Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda na Biashara kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Jesca Jonathani Msambatavangu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Iringa Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda na Biashara kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nashukuru kwa kunipa nafasi. Naipongeza Wizara hii kwa kazi kubwa wanayoifanya pia kwa lile jambo la Mchuchuma, tunawapongeza sana na tunawatakia kila la heri kuhakikisha kwamba linafika mwisho na tunaanza kuona matunda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwa ku-quote hotuba ya Mheshimiwa Waziri ambayo anasema “Mheshimiwa Spika, sekta ya viwanda na biashara kwa kiasi kikubwa inategemea shughuli za sekta binafsi ambayo ndiyo inayowekeza mitaji yao viwandani na kwenye miamala ya kibiashara ili kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa na huduma nchini unakuwepo wakati wote.” Hivyo, Mheshimiwa Waziri anasema jukumu kubwa la Wizara yake yeye ni kusimamia masuala ya utafiti, ushauri, uratibu, kutoa mwelekeo kwenye tasnia hii ya viwanda na biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haipingiki kwamba sekta binafsi ndiyo imebeba viwanda na biashara. Wakristo tunaambiwa katika Mhubiri 10:19 fedha ni majawabu ya mambo yote. Kwa maana hiyo ni kwamba, walioshika majawabu ya mambo mengi ya Taifa letu ni hawa wafanyabiashara ambao Mheshimiwa unawasimamia wewe na ambao umesema ni sekta binafsi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuainisha majukumu yako Mheshimiwa Waziri umesema mnaratibu masuala ya utafiti yanayohusiana na biashara, mnatoa ushauri na mnaonesha mwelekeo. Kwa maana hiyo, sekta hii binafsi inakutegemea sana wewe Waziri wa Viwanda uwasaidie katika kuratibu mambo yao na sekta nyingine au Wizara nyingine ili wafanye vizuri zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri wa Fedha alitusomea hapa mapato ambayo tumekusanya mwaka 2023 nayo yana-reflect hii taarifa yako, kwamba tulikuwa tumekusanya shilingi trilioni 38, ambapo shilingi trilioni 23.6 ilitoka kwenye mapato ya ndani ambayo Mamlaka yetu ya Mapato ilikusanya shilingi trilioni 23.6, hizo shilingi trilioni 13.4 ni fedha za mikopo, hiyo shilingi trilioni moja ni kutoka vyanzo vingine. Kwa hiyo, utaona kwamba fedha nyingi inayokusanywa hata kwenye mapato ya nchi hii inatoka kwenye sekta binafsi, kwa maana hiyo sekta hii inatakiwa iangaliwe kwa umakini mkubwa sana, wafanyabiashara na wawekezaji kwenye viwanda wanatakiwa kutunzwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu manufaa ya biashara kwamba inafanya kuanzisha ajira kubwa sana katika nchi. Biashara inaleta makusanyo ya mapato, biashara inasaidia ujenzi wa miundombinu. Nikafikiria nikaona kumbe katika Mawaziri hawa wewe hapo ndiye Waziri mkubwa wao na wengine wote hawa wangekuwa ni Mawaziri wadogo wadogo kwako. Kwa sababu hakuna barabara bila biashara na fedha wala hakuna afya bila biashara na fedha. Hatuna miundombinu yoyote itakayofanyika kwenye nchi hii kama hatuna fedha. Pia, tumekusanya kodi kutoka kwa wafanyabiashara ambao ni sekta binafsi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Mheshimiwa Waziri lazima ajifunge kibwebwe bila kuwa mpole ahakikishe mtu anayeivuruga Sekta ya Biashara anapambana naye. Kama anashindwa kupambana naye yeye kwa jinsi alivyo kwa sababu wote wana rank moja, basi aangalie hata namna ya kumchongea sehemu ili ashughulikiwe. Kwa sababu hapa kuna dhambi ambayo inawasumbua sana watoza ushuru tangu enzi za Yohana. Yohana alishughulika nayo akashindwa, amekuja Yesu akawaacha nayo mpaka sasa hivi kizazi hiki Manabii na Mitume wanashindwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ipo dhambi ya watoza ushuru na hii imeandikwa katika Kitabu cha Luka 3:12-13 maneno ya Mungu yanasema hivi, “Watozaushuru nao au wakusanyakodi wakamwendea yule Nabii Yohana wakamwuliza hivi, “nasi tunataka kwenda mbinguni, tufanye nini? Nabii Yohana akawaambia, “msibambikize kodi watu.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, dhambi hii ya kubambikiza kodi watu ndiyo inayoharibu sekta binafsi. Mheshimiwa Waziri wewe ni kuratibu, ni ku-coordinate, ni kufanya mambo yawe fair kwenye sekta zote na kuongea na wenzio professional wengine ili kuona umuhimu wa biashara. Wao wanaona tu fedha zinatiririka Hazina hawajui wewe unazidi kuwa mfupi kwa kuhakikisha kwamba biashara huku zinakomaa zinazalisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri sasa asiwachekeechekee, awasemee kama anashindwa kupambana nao kwa sababu leo hii kuna watu bado wanafunga biashara. Iringa kwangu mimi wafanyabiashara wangu wananipigia simu wiki nzima, wanafungiwa biashara karne hii. Tunajifunza kwenye biashara kuwa meneja yeyote mwenye akili anatumia watu kufikia malengo yake na siyo nguvu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa wenzetu hawa wakusanyaushuru na watoza ushuru waangalie kama wana mameneja ambao bado wanatumia nguvu, hawatumii akili wawatoe wawaweke wale wanaotumia akili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nikwambie, Wahasibu sio Mameneja wazuri sana kwa sababu moja ya theory za uhasibu ni conservatism, kuwa rigid tu bila sababu. Yaani mtu anajimwambafai tu, yuko rigid, hataki kumsikiliza mtu, akipita amenuna tu, ndio style. Yaani rigidity au conservatism ni one of the theories ya wahasibu. Tafuteni mameneja. (Makofi)

MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa. (Kicheko)

MWENYEKITI: Taarifa.

TAARIFA

MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, mchangiaji anachangia vizuri sana nataka tu nimpe taarifa mchangiaji kwamba wahasibu hawa huwa wanachojua ni debit and credit wala siyo conservative by nature.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Jesca, unapokea hiyo taarifa?

MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Twaha, mwakilishi wa wananchi kutoka Kibiti ni Mhasibu lakini mimi pia nilisema siku ile ni Daktari wa DBA. Najua theory za wahasibu ni conservatism abishe kama siyo. Conservatism ni one of their theories, yaani ndiyo utaratibu wao na wewe sio mhasibu kama hauko conservative. Sasa ni kanuni na hawa sio mameneja, lakini mameneja ni watu ambao wanaweza wakaongea na mtu wakamtia moyo akamwelewa kwa maneno na akalipa kodi willingly. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nimekwambia Iringa leo watu wanafungiwa biashara, wanaandikiwa kodi za miaka iliyopita. Mtu amepewa notice ya kodi ya mwaka 2013. Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alisema jamani hizi kodi za miaka sita hizi hebu tuachane nazo. Ukishaona mtu siku zote anafuatilia viporo, huyo ameshafika mwisho hana uwezo wa ku-deliver kitu kipya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwenye uwezo wa ku-deliver kitu kipya atatafuta mbinu mpya na vyanzo vipya vya mapato siyo kurudi kutafuta viporo walivyoviacha wenzie huko nyuma. Leo hii unaenda kufunga biashara, umeshindwa kuongea na haya mambo ilishasemwa yasifanyike.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo tena tuna jambo lingine hapo kwa wenzetu hawa wakusanya kodi. Nimesema kudai kodi za zamani, kubambikiza kodi na kutengeneza uadui na wafanyabiashara. Mheshimiwa Waziri lazima wakusanya kodi wajue kwamba hata mishahara yao na suti zao na viti wanavyokalia kule maofisini vinatoka kwa yule mfanyabiashara mdogo anayekuja kumkadiria kodi pale. Yaani wao sio mabosi wao ni watumwa, wale wanaokwenda pale ndiyo wameshika majawabu ya maisha yao na mishahara yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hicho ndicho kinachotuangusha. Hawa TRA wangekuwa na uwezo wa kukusanya zaidi ya hizi shilingi trilioni 23.6. Halafu lazima wajue kwamba wafanyabiashara ni ma-genius na ma-intelligent ndiyo maana wako wachache. Ni watu wanaotumia akili kubwa sana huwezi kumshinda. Uchumi ukishaharibu mazalia yake ni kama uyoga kuurudishia ni shida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa tunahangaika na dola kwamba hazipo. Hapa ni practice iliyofanywa wakati ule wa ku-harass Bureau De Change leo tumepoteza style mpaka turudi kwenye line itatupa shida. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri vitu kama hivi hutakiwi kuviruhusu semelea maana wengine watakusumbua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine naomba sasa, kuna mtu anauliza asemee wapi? Yeye anajua, mbona hajauliza! (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine tunamwomba sana Mheshimiwa Waziri, muwe karibu na hawa wafanyabiashara wadogo kwa sababu kila unayemwona ni tycoon; leo alianza kama mbuyu ulioanza kama mchicha. Kwa hiyo, harassment ya wafanyabiashara wadogo kama machinga ndio hatuna future ya kuja kuwa na wafanyabiashara wakubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri hii ni Sekta yake na anawasimamia Mama yangu. Naomba pamoja na kwamba wamepelekwa kule Maendeleo ya Jamii lakini wale ni wafanyabiashara. Ninyi Wizara zenu zinaingiliana; washikiliwe hawa wakuzwe watakua. Wakikua watatuletea kodi kubwa, wakishatuletea kodi kubwa hapa tuta-solve majawabu ya mambo mengi sana. Tunalalamikia umeme humu, tunadai barabara, tunadai madaraja, tunadai dawa na tunadai bima za afya. Wale ndiyo wameshika majawabu.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, watumishi wa umma nchi hii siyo wengi, nao wanajitahidi sana, wanalipa kodi sana na ni kati ya walipakodi wazuri; nao ni wa kuangaliwa. Wazabuni wa nchi ndio wafanyabiashara, ndio walioshika majawabu. Leo unam-starve mtu ana-save chakula kwenye shule, mama tu anasaga unga humlipi ile hela. Usipomlipa ile hela kwa miezi sita umemuua anaenda kununuaje mahindi aje aendelee kulisha na yeye aendelee na biashara? Kwa hiyo, wafanyabiashara wa ndani, wazabuni, walipwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna ombi lingine.

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa, nimekuvumilia kidogo ili umalizie.

MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, muda umeisha?

MWENYEKITI: Ndiyo.

MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naunga mkono hoja.