Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati Maalum iliyoundwa Kuchunguza Mgogoro wa Ardhi kati ya Mwekezaji kwenye Shamba la Malonje na Vijiji Vinavyolizunguka Shamba hilo Kikiwemo Kijiji cha Sikaungu katika Jimbo la Kwela

Hon. Festo Richard Sanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makete

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati Maalum iliyoundwa Kuchunguza Mgogoro wa Ardhi kati ya Mwekezaji kwenye Shamba la Malonje na Vijiji Vinavyolizunguka Shamba hilo Kikiwemo Kijiji cha Sikaungu katika Jimbo la Kwela

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuchangia kwenye hoja iliyopo mezani. Kwanza, nichukue nafasi hii kukushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuwa Mjumbe wa hii Kamati Maalum kwa ajili ya kutatua mgogoro pale Shamba la Malonje. Pili, nampoongeza sana Mwenyekiti kwa kusoma vizuri na kwa kueleweka sana kwenye hoja iliyopo mezani.

Mheshimiwa Spika, mimi nilipata nafasi ya kushiriki kwenye Kamati hii na imenipa fursa ya kujifunza mambo mengi sana kwenye issue ya uwekezaji nchini. Kwenye hili jambo la Malonje kwanza niunge mkono maazimio yote ya Kamati na niliombe Bunge na niombe Waheshimiwa Wabunge tuunge mkono hiki ambacho tumekizungumza na kukipendekeza kama Kamati kuhusu namna ya kuendea hili jambo ili tuweze kufanikiwa.

Mheshimiwa Spika, watu wanaongezeka, idadi ya watu na inaongezeka kila siku…
Mheshimiwa Spika, nashukuru, kwenye hili jambo la Malonje idadi ya watu nchini inaongezeka na mahitaji ya ardhi yanazidi kuongezeka kila siku. Kwa jinsi ambavyo tumeenda kuona uwandani kwa maana ya site uhitaji wa ardhi kwa wananchi ni mkubwa sana. Kutokana na kuwepo kwa uhitaji mkubwa wa ardhi kuna haja ambacho tumekipendekeza kwamba umiliki wa lile shamba ubatilishwe ili tuweze kwenda kwenye mchakato wa kuligawa upya ili wananchi na wenyewe waweze kupata haki.

Mheshimiwa Spika, ukienda site na ukafanya mikutano na wale wananchi utagundua umuhimu wa maeneo mbalimbali wawekezaji kuwa na mahusiano mazuri na wananchi. Lile jambo lililopo pale tukiliacha leo, tukiliacha kesho, tukiliacha mwakani mwisho wa siku itakuja kuwa na bomu kubwa sana kwa sababu generation (kizazi) kinachozidi kuzaliwa pale kinazaliwa na chuki dhidi ya mwekezaji kwa sababu anaona kuna matukio ambayo yametokea kwenye maeneo yale. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa ili twende kwenye mwanzo mzuri na tuweze kuweka mahusiano mazuri kati ya wananchi wa vile vijiji vinavyozunguka Shamba la Malonje, haya mapendekezo ni muhimu sana na yataleta mustakabali mzuri sana kuhakikisha kwamba mahusiano kati ya mwekezaji, lakini pili mahusiano kati wananchi na eneo la shamba yanaimairishwa.

Mheshimiwa Spika, ukiangalia ukodishwaji wa lile shamba na kufungamanisha suala la kiimani kwamba ili uweze kukodishwa utoe fungu la 10 ufanye, nini ni vitu ambavyo vimekuwa vikivunja sana mahusiano na ukizingatia katika nchi yetu ni nchi ambayo wakulima siyo wakristu tu, wakulima pia wapo wenzetu ambao hawafungamani na ile imani na wangetamani kutumia hilo shamba.

Mheshimiwa Spika, pia, siyo kusudio la Serikali kuona lile shamba linatumika kwa mfumo huo. Kusudio la Serikali lilikuwa ni uwekezaji wa kisasa. Kutokutumika katika uwekezaji wa kisasa maana yake ni kwamba tumekiuka miiko na taratibu za kimkataba ambazo Serikali ilikuwa imejiwekea. Kwa hiyo, kuna umuhimu sana kuona Serikali inalisimamia hili ambalo tumelipendekeza kama Bunge na tutafikia muafaka kwenye hilo jambo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine, nchi kama nchi yawezekana wakati tunaenda kwenye maono ya uwekezaji kwenye Taifa letu tulikuwa na maono mazuri sana kwamba tunahitaji kubinafsisha maeneo ya Serikali kadha wa kadha ili Watanzania au sekta binafsi iweze ku-take off na kuweza kufanya uzalishaji mkubwa. Kwa hiki kinachoendelea Malonje kinatupa maswalli kuna maeneo ambayo tumewezeza viwanda nchini, kuna maeneo ambayo mashamba tumewekeza nchini kama haya maeneo hayafanyiwa tathmini…

MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Sanga, kuna Taarifa. Nani anatoa taarifa? Mheshimiwa Festo Sanga, kuna Taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Dkt. Pallangyo.

TAARIFA

MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami nimpe Taarifa mzungumzaji kwamba hili analolizungumza hapa linatoa taswira njema ya Taifa kwa ujumla kuangalia maslahi na ustawi wa wananchi wake. Pia, nimfahamishe kwamba kule kwangu Eneo la Momela mipaka ilikuja ikawekwa kwa ajili ya kupisha uhifadhi, lakini mpaka ule ukawa umepita kwenye milango ya wananchi. Kwa hiyo, akitoka asubuhi anaingia kwenye hifadhi, matunda yake wanaumizwa au wanachukuliwa hatua za kinidhamu na Mamlaka ya Hifadhi.

Mheshimiwa Spika, pia, kuna Kijiji pale Kata ya Maroroni ambacho kilikuwa kimeshaandikishwa, lakini mpaka wa KIA wakaenda kukifuta. Nashukuru sana. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Festo Sanga, unaipokea Taarifa hiyo?

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Spika, ninaipokea taarifa ya mzee wangu kwa sababu kile nilichokuwa nakizungumza kwamba ningependekeza kama nchi, lazima tuliangalie suala la uwekezaji kwenye Taifa letu limefikia hatua gani? Kuna maeneo mengi ambayo tumeyawekeza. Huu mgogoro wa Malonje ni mmoja tu, ukienda Handeni kuna mgogoro na ukienda maeneo mbalimbali kuna migogoro. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo hii kama Serikali haitachukua tathmini kufuatilia kila mtu aliyemkabidhi shamba, waliyemkabidhi kiwanda katika sekta ya uwekezaji amefanyia nini kile? Hii migogoro itaendelea kujirudia na kujirudia. Kwa hiyo, kuna haja Serikali ipo hapa ndani inatusikiliza, kuna viwanda ambavyo tuliwapa watu, vimekufa haviendelei kufanya kazi. Kuna mashamba watu wameyakumbatia na uhitaji wa watu bado ni mkubwa ila watu wameyakumbatia.

Mheshimiwa Spika, kuna haja Serikali kuunda timu ya watu wenye uzalendo, ya watu ambao watatanguliza maslahi mbele kuhakikisha tunafanya tathmini kwa sababu nchi yetu kuzaliana kumekuwa ni kwa kiwango kikubwa. Kuna haja ya kuangalia kwamba maeneo mengine ya uwekezaji pia tunayaangalia kwa kina ili kulinda maslahi ya nchi yetu Taifa letu, ni hili hili Tanzania ardhi haiongezi ila idadi ya watu inaongezeka.

Mheshimiwa Spika, kwa watu waliokumbatia maeneo ya watu ambayo hayazalishi ni muhimu Serikali ikafanya tathmini ili tuweze kuisadia nchi yetu. Mathalani kwenye issue ya viwanda ambavyo tumekuwa tukivipigania kelele kila siku. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hili suala la Malonje, tumeenda site, yaani unaenda sehemu kutafuta uthibitisho mathalani kwenye vituo vya Polisi kuhusu mtu aliyepigwa risasi unakosa PF3. PF3 haipo na wao wanaonesha kwamba hawana taarifa na hilo jambo. Sasa sisi tunaona kabisa kwamba pia hata hizi mamlaka (vyombo vya dola) ni muhimu kabisa kusimama na wananchi. Kwa sababu wananchi wanapoendelea kukosa imani dhidi yao, hawaendi kuripoti cases ni kitu ambacho kinakuwa ni kibaya kwenye mustakabali wa kusimamia haki kwenye Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ni muhimu sana na niombe Jeshi la Polisi wakaangalia pale Rukwa watoe takwimu na mamlaka zipo hapa waangalie nini mchakato wa hawa watu? Watu wengi wamekuwa wakifanyiwa matukio mengi lakini wanaogopa kwenda kwenye vituo vya Polisi kutoa ripoti kwa sababu wanajua mwekezaji ana nguvu, mwekezaji ana mkono mrefu ambao wao wananchi watakuwa wamekosa haki yao. Kwa hiyo, kuna haja pia ya Serikali kuchunguza hilo jambo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi niunge mkono hoja ambayo ipo mezani na nilishawishi Bunge kwamba, leo hili lipo Malonje, lakini kesho itakuwa eneo lingine. Hii ndiyo iwe basement yetu au tu-set bar kupitia hili ili na maeneo mengine ya nchi tuweze kufanyia tathmini katika suala la uwekezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, watu ambao wanakumbatia mashamba au viwanda tuanze kuwaangalia kwa jicho lingine ili twende kujenga nchi yetu ambayo ina uchumi imara, nchi ambayo ina uzalishaji, nchi ambayo ina amani, nchi ambayo wawekezaji hawashiki ardhi kubwa na baadaye wanageuka kuwa maadui na wananchi wetu.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, nakushukuru kwa kunipa nafasi na ninakushukuru kwa kuniamini kuwa Mjumbe wa Kamati hii Maalum kwa ajili ya Ardhi ya Malonje na mgogoro ule. Ahsante. (Makofi)