Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mbinga Vijijini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi nami ili niweze kuchangia katika Wizara hii ya Viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kuunga mkono hoja. Nampongeza sana Mheshimiwa Waziri, Naibu wake na Wataalam, kwa kweli wanafanya kazi nzuri katika Wizara hii ya Viwanda na Biashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesimama hapa ili niweze kuchangia kwenye maeneo matatu na muda ukiniruhusu ni manne. Kwanza ni ombi, nilizungumza hapa mwaka 2023 kuhusu ombi la kiwanda. Nchi yetu hii imebarikiwa sana kuwa na malighafi nyingi za viwanda. Sifa mojawapo ya mtu kupeleka kiwanda sehemu ni pamoja na kupatikana kwa malighafi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Mbinga tunamshukuru Mungu, tunazo malighafi za kutosha. Tunazo malighafi kwenye kilimo kwa sababu tunazalisha vizuri sana mahindi, kahawa pia tunazalisha mazao mengine kama parachichi na karanga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo bahati sana sasa hivi tunayo makaa ya mawe, zote hizi ni sifa za mtu kupeleka kiwanda katika eneo hilo. Niliomba mwaka 2023 kwamba tunaomba kiwanda. Pale tuna viwanda vya kubangua kahawa, tuna viwanda viwili vina-roast kahawa kwa bahati mbaya hatupati ile kahawa ya mwisho kabisa finest, hatuipati. Ili tuipate ile Kahawa inachukuliwa inapelekwa Bukoba. Tunashukuru Bukoba ni sehemu ya nchi hii lakini ingependeza sana nasi pale Mbinga tungepata kiwanda cha aina hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajua kiwanda kikiwepo mahali husika wananchi wanapata ajira, lakini hata ile malighafi yenyewe tunaiongezea thamani, badala ya kuuza kwa namna tunavyouza sasa hivi, tungeuza kwa gharama zaidi na bei nzuri zaidi. Kwa hiyo, naiomba Wizara, najua Mheshimiwa Waziri halali anazunguka huko duniani. Pia, namshukuru sana Mheshimiwa Rais, pale anapofanya ziara za namna hii ni lazima amchukue Waziri wa Viwanda na wanatembea kuzunguka. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri huko unapokwenda, basi ututafutie kiwanda. Tutafutie kiwanda kwenye kahawa na kwenye mahindi kwa sababu najua tukiuza unga tutapata fedha zaidi kuliko tunapouza mahindi yenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ukitembea kule kwenye upande wanaochimba makaa ya mawe, wanasema waliwahi kuahidiwa kwamba watapelekewa kiwanda. Sasa kila nikipita huwa wananikumbusha hilo. Naomba nalo kwa sababu tuna makaa ya mawe mengi sana kiasi kwamba kuyapeleka tu huku hatutayamaliza, kwa hiyo, tupelekewe kiwanda pale ili wananchi hawa wanufaike na uwepo wa rasilimali za malighafi hizi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo ningependa kulizungumzia leo ni mradi huu wa siku nyingi wa Liganga na Mchuchuma. Nilizungumza hapa mwaka 2023, lakini niishukuru sana Serikali ya Awamu ya Sita kwa nia ya dhati kabisa kutenga hizi fedha shilingi bilioni 15.3 kwa ajili ya kulipa fidia. Hii ni nia thabiti kabisa ya kwamba Serikali hii ina lengo na mradi huu uweze kuendelea. Sasa umechukua muda kidogo toka walipe, mimi binafsi nilidhani kasi ile ingeendelea lakini inaonekana kuna maneno maneno yanaendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Wizara kwenye maneno haya tuyamalize. Mradi huu una historia ya siku nyingi mno. Liganga, liganga lakini kwa kulipa hizi fedha tunadhihirisha kabisa Serikali yetu ya Awamu ya Sita iko tayari mradi huu uanze lakini sasa kwa kasi gani? Tunaomba sana mmalize huo mgogoro.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo maneno kwamba mwekezaji aliyekuwepo hayupo duniani, sina hakika, kama ni kweli basi tuyamalize haya maneno ili mradi huu uchukue kasi na Tanzania yetu inufaike na mradi huu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapata shida sasa hivi unaweza kuona tunaagiza chuma kutoka nje, kumbe Mungu ametujalia nchi hii tuna chuma hapa hapa. Kwa hiyo, mradi huu ukianza maana yake hatutaagiza chuma kutoka nje, tutachota pale, tunazalisha. Vivyo hivyo, itapelekea viwanda vyetu vizalishe malighafi katika nchi yetu isiwe juu. Sasa hivi tunapata shida bei ya bati iko juu, bei ya nondo iko juu, kumbe sasa kupitia malighafi tuliyokuwa nayo hapa, bidhaa hizi zitashuka bei. Nakuomba sana jambo hili tuende nalo kwa kasi kidogo ili liweze kutekelezeka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu nyingine ambayo ningependa kuizungumzia na ambayo Mheshimiwa Waziri na Kamati wameizungumzia ni suala hili la stakabadhi za ghala. Tanzania ni wakulima ili twende vizuri ni lazima tufanye huu mkakati na mpango huu wa stakabadhi za ghala, kwa sababu ununuaji wa mazao holela mara nyingi hauwezi kumnufaisha mkulima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna stakabadhi ya ghala ilivyo sasa hivi, kila mtu angependa kwenye eneo lake tuwe na hii stakabadhi ya ghala japo hatujafikia kule ambako stakabadhi ya ghala inataka, kwa sababu mnajua taratibu za stakabadhi za ghala, mtu akiwa nayo anaweza kwenda benki, kuchukua pesa au kufanya kitu chochote, lakini sasa hatujafikia huko. Ombi langu kwa Waziri ni kwamba ingefaa sana tufikie huko kwa sababu ile ni rasilimali, ile ni fedha lakini hata hapa tulipo tunakwenda vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi juzi tu nimesikia kwa kuunganisha na suala hili la TMX mmefika Songwe mmeuza ufuta na wananchi kule wana shangwe sana. Ningetamani sana hata kwenye zao la kahawa sasa hivi Mheshimiwa Waziri sasa hivi wako wananchi wanalalamika, wameuza kahawa mwaka 2023 mwezi wa Saba mpaka leo hii baadhi ya AMCOS hazijalipa, lakini tukiwa na mifumo hii, nimeambiwa hapa TMX inalipa ndani ya masaa 24.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake ni kwamba wananchi hawa hawawezi kupata hizi kero, wananchi hawa wanapeleka mazao wanauza, wanapata fedha na hivyo kutakuwa na maendeleo ndani ya nchi. Kwa hiyo, nawapongeza sana na nawapongeza wataalamu, wanafanya vizuri, hongereni sana na endeleeni kuchapa kazi ili wananchi wetu wanufaike na mazao yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nilitaka kuongelea hili suala la bei, nimeligusagusa hapa; bei zetu za bidhaa hizi za viwandani ziko juu. Nampongeza Waziri kwa utaratibu aliouanzisha wa kutoa taarifa kila tarehe 15 ya mwezi, ni mzuri, lakini hoja ya kwa nini tunanunua bati la gauge 30 kwa shilingi 25,000? Kwa nini tunanunua nondo milimeta 10 kwa shilingi 25,000? Kwa nini tunanunua malighafi hizi za simenti kwa shilingi 18,000 au shilingi 20,000? Bado bei iko juu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati tunaanzisha baadhi ya viwanda hapa nchini, wananchi waliambiwa sasa tunaenda kupata bidhaa hizi kwa unafuu ikiwemo simenti. Kwa hiyo, naomba sana Mheshimiwa Waziri kuna jambo hapa linapaswa lifanyike, bidhaa hizi bado ziko juu, tutafute namna yoyote ikiwezekana hata tuweke ruzuku ili wananchi wetu hawa wapate hizi bidhaa kwa bei ya chini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema hapa kwamba, sasa hivi nchi yetu hii malighafi ni nyingi. Kwa mfano, malighafi za bati nyingi zinapatikana hapa nchini, malighafi za simenti ikiwemo clinker inapatikana hapa hapa nchini. Sasa kwa nini simenti iuzwe kwa bei ya shilingi 20,000 kwa mfuko? Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri nakuomba sana tutafute namna ili wananchi wetu hawa bidhaa hii waipate kwa bei ya chini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii inawezekana kabisa, maana yake suala la ujenzi sasa hivi baadhi ya maeneo wataendelea kubaki na hawataweza kujenga kwa sababu malighafi hizi ziko juu sana, ili tuende kwa pamoja, basi tuzishushe bei malighafi hizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, naona umewasha kipaza sauti, naunga mkono hoja, ahsante. (Makofi)