri, kipi ni kizito zaidi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikagundua kura za CCM ni nzito zaidi, kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri, kama hujanipa ufafanuzi nafikiria kushika shilingi yako. Nafanya kwa urahimu tu kwa sababu mwalimu wangu wa Kiswahili, Joram Nkumbi, anasema maendeleo na viwanda na biashara ni sako kwa bako, ni chanda na pete. Hivi vitu haviachani, kwa hiyo, nina nia hiyo Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina imani wananchi wangu wa Tarafa ya Mang’ula leo wanasikiliza. Waliniambia, wewe ulipoenda walikuzunguka pale ukaongea kwa nia nzuri. Sasa hebu Mheshimiwa Mbunge sema tukusikie umesema ili nongwa za Tarafa ya Mang’ula Kata ya Mwaya, Kata ya Kisawasawa, Mangu’la A, Mang’ula B, wasikie ili waweze kuona kwamba, nimelifikisha jambo hilo vizuri kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hilo la kwanza. Mheshimiwa Waziri nisaidie mdogo wako nami ninusurike na Serikali za Mitaa na mwakani kwa jambo la kiwanda. Kilombero tumeshafanya mengi sana chini ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, mengi kweli kweli, lakini hili limebaki nongwa kwa sababu vitu vinaharibika. Nafikiri pale kuna nyumba hata zaidi ya 100.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alikirudisha kile kiwanda Serikalini kutoka kwa mwekezaji. Kinamilikiwa na Serikali, lakini ni kwanini uwekezaji haufanyiki na hakifufuliwi kama wenzetu wa Kilimanjaro ambao Kilimanjaro Mashine Tools imeanza kuzalisha? Kwa hiyo, naomba kusisitiza sana kuhusu Mang’ula machine tools.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri la pili ni economics ambayo mimi nimesoma diploma na degree kidogo, mwalimu wetu mmoja alikuwa anasoma Chuo cha IFM alikuwa anatuambia, katika maendeleo ya nchi importation na exportation ni vitu muhimu sana. Anasema uingizaji wa bidhaa ndani ya nchi na utoaji wa bidhaa nje ya nchi ni picha ya nchi ambazo zimeendelea, inatoa bidhaa zake nyingi nje kuuza kuliko inazoingiza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nchi zinazoendelea, ili tuendelee ni lazima tuwe na mkakati wa kina wa kupunguza importation na kuongeza exportation hata kwa kuwa na bidhaa chache kama 100. Zipo nchi hapa ukipeleka kitu chako kitapigwa kodi, ili ku-discourage, ili kukufifisha usipeleke hiyo bidhaa kwa kulinda soko la ndani. Sasa nimesoma na nimepitia bajeti yako, hatuwezi kushika yote, Mwalimu wangu wa uchumi Mheshimiwa Dkt. Mwigulu anajua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna bidhaa chache tukiweka mkakati wa kuzizalisha wenyewe tutapunguza importation na kuna bidhaa ambazo tukiweka wawekezaji, tukiwahamasisha wawekezaji, tutaweza kupunguza kuchukua pesa zetu nyingi kupeleka nje. Mimi nataka kutoa mfano leo kwenye hotuba yako kwenye mafuta ya kula.
Mheshimiwa Mwenyekiti, umesema nchi yetu inahitaji tani 600,000 za mafuta ya kula. Mpaka leo tumeshindwa kuwa na mbegu za kutosha za kuzalisha mafuta ya kula, tuna upungufu wa tani 395,000 za mafuta ya kula. Mheshimiwa Waziri tangazieni dunia huko tunakonunua mafuta ya kula, mwekezaji yeyote akija Tanzania anaweza kuzalisha hizo tani 300,000. Tuna upungufu wa tani 395,000 anaweza kuzalisha tani 300,000 tumpe ardhi, tumpe vimisamaha vyote azalishe tani 300,000, tutapunguza fedha za kwenda kununua mafuta ya kula nje. Sasa leo umeandika kwenye hotuba yako, Mheshimiwa Waziri, viwanda vyote tulivyokuwanavyo, sijui mia saba na ngapi, havina mbegu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, watu wamewekeza kwenye viwanda, mbegu hakuna, na inaweza ikachukua zaidi ya miaka kumi. Tangazia dunia kwamba jamani anayeweza kuwekeza hata tani laki moja za mafuta ya kula hapa tunamtaka. Kesho utapata watu hapa watakuja wengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ni bodaboda. Tumeenda katika nchi moja East Africa hapa, wamekubaliana nchi nzima bodaboda ziko za aina moja. Kuna bodaboda (pikipiki) za mafuta na kuna pikipiki za kuchaji. Tulienda na baadhi ya Wabunge, nikauliza kwa nini nchi nzima hapa naona pikipiki fulani za Honda tu peke yake? Wakasema haya ni makubaliano ya nchi na nchi hiyo yenye kiwanda. Wana-assemble pale, pikipiki thamani yake ni kama milioni moja na laki mbili kwa sababu wamekubaliana, wamewekeza katika bodaboda ambazo zinaajiri vijana wetu wengi na sisi baada ya mafuta ya kula, twende kwenye pikipiki ambazo kila siku vijana wetu wananunua na sisi tunaombwa tununue pikipiki kwa vijana wetu kama ajira. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kubalianeni na watu waje wawekeze kiwanda hapa na kiwanda tunamaanisha, mashine ya kutengeneza injini ya pikipiki, mashine ya kutengeneza mudguard na mashine ya kutengeneza tairi kwa sababu raba tunayo, chuma tunacho, yaani full nondo yaani mashine ianze hapa, mashine ina-assemble injini mpaka taa za kuwaka zile zinaweza zikatengenezwa hapa. Hiyo ndiyo itakuwa full kiwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa katika ile ile habari ya kusema importation na exportation, tazama mwaka 2022 na 2023 umesema nchi za Ulaya, East Africa na Asia, tuweke mkakati wa kudumu na Asia. Mheshimiwa Waziri, angalia umetuandikia mwaka 2023 tumeuza Asia vitu vyenye thamani ya shilingi trilioni 7.4 na 2022 tumeuza shilingi trilioni 10. Kununua; 2023 tumenunua shilingi trilioni 21 na mwaka 2022 shilingi trilioni 23. Hiyo ni Asia peke yake na ukiangalia mle ndani umesema India, China na United Arab Emirates, hawa Wachina wanachukua karibu hii 80%. Tukae nao tuzungumze nao, Mheshimiwa Waziri, China mbali, nimeenda China na Mheshimiwa Spika kanipeleka China. China mbali, mtu anatengeneza pikipiki anaisafirisha mpaka Tanzania na anauza kwa faida. Tukiweka mazingira mazuri, huyo anayetengeneza pikipiki kule na soko lote lililokuwepo hapa Tanzania na East Africa hawezi kuweka hata kiwanda kidogo hapa ili tukapunguza hii deficit ya China. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti yetu shilingi trilioni 40, kama tunafanya biashara ya shilingi trilioni 21 na Asia peke yake na ambayo China wanachukua 80% bara kubwa. Sasa lakini kule China tulivyozunguka vile viwanda vilikuwa vya namna gani? Akina bibi wamekaa wana-assemble miamvuli. Mheshimiwa Waziri Simbachawene, akina bibi wamekaa wanafungafunga miamvuli mpaka kule mwisho wanaiweka kwenye nylon wanai-assemble kwenye maboksi inakuja Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeenda kwenye viatu wanakusanyakusanya ngozi, huyu anagonga msumari Ngozi, kiatu kinaenda kule, mwisho kina-assemble kwenye maboksi kiatu kinatoka. Pia, mifuko hii ya kuweka, mtoto kule kaanza bibi yuko huku, mmoja kazi yake ni kusogeza tu, viwanda vya kawaida kabisa. Kwa hiyo, kuwaambia wenzetu Wachina, tuna urafiki nao mzuri, acheni hiyo biashara ya kusafirisha makontena kwenye maji huko, njooni hapa kuna eneo hapa business park mtapata msamaha fulani mwekeze hapa tuwe na bidhaa chache tunazoweza kuanza nazo kama bidhaa za msingi katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tutaingiza kijiti cha kuchokonolea meno sijui kwa Kingereza mnaitaje?
MBUNGE FULANI: Tooth pick.
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, tooth pick, nini? Mimi Mswahili; ya kuchokonolea masikio, yakuchokonolea pua, kitana, soksi, kiatu, kila kitu tunaingiza tu. Tuseme bidhaa hizi 1,000 Tanzania importation marufuku. Hatuwezi kuingia katika dunia ya globalization tunaachia tu, Mwalimu Nyerere alisema sisi tunaachia tu tunafungua madirisha wanaingia mbu, panya na kadhalika, lazima tuwe na vipaumbele, bidhaa chache.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwalimu wangu wa economics wa diploma na degree alinifundisha lazima tuseme bidhaa chache katika nchi ya Tanzania ukiziingiza utatandikwa kodi, hutaingiza. Nasi tuchukue bidhaa zetu kama hizo za chakula kule kwangu, Mheshimiwa unajua kunalimwa mpunga, lakini mpaka leo wananchi wanauza mpunga kama mpunga. Watu wanatoka India wanakuja kununua mpunga. Sasa wanaenda kuuchakata huko Dar es Salaam sijui wapi, mashine za kisasa wangeleta pale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tuna shida ya mashine ya kukausha mpunga, bado tunataandika majamvi tunaanika mpunga kwa kutegemea jua. Wakulima wetu hawawezi kuingiza mashine za kukausha mpunga? Haya, hao wawekezaji wa hizo mashine waje waone soko watuuzie hizo mashine, wazitengenezee hapa hapa, wakulima wetu waweze kusindika mpunga ule unaonunuliwa India kwenye packet supermarket utoke hapa moja kwa moja. Hiyo ndiyo exportation unayosema. Sasa mimi nimesema kwa uchache kwa sababu kaka yangu Mheshimiwa Dkt. Mwigulu namwona pale, yeye ni mtaalamu wa uchumi atakuja kufafanua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, Waziri kapewa bajeti 38% ya pesa zilizotengwa, sasa huyu Mheshimiwa Dkt. Mwigulu, Waziri wa Fedha tutamuua bure hapa kwa sababu kila ukienda kwenye Wizara kuna shida kwa sababu ya miradi mikubwa tunayofanya. Ni muhimu kupanga kutokana na tunachokusanya kila mwezi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naunga mkono hoja. (Makofi)