Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ludewa
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi na nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa uwasilishaji wa bajeti yake kwa umahiri mkubwa. Nina imani umahiri huo utakwenda mpaka kwenye utekelezaji wa miradi ile ya Mchuchuma na Liganga. Hali kadhalika, niungane na Wabunge wengine kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kuonesha dhamira yake ya dhati kwamba sasa miradi ile iweze kukwamuliwa, Mradi wa Mchuchuma na Liganga. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachokiomba tu ni kwamba yale majadiliano hatua yalipofikia, Wizara ingeangalia multiply effects waangalie manufaa ambayo nchi yetu inaweza kupata kutokana na kuanza kwa miradi hii. Kuna ajira nyingi pale za vijana, lakini tutaokoa fedha nyingi sana za kigeni kuagiza chuma nje ya nchi. Wanachoomba tu wananchi wa Ludewa ni viwanda, kipaumbele cha kujenga viwanda kiwekwe Ludewa. Kiwanda cha Chuma kijengwe pale Liganga kama ambavyo mpango ulikuwa toka awali na mambo mengine pia yaweze kufanyika eneo ambapo malighafi inapatikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kuishukuru sana Serikali kwa kuwalipa fidia wananchi wale kiasi cha shilingi bilioni 15.4. Imekuwa ni upendo mkubwa kwa wananchi wale, imewapa moyo na faraja kubwa, wanaamini kwamba Serikali iko nao sambamba na wako tayari kuendelea kuiunga mkono Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi wananchi wa Mundindi baada ya kulipwa zile fidia kiasi cha shilingi milioni 800 na pointi walikaa mkutano wa Serikali ya Kijiji, wakakaa mkutano wananchi wote wa kijiji wakaazimia kwenye ile fedha ambayo walilipwa kwenye mashamba ya kijiji wakaenda kununua bond kwenye Benki ya CRDB, Kijani Bond. Fedha ile imeshaanza kuzaa, wamevuna awamu ya kwanza shilingi milioni 40.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, fedha hiyo, wameitumia katika kuwalipia bima wananchi wa kijiji hicho wasiopungua 3,000, kila mwananchi atalipiwa bima lakini chanzo ni fidia hii ya eneo la Liganga na Mchuchuma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hali kadhalika wakiendelea kuvuna wanakusudia kukarabati shule za msingi kwenye kijiji hiki, lakini wananchi wengine mmoja mmoja nao wameweza kutokana na elimu ambayo tuliwapa fedha hizi wamezitumia kwa manufaa makubwa sana. Niliona nilisemee hili la Mundindi ambao wamenunua bond CRDB kwa sababu ni kitu ambacho ni cha kipekee. Kwa hiyo, nampongeza sana Mheshimiwa Diwani wa Kata ile Mheshimiwa Wise Mgina na viongozi wote wa vijiji kwa maono, halikadhalika halmashauri na Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa Mtaka kwa kuweza kulisimamia jambo hili vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia pale Liganga kulikuwa na miradi miwili, kulikuwa na mradi ulikuwa unaitwa Kasi Mpya na kulikuwa na ule Main Liganga ambao ni wa Mchina. Sasa ule mradi mdogo kuna mwekezaji mdogo ambaye ana viwanda huko Mkuranga Mkoa wa Pwani anatumia chuma chakavu. Chuma chakavu sasa hivi imekuwa ni adimu sana kupata, alikuwa anatarajia awekeze pale Viwanda Ludewa kwenye ile Liganga ndogo lakini bahati mbaya majadiliano nayo yamechukua muda mrefu sana. Imechukua siyo chini ya miaka miwili, mitatu kujadiliana naye.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nafahamu kulikuwa na Azimio la Baraza la Mawaziri ambalo ikawa inahitajika tena hii negotiation na huyu mwekezaji irudi tena huko kwa maamuzi. Nisingependa kusema ni majadiliano gani, lakini namwomba sana Mheshimiwa Waziri, basi aharakishe hii ili mradi ule nao uweze kuanza. Kwa sababu ikianza tu ile Liganga ndogo tayari pale tutatoka jasho, pato la Taifa litaongezeka, tutaokoa dola nyingi ambazo tunatumia kuagiza chuma nje ya nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Serikali inakusudia kujenga reli kutoka Mtwara – Mbamba bay, tawi la Mchuchuma na Liganga. Kwa hiyo, chuma kitakachotoka pale kinaweza kikaokoa dola ambazo tunaagiza chuma nje ya nchi. Halikadhalika, tunavyozungumza agenda ya viwanda hapa nchini itakuwa na manufaa makubwa iwapo kutakuwa na malighafi, kutakuwa na chuma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo hili la Maganga Matitu kulikuwa na wananchi ambao walifanyiwa uthamini walikuwa bado hawajalipwa. Sasa wanavyoona wenzao wanapata bima za afya, wananunua matrekta, wananunua magari, wao bado, wameniomba mimi Mbunge wao nije niwasemee ili Mheshimiwa Waziri aweze kusimamia jambo hili ili nao wao walipwe kwa sababu fedha siyo nyingi kama ya mwanzo. Wana imani kwamba kama Mheshimiwa Rais aliweza kulipa shilingi bilioni 15 na hizi bilioni chache haziwezi kumpa shida. Kwa hiyo, naomba sana wale wananchi wa eneo la Maganga Matitu waweze kulipwa fidia zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hali kadhalika, kuna lile eneo la makaa ya mawe kule Mchuchuma Kijiji cha Nkomang’ombe kuna wale wananchi wa eneo la Ketewaka ambao nao walifanyiwa uthamini fedha siyo nyingi kama za mwanzo, nao wana imani kama Mheshimiwa Rais aliweza kulipa shilingi bilioni 15 wana imani nao wanaweza kwenda kulipwa fidia hizi mapema sana ili nao waweze kufanyia shughuli mbalimbali za maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uniruhusu pia niweze kutoa pole kwa wale wananchi wa Kitongoji cha Mhumbi jirani sana na mradi huu wa Ketewaka. Waliona maji kutoka kwenye chanzo chao yanatoka machafu kama siku tatu, leo walikwenda eneo hilo kukagua kuona kwa nini maji yanakuwa machafu. Sasa walipofika huko wakaona ule mlima una ufa unaitwa Mlima Mhumbi, una ufa mkubwa halafu unatoa kelele (sauti). Sasa wale wananchi kwa sababu ni tukio ambalo hawajawahi kuliona hawajalizoea wakakimbia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tumeweza kuwasiliana na watu wa GST watatuma wataalamu ila tu wameshauri wananchi wasisogee eneo hilo wachukue tahadhari, kwa sababu wanasema tayari eneo kama la ekari moja pametokea maporomoko ya ardhi, lakini pia ule mlima unavyotoa kelele kunakuwa kama na matope. Sasa hatuna uhakika kama ni volcanic activity au mass wasting au nini, lakini wataalamu wameahidi kwenda. Eneo liko jirani sana na eneo hilo la wananchi ambalo wanadai fidia. Ni wananchi wa Kitongoji hiki cha Mhumbi ndio ambao wanadai fidia za eneo la Ketewaka, kwa hiyo, niombe hawa waweze kulipwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Wizara hii ilichukua agenda ya barabara wakati wa majadiliano na mwekezaji, ile barabara inayoanzia Mkiu - Liganga kwenda Madaba na barabara inayounganisha Liganga na Mchuchuma kilometa 70 na kile kipande cha kutoka Mawengi. Zipo barabara ambazo mwekezaji angetoa fedha ziweze kujengwa kwa kiwango cha zege. Kama hili litafanikiwa kwenye hayo majadiliano, nina imani litakuwa limerahisisha sana shughuli za uchukuzi na usafirishaji wa maeneo haya. Uwekezaji huwa unaenda sambamba na barabara bora za maeneo haya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, machache, nishukuru sana kwa kupewa nafasi, nipongeze sana Wizara hii kwa kazi nzuri na naomba fidia zile kwa wananchi wachache waweze kulipwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)